MABINGWA
watetezi wa kombe la Mapinduzi, klabu ya Azam FC imetamba kwenda
kutetea taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo katika michuano inayoanza
kutimua vumbi januari mosi mwakani.
Jafari
Idd Maganga, Afisa habari wa klabu hiyo amesema panapo majaaliwa timu
hiyo inatarajia kung`oa nanga jijini Dar e salaam januari 1 mwaka huu
kuelekea visiwani Zanzibar tayari kuanza harakati za kutafuta kombe
hilo.
“Michuano
hii ni muhimu sana kwetu. Kocha mkuu Mcameroon, Joseph Marius Omog
atakuwa na nafasi nyingine ya kupima kikosi chake na kuelewa wapi kuna
matatizo ili kuiandaa timu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu
soka Tanzania bara na michuano ya kimataifa”. Alisema Jafar.
Jafar aliongeza kuwa tangu timu ipate kocha mpya, wachezaji wamekuwa wakipambana kutafuta nafasi katika kikosi cha kwanza.
“Mapinduzi
Cup itawajenga wachezaji wetu. Kila mchezaji anataka kuonekana mbele ya
kocha, ushindani umeongezeka zaidi, bila shaka baada ya kumalizika kwa
michuano hii muhimu, Kocha Omog atakuwa amepata kikosi chake”.
“Kikosi
kipo safi, wachezaji wanaonesha juhudi kubwa. Cha msingi wote wanaelewa
nini cha kufanya, dira ya Azam fc ipo wazi kabisa kuwa inataka kupata
mafanikio makubwa zaidi anga za kitaifa na kimataifa”. Alisema Jafar.
Mashaindano
ya mapinduzi yatakuwa ya kwanza kwa kocha Omog, achilia mbali ile
mechi ya kirafiki iliyocheza Alhamisi ya kujaribu mfumo wa Tiketi za
electroniki ndani ya uwanja wa Chamazi dhidi ya Ruvu shooting.
Katika
mchezo huo, Omog aliiongoza Azam FC kupata ushindi wake wa kwanza wa
mabao 3-0 , ambapo mshambuliaji mpya kutoka Ivory Coast, Mouhamed Kone
alifunga bao mojawapo, huku mengine yakifungwa na Jonh Raphael Bocco
`Adebayor` na Kipre Herman Tchetche kwa mkwaju wa penati.
Kombe
la Mapinduzi mwaka huu litajumuisha timu 12 kutoka ndani na nje ya nchi
ambazo zimegawanywa katika makundi matatu yenye timu nne.
Kundi
A: kuna timu za Pemba Combine, Chuoni, URA kutoka Uganda na Mbeya City,
huku kundi B likiwa na klabu za Simba, KMKM, AFC Leopard ya Kenya
pamoja na KCC kutoka Uganda.
Wana
Lambalamba, Azam fc ambao ndio mabingwa watetezi wapo kundi C na timu za
Tusker fc ambao ni makamu bingwa, Dar Young Africans na Unguja Combine.
Pazia
la michuano hiyo litafunguliwa rasmi januari mosi ambao mechi ya kwanza
itakuwa saa 10:00 jioni baina ya KMKM dhidi ya KCC, kwenye uwanja wa
Amaan, mjini Unguja.
Mechi
ya ufunguzi itapigwa saa 2:00 usiku ambapo wekundu wa Msimbazi, Simba
Sc watakuwa na kibarua kizito dhidi ya AFC Leopard kutoka nchini Kenya
na mgeni rasmi atakuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Italia, Cesare
Prandelli.
Shughuli
itaendelea januari 2 ambapo katika uwanja wa Amaan, Azam fc watashuka
dimbani saa 10:00 jioni kukipiga na Unguja Combine, na usiku saa 2:00,
Dar Young Africans watakuwa kibaruani dhidi ya Tusker fc.
Katika
uwanja wa Gombani Pemba, URA watakabiliana na Chuoni (kundi C) majira
ya saa 8:00 mchana, huku Mbeya City ikishuka dimbani dhidi ya Pemba
Combine, saa 10:00 jioni katika mchezo wa kundi A.
Fainali
ya michuano hii itapigwa siku ya sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya
Zanzibar, januari 12 na mechi ya fainali itapigwa saa 2:00 usiku katika
uwanja wa Amaan mjini Unguja.

EmoticonEmoticon