Na Mwandishi wetu – Maelezo
……………………………..
Serikali
imeshauriwa kuiomba China kutekeleza ahadi yake ya kufunga masoko yote
ya meno ya Tembo ili kuweza kulinda usalama wa muda mrefu wa wanyama
hao kwani nchi hiyo ni mtumiaji mkubwa wa meno hayo na kwa kufunga
biashara hiyo kutapelekea kuanguka kwa haraka kwa biashara katika
sehemu nyingine ulimwenguni.
Ombi hilo
limetolewa leo na Taasisi inayopinga uwindaji haramu wa tembo wakati
wakisoma barua yao ya wazi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. John Pombe Magufuli mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa
mikutano wa Idara ya Habari uliopo jijini Dar es Salaam.
Akisoma barua
hiyo Shubert Mwarabu ambaye ni mratibu wa kampeni ya okoa Tembo wa
Tanzania alianza kumpongeza Mhe. Rais kwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu
ya tano na kuisihi Serikali kutumia urafiki wa kihistoria kati yake
na China kufunga masoko ya meno ya Tembo yaliyopo nchini China.
Alisema
takribani asilimia 90 ya meno ya Tembo toka Tanzania yanauzwa China,
ambapo biashara halali ya meno ya Tembo inatumika kama mwavuli wa
biashara haramu ya meno ya Tembo ambacho ndio chanzo kikuu cha tatizo la
ujangili wa Tembo.
“Tunakuandikia
barua leo kukuomba kuchukua hatua juu ya suala la kupungua kwa kasi
idadi ya Tembo nchini kutokana na ujangili kwa ajili ya biashara haramu
ya meno ya Tembo”.
“Kutokana na
Ripoti ya Sensa ya TAWIRI 2014 Miaka hamsini iliyopita, kulikuwa na
Tembo 300,000 nchini Tanzania. Mwaka 2009, kulikuwa na Tembo 109,000.
Leo, inakadiriwa kuna Tembo 43,000 tu waliobaki – upungufu wa asilimia
60 ndani ya miaka mitano tu”, alisema Mwarabu.
Aliendelea
kusema wanatambua hatua zilizofanyika kukabiliana na tatizo la ujangili.
Uundaji wa mikakati ya kitaifa dhidi ya ujangili, juhudi za Kikosi Kazi
cha National and Transnational Serious Crimes Investigation Unit
(NTSCIU) na kuongeza rasilimali kwa mamlaka ya wanyamapori ni hatua
muhimu.
Alisisitiza,
“Nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika uhifadhi wa Tembo hapo kabla.
Mwaka 1989, Tanzania iliongoza jitihada za kupiga marufuku biashara ya
meno ya Tembo ulimwenguni tulipochukua hatua kukomesha mauaji ya Tembo,
dunia nzima ilituunga mkono. Ni lazima turejeshe upya dhamira yetu kwa
ahadi tuliyojiwekea kwa hatua ya kimataifa zaidi ya miaka ishirini
iliyopita, na kuleta ukomo wa biashara yote ya meno ya Tembo”.
“Tunaiomba
serikali kuwakamata na kuwashitaki wafanyabiashara wakubwa wa meno ya
Tembo nchini, bila kujali utaifa, hadhi au mamlaka, kuteketeza hadharani
ghala ya meno ya Tembo Tanzania – inayosadikika kuwa kubwa kuliko yote
ulimwenguni kwani ni gharama kutunza na kulinda ghala la meno ya Tembo Tanzania”.
EmoticonEmoticon