RC BATILDA AWAONYA WATAKAONG’OA ORODHA YA WAPIGA KURA

September 17, 2024


Na Oscar Assenga, TANGA.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi,Dkt Batilda Burian amesema kwamba mkoa huo umejiandaa kikamilifu kuelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa huku akiwaonya watu wenye tabia ya kung’oa orodha ya wapiga kura wasisubutu kufanya hivyo.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu ambapo alisema watakaojaribu kufanya hivyo hawatasalimika badala yake watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo faini ya Laki tatu,kifungo cha miezi 12 au vyote vya pamoja

Balozi Batilda aliyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuelezea maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Mkoa huo ambapo alisema hawataki kuona vitendo hivyo vinatokea kwenye mkoa huo.

Alisema kwa sababu orodha hiyo imewekwa maalumu kwa ajili ya kuwawezesha wapiga kura wa eneo Fulani kuweza kuhakiki majina yao ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi huo hivyo wanapotokea watu wanang’oa ni uvunjifu wa sheria.

“Lakini pia kutoa taarifa za uongo ili uweze kugombea nafasi ya za uongozi pamoja na wale ambao watajiandikisha zaidi ya mara moja anatoka sehemu moja hadi nyengine hao nao wakibainika watachukuliwa hatua kali”Alisema

Aidha alisema kwamba pia wale ambao watabainika wamepiga kura zaidi ya mara moja au kutishia wapiga kura ni kosa na watachukuliwa hatua za kisheria sambamba na wale ambao watafanya kampeni wakati wa uchaguzi.

“Lakini kwa wale ambao wataonyesha ishara au kuvaa mavazi yanayomuashiria mgombea hayo mabango yakionekana wakati wa uchaguzi ni kosa na watakaobainika watashughulikiwa”Alisema

Onyo hilo pia alilitoa kwa wale wenye tabia ya kuwazuia wasimamizi wa Uchaguzi kutekeleza majukumu yao wakati wa zoezi la watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kuhusu ukomo wa Viongozi wa Serikali za Mitaa.

Alisema kwamba viongozi hao ukomo wao utakuwa ni Octoba 25 mwaka huu kwa viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji na siku saba za ukaguzi na kuanzia Octoba 1 mpaka 7 utakuwa ni muda wa kuchukua fomu na kurudisha na Octoba 8 na 9 utakuwa uwasilishaji pingamizi kuhusu uteuzi na kuanzia Octoba 20-26 itakuwa ni kipindi cha kampeni.

“Kwa mkoa wa Tanga tunatarajia kuwaandikisha wapiga kura wasiopungua chini ya asilimia 80 na kuendelea kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.

Hata hivyo alisema nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo hutegemea aina ya Halmashauri inayofanya uchaguzi kama ni Mamlaka ya Wilaya au Mji kwa upande wa mkoa wa Tanga wana maeneo ya utawala yanayohusika kwenye uchaguzi ni mamlaka ya mji mdogo ni tatu,Kata 245,mitaa 270,vijiji 763 na Vitongoji 4,531.



Share this

Related Posts

Previous
Next Post »