Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema adha ya
mafuriko yanayotokea kila mwaka wakati wa msimu wa Mvua za Masika na
kuwakumba Wananchi yataondoka au kupungua zaidi baada ya kukamilika kwa
miradi tofauti iliyonzishwa na Serikali chini ya Mradi wa huduma za
Jamii Mijini.
Alisema
mafanikio ya mradi huo tayari yameanza kuonekana katika ujenzi wa
michirizi ya maji ya mvua kwenye maeneo ya Daraja Bovu, Mnazi Mmoja,
Kijangwani na baadhi ya maeneo ya Jang’ombe na Wananchi wake tayari
wanafaidika na matunda ya mradi huo.
Balozi
Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la
Msingi la Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani Forodhani
Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa harakati za shamra shamra za
kusherehekea miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi imejipanga kuimarisha miradi hiyo ikiwa sehemu
ya Jududi za utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015
ikilenga kuwaondoshea usumbufu unaowakumbwa wananchi walio wengi hasa
wale wa maeneo ya Ng’ambo ya Mji.
Balozi
Seif alisema ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani
Forodhani Mjini Zanzibar ukiwa miongoni mwa miradi ya Jamii Mijini ni
muhimu kwa maendeleo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliobahatika kuwemo
kwenye Miji ya urithi wa Dunia ambao unategemewa kwa uchumi wa Taifa
kwa upande wa Sekta ya Utalii.
Mapema
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar Nd. Khamis Mussa Omar alisema chimbuko la mradi wa ujenzi wa
ukuta wa Mizingani umetokana na athari kubwa iliyojitokeza siku za nyuma
ya kasi kubwa ya maji ya Bahari iliyoathiri eneo hilo.
Alisema
Ujenzi wa Ukuta huo ulioanza Tarehe 22 April 2015 ukiwa na urefu wa
Mita 320, upana Mita sita na ongezeko na mita sita kuelekea usawa wa
Bahari unatarajiwa kukamilika rasmi ndani ya Mwaka huu wa 2017.
Alieleza
kwamba asilimia 65% ya ujenzi huo imekamilika kwa upande wa ukuta
wenyewe na kazi iliyobaki na kuendelezwa kwa hivi sasa ni ujenzi wa
bustani pamoja na bara bara ya watembeao kwa miguu.
Akimkaribisha
Balozi Seif kuzindua ujenzi huo wa Ukuta, Waziri wa Fedha na Mipango
Dr. Khalid Salum Mohamed alisema uimarishaji wa Mji Mkongwe kupitia
mradi wa Jamii Mijini utakuwa chachu ya kuimarika kwa Sekta ya Utalii
Nchini.
Dr.
Khalid aliwaomba Wamiliki Binafsi wa majengo yaliyomo ndani ya Mji
Mkongwe kushirikiana na Serikali Kuu katika kuyaweka kwenye mazingira
bora yatakayotoa haiba nzuri ya Mji wa Zanzibar unaotegemewa katika
makusanyo ya Mapato ya Taifa kupitia sekta hiyo ya Utalii.
Ujenzi
wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar
unasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kupitia Mkono wenye masharti nafuu wa shilingi Bilioni
7,222,577,890 kutoka Benki ya Dunia.
Kampuni
ya Seyani Brothers ya Mjini Dar es salaam ndio iliyopewa jukumu la
kujenga Ukuta huo chini ya Msimamizi Mshauri muelekezi Kampuni ya
Aurecon kutoka Nchini Afrika Kusini.
Makamu
wa Pili a Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiweka jiwe la Msingi la Ujenzi
wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini
Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za kusherehekea miaka 53 ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Wa
kwanza kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ Dr. Khalid Salum
Mohamed ambapo wa nyuma yake ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar
Mh. Zubeir Ali Maulid. Picha na OMPR – ZNZ.
EmoticonEmoticon