SERIKALI YA MKOA WA TANGA YASIFU JUHUDI ZINAZOFANYWA NA SHIRIKA LA AGPAHI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Zena Saidi amesifu jitihada zinazofanywa na Shirika la  Ariel Glaser Pediatric AIDS Health Care Initiative (AGPAHI) kwa kuhakikisha watoto wanapata huduma stahiki za afya na kisaikolojia.
Mhandisi Zena (pichani)aliyasema hayo leo wakati akisoma hotuba yake katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani iliyoadhimishwa kwenye viwanja vya shule ya Sekondari Popatlal Jijini Tanga.
“Ninayo furaha kubwa sana kuwepo hapa kushiriki na kuona jitihada zinazofanywa na shirika la AGPAHI kwa watoto wa mkoa wa Tanga ….Nafahamu kuwa mkusanyiko huu una watoto,vijana na wahudumu wa afya kutoka hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tanga (Bombo  Hospitali),vituo vya afya vya Ngamiani, Makorora na Pongwe.

Shirika hilo ambalo lilianza kufanya kazi mwezi Oktoba 2016 katika mkoa wa Tanga kwa kutoa huduma za matunzo na matibabu kwa watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) limekuwa ni chachu kubwa kuwafikia watoto na vijana kupitia vikundi.

Mhandisi Zena alisema “mara tu baada ya shirika hilo kuanza kazi mkoani Tanga, taratibu za uundwaji wa vikundi vya watoto (maarufu kama Ariel Clubs) ulianza na sehemu ambazo vikundi vilikuwepo awali viliimarishwa na Shirika la AGPAHI na kupewa mbinu za kuwafanya waendelee kuwa imara”.  Pia, shirika la AGPAHI lilitoa mwongozo kwa wahudumu wa afya jinsi ya kuanzisha vikundi vya watoto  na vijana vinavyoundwa kwenye vituo vya kutolea huduma za matunzo na matibabu (CTC) husika vinavyohusisha watoto wenye umri wa kuanzia miaka 6-17.

Awali akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja Mawasiliano  wa Shirika la AGPAHI Jane Shuma alisema katika kusheherekea siku ya Ukimwi duniani kwa mkoa wa Tanga waliona washirikiane na serikali ya mkoa na kuandaa mjumuiko huo ambao utakuwa ni fursa ya kuwakutanisha watoto na vijana kuweza kupata elimu kwa njia ya michezo .

Alisema mjumuiko huo una watoto na vijana wapatao 200 waliotoka katika klabu za vituo vya Afya Ngamiani,Makorora,Pongwe na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo. Aliongeza kuwa lengo la mjumuiko huo ni kuwaweka pamoja watoto na vijana walio katika huduma za matunzo na matibabu kutoka vituo vya Afya Ngamiani,Makorora,Pongwe na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo ili kuweza kufahamiana,kujenga urafiki kati yao,kupata burudani,furaha na matumaini.

Vilevile lengo lingine ni kuwapa fursa watoto na vijana kushiriki kwenye michezo kwa pamoja,kupeana matumaini kwa njia ya michezo na kusaidia kuwahamasisha watoto na vijana wenzao kuendelea kubaki kwenye huduma za matunzo na matibabu kwenye maeneo mbalimbali wanapotokea.

“Lakini pia kupata elimu ya Afya ya ziada kwa pamoja kulingana na umri wao ….elimu zaidi kuhusu uwazi na ufuasi mzuri wa dawa na afya ya makuzi. Hata hivyo alisema dhamira yao ni kuona huduma hizo wanazozitoa kwa watoto na vijana zinaleta mtazamo chanya kwenye maisha yao na jamii inayowazunguka.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Moses Kisibo alisema kuwa wataendelea kushirikiana na wadau wote likiwemo Shirika la AGPAHI katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi ili kuhakikisha maambukizi yanashuka. Aliongeza kusema kuwa, Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga fungu kwa ajili ya watoto wanaoishi naVVU hivyo wataona namna nzuri ya kuweza kuwafikia walengwa.

Aidha pia aliitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa na kuwatenga vijana na watoto wanaoishi na maambukizi ya VVU badala yake tuwape ushirikiano ili waweze kutimiza ndoto zao.

Kuhusu vikundi vya watoto -- watoto wanapokuwa kwenye vikundi wananufaika na mambo mbalimbali ikiwemo kupata huduma za kisaikolojia,kupata elimu ya afya,lishe,stadi za maisha ikiwemo kupata marafiki na kupeana moyo na wenzao ambao wako katika hali sawa ya maambukizi. Hadi sasa, Shirika la AGPAHI  limeweza kuunda jumla ya vikundi vya watoto vipatavyo 11 katika mkoa wa Tanga vyenye watoto wapatao 1119.

Meneja Mawasiliano  wa Shirika la AGPAHI Jane Shuma akitoa hotuba yake katika maadhimisho hayo

 Mratibu wa Shirika la AGPAHI mkoa wa Tanga,Ben Nahayo akitoa neno kwenye maadhimisho hayo kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga,Mhandisi Zena Saidi kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga,Moses Kisibo
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt Selemani Msangi akizungumza 
 Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga,Moses Kisibo akizungumza
 Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Moses Kisibo kushoto akiwa na Mratibu wa Shirika la  AGPAHI mkoa wa Tanga,Ben Nahayo
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Zena Saidi akiagana na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Dkt Selemani Msangi
  Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Zena Saidi akiagana na watoto hao
  Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Mhandisi Zena Saidi akipiga picha na miongoni mwa watoto 
 Mmoja kati watoto akizungumza katika maadhimisho hayo
 Sehemu ya watoto wakifuatilia kwa umakini hotuba ya mgeni rasmi wakati wa maadhimisho hayo
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Saidi akiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya maadhimisho hayo kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Tanga,Moses Kisibo kushoto ni
Meneja Mawasiliano  wa Shirika la AGPAHI Jane Shuma
 Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga Mhandisi Zena Saidi ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo akiondoka kwenye viwanja vya shule ya sekondari Popatlal kushoto ni  Meneja Mawasiliano  wa Shirika la AGPAHI Jane Shuma
 michezo ikichukua nafasi yake kwa watoto
 Michezo ikiendelea kwa watoto hao
 sehemu ya watoto wakiwa wanashiriki kwenye michezo
Powered by Blogger.