JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
UPIGAJI MARUFUKU MATUMIZI YA POMBE ZINAZOFUNGASHWA
KATIKA
VIFUNGASHIO VYA
PLASTIKI (VIROBA)
Kufuatia kauli ya
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa aliyotoa tarehe
16/02/2017 huko Mererani, Mkoani Manyara
kuhusu kusitisha utengenezaji, uuzaji na matumizi ya pombe zinazofungashwa
kwenye vifungashio vya plastiki kuanzia tarehe 1 Machi 2017; na kufuatia Tamko la Serikali kuhusu dhamira hiyo
lililotolewa Bungeni tarehe 2 Mei, 2016 na kwenye matangazo yaliyotolewa kwenye
vyombo vya habari tarehe 01 Desemba, 2016, Ofisi ya Makamu wa Rais inachukua fursa hii kutangaza utaratibu wa utekelezaji
wa maamuzi hayo ya Serikali.
(i)
Waziri mwenye
dhamana ya Mazingira atatunga Kanuni zitakazodhibiti uzalishaji wa vifungashio
(viroba) vya pombe kali, kwa mujibu wa Kifungu 230 (2) (F) cha Sheria ya
Mazingira ya 2004. Kanuni hizi
zitaweka sharti la kutaka pombe kali inayozalishwa viwandani zifungashwe
kwenye chupa zinazoweza kurejelezwa (recycled) na kwa ujazo usiopungua
milligram 250.
Pia Kanuni hizo zitapiga marufuku uzalishaji, uuzaji,
uingizaji nchini na matumizi pombe zilizofungwa kwenye viroba na mitambo ya
malighafi ya vifungashio vya plastiki (viroba) vitakavyotumika kufungashia pombe
kali. Atakayebainika kukiuka masharti
ya Kanuni hizi atawajibishwa kulipa faini, kufungwa jela au vyote kwa pamoja
kama itakavyoainishwa kwenye Kanuni.
(ii) Dhamira ya Serikali sio kupiga marufuku vinywaji vya
pombe kali bali ni kutekeleza Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania 1977 ambayo inatoa haki ya kuishi katika mazingira yaliyo safi, salama
na yenye afya. Haki hiyo pia imetiliwa
mkazo katika sheria ya Mazingira ya 2004. Hivyo, dhamira ya Serikali ni kudhibiti upatikanaji kwa
urahisi wa pombe kali kunakotokana na kufungwa katika plastiki na kwa ujazo
mdogo, kunakopelekea kuongezeka kwa matumizi ya pombe kali hadi kwa watoto
wadogo; kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kuzagaa kwa vifungashio
hivyo; na kudhibiti ukwepaji mkubwa wa kodi kutokana na urahisi wa teknolojia
na gharama za kutengeneza pombe kali inayofungashwa kwenye viroba. Inakadiriwa
kwamba Serikali inapoteza shilingi bilioni 600 kwa mwaka kutokana na ukwepaji
kodi kwenye biashara ya pombe za viroba.
(iii)
Utekelezaji wa
maamuzi haya ya Serikali unaanza mara moja.
Ingawa haitegemewi, lakini iwapo kuna Wazalishaji watakaohitaji muda wa
ziada wa kuhamia kwenye teknolojia ya chupa, wataomba kibali maalum cha muda
mfupi ambacho hakitatolewa hadi muombaji awasilishe kabla ya tarehe
28/02/2017:- yafuatayo:-
i)
Ushahidi/Barua
kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamba amelipa kodi katika kipindi cha
miaka mitatu iliyopita.
ii)
Ushahidi/Barua/Cheti
kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)
kwamba mzalishaji amekuwa na kibali cha
usalama wa kinywaji kwa miaka yote ambayo amekuwa anazalisha;
iii) Cheti au Barua kutoka
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwamba mzalishaji anauza bidhaa inayokidhi viwango
iv) Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) au
Ukaguzi wa Mazingira (EA) kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC)/Ofisi ya Makamu wa Rais;
v)
Ushahidi kwamba
katika kipindi cha mpito mzalishaji atatumia teknolojia ya kudhibiti utengenezaji
wa vifungashio bandia (anti-counterfeit technology);
vi) Uthibitisho kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na
Leseni (BRELA) kuhusu usajili wa kampuni
na usajili wa chapa ya kinywaji (brand).
Zipo pombe za viroba zinazoingizwa nchini kutoka nje
ya nchi, hasa kwenye Mikoa na Miji ya mipakani.
Wakuu wa Wilaya , kupitia Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na
Kamati za Mazingira, wanaelekezwa kufanya operesheni ya kukamata na kuzuia
viroba vinavyoingizwa nchini kinyume cha utaratibu. Operesheni hii pia inahusu
udhibiti wa pombe haramu ya gongo.
Serikali imeunda Kikosi Kazi cha Kitaifa kwa ajili ya
kufanya ukaguzi na ufuatiliaji na hatua hizi.
Kikosi hicho kinajumuisha Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Baraza la Taifa la Hifadhi
na Usimamizi wa Mazingira, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Shirika
la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji
na Jeshi la Polisi. Doria za ukaguzi wa utekelezaji wa hatua hizi zitaanza wakati
wowote kuanzia sasa na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaokiuka. Ofisi ya Makamu wa Rais itaratibu Kikosi
hiki.
Kuhusu mifuko ya plastiki, Kanuni za Udhibiti zinaandaliwa
na zuio litatangazwa wakati wowote.
Tunapenda kuwaasa wazalishaji, waagizaji na wauzaji wa mifuko hiyo nao kujiandaa.
Hatua hizi za Serikali sio za ghafla au kushtukiza
kwani taarifa ilitolewa Bungeni takribani mwaka mmoja sasa. Aidha Serikali
ilitoa taarifa rasmi mwezi Agosti 2016 na Desemba 2016 kuhusu dhamira ya
kuchukua hatua hizi. Serikali ilitarajia
kwamba wazalishaji wa pombe za viroba na mifuko ya plastiki watakuwa
wamejiandaa kubadilisha teknolojia.
Ofisi ya Makamu wa Rais
20/02/2017
20/02/2017
EmoticonEmoticon