BLOG

SOMA TARUJA LEO

SOMA TARUJA LEO

TAWODE

TAWODE

Thursday, October 31, 2013

CCM WILAYA YA TANGA KUFANYA MKUTANO WA HADHARA KIJIJI CHA PANDE B JUMAMOSI.

Na Oscar Assenga, Tanga.
CHAMA cha Mapinduzi CCM wilaya ya Tanga kinatarajia kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Pande B kata ya Kiomoni jijiniTanga lengo likiwa kuwashukuru wananchi kwa kukiwezesha chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi serikali ya kijiji hicho uliofanyika hivi karibuni.
 
Katibu wa Siasa, Uenezi wa Chama hicho wilaya ya Tanga, Lupakisyo Kapange alisema mikutano hiyo itafanyika Jumamosi wiki hii eneo la Lwande na baadae jioni watafanyia kwenye kitongoji cha Kivuleni katika kata hiyo ambapo viongozi mbalimbali watapata nafasi ya kuzungumza na wananchi hao.
 
Kapange alisema ushindi wa chama hicho unaonyesha jinsi gani wananchi walivyokuwa na imani kwao kutokana na kazi kubwa wanayoifanya kuwaletea maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa zahanati na barabara.
 
Katika uchaguzi huo wa serikali ya Kijiji cha Pande B wapiga kura waliokuwa wamejiandikisha walikuwa ni 686 waliopiga kura ni 674,zilizoharibika ni 97 hivyo kura halali kuwa ni 577 ambapo kati ya hizo,Chama cha Mapinduzi (CCM)kilipata kura 418,Chama cha Wananchi (CUF) kilipata kura 128 na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA )walipata kuwa 31.
 
Kwa upande wa wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji cha Pande B Chama cha Mapinduzi kilifanikiwa kupata wajumbe 11 ambao ni Ally Jabiri,Ally Mohamed, Kauli Makame,Yakwesa Samweli,Salim Kibwana,Salim Bakari, Ally Mchaga,Said Abdallah,Mtoa Bakari,Hussein Salim na Said Kilo.
 
Aidha alisema chama hicho kitaendelea kushirikiana na wananchi katika maeneo mbalimbali wilayani hapa ili kuhakikisha wanaharakisha kasi ya maendeleo yao pamoja na kueleza sera za chama hicho.
 
Hata hivyo Kapange aliwashukuru wananchi wote wa wilaya ya Tanga kwa kuungana na mkoa katika shughuli mbalimbali za kiserikali na kichama ikiwemo mapokezi makubwa ya viongozi wa kitaifa .

WANANCHI WENYE HASIRA WAUCHOMA MOTO MSIKITI WA ANSAR SUNNI KILINDI.

PASKAL MBUNGA,KILINDI
WANANCHI wenye hasira na ambao bado hawajafamika wameuchoma moto na kuubomoa kabisa msikiti unaotumiwa na  waumini wa dhehebu la dini ya kiislamu la Ansar Sunni wanaoaminika kuwa chanzo cha  chokochoko  na machafuko yaliyosababisha  mauaji ya watu hivi karibuni katika kijiji cha Lulago, Kata ya Lwande wilayani Kilindi.
 
Sambamba na ubomoaji huo wa msikiti, lakini pia wamezichoma moto nyumba 16 zinazokaliwa na wafuasi hao wa Ansar baada ya wao kukimbilia misituni wakikwepa kukamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama kutokana na kuhusika kwao na mauaji ya mwanamgambo kijijini hapo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari i waliotembelea kijiji hicho mwanzoni mwa juma hili, Mwenyekiti wa kijiji cha Lulago, Mohamed Waziri Mwariko (48), alisema kwamba baada ya kuzusha furugu na machafuko kijijini hapo  juma lililopita ambapo walimwua askari mgambo kwa kumkata mapanga, , walikimbia na kwenda kujificha misituni ambapo mpaka sasa hawajonekana.
 
Mwariko alisema wafuasi hao ambao wanajinadi kuwa ni waislamu safi na kuwaita waislamu wengine ni makafir, walianza kukinzana na uongozi wa serikali ya kijiji kwa kuwashawishi watu wasiiti serikali iliyoko madarakani wakidai kuwa ni ya kikafir na hivyo kukataza wasilipie ushuru kwa kijiji.
 
Akisimulia chanzo cha vurugu kilichopelekea mauaji hayo, Mwariko alisema kuwa tarehe 23 Oktoba mwaka huu, mfanya biashara Haji Mtana alinunua iliki gunia mbili na kulipia ushuru wa  kijiji wa shilingi 20,000 ambapo walitokea wafuasi hao na kumtaka mnunuzi huo asilipie kwa madai kuwa serikali ya kijiji na serikali kuu zote ni za kikafiri.
 
Uongozi wa kijiji ulipowaita kuja kutoa maelezo ya matamshi yao, walikataa wito na ndipo uongozi wa kijiji uliwatumia mgambo ambaye walimwua  kwa kumkata mapanga na kisha kuanza kutamba kijijini hapo kwa kufyatua ovyo risasi.
 
Mwenyekiti huyo alieleza kwamba pamoja na uongozi wa kijiji kutoa taarifa polisi, lakini wananchi waliingiwa na hofu baada ya kuchinjwa mgambo huyo kwani wananchi walizihama nyumba zao na kukimbilia porini kujificha
 
”:Kwa kusaidiana na majeshi ya ulinzi na usalama, wananchi hao waliweza kuwakamata wafuasi 16 pamoja na silaha walizotumia zikiwemo bunduki 4 bastola 2, mapanga 18 na visu 12”, alisema Mwariko na kuongeza kwamba viongozi wakuu wa kikundi hicho walikimbilia misituni  na hawapatikana hadi sasa..    
 
Mwenyekiti huyo wa kijiji alisema kutokana na hasira walizokuwa nazo wanakijiji juu ya watu hao ambao walihamia kijijini hapo mwaka 2009 wakitokea Dar es Salaam hawataki warudi tena katika maeneo yao waliyoyahama.
 
Idadi kubwa ya wakazi wa Kijiji cha Lulago chenye watu 4063 ni Waislamu ambao ni karibu 99.5% ya wakazi wote. ,

UVCCM KOROGWE WATAKIWA KUUNDA VIKUNDI VYA UZALISHAJI MALI.

Korogwe
JUMUIYA ya Vijana wa chama cha mapinduzi UVCCM mjini Korogwe imetakiwa kuonyesha uhai wao kwa kuimarisha umoja wao na kuunda vikundi vya uzalishaji mali ambavyo vitawawezesha katika kujikwamua kiuchumi badala ya kujitumbukiza kwenye migogoro yenye kuzorotesha maendeleo yao.

Mwenyekiti wa UVCCM Korogwe mjini, Thomas Ngonyani Majimarefu ametoa kauli hiyo wakati alipozungumza na wanachama na viongozi wa jumuiya hiyo tawi la Old Korogwe wakati alipofanya ziara yake kwenye eneo hilo kama sehemu ya kutoa shukrani zake mara baada ya kuchaguliwa kushikilia kiti hicho cha wilaya.

Ngonyani amesema kwamba ili jumuiya hiyo iwe imara kuna kila haja kwa viongozi khakikisha wanakuwa na wanachama walio hai huku wakithubtu kjianzishia miradi ambayo itawasaidia kjikwamua kiuchumi utaratibu ambao utasababisha vijana wengi kuvtiwa kujiunga na umoja wao na kuharakisha maendeleo.

Naye Katibu wa jumuiya hiyo ya vijana eneo la Korogwe mjini Anna Jorojick aliwakumbusha vijana hao umuhimu wa kutunza siri za vikao vyao ili kutotoa fursa kwa wengine kufanya propaganda ambapo zitasababisha hujuma ndani ya maazimio yao waliojiwekea njia aliyoeleza pia kuimarisha umoja wao.

Serikali yatangaza viwango vipya vya ufaulu elimu ya sekondari

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu  ya mwanafunzi  na ufaulu leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Elimu Profesa Eustella Bhalasesa.

 Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome (hayupo pichani).

Waandishi wa habari na maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome(hayupo pichani). Picha zote kwa hisani ya Handeni Kwetu blog

MAKAMBA AZIPIGA TAFU SHULE ZA SEKONDARI BAGA NA TAMOTANa Raisa Saidi,Bumbuli,  
Mbunge  wa  jimbo  la  Bumbuli  January Makamba  amekabidhi  msaada  wa  shilingi  milioni mbili  katika  shule  ya  sekondari  ya Baga na  Tamota   kwa  ajili  ya  ujenzi  wa  Maabara   kwa lengo la  kuinua  masomo  ya  sayansi.

Pamoja na msaada huo wa milioni moja moja kwa kila shule pia ametoa  msaada  wa  mabati  mia moja kwa kila shule kwa ajili ya  kuezekea  vyumba  vya  madarasa  na nyumba  za walimu   katika  shule hizo.

Alitoa msaada huo wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya kidato cha nne kwenye shule hizo.

Makamba  ambae  pia  ni  Naibu  Waziri wa  Mawasiliano  Sayansi  na  Tenknolojia  alisema  kuwa  lengo  la  kutoa  misaada  hiyo  ni  kutaka  kuongeza  na  kuinua  kiwango  cha   elimu   katika  shule   zilizopo  katika  jimbo hilo.

Mbunge huyo  alisema kuwa msaasa huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali katika kuhakikisha kila shule ya kata inakuwa na  maabara katika kuhakikisha kiwango cha ufaulu na hususani katika masomo ya sayansi hapa nchini kinaongezeka.

Wazazi na walimu wa Shule hizo  wameeleza kufurahishwa kwao na juhudi za Mbunge wa Jimbo hilo, January Makamba katika kukukuza kiwango cha elimu na kuondokana na usemi usemao Wasambaa hawajasoma na ni watu wa sokoni tu.

 Diwani wa kata ya Milingano Hozza Mandia akiwa katika mahafali hayo alisema kuwa juhudi  za Mbunge huyo ni  mfano mzuri  wa  kuigwa  na  wanasiasa  wengine  ili  kuwaletea  maendeleo   wananchi huku akiongeza kuwa  jitihada  hizo zinapaswa kuungwa mkono.   

TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI LEO.

Release No. 188
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 31, 2013

SALAMU ZA PONGEZI ZAMIMINIKA KWA MALINZI
Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Jamal Malinzi ameendelea kupokea salamu za pongezi baada ya kushinda wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Salamu nyingine za zimetoka kwa Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter ambapo amempongeza Malinzi kwa kuchaguliwa na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake ya kuongoza mchezo huo nchini.

Blatter amesema ana uhakika ufahamu wake na uwezo wake katika uongozi ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini, na kuongeza kuwa milango ya FIFA iko wazi wakati wowote anapotaka kujadili masuala yanayohusu mchezo huo.

“Nakutakia wewe na kamati mpya ya Utendaji iliyochaguliwa kila la kheri, nguvu, na kila aina ya mafanikio kwa changamoto zilizo mbele yenu,” amesema Rais Blatter katika salamu zake.

Wengine waliomtumia Rais Malinzi salamu za pongezi ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya, Rais wa Heshima wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Arumeru (ADFA), Peter Temu.

YANGA, JKT RUVU UWANJANI KESHO
Raundi ya 12 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Novemba 1 mwaka huu) kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Yanga itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A. Tiketi zitauzwa siku ya mechi uwanjani katika magari maalumu kuanzia saa 4 asubuhi.


Novemba 2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).

Raundi hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7 mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.

Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

KOCHA JAMHURI ABWAGA MANYANGANa Masanja Mabula -Pemba .
Kocha Mkuu wa Timu  Jamhuri Said Mohammed ameamua kuikacha timu hiyo baada ya kudai kuwa hakuna utulivu ndani ya timu hali ambayo imepelekea kuweko na makundi kati ya Viongozi jambo ambalo limepelekea matokeo mabaya kwenye michuano  ligi kuu ya Zanzibar .

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi , kocha huyo mwenye leseni ya daraja la C linalotambuliwa na Shirikisho la Mpira la Afrika ( CAF) amesema kuwa uwamuzi wa kuicha timu umekuja baada ya kuona kuwa baadhi ya viongozi wanahusika katika kuihujumu timu .

Amesema kuwa pamoja na mapungufu yaliyopo ndani ya kikosi cha timu hiyo Kongwe Visiwani hapa , lakini baadhi ya viongozi wamehusika moja kwa moja katika matokeo mabaya uwanjani .

"Haiwezekani kiongozi unasema kwa kuwaambia wachezaji kuwa tunnakwenda uwanjani kufungwa , badala ya kuwa wewe uwe ni chachu kuwahamisha wachezaji kufanya vizuri , kama sio hujuma ni nini mwandishi ? alihoji .

Aidha ameeleza kwamba kwa mujibu wa timu inavyocheza mpira uwanjani , hakuna sababu ya kuwa tushike nafasi ya chini kwenye msimamo , na kutokana na hali hiyo nimeona bora niachie ngazi kuonoa timu hiyo .

" Mimi nafanya kazi kwa bidii  , maarifa na nguvu zote , lakini kutokana na hali hii ndiyo maana nimeamua kuachia ngazi , naamini sasa viongozi watatambua kwamba hujuma zao hazilengi katika kuimarisha timu bali zinabomoa " alieleza .

Akizungumzia malengo yake ya badaye kocha Said amesema kuwa kwa sasa hana mpnago wa kufundisha timu kutokana ambapo anataka kutuliza akili yake baada ya kutumia muda mwingi katika klabu ya Jamhuri .

"Unajua nimetoka kufundisha timu yenye mashabiki wengi , kwa sasa siwezi kukurupuka na kuamua kutafuta timu ya kufundisha kwa kipindi hiki " alifahamisha .

Akizungumza na gazeti hili , Meneja wa Timu hiyo Abdalla Mohammed Elisha amekiri kupokea taarifa za kocha huyo kujiuzulu , na kuongeza kwamba sababu za kocha kuachia ngazi hazielewi .

"Ni kweli kocha wetu ameiacha timu kuanzia jana (juzi) lakini sababu zilizomfanya aiache timu mtafute na muulize yeye ,  mimi sizielewi na naamini ni uwamuzi wake mwenyewe "

Elisha amekanusha kwamba kocha huyo haelewani na baadhi ya viongozi wa timu hiyo na kwamba uwamuzi wa kuachia ngazi ni wake binafsi .

Tayari zipo taarifa kwamba kocha huenda akajiunga na timu ya Konde Star inayoshiriki ligi daraja la kwanza Taifa Pemba ambayo alikuwa anaifundisha kabla hajajiunga na timu ya Jamhuri .

Wednesday, October 30, 2013

UKUMBI WA MAZOEZI KIKWAZO NGUMI ZA RIDHAA TANGA.

Na Oscar Assenga,Tanga.
CHAMA cha Ngumi za Ridhaa mkoa wa Tanga(TBA)kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na ukumbi wa kufanya mazoezi kwa mabondia kitendo ambacho kinawapa wakati mgumu mabondia wakati wa kufanya mazoezi.


Mwenyekiti wa Chama hicho,Mansour Soud Semfyoa aliiambia Tanga Raha kuwa hali hiyo inawafanya mabondia hao kushindwa kutimiza ndoto zao na kuziomba mamlaka husika ikiwemo uongozi wa serikali ya wilaya kuwasaidia ili kuweza kupatikana ukumbi wa mazoezi.

Soud alisema suala lengine ambalo linawapa changamoto ni uhaba wa vifaa vya kufanyia mazoezi kwa mabondia waliopo mkoani hapa hivyo kuwaomba wadau kuwasaidia ili viweze kupatikana.

MWENYEKITI WA CHAMA CHA NGUMU ZA RIDHAA MKOA WA TANGA,MANSOUR SOUD SEMFYOA
Mwenyekiti huyo alisema chama hicho kimefanya jitihada mbalimbali ili kuweza kupatikana ukumbi wa Tangamano ambapo uongozi wa chama hicho  tayari umeshaandika barua kwenda kwa mkurugenzi wa Jiji lengo likiwa ni kumuomba wautumia ukumbi wa Tangamano.

Alisema majibu ya barua hiyo iliwajibu wamekubaliwa katika ukumbi wa Communite Centre Makorora ambapo wataungana na vikundi vyengine na kuelezwa kuwa wanatakiwa walipie sh.elfu hamsini ili waweze kupewa eneo hilo.

Aidha alisema mikakati waliokuwa nayo hivi sasa ni kuuendeleza mchezo wa ngumi ambao unaonekana kupotea mkoani hapa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali lengo likiwa ni kupata mabondia wazuri ambao watautangaza mkoa huu.

Aliongeza kuwa wanampango wa kuupeleka mchezo huo mashuleni ambapo kwa kuanzia wataanzia katika shule za msingi na sekondari na baadae vyuo vikuu lengo ni kuwapa vijana hao uelewa kuhusu mchezo huo.

Soud alisema pia wanatarajia kuanzisha miradi ambayo itakisaidia chama hicho kujiendesha chenyewe kuliko kutegemea misaada ambao wakati mwengine inaweza kukwamisha malengo yao waliojiwekea.