BLOG

SOMA TARUJA LEO

SOMA TARUJA LEO

TAWODE

TAWODE

Saturday, November 30, 2013

NEWS ALERTL IGP MWEMA AFANYA MABADILIKO KADHAA KATIKA JESHI LA POLISI


 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema   amefanya mabadiliko ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera pamoja na baadhi ya Wakuu wa Upelelezi wa mikoa na  wakuu wa Polisi wa Wilaya katika baadhi ya mikoa hapa Nchini. 

 Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Philipo Kalangi  amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam, kuwa Mkuu  wa kikosi cha kusimamia usalama wa Mazingira na nafasi yake  inachukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi  (SACP) George Mayunga ambaye alikuwa Mkuu wa kikosi cha  kusimamia mazingira Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam.

KOCHA WA CAMEROON ASAINI MIAKA MWILI AZAM

Kocha mpya wa Azam FC. Joseph Marius Omog (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kusaini mkataba wa kuifundisha timu hiyo.


KLABU ya Azam inapenda kuufahamisha umma hususan wapenzi wa mpira wa miguu kuwa imeingia mkataba na kocha Joseph Marius Omog raia wa Cameroon kwa kipindi cha miaka miwili (2) kuanzia leo.

Kocha Omog ni bingwa kwani anakuja kuifundisha Azam akiwa ametoka kuiongoza klabu ya A.C Leopards ya Jamhuri ya Kongo (Brazaville) kutwaa ubingwa wa ligi ya nchi hiyo kwa misimu miwili mfululizo (2012 na 2013).

Timu hii ilikuwa haijatwaa ubingwa wa ligi kwa zaidi ya miaka 30. Kwa mwaka huu wametwaa ubingwa wakiwaacha wapinzani wao, Diables Noirs kwa pengo la pointi kumi (10) wakikusanya pointi 87 katika ligi yenye timu 18.

Pia ni mwaka jana tu (2012) aliiwezesha A.C Leopards kunyakua ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwa kuzipiga kumbo timu ngumu na zenye uzoefu mkubwa kama vile Mas de Fes ya Morocco, Heartlands ya Nigeria na Sfaxien ya Tunisia.

Mafanikio hayo ya kutwaa ubingwa wa Afrika yalifikiwa baada ya miaka 38 tangu klabu ya Jamhuri yas Kongo ifanye hivyo, na kumfanya kocha Omog kuwa moja ya makocha wa kupigiwa mfano barani Afrika.

Kigoda: Kamanda wa Vijana Mkoa wa Tanga (UVCCM)WAZIRI wa Biashara na Viwanda nchini, Dr.Abdalla Kigoda ameteuliwa kuwa kamanda wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Tanga (UVCCM) katika uteuzi ambao ulifanywa na kamati ya utekelezaji Taifa chini ya Mwenyekiti wao Sadifa Juma.

Akizungumza na Tanga Raha, katika ofisi za Umoja huo mkoani hapa, Mwenyekiti wa Umoja huo, Abdi Makange alisema mchakato huo ulianzia ngazi ya mkoa ambapo wao waliamua kumpendekeza Kigoda na hatimaye kupata baraka kutoka kamati ya utekelezaji na kumuidhinisha kwa kumpitisha.

LAAC WAIAGIZA HALMASHAURI HANDENI KUPELEKA ZAIDI YA MILI 105 KWA VIJIJI RUZUKU YA SERIKALI.

MWENYEKITI wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajabu Mbaruku imeiagiza Halmashauri ya wilaya ya Handeni kuhakikisha kwamba inapeleka kiasi cha sh.milioni 105,779,260 kwa vijiji vilivyostahili kuzipata ikiwa ni michango ya lazima ya asilimia 20 ya ruzuku ya serikakali kuu kwa ajili ya maendelo vijijini,

Kauli ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo ilitokana na halmashauri hiyo kushindwa kuzipeleka vijijini fedha za ruzuku ya serikali kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo hali ambayo inapelekea kuchangia kudhorotesha kasi yao katika shughuli mbalimbali.
Licha ya kutoa agizo hilo pia aliiagiza halmashauri hiyo kuandaa mchanganuo wa madeni inayodai na kudaiwa kwa kuonyesha majina ya wadai na wadaiwa ikiwemo kuchukua hatua za makusudi za kupatikana kwa fedha zinazodaiwa.

Rais Kikwete atimiza ahadi yake ya kujenga daraja la Mwanhuzi wilayani MeatuRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiongozwa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kukagua daraja la Mwanhuzi lililoko Meatu Mkoani Simiyu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiongozwa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kukagua daraja la Mwanhuzi lililoko Meatu Mkoani Simiyu.

MAKAMU WA RAIS DKT.BILAL AENDESHA ZOEZI LA HARAMBEE YA KUCHANGIA MADAWATI MFUKO WA MAENDELEO YA ELIMU JIMBO LA KENGE


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi chaeti, Mkurugeniz wa Kagera Sugar, Hamadi Yahaya, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake wa kuchangia maendeleo ya Elimu ya Jimbo la Nkenge mkoa wa Kagera,wakati wa hafla ya harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Nkenge kununua madawati ili kusadia shule za msingi za Jimbo hilo. Harambee hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam, jana usiku. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Asumta Mshana na (kushoto kwa Makamu) ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanal Fabian Masawe.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza wakati wa hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Elimu Jimbo la Nkenge kununua madawati ili kusadia shule za msingi za Jimbo hilo. Harambee hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam, jana usiku. Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nkenge, Asumta Mshana na (kushoto kwa Makamu) ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanal Fabian Masawe.

WAZEE WA NGWASUMA KUWAPAGAWISHA WAKAZI WA MOROGORO.


BENDI ya Mziki wa Dansi ya nchini FM Academia “Wazee wa Ngwasuma”inatarajiwa kufanya onyesho kali la Mlipuko wa Burudani mkoani Morogoro  Desemba 6 mwaka huu katika ukumbi wa Kingstone Night Club.

Onyesho hilo linatarajiwa kuanza majira ya saa tatu usiku ambalo litakuwa la aina yake kutokana na aina ya wanamuziki wa bendi hiyo iliyojizolewa umaarufu mkubwa hapa nchini.


FAINALI YA KOMBE LA UHAI CHAMAZI

Mechi ya Fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha timu za umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu itachezwa kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.


Friday, November 29, 2013

CHADEMA TANGA YAPONGEZA UAMUZI WA KUVULIWA UONGOZI KATIBU MSAIDIZI

Na Oscar Assenga, Tanga
SIKU Chache baada ya Kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa (Chadema) kuamua kumvua uongozi ndani ya chama hicho aliyekuwa katibu Msaidizi Zitto Kabwe chama hicho mkoani hapa kimeipongeza hatua hiyo kwa kusema italeta umakini mkubwa kwa viongozi waliobaki.Uamuzi huo ulitolewa kwa mujibu ibara ya 7.7.16 kifungu (V) ambayo inaeleza kuwa kamati hiyo ina mamlaka ya kumwachisha ujumbe wa kamati kuu mjumbe mteule ambaye ataenda kinyume cha katiba, kanuni na maadili au kushindwa kukidhi matakwa ya kuteuliwa kwake.

COASTAL UNION YATINGA FAINALI YA UHAI CUP KWA MARA YA PILI MFULULIZO


WAFUGAJI KILINDI WACHOSHWA NA MATUKIO YA KIKATILI YA MIFUGO YAO

Na Elizabeth Kilindi,Kilindi.

MVUTANO   unaoashiria mapigano na mauaji kwa mara nyingine tena unafukuta baina ya wakulima na wafugaji  Wilayani Kilindi Mkoani Tanga baada ya wafugaji kuchoshwa na  matukio ya  kikatili ya mifugo yao kuuawa  kwa kuwekewa  sumu kwenye malisho na  kufia porini.


Tukio hilo la kusikitisha lilitokea  juzi katika kitongoji cha Kipaluke, Kijiji cha Kigwama, Kata ya Msanja Tarafa ya Mswaki Wilayani Kilindi  ambako ng'ombe nane  walifia porini  kati ya 14 waliyodaiwa  kula majani yenye sumu.PANGANI YAZINDUA UTARATIBU WA UTOAJI VIBALI SHUGHULI ZA UFUGAJI MDOGO

Na Burhan Yakub,Pangani.
Wilaya ya Pangani imezindua rasmi cha kitabu cha utaratibu wa
utoaji wa vibali vya shughuli za ufugaji mdogo wa viumbebahari ambao utawawezesha wakazi wa mwambao wa pwani kufanya shughuli za uzalishaji mali bila kuathiri mazingira.

Kitabu hicho  kilichozinduliwa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtasiwa hivi karibuni kikiwa kimeandaliwa na mradi ujulikanao “Pwani Project”kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Pangani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho,Mkurugenzi wa mradi wa Pwani,Baraka Kalangahe alisema yaliyoandikwa ni hali halisi ya sasa ya ufugaji mdogo wa viumbebahari na matatizo yanayoikabili tasnia ya maendeleo ya ufugaji mdogo wa viumbe bahari katika Wilaya ya Pangani.

Mengine yaliyoandikwa ni taarifa muhimu za maeneo yanayofaa kwa ufugaji mdogo wa viumbebahari katika Wilaya ya Pangani, maeneo yanayofaa kwa vijiji vya Buyuni, Mkwaja, Mikocheni, Sange,Kipumbwi, Mikinguni,Stahabu,Ushongo Bweni , Mkwajuni,  Pangani Magharibi, Mwembeni,Msaraza na   Kigurusimba.

Mkurugenzi huo pia alisema Kitabu hicho kinatoa mwongozo wa utoaji wa vibali, ufuatiliaji na udhibiti.

Akizungumza baada ya kuzindua kitabu hicho,Mkuu wa Wilaya alisema mradi huu utasaidia kuongeza thamani ya bahari nakuonya kuwa mtendaji atakayesababisha kuzorota katika eneo lake atamuwajibisha.

WAZIRI KIGODA MGENI RASMI TAMASHA LA HANDENI KWETU

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda Biashara na Masoko ambaye pia ndio mbunge wa Handeni, Dkt Abdallah Kigoda, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Utamaduni, lililopangwa kufanyika Katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni mkoani Tanga, Desemba 14 mwaka huu.

Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya kwanza wilayani hapa, huku likitarajiwa kuwa la aina yake kutokana na maandalizi yanayoendelea kushika kasi, ambapo kwenye uwanja huo, Tamasha hilo litaanza saa 2 asubuhi hadi saa 12 za jioni.

Akizungumza jana mjini Handeni, Mratibu wa Tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema maandalizi yamezidi kushika kasi kwa kuangalia mazoezi ya vikundi kadhaa vitakavyotoa burudani katika tukio hilo.

“Tunashukuru Mungu kuona mambo yanazidi kuwa mazuri kwa kuhakikisha kuwa Desemba 14 mwaka huu tunafanya tamasha lenye mguso na kila mmoja wetu kufaidishwa.

“Huu ni wakati wa kila mtu kujipanga ili aje kushiriki kwa namna moja ama nyingine, ukizingatia kuwa juhudi hizi zote zipo kwa ajili ya kujenga ushirikiano kwa watu wote,” alisema Mbwana.

Wadhamini katika tamasha hilo ni pamoja na gazeti la Mwananchi, Clouds Media Group, ni Phed Trans, Clouds Media Group, Grace Products, Screen Masters na mtandao wao wa Saluti5.com, Dullah Tiles & Construction Ltd, Katomu Solar Specialist, PLAN B SOLUTIONS (T) LTD, Country Business Directory (CBD) na Michuzi Media Group duka la mavazi la Chichi Local Ware, Smart Mind & Arters chini ya Anesa Company Ltd, ikidhamini kwa kupitia kitabu chao cha ‘Ni Wakati Wako wa Kung’aa’, Lukaza Blog, Kajunason Blog, Jiachie Blog, Pamoja Pure Blog na Taifa Letu.com.

WACHEZAJI KIZIMBANI UNITED WATOA YA MOYONI.

Na Masanja Mabula -Pemba .

Hatimaye wachezaji na mashabiki wa Klabu ya Kizimbani United wametoa ya moyoni na kusema kuwa sababu zilizopelekea timu hiyo kufanya vibaya kwenye michuano ya ligi kuu Zanzibar ni kuwepo na upendeleo wakati wa upangaji wa timu .

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi , wamesema kuwa tatizo la upangaji wa timu limekuwa ni kikwazo cha kuweza kufanya vizuri ambapo baadhi ya wachezaji wamekuwa wakipangwa kutokana na kuwa na uhusiano wa Kocha pamoja na viongozi wa timu .

Wamesema kuwa licha ya baadhi yao kuwa na viwango  lakini wamekuwa wakikalia benchi , kwa sababu ya kutokuwa na usuhuba na viongozi pamoja na kocha jambo ambalo limeiweka pabaya timu hiyo .

"Unajua kama huna usuhuba na viongozi pamoja na Kocha ,basi utakalia benchi mpaka uchoke , hata kama unakiwango kama Messi na  hii ndiyo iliyopelekea timu kufanya vibaya kwenye michuano ya ligi kuu ya Zanzibar " alieleza mmoja wa wachezaji jina tunalo .

Aidha nao mashabiki wa timu hiyo wamesema kuwa kitendo cha kuchezesha wachezaji wasio na uwezo kunaweza kuleta athari kwa klabu ikiwa ni pamoja na kushuka daraja .

Meneja wa Klabu hiyo Juma Saleh amekanusha taarifa hizo na kusema kuwa mchezaji anaweza kujihakikishia namba kutokana na juhudi yake mazoezini na kwamba suala la upendeleo halipo ndani ya klabu hiyo .

"Kocha anaangalia juhudi ya mtu mazoezini , na bidii ya mchezaji ndiyo inayomfanya mchezaji ajihakikishie namba kwenye kikosi , lakini suala la viongozi kuwa na wachezaji wao halipo ndani ya klabu yetu " alifahamisha meneja .

 Naye Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya klabu hiyo Juma Mzee amesema kuwa wachezaji wanaolalamika kutochezeshwa hawana elimu na hawajifahamu nini wanatakiwa wafanye , kwani lengo la viongozi ni kuona kuwa timuinafanya vyema na  inasonga mbele .

"Tatizo la wachezaji wetu hawana elimu pamoja na nidhamu ya mchezo , hili ndio chanzo cha baadhi yao kulalamika kwamba hawapewi nafasi ya kucheza , mimi najua wachezaji wote wamechezeshwa kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo  " alifahamisha .

Timu ya soka ya Kizimbani United kwa sasa inaendelea na mazoezi ikiwinda na michuano ya super 8 baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Zanzibar na kuambulia alama 8 katika mechi kumi na moja ilizocheza .

NGWASUMA:KUPAGAWISHA UKUMBI WA KINGSTONE MOROGORO DESEMBA 6Na Raisa Said,Tanga.
BENDI ya Mziki wa Dansi ya nchini FM Academia “Wazee wa Ngwasuma”inatarajiwa kufanya onyesho kali la Mlipuko wa Burudani mkoani Morogoro  Desemba 6 mwaka huu katika ukumbi wa Kingstone Night Club.

Onyesho hilo linatarajiwa kuanza majira ya saa tatu usiku ambalo litakuwa la aina yake kutokana na aina ya wanamuziki wa bendi hiyo iliyojizolewa umaarufu mkubwa hapa nchini.

Akizungumzia onyesho hilo,Meneja wa Ukumbi wa huo,Juma Abajalo alisema maandalizi yake yanaendelea vizuri ambapo wasanii wa bendi hiyo watawasili mkoa wa Morogoro siku moja lengo likiwa ni kuhakikisha wanakata kiu ya wapenzi wa mziki wa dansi mkoani humo.

Abajalo alisema onyesho hilo linatarajiwa kuwa la aina yake ambapo aliwataka wakazi wa mkoa wa Morogoro kujitokeza kushuhudia burundani ambazo zitapakana siku hiyo ambapo wasanii hao watapata nafasi ya kulitawala jukwaa mahiri litakalokuwa kwenye ukumbi huo maarufu mkoani hapa.

“Ninachoweza kusema maandalizi ya kuelekea onyesho hilo yamekamilika kwa asilimia kubwa hivyo tunawaomba wapenda burudani mkoani hapa kukaa mkao wa kula “Alisema Abajalo.

Abajalo alisema ukumbi huo wa Kingstone Night Club onyesho hilo linafanyika baada ya ukarabati mkubwa uliofanywa na wamiliki wake lengo likiwa ni kuwapa mambo mazuri wapenzi wa burudani mkoani humo.

Thursday, November 28, 2013

DUNIA MZOBORA KUZIKWA LEO MAKABURI YA KISUTU, DAR ES SALAAM

DUNIA MZOBORA
DAR ES SALAAM, Tanzania
MHARIRI Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora, ambaye amefariki dunia jana, anazikwa leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam

Habari zimesema Mzobora (49), ambaye alifariki dunia ghafla jana saa 12 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa amepelekwa kwa matibabu zaidi, akitokea Hospitali ya Aga Khan pia ya Dar es Salaam, anazikwa leo saa 7 mchana katika makaburi hayo

Mussa, mdogo wa marehemu, alisema jana kuwa Mzobora alianza kujisikia vibaya juzi usiku  nyumbani kwake,Tabata Mawenzi na kupelekwa Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa Muhimbili. Alifariki muda mfupi baadaye wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.

Mzobora, ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Naibu Msanifu Mkuu wa Uhuru, alifanya kazi hadi kumalizika kwa gazeti la Uhuru toleo la jana, akikaimu nafasi ya msanifu mkuu, akiwa buheri wa afya.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa ndugu wa familia, zilisema maziko ya marehemu yatafanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mzobora, ambaye alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Uhuru Publications Limited mwaka 1989, akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu, mkoani Kigoma.
Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.

Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa msanifu kurasa wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo kwa wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa mwandishi wa habari daraja la pili mwaka 1994.

Mwaka 1995, alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine), Mwanza na kuhitimu stashahada ya juu ya uandishi wa habari mwaka 1998.

Baada ya kurejea kazini, alipandishwa vyeo ngazi mbalimbali kuanzia mwandishi mwandamizi daraja la pili na hadi kufariki dunia kwake, alikuwa Mhariri Daraja la Pili.

Miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni pamoja na Kaimu Msanifu Mkuu wa Uhuru, Kaimu Mhariri wa Mzalendo na Kaimu Mhariri wa Makala.

Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006, Mzobora alijiunga tena na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwanza kwa masomo ya shahada ya uzamili katika mawasiliano ya umma na uandishi wa habari. Marehemu ameacha mke na watoto.

Wakati huo huo; Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za pole Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, kufuatia kifo hicho.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa Waandishi wa habari shupavu na mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa akilitumikia Gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU,” alisema Rais Kikwete.

Alisema alimfahamu Mzobora, enzi za uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma katika kazi zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha Umma kwa kutumia vyema kalamu yake.

Katika salam hizo, Rais Kikwete ametoa pole pia kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru na Waandishi wote wa habari nchini, kwa kumpoteza mwenzao waliyekuwa wakifanya naye kazi kila siku.

“Aidha, kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza baba, kiongozi na mhimili wa familia,” alisema Rais Kikwete.

Amewahakikishia wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, na anamuomba  Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu, Amina.

Amewataka wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia baada ya kumpoteza mtu muhimu aliyekuwa kiungo cha familia yao, kwani yote ni mapenzi yake Mola.

Wednesday, November 27, 2013

NAIBU WAZIRI UMMY MWALIMU APOKEA SHLLLINGI MILIONI 100 KWA NIABA YA TAYOA KUTOKA NBC KUSAIDIA VIJANA!!


 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu (kushoto) akipokea mfano wa hundi ya shs milioni 100 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Bi. Mizinga Melu kusaidia mradi wa mafunzo ya masuala ya ajira na ujasiriamali kwa vijana wa Shirika la kuelimisha vijana nchini (TAYOA). Hafla ilifanyika wakati wa tukio la uzinduzi wa mradi huo unaodhaminiwa na NBC jijini Dar es Salaam jana. Katikani ni Mkurugenzi Mkuu wa TAYOA, Peter Masika.
 Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Bi. Mizinga Melu (katikati) na Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa NBC, Bi. Mwinda Kiula Mfugale wakionyesha vipeperushi kuashiria uzinduzi wa tofuti ya vijanatz.com ikiwa na habari kuhusu ajira (kazitz.com), fedha (fedhatz.com) na ujasiriamali (biasharatz.com). Hafla hiyo ilikwenda sambamba na uzinduzi wa mradi wa mafunzo ya masuala ya ajira na ujasiriamali kwa vijana  wa Shirika la kuelimisha vijana nchini (TAYOA) unaodhaminiwa na NBC.
3: Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Mizinga Melu akishikana mikono na Mkurugenzi Mkuu wa TAYOA, Peter Masika baada ya kukabidhi  mfano wa hundi ya shs milioni 100 zilitotolewa na benki hiyo kusaidia mradi wa mafunzo ya masuala ya ajira na ujasiriamali kwa vijana wa Shirika la kuelimisha vijana nchini (TAYOA). Hafla ilifanyika wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo unaodhaminiwa na NBC. Kushoto ni Naibu Waziri wa Maendeleo aya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu na kulia ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa NBC, Mwinda Kiula Mfugale.
 Mkurugenzi Mkuu wa TAYOA, Peter Masika (kushoto), Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu (kulia), na Meneja Mkuu wa Mawasiliano wa NBC, William Kallaghe wakibadilishana mawazo katika hafla hiyo.
 Mkurugenzi Mkuu wa TAYOA, Peter Masika (kushoto), Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu (kulia), na Meneja Mkuu wa Mawasiliano wa NBC, William Kallaghe wakibadilishana mawazo katika hafla hiyo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Mizinga Melu akizungumza na vijana na wageni wengine kuhusu huduma za kibenki na kuhusu mikakati ya benki kusaidia suala la ajira na ujasiriamali kwa vijana katika hafla hiyo.
Wasanii wakitoa burudani kusindikiza uzinduzi wa mradi wa mafunzo ya masuala ya ajira na ujasiriamali kwa vijana wa Shirika la kuelimisha vijana nchini (TAYOA) unaodhaminiwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) jijini Dar es Salaam

UHAMIAJI TANGA WAKABILIWA NA UPUNGUFU WA VIFAA VYA BAHARINI


Na  Raisa  Said,Tanga
IDARA ya  Uhamiaji  mkoani  Tanga  inakabiliwa na  changamoto  ya Ukosefu wa  vifaa vya baharini  boti  na  meli  kwa ajili ya doria za baharini dhidi ya wahamaaji haramu wanaongia nchini kwa njia za mwambao wa Pwani.
 
Hayo yamesemwa na Afisa Uhamiaji Mkoa wa Tanga  Sixtus Nyaki wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini  kwake   kuhusu hali ya wimbi la uhamiaji haramu katika Mkoa huu kwa sasa, ambapo alisema kwa sasa wanalazimika  kutumia  boti  la  jeshi la  polisi mkoani.
 
“ Tunatumia boti moja la polisi kwa ajili ya doria za mara kwa  mara  za  baharini ,kitu ambacho  wakati mwingine tunashindwa kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu kutoka na boti hiyo kutumika kwa doria nyingine na Jeshi la Polisi”alisema Nyaki.
 
Nyaki alisema ukubwa wa mipaka ya baharini hadi nchi kavu ni mikubwa hivyo kusababisha kushindwa kuithibiti kwa pamoja hali inayosababisha wahamiaji haramu wengi kuvuka na kuingia nchini  kwanjia za panya.
 
Afisa  huyo alisema ushiriki wa wananchi katika biashara ya kusafirisha wahamiaji haramu imekuwa ni chanzo cha tatizo hilo kuwa kubwa kwani wengi wao wanategemea kuishi kwa kusafirisha wahamiaji hao na kuchangia ongezeko la wahamiaji hao.
 
Hata hivyo  aliongelea  juu  ya  kiasi cha wahamiaji   haramu   waliokamatwa katika kipindi cha Octoba  hadi sasa   kuwa  ni kiasi cha wahamjia 68 wamekamatwa sehemu mbalimbali za mkoa  huu.
 
Aliwataja wahamijai hao waliokamatwa  kuwa  wengi ni kutoka katika nchi ya Ethiopia na wengine kutoka nchi  mbalimbali duniani hapa na wengine  wakiishi nchini kinyume cha sharia.
 
Wahamiajia hao na idadai yao ni Waethiopia 48,Wakenya 6,Waganda 5,Wajerumani 3,Wanaijeria 2,Mreno 1,Msomali 1,naraia wa Peru 1.

TANROADS TANGA YAPITISHA MAOMBI YA KUPANDISHWA HADHI BARABARA BUMBULI.


   (Meneja wa Tanroads mkoa wa Tanga,Mhandisi Alfred Ndumbaro|}
 
Raisa Said,Tanga.
 
Bodi ya Barabara Mkoani Tanga (TANROADS) imepitisha maombi ya kupandishwa hadhi barabara zenye urefu wa kilometa 130 zinazounganisha vijiji 9 katika Halmashauri mpya ya Bumbuli, mkoani Tanga.
 
Akiwakilisha ombi hilo kwa wajumbe wa Bodi ya barabara iliyokutana hapa mwishoni mwa juma lilipita, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Bumbuli, Beatrice Musomisi alisema amewasilisha maombi kwa ajili ya kupandishwa hadhi barabara za halmashauri ya Bumbuli ili ziweze kuhudumiwa na wakala wa barabara Tanzania (TANROADS).
 
Msomisi alisema kwamba barabara hizo ni muhimu kwani zinaunganisha makao makuu ya Bumbuli na halmashauri za wilaya ya Lushoto na Korogwe kupitia kwenye barabara za mkoa za Mombo/Lushoto/Soni/Bumbuli/Dindira na Kwamote pamoja na Mashewa na Bombo Mtoni.
 
Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Bumbuli alizitaja barabara zitakazounganishwa na vijiji 9 kuwa ni Soni/Mponde/Funta/Tamota/Kerenge ambazo zina urefu wa kilomita 60.
 
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni pamoja na Mbelei/Mgwashi/Milingano/Mashewa zenye urefu wa kilomita 70.
 
Hata hivyo, Msomisi alifafanua kuwa kupandishwa hadhi kwa barabara hizo kutasaidia usafirishaji wa mazao ya wakulima katika jitahada za kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kuinua maendeleo ya Halmashauri ya Bumbuli kwa ujumla.
 
Kwa mujibu wa Meneja wa Tanroads Mkoani hapa, Eng. Alfred Ndumbaro maombi hayo ya barabara yamefuata taratibu zote ndani ya Halmashauri ya wilaya na kwamba vikao husika vilikaa na kupitisha maombi hayo.
 
Meneja huyo wa barabara alizitaka halmashauri za wilaya kuzipa umuhimu wa matunzo barabara zote zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kuwa ni chanzo cha maendeleo.

MAKAMBA :MGOGORO WA KIWANDA CHA MPONDE SIO WA KISIASA.

RAISA SAIDI,BUMBULI.
Naibu  Waziri  wa  Mawasiliano  Sayansi na  Teknolojia  January  Makamba  amewataka  baadhi  ya watu  kuondokana  na dhana  ya  kusema  mgogoro  wa  kiwanda cha  chai  cha  Mponde   ni siasa   badala  yake amewataka  kuiacha  serikali  indelee na taratibu zake  za  kulitafutia  ufumbuzi  swala hilo.
Makamba  ambaye pia   ni  Mbunge  wa  jimbo  la  Bumbuli  alisema  yeye kama  mbunge  wa  eneo hilo  lazima  ashirikiane  na  wananchi  wake  na  si kikundi  cha  watu wachache  licha ya kutukanwa  kwa  kuwaunga mkono  wananchi  wake.

Naibu  waziri  huyo  alieleza  kusikitishwa  kwake  na  baadhi ya  watu  kusema  swala  hilo  ni  la  kisiasa na  kwamba  linamaslahi  binafsi  ambapo alisema  ni upambuvu   nakwamba  tangu  2010  wakati  wa  uchaguzi ulishapita  sasa  ni wakati  wa  kuleta  maendeleo  kwa  wananchi  waliomuamini  na  kumtuma  kuwa  muwakilishi wao  bungeni na   si vinginevyo.

“Siamini   kama  kuwaunga  mkono  wananchi  walionichagua yanatokana na tofauti za kisiasa kwani eneo hili linamilikiwa na Chama kimoja ambacho ni Chama cha Mapinduzi na wala sina  maslahi binafsi katika suala hilo” Alisema  Makamba  nakuongeza  kuwa  yeye  anawasimia  wakulima  wa zao la  chai  kupata  haki yao  ya  msingi .


Kiwanda cha Mponde  kimefungwa  takribani  miezi  mitano  sasa kufuatia wakulima kususa kupeleka majani mabichi ya chai kwa madai ya kutaka Uongozi wa Chama cha Wakulima wa Chai Usambara (UTEGA) uitishe Mkutano Mkuu na kuwasomea mapato na matumizi ya chama hicho ikiwa ni pamoja na mapato ya kiwanda ambacho kinamilikiwa na chama hicho.


Hivi  karibuni Makamba, alimwaga machozi hadharani katika kijiji cha Mponde Kweminyasa kutokana na taarifa za watu watano kujeruhiwa kwa risasi za moto kufuatia vurugu zilizotokea  kati ya wakulima wa zao la chai  na Jeshi la polisi.


Vurugu hiyo ilitokea kutokana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu Chiku Gallawa kuamuru kiwanda cha chai cha Mponde kilichokuwa kimefungwa kwa mwezi mmoja na nusu wakati  huo kifunguliwe kwa nguvu chini ya usimamizi wa Polisi jambo  ambalo  zilisababisha  vurugu  kubwa  mpaka  watu  kujeruhiwa  kwa  risasi za  moto.Makamba alisema kuwa kuna haja kubwa ya kuwepo maridhiano katika kufungua kiwanda hicho badala ya kutumia nguvu. “Unaweza kufungua kiwanda kwa bunduki lakini huwezi kukiendesha kwa bunduki,” alisema na kuwataka wakulima wa Chai wa Mponde kuwa na subira na uvumilivu kwa sababu haki yao haiwezi kupotea kwa sababu kiwanda hicho ni mali yao.

MAKAMU MWENYEKITI UTEGA AONJA JOTO YA JIWE,ATIMULIWA MKUTANONI.   (MBUNGE WA JIMBO LA BUMBULI JANUARI MAKAMBA|}
NA RAISA SAID,BUMBULI.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima wa Chai{UTEGA} katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli Richard Mbuguni alipata wakati mgumu baada ya wakulima wa zao la chai kumtaka aondoke  katika mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa juma kwa  kile  kilichoelezwa  kukosa  imani nae.

Uamuzi huo  wa wakulima  ulikuja baada  ya wao kuona hakuna  haja  ya  makamu mwenyekiti  huyo   kuendelea  kushiriki  kikao hicho  huku  wakidai  ni  mmoja  wa wasaliti  wa zao  hilo na ambao  wako upande  wa mwekezaji  ambaye  alikuwa  akiwanyanyasa  wakati wote licha  ya wao kuwaweka  madarakani  viongozi  hao.

Wakizungumza  kwa  nyakati  tofauti  wakulima  hao  wapatao  zaidi  ya 1000  ambao  walionekana  kuwa  na  jazba,  walisema  hawawezi kushirikiana  na  mtu  ambaye  anawanyonya    na  anayesabisha  uchumi  wa  Bumbuli   kushuka  kwa  kuendelea  kumkumbatia  muwekezaji  na  kuwasaliti wao ambao  ndio  wamiliki wa  kiwanda hicho.

Mmoja  wa  wakulima hao  alietambulika  kwa jina  la  Mustafa Soa,  mkazi  wa  kijiji  cha  Kweminyasa   alisema  wao kama  wakulima  hawezi  kujadili  mambo  yao  wakati   viongozi wa Chama  cha Utega  wakiendelea  kuwepo  katika  maeneo  ya mkutano   kwa kuwa  wao  tangu  zamani  hawako  pamoja nao.

Awali  ofisa  Tarafa  wa  Bumbuli  Ismail  Kimweri   katika  kuwatuliza  wakulima  hao  ili  wamuache  makamu  mwenyekiti  ashiriki  mkutano  huo alifikia  hatua  ya  kuwaimbia  wimbo  kwa lugha ya  kisambaa  wenye  maneno  “ Mkazio Kuhembezana wenye  maana  ya  unyumba  ni  mapatano  ambao  uligonga  mwamba.

Akizungumza  katika  mkutano huo wa kujadili uuzaji wa  majani  ya  chai  nje ya kiwanda cha Mponde, ambacho kwa sasa kimefungwa,  Mbunge  wa  Jimbo  la  Bumbuli  January  Makamba  aliwasihi  kuwa  wavumilivu  katika  kipindi  hiki cha mpito na kuwataka  waendelee kutunza zao la chai  na  wauze  majani  ya  chai  kwenye  viwanda  vingine vya  jirani ili waweze kujikimu  kimaisha.

Makamba  ambaye pia ni  Naibu  Waziri  wa  Mawasiliano  Sayansi  na  Teknolojia, alisema  amekwisha zungumza na menejimenti za viwanda hivyo ili viongeze uzalishaji na vifaa vya kusafirishia chai kutoka mashambani hadi kwenye viwanda.

Hata  hivyo  mbunge huyo  aliwataka   wakulima  hao  kuendelea kuwa  na subira  kwa kuwa  ufumbuzi  wa  kufunguliwa  kwa  kiwanda  hicho  unakaribia  kufikia  ukingoni  kwa kuwa  suala  hilo  liko  mikononi  mwa  ngazi  za  juu za  serikali.