Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Rais Eng. Ngosi Mwihava (kushoto) akiwa na Bw. Ali Mufuruki Mwenyekiti wa Bodi,
wakati wa halfa ya uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya
Maizngira jiini Dar es Salaam.
Sehemu ya Wajumbe wa Bodi (mstari wa
mbele) wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano
na Mazingira Mhe. January Makamba katika hafla ya uzinduzi wa Bodi na Mfuko wa
Dhamana ya Mazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiwa katika picha ya pamoja
na wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya Mazingira, mara
baada ya kuizindua hii leo, Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam.
Na Lulu Mussa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Muungano na Mazingira Mh. January Makamba hii leo amezindua
Bodi ya Mfuko wa Taifa wa dhamana ya Hifadhi ya Mazingira
Nchini iliyo chini ya Mwenyekiti Ali Mufuruki.
Waziri Makamba amesema Uzinduzi wa Mfuko na
Bodi hiyo utasaidia upatikanani wa fedha za usimamizi wa Mazingira
Nchini. “Ni matarajio yangu tutafanya kazi pamoja kuhakikisha mfuko
unakuwa na fedha ya kutosha na unafanya kazi ili kukidhi malengo yaliyodhamiriwa
hususan uboreshaji wa mazingira nchini” Alisisitiza Waziri Makamba
Waziri Makamba amesema uteuzi wao una maana
kubwa na kuwataka wajumbe wa Bodi hiyo kufanya kazi kwa kujituma na
kuhakikisha kuwa Hifadhi ya Mazingira inakuwa ni ajenga ya kitaifa.
Waziri Makamba amewafahamisha wajumbe kuwa Sheria ya Mazingira ya
mwaka 2004 Kifungu cha 213 imeanzisha Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi
ya Mazingira ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo fedha za kutosha za kulinda
na kusimamia hifadhi ya mazingira nchini.
Aidha, tangu kuanzishwa kwa Mfuko huu kisheria, kumekuwepo
na maandalizi mbalimbali ya kuhakikisha kwamba mfuko unaanza kufanya
kazi mapema iwezekanavyo. Baadhi ya maandalizi hayo ni: Kufanya utafiti
kuhusu vyanzo vya fedha kwa ajili ya Mfuko; kuandaa mwongozo wa kusimamia
fedha za Mfuko; kuandaa kanuni za uendeshaji Mfuko; na kuwasilisha Wizara
ya Fedha na Mipango mapendekezo ya vyanzo vya mfuko ili kupata utaratibu
muafaka kwa kupata fedha hizo kwa ajili ya Mfuko.
Waziri Makamba amefanunua kuwa Malengo ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya
Mazingira kama yalivyobainishwa kwenye Sheria ya Mazingira ni pamoja
na: Kusaidia utafiti unaolenga kuboresha hifadhi ya mazingira; Kujenga uwezo wa taasisi mbalimbali zikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais, NEMC na nyinginezo katika
hifadhi ya mazingira; Kutoa tuzo zinazolenga uhamasishaji wa hifadhi ya
mazingira; Kutoa majarida yanayohusu hifadhi ya mazingira.
Malengo mengine ni pamoja na kutoa ufadhili kwa ajili ya mafunzo yanayohusu shughuli za
mazingira; Kusaidia jamii kwa kutoa misaada kwa ajili ya kutekeleza
prgramu za hifadhi ya mazingira; na Kulipia gharama za mikutano
ya Kamati ya Mazingira ya Ushauri ya Taifa (National Environmental Advisory
Committee - NEAC) na Bodi ya Wadhamini wa Mfuko, Waziri Makamba alisisitiza.
Waziri Makamba amesema kuwa juhudi za Serikali katika
hifadhi ya mazingira zitakuwa endelevu na kuhakikisha kuwa Bodi itakuwa
mstari wa mbele katika kuhakikisha hifadhi ya mazingira inasimamiwa
na kuendeshwa kwa mujibu wa Sheria kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa
wa Dhamana ya Hifadhi ya Mazingira Bw. Ali Mufuruki amemuhakikishia
Mhe. Waziri Makamba kuwa yeye na wajumbe wa bodi yake wako tayari kufanya
kazi hiyo kwa heshima kubwa na kuhakikisha kuwa hifadhi na usimamizi
wa mazingira unakua endelevu.
Bodi hiyo inaongozwa na Bw Ali Mufuruki ambaye Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Kampuni
ya Infotech, Mwajuma Mbogoyo, Imelda Teikwa, Profesa Razak Bakari Lokina
na Hatibu Senkoro. Wengine ni Alesia Mbuya, Baraka Juma Kalangahe, Dkt.
Andrew Komba na Profesa Yunus Mgaya.
EmoticonEmoticon