Kocha Mkuu wa City Meja Mstaafu Abdul Mingange, leo jioni aliungana
na kikosi chake kupata darasa maalumu kutoka kwa wataalamu wa shirika
la bima ya taifa ya afya waliotembelea kambi ya timu yake maalumu kabisa
kwa shughuli hiyo.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa darasa hilo
maalumu lililofanyika kwenye kambi ya City iliyopo katikati ya jiji la
Mbeya, Kocha Mingange alisema kuwa limekuwa ni jambo nzuri kwa madaktari
na wataalamu kutoka NHIF kufika kambini hapo kwa ajili ya kutoa elimu
kwa wachezaji na viongozi kuhusu umuhimu wa bima ya afya hasa
ukizingatia uwepo wa matukio mengi ya bahati mbaya kwenye soka.
“Dunia nzima inafahamu kuwa soka sasa ni kazi,tofauti na zamani
ambapo mchezo huu ulichukuliwa kama burudani, kwa hiyo ndani ya kazi
yapo matukio ambayo hutokea ya kigusa afya, hayo yanahitaji matibabu,
sasa somo la leo limekuwa muhimu kwetu kwa sababu tumejuwa umuhimu wa
bima ya afya, njinsi gani inaweza kutusaidia tukipata matatizo kwenye
kazi yetu,binafsi nimefurahi na nimejaza fomu hii ya NHIF” alisema.
Akiendelea zaidi kocha Mingange ambaye msimu uliopita aliifundisha
timu ya Ndanda Fc ya Mtwara aliweka wazi kuwa mpango huu wa shirika la
bima ya taifa ya afya litawasaidia wachezaji wengi kupata matibabu ya
uhakika pale wanapokuwa wamepata matatizo makubwa ambayo pengine
yangaweza kuwaweka kando na soka mapema kwa kushindwa kumudu gharama.
“Nchi yetu inao wachezaji wengi ambao wamelazimika kustaafu soka
kutokana majeraha makubwa waliyoyapata viwanjani,licha ya jitihada zao
kubwa lakini ikashindika kurudi kucheza kutokana na gharama kubwa za
matibabu,sasa hii NHIF imekuja kuondoa hilo,naomba vijana waiunge mkono
kwa kujaza fomu zao kwa sababu sasa uhakika wa matibabu upo iwe ndani au
nje ya nchi hawa jamaa watafanya kazi kwa ajili yao” alimaliza.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni shirika la bima ya taifa ya afya nchini
limeingia mkataba na shirikisho la soka Tanzania TFF kwa lengo la
kutoa huduma za matibabu na bima kwa afya za wachezaji wa vilabu vyote
vinavyoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.
EmoticonEmoticon