Na Amina Omari,Tanga
Kiwanda cha kutengeneza mikate cha (TANGA MODERN  BAKERY )kimekua cha pili kufungiwa shirika la viwango Tanzania TBS katika kipindi kisichozidi wiki moja mkoani Tanga baada ya kubainika kuwa kinazalisha mikate bila  kufuata taratibu za viwango bora vya uzalishaji.
 
Akizungumza katika oparesheni hiyo, Afisa Uhusiano wa TBS Rhoida  Andusamile alisema wamezuia uzalishaji katika kiwanda hicho baada ya kubaini kuwa wamiliki wakiwanda hicho wamekua wakitengeneza mikate ambayo inatengenezwa bila kufuata taratibu za shirika la viwango nchini.
 
Alisema mikate ni bidhaa ambayo ipo katika viwango vya lazima vya ubora hivyo kiwanda hicho kwa muda mrefu kimekuwa  kinazalisha bidhaa bila kuwa na nembo ya ubora ya kutoka TBS.
 
“Niwajibu wetu kuhakikisha kila mzalishaji  nchini anazalisha bidhaa zenye ubora kwa lengo la kuwakinga walaji na madhara ya kiafya hivyo tumekuwa tukiendesha ukaguzi wa mara kwa mara katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini lengo ikiwa ni kumlinda mlaji”Andusamile.
 
Nae mkaguzi washirika hilo Deusdedit Paschal alisema bakery hiyo ilitakiwa kabla haijaanza uzalishaji wapeleke  sampuli za mikate TBS kwa ajili ya kuangalia ubora pamoja na ukaguzi kufanyika lakini yote hayo hayakufanyika.
 
Alisema kwa miaka 16 kiwango hicho kimekuwa kizalisha mikate hiyo pamoja na bidhaa nyingine kama keki bila ya ya kuwa na mikataba na TBS wala nembo ya ubora pamoja na ukaguzi.
 
Kwa upande wake  Meneja wa kiwanda hicho Hilal Salim alikiri kuendesha uzalishaji bila kuwa na nembo ya kuthibitisha ubora wa bidhaa yake ,hata hivyo alliomba TBS kutokifungia kiwanda hicho kwani wananchi wengi wataathirika na ukosefu wa bidhaa zake
 
Hata hivyo baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho walisema kufungiwa kwa kiwanda hicho kutawathiri kiuchumi kwani walikuwa wanatagemea ajira hiyo kuendesha   familia zao.
 
Mei 22 mwaka huu shirika la viwango nchini TBS lilifungia kiwanda cha kutengeneza maji cha Al Hayaa kutoka na kuendeleza uzalishaji wa bidhaa hiyo bila kuwa na  leseni ya ubora.