MBUNGE WA PANGANI AWEKA MIKAKATI YA UJENZI WA SOKO LA KISASA LA SAMAKI PANGAN

June 16, 2017
MBUNGE wa Jimbo la Pangani (CCM) Jumaa Aweso amesema mkakati mkubwa alionao hivi sasa ni ujenzi wa soko la kisasa la Samaki katika wilaya hiyo ili kuwakomboa wavuvi kiuchumi wao na jamii zao kutokana na kukosa sehemu sahii ya kufanyia shughuli zao.
Hayo aliyasema wakati akizungumza na mtandao huu ambapo alisema wilaya ya Pangani shughuli za uvuvi zimekuwa ndio kazi kubwa kwa jamii hiyo lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa soko maalumu la kufanyia biashara zao.

Alisema kutokana na kuwepo kwa changamoto hiyo anakusudia kupelekea ombi kwa serikali kwenye vikao vya bunge ili serikali ione namna ya kuwajengea soko la kisasa wananchi wake ili waweze kuondokana na adha wanayoipata mara baada ya kuvua samaki hao.

“Miongoni mwa majukumu niliyoyabeba kwa wananchi wake na kuyafikisha bungeni ni pamoja na suala la kujengwa soko la kisasa la samaki ambalo ndio mkombozi wa kuinua kiuchumi kwa jamii ya wakazi wa Jimbo la Pangani kwani limezungukwa mto Pangani ikiwemo bahari ya hindi “Alisema.

“Kama unavyojua Jimbo langu la Pangani asilimia kubwa wananchi wake wanajishughulisha na shughuli za uvuvi hivyo lazima tutawekee miundombinu imara ikiwemo soko la kuuzia na kuhifadhia samaki wanaovuliwa kwa ajili ya kuuzwa “Alisema.

Kauli ya Mbunge huyo inatokana na kuwepo ombi kutoka kwa wavuvi wilayani humo wakiitaka Serikali ya awamu ya tano chini ya Dokta John Magufuli kuangalia namna ya kuwajengea soko la kisasa la kuuzia samaki ili kuweza kuondokana na adha ambayo wamekuwa wakikumbana nayo hivi sasa.

Akizungumza jana mmoja wa wavuvi hao, Shamba Baakari alisema kutokana na kutokuwepo kwa soko hilo linapelekea wavuvi kukosa uhakikisha wa mahali sahihi ya kufanyia shughuli zao ikiwemo kusaidia kulipa kodi.

“Ukosefu wa soko la uhakika la kufanyia shughuli zetu limekuwa kikwazo cha kushindwa kufikia malengo yao hivyo tunaamini kilio hiki cha uwepo wa soko la kisasa utafanyiwa kazi na mamlaka husika kwa lengo la kuongeza tija kwa wavuvi “Alisema.

Naye kwa upande wake,Mahamud Rubonzo ambaye ni mkazi wa wilayani alisema asilimia kubwa ya vijana wilayani  humo wanategemea ajira zao kutokana na shughuli za uvuvi hivyo kutokuwepo kwa soko kunazorotesha shughuli hiyo na kuongeza ugumu wa maisha kwa vijana wengi Wilayani humo.

Alisema iwapo soko hilo litakuwepo litasaidia wavuvi kushindwa kupata hasara ya kuharibikiwa na samaki hasa wale ambao wanakuwa hawajauzika kwa siku husika kwani wanaweza kupata sehemu pa kuhifadhiwa .

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »