BLOG

SOMA TARUJA LEO

SOMA TARUJA LEO

TAWODE

TAWODE

Thursday, February 28, 2013

TRBA kuandaa NBL msimu huu

Na Oscar Assenga, Tanga. CHAMA cha Mpira wa Kikapu mkoa wa Tanga (TRBA) kimepokea wa mikono miwili kuteuliwa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Kikapu ya Taifa (NBL) ambayo yatafanyika mkoani Tanga Aprili Mosi mpaka Aprili 7 kwenye uwanja wa Mkwakwani. Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Chama hicho, Khamisi Jaffary alisema wanashukuru kutokana na mwaliko huo nakueleza baada ya kufanyika mashindano ya Taifa Cup mwaka jana wakazi wa Tanga watapata fuksa ya kushuhudia mashindano mengine ya NBL mkoani hapa. Jaffari alisema mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha vilabu 15 ambavyo vitakuwa zikihusisha timu za wanawake na wanaume kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini. Aidha aliwataka wadau wadau wa michezo mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kukisapoti chama hicho ili kiweze kufanikisha mashindano hayo pamoja na kuzisaidia timu za mkoa wa Tanga ili ziweze kutimiza malengo ya kuwa bingwa wa mashindano hayo msimu huu. Mwenyekiti huyo alisema maandalizi ya mashindano hayo kwa timu za mkoa wa Tanga yanaendelea vizuri ambapo vilabu vya mchezo huo tiyari vimekwisha kuanza mazoezi kwenye viwanja mbalimbali kwa ajili ya ushiriki wao. “Ki ukweli nimekaa na vilabu vya mkoa wa Tanga ambapo tutakuwa na timu mbili ambazo zitashiriki ambapo tulikubaliana ni lazima wahakikishe ubingwa wa mashindano hayo unabaki hapa nyumbani “Alisema Jaffary. Mwisho.

Tuesday, February 26, 2013

KOCHA AZAM FC afungiwa

DAR ES SALAAM. KOCHA AZAM AFUNGIWA KWA KUCHOJOA BUKTA Kocha Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. OFISA habari wa shirikisho la soka nchini,Boniface Wambura amesema adhabu hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya VPL na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali. Naye Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa faini ya sh. 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu. Ally Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na rungu la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu. Alitenda kosa hilo kwenye mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba. Matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba 13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu yake wacheze rafu. Naye Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa faini ya sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit Camp iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Pia Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers. Kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita. Vilevile timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam. Pia Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Nayo klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24 mwaka jana. Timu ya Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Faini ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya kuonesha vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Nayo Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), Hamis Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa mjini Morogoro. Polisi Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kupotea. Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting). Klabu hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa, Moro United. Mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya Transit Camp, Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka uzio na kwenda kupigana na washabiki. Kwa vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Monday, February 25, 2013

Ligi kuu Tanzania bara

Na Oscar Assenga,Tanga. Aurora: Aitahadharisha Ruvu Shooting. MWENYEKITI wa timu ya Coastal Union ya Tanga, Hemed Aurora “Mpiganaji”amesema mechi yao na Ruvu Shooting itakuwa ni ngumu hivyo watalazimika kupambana kufa na kupona ili kuchukua pointi tatu muhimu. Akizungumza jana, Aurora alisema mechi hiyo itakuwa haitabiriki kwani timu yao imejipanga vilivyo ili kuweza kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wao wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Mabatini ambapo Coastal Union ilichapwa mabao 2-0 na Ruvu Shooting. Aurora alisema kikosi cha timu hiyo kipo imara kwa ajili ya kuhakikisha timu hiyo inachukua pointi tatu muhimu ili kuweza kukaa katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ligi hiyo ambapo msimu huu inaonkena kuwa na ushindani mkubwa. Aidha alimtaka ,Msemaji wa timu ya Ruvu Shooting,Masau Bwire kuacha kuzungumzia maneno ambayo sio ya msingi na ya kupotosha umma badala yake aileze maneno kimichezo yakwamba timu yao imejipangaje kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi. “Maneno ambayo aliyoyazungumza Masau Bwire sio mazuri wala ya kiungwana kwani tulitegemea aelezee namna timu yake iliyojipanga kwa ajili ya mchezo huo na sio vyenginevyo “Alisema Aurora. Kwa upande wake,Kocha Mkuu wa timu hiyo,Hemed Morroco alisema wachezaji wake wapo imara kuweza kuhakikisha timu hiyo inabakiza pointi tatu muhimu hapa nyumbani. Mwisho. MGAMBO:Polisi Moro watakoma na mziki wetu. TIMU ya Mgambo Shooting ya Tanga imesema itahakikisha inacheza kwa umakini na kujipanga ili kuweza kuchukua pointi tatu muhimu wakiwa ugenini kwenye mechi yao na Polisi Moro. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa kesho (leo) kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro. Akizungumza juzi kabla ya kuandoka mkoani hapa, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mohamed Kampira alisema kikosi cha timu hiyo kimeondoka na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi na sio vyenginevyo. Kampira alisema kikosi chake kina hari nzuri ya kuibuka na ushindi kwani maandalizi waliyoyafanya wanawapa mtazamo mzuri wa kufanya vizuri kwenye mechi hiyo ambayo itakuwa ni yenye ushindani zaidi kuliko inavyofikiriwa. Alisema mbinu ambazo walizitumia kuifunga JKT Ruvu ndizo ambazo watazitumia kuweza kuifunga Polisi Moro lakini watalazimika kuongeza umakini zaidi ili kuweza kupata matokeo mazuri. “Tunakwenda Morogoro kwa lengo la kurudi na pointi tatu muhimu na sio vyenginevyo hivyo tunawaomba wakazi wa mkoa wa Tanga wanaoishi mkoani humo wajitokeze kwa wingi “Alisema Kampira. Hata hivyo,Kampira alisema lengo kubwa la timu hiyo mzunguko huu wa pili ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kila mechi watakayocheza ili kumaliza mzunguko wa pili wakiwa nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi. Mwisho.

Thursday, February 21, 2013

DC Mwanga atoa maamuzi mazito .

Na Oscar Assenga, Lushoto. MKUU wa wilaya ya Lushoto, Alhaji Majid Mwanga ameagiza Mtendaji wa kata Usambara David Mpilipili na Mtendaji wa Kijiji cha Kivilicha, Neehemia singano wakamatwe na waweke ndani kutokana na matumizi mabaya ya fedha za serikali sh. milioni 22 za miradi ya maendeleo. Mkuu huyo wa wilaya alifikia hatua hiyo baada ya watumishi hao kudaiwa kuchakachua fedha hizo za mradi wa zahanati ya kijiji cha Kivilicha huku akishiriana na mkandarasi aliyepewa kazi ya kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo. Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara juzi uliofanyika kijiji hapo mara baada ya kumalizika kikao cha kamati ya maendeleo ya kata (WDC) na baade kamati ya ulinzi na usalama kukaa kwenye darasa la shule ya msingi Kivilicha kisha kutoa taarifa kwa wananchi. Mwanga aliwaambia wananchi baada ya kujadili kwa kina ,kupata maelezo ya watu mbalimbali na pia wengine kukiri kuwa wamekula fedha za wananchi,basi maamuzi yaliyotolewa ni kuwakamata Ofisa Mtendaji wa kata ya Usambara David Mpilipili. Wengine waliohusika ni watia saini benki za miradi ya kata hiyo kuwa ni Mratibu wa elimu kata Godchance shao na Ofisa Ugani wa Kata Nurdini Gembe ambao wanadaiwa walitia saini na kutoa sh.milioni 18 kwa ajili ya kumlipa mkandarasi. Baada ya maamuzi hayo kufikia kamati ya ulinzi na usalama,waliamuru mtendaji wa kata ya Usambara ,David Mpilipili kuwekwa ndani ili kuweza kumhoji fedha karibu sh.Milioni 25.9 alizitumia katika matumizi gani na amezifanyia nini. Mwengine ni mtendaji wa kijiji cha Kivilicha Nehemia Singano,japo alikuwa hayupo kwa wakati huu kwenye wilaya hiyo na kuhaidi kutafuta kila njia ya kuhakikisha wanawajibishwa na kujibu tuhuma zinazowakabili. Mwanga alisema,pamoja na kufanya ubadhirifu wa fedha za zahanati,Mpilipili alikuwa pia sh.milioni 1.6 zilizokuwa zije ngewe chumba cha darasa la shule ya sekondari Kivilicha akidai ametumia fedha hizo kwa ajili ya usafiri wa kwenda halmashauri mara wa mara na kununulia makaratasi ya ofisi. Mkazi wa Kijiji hicho,Mwajuma Athumani alimueleza mkuu wa wilaya kwenye mkutano huo kuwa walichangia kwa shida sh.milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati yao ikiwa ni pamoja na kubambuliwa kuku,mbuzi na ng’ombe wao kama mtu akishindwa kutoa mchango. Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo,Said Mbaga alimweleza mkuu wa wilaya kuwa fedha alizokula mpilipili zimafanya wananchi wakatae kuchangia shughuli za maendeleo kwenye kata hiyo. Mkuu wa wilaya Mwanga alitoa siku 14 timu ya ukaguzi wa ujenzi wa zahanati hiyo iwe imekwenda kwenye kijiji hicho kuangalia thamani halisi ya ujenzi huo zabuni iliyotolewa na malipo Mwisho.

Friday, February 8, 2013

Habari kutoka katika shirikisho la Kandanda hapa nchini TFF

10 WAKATA RUFANI KAMATI YA RUFANI YA UCHAGUZI TFF
RUFANI kumi zimewasilishwa mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika Februari 22 na 24 mwaka huu.

Wakati uchaguzi wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) utafanyika Februari 22 mwaka huu, ule wa TFF wenyewe utafanyika Februari 24 mwaka huu.

Waliowasilisha rufani mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Idd Mtiginjola ni pamoja na waombaji uongozi saba walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho. Warufani hao ni Omari Mussa Nkwarulo na Michael Richard Wambura walioomba kugombea urais na umakamu wa rais.

Wengine ambao waliomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali ni Farid Nahdi (Morogoro na Pwani), Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Omari Isack Abdulkadir (Dar es Salaam), Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya) na Shaffih Kajuna Dauda (Dar es Salaam).

Warufani wengine ni wadau ambao waliweka pingamizi dhidi ya baadhi ya waombaji uongozi katika TPL Board na TFF, pingamizi ambazo zilitupwa mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa sababu za kiufundi.

Wadau hao waliokata rufani ni Agape Fue dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Jamal Malinzi kugombea urais, Medard Justinian dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Athuman Nyamlani kugombea urais, na Frank Mchaki dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Hamad Yahya kugombea uenyekiti wa TPL Board.

Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF imetoa siku ya kesho (Februari 9 mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 8 mchana kwa wote wenye maslahi na rufani hizo (interested parties) kupitia rufani hizo na kuwasilisha hoja zao kwa maandishi.

Kwa watakaoshindwa kufanya hivyo watapata fursa ya kuwasilisha hoja zao kwa mdomo, ambapo wanaweza kuwa wenyewe au wanasheria wao siku ya usikilizwaji wa rufani hizo. Rufani zitasikilizwa Jumapili (Februari 10 mwaka huu) kuanzia saa 2 asubuhi.

OLJORO MWENYEJI WA SIMBA VPL 2012/2013
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 inaingia raundi ya 16 kesho (Februari 9 mwaka huu) kwa mechi nne ambapo Oljoro JKT itaikaribisha Simba jijini Arusha.

Mechi hiyo namba 129 itafanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid huku Simba ikiingia na kumbukumbu ya sare katika mechi yake iliyopita dhidi ya JKT Ruvu wakati wenyeji wao wakiwa wameshinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 3,000 tu utatumika kwa mechi kati ya wenyeji Kagera Sugar na Mgambo Shooting. Mwamuzi wa mechi hiyo atakuwa Amon Paul kutoka Musoma mkoani Mara.

Toto Africans baada ya kufanya vibaya katika mechi tatu zilizopita ugenini imerejea nyumbaji jijini Mwanza itakapoumana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo utaochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Mwamuzi Simon Mberwa kutoka mkoani Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya wenyeji Tanzania Prisons na African Lyon ambayo imepata huduma za kocha mpya Salum Bausi kutoka Zanzibar. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza kwa Bausi kuiongoza timu katika VPL.

Maofisa wengine wa mechi hiyo ni mwamuzi msaidizi namba moja Abdallah Rashid, mwamuzi msaidizi namba mbili Abdallah Mkomwa wote kutoka Pwani wakati mwamuzi wa mezani ni John Kanyenye wa Mbeya. Kamishna wa mechi hiyo ni Rashid Rwena kutoka Ruvuma.

Mechi kati ya Mtibwa Sugar na Azam iliyokuwa ichezwe kesho imesogezwa mbele kwa siku moja ambapo sasa itafanyika Jumapili (Februari 10 mwaka huu) katika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.
                     
FDL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI WIKIENDI
Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao inaendelea kutimua vumbi wikiendi hii kwa mechi kumi na moja zitakazopigwa kwenye viwanja mbalimbali.

Kundi A keshokutwa (Februari 10 mwaka huu) Mbeya City itacheza na Polisi Iringa katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Mkamba Rangers itaumana na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Mkamba) wakati JKT Mlale itakuwa mwenyeji wa Kurugenzi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Green Warriors na Ndanda zitacheza kesho (Februari 9 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika moja ya mechi za kundi B. Mechi nyingine kundi hilo kesho ni kati ya Tessema na Villa Squad kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Keshokutwa (Februari 10 mwaka huu) Transit Camp itacheza na Ashanti United kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wakati Polisi Dar es Salaam na Moro United zitavaana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Kundi C kesho (Februari 9 mwaka huu) ni Polisi Dodoma vs Polisi Tabora (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Polisi Mara vs Mwadui (Uwanja wa Karume, Musoma), Morani vs Kanembwa JKT (Uwanja wa Kiteto, Manyara) na Rhino Rangers vs Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF

Thursday, February 7, 2013

Coastal Union kuondoka kesho Tanga,African Sports Usipime.


Na Oscar Assenga, Tanga.
TIMU ya Coastal Union ya Tanga “Wagosi wa Kaya”inatarajia kuondoka mkoani hapa kesho saa saba mchana kuelekea mkoani mkoani Mwanza kwa ajili ya mechi yao ya Ligi kuu Tanzania bara dhidi yao na Toto African “Wanakesha Mapande mchezo unaotarajiwa kuchezwa  kwenye uwanja wa CCM Kirumba mkoani humo.
Akizungumza jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hemed Morroco alisema maandalizi ya mechi hiyo yanaendelea vizuri na kila kitu kimekwisha kamilika na wachezaji wote wapo imara kwa mchezo huo na hawana majeruhi.
Morroco alisema kutokana na matayarisho aliyoyafanya kabla ya mechi hiyo wanaimani ya kuibuka na ushindi ili kuweza kujiongeza pointi na kuzidi kusonga mbele kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo mzunguko huo unaonekana kuwa na upinzani mkubwa.
Alisema kuwa timu hiyo inatarajiwa kuondoka na wachezaji wapatao 20 na viongozi 5 ndio ambao wataiongoza timu hiyo kwenye msafara huo kwenda mkoani humo ambapo Morroco alisema wanamatumaini makubwa ya kuibuka na ushindi .
Kocha huyo alisema tiyari wamekwisha kurekebisha tatizo walilonalo ambalo lilijitokeza kwenye mechi iliyopita na kuhaidi kucheza ki umakini mkubwa kwa lengo la kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo ambao utakuwa unatazamiwa kuwa mgumu.
Mwisho.
“African Sports yamaliza Ligi ya Mkoa wa Tanga kwa kishindo” Na Oscar Assenga, Tanga.
TIMU ya African Sports “Wanakimanumanu”juzi ilimaliza vema mzunguko wa kwanza wa ligi ya Mkoa wa Tanga baada ya kuibamiza Lushoto Shooting mabao 5-0,mchezo uliopigwa uwanja wa Mkwakwani mjini hapa na kuwa timu pekee ambayo inaongoza ligi hiyo kwa kuwa na pointi 29 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ile kwenye ligi hiyo.
Katika mchezo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani wa hali ya juu hasa katika kipindi cha kwanza hali ambayo ilipelekea kumalizika huku timu zote zikitoka uwanjani zikiwa nguvu sawa ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi.
Wakionekana kujipanga vilivyo kwenye kipindi hicho, African Sports waliingia uwanjani hapo wakiwa na ari na nguvu mpya baada ya kufanya mabadiliko kwa baadhi ya wachezaji wake na kufanikiwa kuandika bao la kwanza dakika 47 kupitia Shekue Salehe kwa njia ya penati iliyotokana na mchezaji wa African Sports Abasi Peter kukwatuliwa na mchezaji wa Lushoto Shooting Athumani Juma eneo la hatari na mwamuzi wa mchezo huo kuamuru ipigwe penati.
Baada ya bao hilo, kupatikana African Sports waliweza kuongeza jitihada za kutafuta mabao langoni mwa Lushoto Shooting na kuweza kupata bao la pili dakika ya 62 ambalo lilifungwa na Shekue Salehe baada ya kutumia uzembe wa mabeki kupachika wavuni bao hilo.
Kutokana na hali hiyo, Lushoto Shooting nao waliweza kujipanga na kucheza kwa umakini lakini ubutu wa safu za umaliziaji ndio kitu ambao kiliwaangusha na kushindwa kupata bao lolote licha ya kupata nafasi za wazi.
African Sports kwa kuonyesha kuwa wao ni mahiri katika soka waliweza kuwachezesha Lushoto Shooting nusu uwanja kwa dakika kadhaa na kuweza kuandika bao lao la tatu dakika 67 kupitia Shekue Salehe baada ya kumalizia kazi iliyofanywa na Ramadhani Omari.
Katika mchezo huo bao la nne la African Sports lilifungwa na Shekue Salehe ambaye alikuwa nyota wa mchezo huo kwa kupachika mabao yote ambapo bao hilo alilifunga dakika ya 78 na jengine akilifunga dakika ya 78 na kuhitimisha karamu ya mabao langoni mwa Lushoto Shooting.
Akizungumza mara baada ya kumalizika mchezo huo,Mlezi wa timu hiyo,Rajabu Kilua alisema mafanikio ya timu hiyo yanatokana na mshikamano uliopo baina ya mashabiki wa timu hiyo pamoja na viongozi wake na kuwataka waendelee kuiunga mkono timu hiyo katika harakati zake za kurejea ilipotoka.
Mwisho.

Tuesday, February 5, 2013

Tufanye hivi

Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga,Kapange katika akitetea jambo na Katibu wa UVCCM wilaya ya Tanga,Gerald Mwadalu wakati wa halfa ya ufungaji wa Kambi ya Mafunzo ya vijana iliyofanyika kwenye kata ya Tongoni jijini Tanga,Picha na Oscar Assenga,Tanga.

Mnaona Jamani.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga,Gustav Mubba akionyesha kadi zilizorudishwa na Mkurugenzi wa Siasa Chadema Kata ya Tongoni ,Ally Mohamed aliyeshikilia kipaza sauti wakati wa ufungaji wa kambi ya mafunzo kwa vijana wa Chama cha Mapinduzi iliyofanyika kwa muda wa siku saba kwenye kata hiyo,Picha na Oscar Assenga,Tanga.

Kamanda Chukua hiyo ni yako!

Kamanda chukua hiyo ni yako.

Narudisha Kadi za Chadema nachukua za CCM

Aliyekuwa mgombea udiwani kata ya Tongoni mwaka 2010 na Mkurugenzi wa Siasa  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kata hiyo,Ally Mohamed alizungumza na umati uliofurika kwenye mafunzo hayo kabla ya kukabidhi kadi za Chama hizo kwa katibu wa CCM mkoa wa Tanga,Gustav Mubba aliyevaa koti la Kijana na Kofia ya Chama cha Mapinduzi,Picha na Oscar Assenga,Tanga.

Kidumu chama cha Mapinduzi.

Mkuu wa wilaya ya Tanga,Halima Dendegu akiwasalimia wananchi wa kata ya Tongoni wakati wa ufungaji wa Kambi kwa vijana wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga,pembeni yake ni Katibu wa CCM wilaya ya Tanga,Lucia Mwiru,Picha na Oscar Assenga,Tanga.

Vijana Msikubali kuyumbishwa.

Katibu wa CCM wilaya ya Tanga,Lucia Mwiru akiwahutubia wananchi wa kata ya Tongoni jijini Tanga wakati wa ufungaji wa Kambi ya Vijana wa Chama hicho .

DC Dendegu akitazama gwaride la Vijana wa Chama cha Mapinduzi.

kutoka kushoto ni Meya wa Jiji la Tanga,Omari Guledi,Mkuu wa wilaya ya Tanga,Halima Dendegu na aliinama mezani akiandika ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga,Gustav Mubba,Picha na Oscar Assenga,Tanga,

Kidumu chama Cha Mapinduzi

Katibu wa Siasa na Uenezi chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga,Kamanda Kapange akihutubia umati wa wananchi katika ufungaji wa kambi hiyo.

Picha na Oscar Assenga,Tanga.

Umati wa Wananchi wa Kata ta Tongoni wakimsikiliza Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga,Gustav Mubba

Wananchi  na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Tongoni jijini Tanga wakimsikiliza Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga,Gustav Mubba aliyekuwa akihutubia kwenye hadhara ya kufunga mafunzo ya Kambi kwa Vijana wa Chama hicho yaliyofanyika mwishoni mwa wiki

Katibu CCM,Gustav Mubba akifuatilia Gwaride la Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga,Gustav Mubba akitazama Gwaride ambalo lilikuwa likipigwa na Vijana wa Chama hicho wakati wa ufungaji wa Kambi ya Chama hicho iliyofanyika kata ya Tongoni nje kidogo ya jiji la Tanga,kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Tanga,Halima Dendegu na kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga,Kassimu Mbuguni.Picha na Oscar Assenga,Tanga.

HII ndio CCM bwana.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Tanga,Gustav Mubba(kulia) akimvalisha Kofia ya Chama hicho,aliyekuwa Mkurugenzi wa Siasa Chadema kata ya Tongoni,Ally Mohamed aliyejiunga na Chama hicho wakati wa ufungaji wa kambi ya mafunzo kwa vijana wa chama cha Mapinduzi iliyofanyika eneo hilo lililopo nje kidogo ya Jiji la Tanga,anayeshuhudia kushoto ni katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Tanga Luccia Mwiru na Katibu wa UVCCM wilaya ya Tanga,Gerald Mwadalu.Picha na Oscar Assenga.

Sunday, February 3, 2013

Mkwassa aanza visingizio baada ya sare na Mgambo Shooting.

Na Oscar Assenga, Tanga.
KOCHA Mkuu wa timu ya Ruvu Shooting,Charles Mkwasa amesema kilichoplekea kushindwa kuibuka na ushindi kwenye mechi ya Ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara dhidi yao na Mgambo Shooting kilichangiwa na upepo mkali uliokuwa ukivuma wakati mechi hiyo ikiwa inaendelea.


Mkwasa alisema hayo mwishoni mwa wiki mara baada ya kumalizika mechi hiyo ambapo timu hizo zilitoka suluhu pacha ya kutokufungana na kueleza kuwa licha ya wachezaji wake kucheza kwa umakini lakini walipofika mbele walishindwa kumalizia kutokana na hali hiyo.

Alisema kuwa baada ya kumalizika mechi hiyo nguvu zao zote watazielekeza kwenye mechi yao na Mtibwa Sugar ambayo watakutana nayo siku za hivi karibuni na kuhaidi ushindi wa kushindo ili kuweza kujiweka nafasi ya juu kwenye msimamo wa ligi kuu.

Hata hivyo aliongeza kuwa licha ya kuwepo kwa upepo huo lakini mechi yao ilikuwa ni ngumu kutokana na timu zote kuonekana kuupania mchezo huo ambao ulikuwa na umuhimu kwao kushindwa na hata wapinzani wao.

     “Sasa nguvu zetu zote tunaziamishia kwenye mechi yetu na Mtibwa Sugar ambapo tumepania kushinda ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kwani kila mechi kwetu ni ushindi ni lazima “Alisema Mkwassa.


Akizungumzia ligi hiyo mzunguko wa pili,Mkwassa alisema timu nyingi zinaonekana kujipanga kwa ajili ya raundi hiyo ya lala salama na kueleza kuwa itakuwa ni ngumu kutokana na kila timu kutaka kufanya vizuri na kujinusuru kushuka daraja.

Mwisho

CCM wilaya ya Tanga yavuna wanachama 119 kutoka vyama vya upinzani wakiwemo Chadema.

CHAMA cha mapinduzi CCM wilaya ya Tanga kimefanikiwa kupata wanachama wapya 119 kutoka vyama vya upinzani kikiwemo kile cha CHADEMA hivyo kuamsha matumaini ya kurejesha kata ambazo zilichukuliwa na upinzania kwa nafasi ya udiwani hapo 2010.

Hayo yalijitokeza mwishoni mwa wiki wakati wa sherehe maalumu ya kufunga kambi kwa vijana wa chama cha mapinduzi CCM iliyokuwa imepigwa eneo la Tongoni nje kidogo ya jiji la Tanga ambapo mgeni rasmi kwenye shughuli hiyo alikuwa katibu wa CCM mkoa wa Tanga Gustav Mubba.

Wanachama waliojiunga na CCM wakitokea upinzania wamo mwanachama aliyewahi kuwani udiwani kwa uchaguzi uliopita kupitia CHADEMA kwenye kata hiyo ya Tongoni Mohamed Aly na katibu wake Bakari Mwinyihamisi ambao waliponda sera za chama chao.

Baada ya kuapishwa na kupewa kadi za CCM walisema wamerejea chama tawala kubaini kuwa kimekuwa na sera zenye kutekelezeka tofauti na kile cha CHADEMA ambacho kina makundi huku upande mwingine kikionekana kuwa na misingi ya udini na ukabila.

Mbali na kuelezea kutoridhishwa na sera za CHADEMA pia katika shughuli hiyo mwanachama aliyekuwa katibu wakati huo Bakari Mwinyihamisi alichukua hatua ya kurejesha katiba ya chama alichojiunga awali ambapo alimpatia katibu wa CCM mkoa wa Tanga Gustavu Mubba.

Akizungumza mara baada ya kuwapatia kadi za CCM wanachama hao wapya katibu Gustav Mubba alisema kwamba hatua waliyochukua vijana hao kujiunga na chama chake inapaswa kuchukuliwa na watu wengine ili kuimarisha nguvu kusukuma mbele maendeleo.

Alisema kwamba CCM ni chama imara ambacho kama kikipata wanachama wa kutosha na wenye kuimarisha mshikamano wataweza kuharakisha maendeleo ya watanzania hasa ikizingatiwa kwamba kina sera nzuri na zenye kutekelezeka tofauti na wapinzania.

Katika shughuli hiyo ambayo pia iliwakutanisha baadhi ya wafanyabiashara maarufu jijini Tanga Katibu Mubba aliwaahidi vijana hao kuwanunulia seti ya Televisheni kwa ajili ya kupata burudani mbalimbali zikiwemo za mipira ya nje vyombo ambavyo pia wataweza kuvitumia kibiashara na kumudu kujiingizia kipato katika umoja wao.

Vilevile wafanyabiashara ambao walikuwa wamehudhuria sherehe hizo waliahidi kushirikiana bega kwa bega na vijana hao waliochukua maamuzi ya kujiunga na CCM ambapo walisema wataangalia namna ya kuwawezesha kiuchumi ili kujikwamua kiuchumi.

Wanachama wa Chadema waliojiunga na chama hicho walikuwa ni 19,wengine walitoka kwenye jumuiya za chama cha mapinduzi ambapo CCM walikuwa ni 40,UWT 20,UVCCM 40 ambapo waliapa mbele ya mgeni rasmi ambaye alikuwa ni katibu wa CCM Mkoa wa Tanga,Gustav Mubba.

Mwisho.

Saturday, February 2, 2013

Vijiji Hamsini Tanga kunufaika na huduma ya Umeme

Na Oscar Assenga,Tanga.
WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) Mkoa wa Tanga umepanga kupeleka umeme katika vijiji hamsini vilivyopo katika wilaya tano zilizopo mkoani hapa katika mwaka wa fedha 2012-2013 ili kuweza kusogeza huduma hiyo karibuni na wananchi wa vijiji hivyo
Mhandisi wa Nishati hiyo toka Secretarieti ya Mkoa wa Tanga, Amon Kyomo alitoa kauli hiyo katika kikao cha kamati ya ushauri ya Mkoa (RCC) kuwa wilaya zilizopo kwenye mpango huo ni Handeni,Korogwe,Mkinga ,Lushoto na Pangani ambapo vijiji vitakavyonufaika katika wilaya ya Handeni ni Kideleko, Kigombe, Madebe, Nyasa na Gole.
Kyoma alisema katika wilaya ya Korogwe vijiji zitakavyopata nishati hiyo ni Maili Kumi,Taasisi ya Utafiti ya(TOFARI), Kwamgwe,, Jambe,Kwamsisi ,Kwamndolwa, Kwakombo, Kwameta,Kwange, Msambiazi,Daraja, Gereza,Kwanzindawa,Mgobe.
 
Alivitaja vijiji vyengine kuwa ni kituo cha afya Kwarukonge, Miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji ya Kitivo na Mombo ambapo umeme huo utapelekwa huku kwa ajili ya kuwapatia wananchi wake umeme.
 
Katika wilaya ya Lushoto,Mhandisi huyo alisema vijiji vipatavyo ishirini na sita vitanufaika na nishati hiyo ambavyo ni Mlalo kupitia vijiji vya Mnadani,Mtumbi,Mshangai,Kwekangana ,Mathego, Malibwi, Manolo, Hambogo, Ngwelo,Dindira,Kijungu Moto, Kijango,Kwamazandu, Lusanga,Makumba,Mkwakwani,Vugiri,Makose,Nkalai,Sunga,Kihitu,Malindi  na Rangwi.
 
Aliongeza kuwa katika wilaya ya Mkinga, wanatarajiwa kupeleka umeme katika vijiji vya Manza Bay, Daluni na Gombero na wilaya ya wilaya ya pangani wanatarajiwa kupeleka huduma hiyo katika vijiji vya Mkalamo na Mbulizaga.
 
Kyoma alisema tiyari zabuni ilikiwsha kutangazwa tokea mwezi Novemba mwaka jana na matarajio yao hadi kufikia mwezi march mwaka huu Mkandarasi ataanza kazi rasmi ya kufikisha huduma ya nishati kwa kutumia mfumo wa “turnkey”
 
Mwisho.

CCM Tanga yawacharukia wapinzani kuacha kuwachafua viongozi wanawakeNa Oscar Assenga,Tanga
Wananchi wameshauriwa kuwa makini na viongozi wa kisiasa wanaotumia majukwaa kwa ajili ya kuwatukana na kuwa kashfu  viongozi wa serikali walioko madarakani  hasa wanawake kuwa sio watendaji wazuri.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Tanga Kassim Mbunguni wakati akifungua tawi la vijana wa Bodaboda barabara ya 20 katika kata ya Ngamiani Kusini jijini hapa.
Alisema mwanasiasa makini hawezi  kusimama jukwaani na kuhoji uhalali wa utendaji na maamuzi katika viongozi wa kike na wakiume bali ni kuwahamsisha wanachama wake katika  utekelezaji wa shughuli za maendeleo  .
“Ndugu zangu wananchi ukiona mwanasiasa,Mbunge au diwani anahoji uhalali wa viongozi tena kwa kuwabagua kuwa wanawake hawawezi kuendesha nchi huyo ni kumwangalia kwa macho mawili ni mbinafsi na asiependa maendeleo”alisema Mbuguni.
Alisema kazi ya mwakilishi wa wananchi kutetea maslahi ya wannachi wake katika eneo analotoka na kuhakikisha anahimiza kuchangia na kusimamaia miradi ya maendeleo kwa ukamilifu sio kutumia majukwaa kukashifiana na matusi.
Mbuguni alisema anashangazwa na vyama vya upinzani katika jiji la Tanga kuhamasisha wananchi kutoshiriki usafi wa mazingira katika maeneo yako ilihali wao wanatoka kushiriki zoezi hilo katika maeneo yao.
Aliwataka wananchi kujihadhari na wanasiasa ambao kazi yao ni kuhamasisha vurugu na machafuko halafu machafuko yakianza wao wanakimbia kujificha na kuwasababishia matatizo watu wasio na hatia.
Nae Katibu wa Uenezi alisema uwepo wa viongozi wakike katika jiji hilo na Mkoa sio kwa lengo la kushusha maendeleo ya mkoa kama wapinzani wanavyonadi bali ni katika kuhakikisha ushirikishwaji wa jinsia zote katika kuchangia kasi ya maendeleo.
Hivyo aliwataka viongozi wa upinzani kuacha kutumia majukwaa kwa ajili ya kuwachafua viongozi wa serikali wanawake walioko katika Mkoa huo kwani wamechagulia kutoka na uwezo wao wa kiutendaji.
Jumla ya vijana 45 walipewa kadi za uwanachama wa CCM baada ya kujiengua kutoka chama cha Wananchi CUF

DC Mwanga awataka wahitimu wa mafunzo ya mgambo kuwa wazalendo

Na Oscar Assenga,Lushoto

MKUU wa wilaya ya Lushoto,Alhaji Majid Mwanga amewataka wahitimu mafunzo ya mgambo kutilia mkazo suala la uzalendo kwa manufaa ya umma ikiwashauri kuwa mabalozi wazuri watakaotumia elimu waliyoipata kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi kutokomeza mazao ya bangi na mirungi.
Mwanga alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akifunga mafunzo ya awali kwa wahitimu wa mgambo 136 ambapo kati yao wanaume walikuwa 133 na wanawake watatu hafla ambayo ilifanyika kata ya Gare katika wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.
 Mkuu wa huyo wa wilaya alielezea masikitiko ya kuwepo kwa takwimu zinazoiweka Lushoto kwenye sura mbaya miongoni mwa jamii akisema  takwimu zinaonyesha ni moja ya wilaya zinazoongoza kwa kilimo cha bangi,mirungi,utengenezaji na unywaji pombe haramu ya gongo hali ambayo isipodhibitiwa kutakuwa na walevi ama ‘mateja’ wengi.
 "Pamoja na kuwa leo mnahitimu niwaombeni mshirikiane na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kutokomeza bangi na mirungi kule mlimani,takwimu zinaonyesha kuwa hali siyo nzuri  Lushoto ni miongoni mwa wilaya zinazoongoza kwa kilimo cha bangi,mirungi,utengenezaji na unywaji gongo,tumieni uzalendo wenu”alisema Alhaji Mwanga.
Katika hotuba yake kwa askari hao wa mgambo Alhaji Mwanga pia aliwataka kutumia mafunzo waliyoyapata kudhibiti biashara zote haramu utofanyika kwenye maeneo yao ya vijiji huku akizitaja baadhi yake kuwa ni upasuaji wa mbao kinyume cha sheria na nyinginezo zilizokatazwa.
Akijibu hoja juu ya wahitimu hao kulalamikia kampuni binafsi za ulinzi kuwasahau kuwapatia ajira Alhaji Mwanga alisema kwamba ataitahidi kwa hali na mali kutumia nafasi yake kufanya mkutano na wamiliki wa kampuni hizo kuwaeleza umuhimu wa kuajiri vijana waliopitia mafunzo ya mgambo njia ambayo aliieleza kuwa itasaidia kutoa fursa kwa baadhi yao kupata ajira.
Hata hivyo alisema iko haja  kwa vijana hao wanaomaliza mafunzo hayo ya mgambo kujiendeleza kielimu badala ya kukata tamaa na kuridhika na elimu ya darasa la saba waliyonayo akisema kwamba wakisoma zaidi kuna nafasi kubwa ya kuairiwa sehemu mbalimbali nchini.
 "Mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama tumesikia kilio chenu,tutajitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kukaa na wamiliki wa kampuni za ulizi kuwaelimisha umuhimu wenu kwa kazi za ulinzi baada ya kuwa mmepata mafunzo yanayostahili hasa yale ya uzalendo”alisema mkuu huyo wa wilaya huku akiwataka wahitimu hao kushiriki kazi za maendeleo kwenye maeneo yao.
Kuhusu suala la uhifadhi wa mazingira mkuu huyo wa wilaya aliwataka askari hao wa mgambo kusaidiana na wananchi wengine kulinda na kutunza vyanzo vya maji,kuwadhibiti wale wanaokata miti na kuchoma moto ovyo sanjari na wanaopasua mawe kwa lengo la kupata fedha za haraka huku wakitambua kuwa kufanya hivyo kumechangia kuharibu mazingira ya mji.
“Ninasikitishwa sana na vitendo vya upasuaji mawe vinavyofanyika kwenye milima,sasa nasema huu ni uharibifu wa mazingira hivyo kuanzia sasa ni marufuku mtu yeyote kupasua mawe na kokoto kule Mlima Vuli,na niendelee kuwaomba askari ninyi mnaohitimu leo mkiona mtu anaharibu mazingira mkamateni na kumhoji pia afikishwe kunakohusika”alisema DC Mwanga.
Katika hotuba yake aliyoisoma kwa wahitimu hao wa magfunzo ya awali ya mgambo mkuu huyo wa wilaya alizama kwa undani juu ya athari za matumizi ya madawa ya kulevya aina ya bangi na mirungi akisema inachangia kudhoofisha nguvu kazi na hivyo kuzorotesha ukuaji wa uchumi.
Hivyo Alhaji Mwanga aliwaasa wananchi wa wilaya ya Lushoto kutowaficha wale wote wanaojihusisha na vitendo viovu vya ulimaji mazao haramu badala yake aliwahimiza kutoa msaada wa kuwafichua ili hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao na tatizo kukoma kabisa.

DC Lushoto akemea vikali tabia ya wazazi kubariki vitendo vya wanafunzi kupewa ujauzito.

Na Oscar Assenga,Lushoto

MKUU wa wilaya ya Lushoto Alhaji Majid Mwanga amekemea vikali tabia za baadhi ya wazazi kubariki vitendo vya watoto wa kike kupatiwa ujauzito na kukatizwa masomo yao ambapo mashauri hayo yanayochangia kuharibu mustakabali wa maisha kwa vijana wa kike humalizwa majumbani baada ya wahusia kutozwa faini kwa wakilipishwa mbuzi ama ng’ombe.
Badala yale Alhaji Mwanga aliwataa wazazi hao kufuata sheria kanuni na taratibu kwa uhakikisha wahusika utiaji wa mimba wanafunzi wanafikishwa kwenye vyombo vya kisheria ambapo aliwaomba madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo wazazi kutoa ushiriiano kwa serikali ili kulimaliza tatizo hilo linalowasababisha watoto wa kike kukatiza masomo yao.
Alisema wakati serikali ikiweka mazingira mazuri ya elimu kuwawezesha watoto wote kusoma ili kuendesha maisha yao ya baadaye kwa uhakika baadhi ya watu waiso waadilifu hushiriki vitendo vya mmomonyoko wa maadili wakiwarubuni watoto wa kike na kuwapachika mimba utotoni.
Alhaji Mwanga alibainisha kwamba uongozi wake hauko tayari kwa suala la wanafunzi uendelea katika wilaya yake ambapo aliwahimiza madiwani kuwa mstari wa mbele kuwafishua wanaotia mimba wanafunzi huku akiahidi kuwachukulia hatua kali za isheria wale wote watakaobainika.
Vilevile mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba asingependa usikia kuna mwanafunzi amechaguliwa kuingia idato cha kwanza ameshindwa kufanya hivyo kwa maelezo kuwa wote waliochaguliwa wanastahili kusoma pasipo kuweko kwa kisingizio cha aina yeyote ile.
Alisema,baada ya mwanafunzi uchaguliwa kinachohitajika ni mzazi kumuandaa kwa mahitaji ya kawaida kama sare  ambapo alieleza kuwa haitakiwi mzazi kutoa viosingizio vya kuwepo kwa michango iliyosababisha kutompeleka mtoto wake shule kwa vile maelekezo yalishatolewa kwa walimu na kama kuna matatizo zaidi ngazi husika ikiwemo ofisi yake ijulishwe.
Kwa upande mwingine mkuu huyo wa wilaya ya Lushoto alielezea umuhimu wa watendaji wa serikali kutekeleza majukumu yao kwa umma kama walivyoelekezwa huku akisema kwamba yule atakayekwenda kinyume ni haki kwa mamlaka husika kumchukulia hatua za kinidhamu.
Aidha aliwakumbusha madiwani wa halmashauri hiyo ya wilaya ya Lushoto kuwasimamia kwa maribu watendaji wao ili kuhakikisha wanawajibika kama inavyohitajika njia itakayosaidia kuondosha malalamiko kwa wananchi huku ilani ya uchaguzi ya CCM ikitekelezwa kwa tija.
Mbali na hayo Alhaji Mwanga aliwakumbusha madiwani umuhimu wa uwashirikisha wananchi katika masuala yanayohusu utekelezwaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao akisema kwamba kufanya hivyo kutasaidia kuithamini na kuilinda na itaweza kuwa endelevu na uleta tija.
Alhaji Mwanga katika mkutano huo wa baraza la madiwani alitumia fursa aliyoipata kuhutubia kwa kueleza mapungufu ambayo yameitokeza kwenye mfuo wa afya wa CHF akisema kuwa wilaya ya Lushoto hivi sasa haifanyi vizuri kama ilivyouwa awali kwa vile changamoto ni nyingi.
Alisema wakati wananchi wakiwa wanahimizwa uchangia mfuko huo wanapofika kwenye Zahanati ama hospitalini huambiwa kwamba hakuna dawa hali inayoashiria kwamba fedha zao zimetumika ndivyo sivyo akiwataka madiwani kuwabaini wasaliti wa CHF ili hatua zichukuliwe.
Pamoja na kuyasema hayo Alhaji Mwanga aliwashauri wajumbe wa baraza hilo la madiwani kuendelea na utaratibu wa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa uchangia mfuko wa CHF kwa madai kuwa ukisimamiwa vizuri utaleta tija kama ilivyothibitika maeneo mengine nchini.
Akihitimisha hotuba yake mkuu huyo wa wilaya aliyataka mabaraza ya madiwani ya halmashauri ya wilaya ya Lushoto na lile jipya la Bumbuli kuanzisha utaratibu wa kuonyesha mikutano kwa kutumia utaratibu wa Video Conference ili hata waliopo kwenye shughuli zao waone jinsi viongozi wao wanavyochangia ama kutoa hoja zinazoyagusa maeneo yao wanayoyaongoza.
Mwisho.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

SAMATA, ULIMWENGU MBIONI KUTUA NCHINI
Washambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanatarajia kutua nchini kesho (Februari 3 mwaka huu) tayari kwa mechi ya Cameroon itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Samata na Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) watawasili saa 11.10 jioni kwa ndege ya PrecisionAir na kwenda moja kwa moja kambi hoteli ya Tansoma.

Wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanaanza kuripoti kambini leo jioni (Februari 2 mwaka huu) mara baada ya mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar.

Mechi hiyo iliyo katika Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) pia itatumika kwa ajili ya kutoa ujumbe wa vita dhidi ya Malaria viwanjani, ugonjwa unaoongoza barani Afrika kwa kusababisha vifo vya watoto na wajawazito.

TFF kama ilivyo Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na FIFA imekuwa msitari wa mbele katika kueneza kampeni ya vita dhidi ya Malaria inayoongozwa United Against Malaria (UAM). Rais wa TFF, Leodegar Tenga na nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o ni miongoni mwa mabalozi wa vita dhidi ya Malaria barani Afrika.

WACAMEROON KUANZA KUTUA DAR KESHO
Kundi la kwanza la Cameroon likiongozwa na kiungo wa zamani wa Toulouse ya Ufaransa ambaye sasa yuko Al Ahli ya Falme za Kiarabu (UAE), Achille Emana na Meneja wa timu hiyo Rigobert Song litatua nchini kesho (Februari 3 mwaka huu) saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM.

Wachezaji wengine katika kundi hilo ni Vincent Aboubakary anayechezea timu ya Valenciennes iliyoko Ligi Kuu ya Ufaransa, kipa Charles Itandje anayedakia timu ya POAK FC ya Ugiriki, Kocha wa viungo Sylvain Monkam.

Mshambuliaji wa Anzhi Makhachkala ya Urusi ambaye ndiye nahodha wa Cameroon, Samuel Eto’o ataongoza kundi la pili litakalowasili nchini Februari 4 mwaka huu (saa 3.45 asubuhi) kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi, Kenya.

Wengine katika ndege hiyo Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik wakati Kocha wa timu hiyo Jean Paul Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Afrika Kusini.

Februari 4 mwaka huu kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa.

Wachezaji waliobaki wakiongozwa na kiungo wa Barcelona, Alexandre Song watawasili Februari 5 mwaka huu kwa muda tofauti kwa ndege za KLM na Kenya Airways.

TENGA AONGEZA WAWILI KAMATI YA NIDHAMU
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ameteua wajumbe wawili kuingia kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya nafasi mbili kuwa wazi kutokana na mmoja kuteuliwa kuongoza kamati nyingine ya TFF na mwingine kufariki dunia.

Iddi Mtiginjolla ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu hivi karibuni aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF baada ya Shirikisho kufanya mabadiliko ya katiba yaliyotokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA), wakati mjumbe mwingine wa Kamati ya Nidhamu, Shaaban Semlangwa alifariki dunia katikati ya mwaka uliopita.

Wajumbe wapya walioteuliwa ni Jesse Mguto- alikuwa Hakimu Mkazi na kwa sasa ni mwanasheria na Wakili wa Mahakama Kuu. Ana Digrii ya Sheria. Mwingine ni Yohane Masala ambaye kwa sasa ni Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali (Principal State Attorney). Ana Digrii ya Kwanza na ya Pili ya Sheria na Digrii ya Pili katika masuala ya Amani na Haki (MA in Peace and Justice).

Rais Tenga amesema ana imani na uwezo wa watu hao na kwamba watafanya kazi yao kwa uadilifu ili Shirikisho liendelee kuboresha utawala bora.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)