Showing posts with label biashara. Show all posts
Showing posts with label biashara. Show all posts

SERIKALI HAITAVUMILIA WAFANYABIASHARA WA MKONGE WANAOFANYA UDANGANYIFU KATIKA MASOKO YA NJE

September 15, 2026 Add Comment

 




Na Oscar Assenga, TANGA

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara ,Dennis Londo amesema Serikali haitawavumilia wafanyabiashara wa mkonge wanaofanya udanganyifu katika masoko ya nje huku akiitaka Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) kuchukua hatua za haraka dhidi ya wafanyabiashara wanaodaiwa kuchukua fedha kutoka kwa wanunuzi wa nje bila kupeleka bidhaa walizoahidi, ikisema vitendo hivyo vinahatarisha uaminifu wa Tanzania katika masoko ya kimataifa.

Amesema tabia hiyo ya baadhi ya wafanyabiashara inachafua taswira ya nchi na kuwaweka katika mazingira magumu wafanyabiashara wengine wanaofuata taratibu na kufanya biashara kwa uaminifu.

Londo alitoa kauli hiyo jijini Tanga wakati wa kikao kazi kati ya TSB, Chama cha Wakulima wa Mkonge (SAT) na wafanyabiashara wa zao hilo.

Amesema Tanzania inaendesha uchumi wa soko huria, lakini uhuru huo haupaswi kutumiwa kama mwanya wa kufanya biashara kinyume cha sheria au kukiuka misingi ya uaminifu katika masoko ya kimataifa.




“Nimesikia hapa wafanyabiashara wakilalamika kwamba wakati mwingine wanataka kukamatwa kwa sababu kuna baadhi ya wafanyabiashara wamefanya udanganyifu kwenye soko. Mtu akifanya hivyo anashindwa kujua kwamba huku nje yeye anatambulika kama Tanzania na wala si kampuni yake,” amesema.

Amesema Serikali haiwezi kuvumilia vitendo vinavyoweza kuilazimisha nchi kutumia muda na rasilimali nyingi kurejesha uaminifu na taswira yake katika masoko ya kimataifa.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri ameiagiza TSB, kwa kushirikiana na wadau wengine wa zao hilo, kuchukua hatua mapema dhidi ya wafanyabiashara watakaobainika kufanya vitendo hivyo ili kulinda soko la mkonge na maslahi ya wafanyabiashara wanaofuata sheria.




“Pamoja na kwamba Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kibiashara, hatuwezi kuvumilia hilo,” amesema.
TSB: WACHUKUA FEDHA, HAWAPELEKI MIZIGO

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TSB, Saddy Kambona, amesema changamoto hiyo ni miongoni mwa mambo aliyokutana nayo katika ziara zake kwenye masoko ya mkonge duniani.

Amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakichukua fedha kutoka kwa wanunuzi wa nje, lakini baadaye kushindwa kupeleka mizigo, hali ambayo imeanza kuchafua jina la Tanzania katika masoko hayo.




“Kwenye ziara yangu nimekutana na malalamiko kwamba kuna wafanyabiashara wamechukua fedha halafu wameshindwa kupeleka mizigo. Watu wanafanya udanganyifu kwenye masoko ya nje,” amesema Kambona.

Amesema wafanyabiashara watakaobainika kufanya vitendo hivyo wanaweza kuchukuliwa hatua, ikiwamo kufutiwa usajili au leseni zao.

Kwa mujibu wa Kambona, hatua hizo zinalenga kulinda uaminifu wa biashara ya mkonge kutoka Tanzania na kuhakikisha wafanyabiashara wanaofanya biashara kwa kufuata taratibu hawaathiriwi na vitendo vya watu wachache.


UZALISHAJI MKONGE WAPANDA

Pamoja na changamoto hiyo, Kambona amesema uzalishaji wa mkonge nchini umeendelea kuongezeka, kutoka tani 36,000 mwaka 2020 hadi kufikia tani 75,000 mwaka 2025.

Amesema mwaka 2020 wakulima wakubwa walichangia asilimia 68 ya uzalishaji wa mkonge, huku wakulima wadogo wakichangia asilimia 32.

Hata hivyo, amesema hali hiyo imebadilika kutokana na juhudi za kuwawezesha wakulima wadogo, ambapo mwaka 2025 walichangia asilimia 55 ya uzalishaji, huku wakulima wakubwa wakichangia asilimia 45.


WAFANYABIASHARA: TUNABEBESHWA DHAMBI ZA WACHACHE

Wafanyabiashara wa mkonge walioshiriki kikao hicho wamesema vitendo vya wachache vimekuwa na madhara kwa wafanyabiashara waaminifu kutoka Tanzania, ambao wakati mwingine hujikuta wakihusishwa na tuhuma au kesi zinazotokana na biashara zisizofanyika kwa uaminifu.

Gasper Daudi wa Harvest Agritech Limited amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakisababisha matatizo katika masoko ya nje, hali inayowaathiri hata wale wanaofanya biashara kwa kufuata sheria.



Amesema ni muhimu Serikali na TSB kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha wafanyabiashara wanaokiuka taratibu wanachukuliwa hatua mapema.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Aja Tanzania Limited, Happiness Nyiti, ameomba Wizara ya Viwanda na Biashara kuweka mpango maalumu wa kurejesha uaminifu katika masoko ambayo tayari yameathiriwa na vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara.


“Vitendo hivi vinachafua taswira ya nchi yetu. Tunaomba Naibu Waziri atusaidie kuweka mpango mzuri wa kutengeneza taswira ya nchi yetu kwenye maeneo ambayo yanaonekana waziwazi kwamba imani ya wafanyabiashara wa zao hilo kutoka Tanzania imeshuka,” amesema Nyiti.



Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa Tanzania ina wafanyabiashara wengi wanaozingatia ubora na uaminifu, lakini juhudi zao zinaweza kuathiriwa na vitendo vya wachache.

Amesema kurejesha uaminifu katika masoko ya kimataifa kutasaidia kuongeza fursa za biashara na kuchochea zaidi uzalishaji wa mkonge nchini.

STENDI KANGE KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA

September 01, 2026 Add Comment

 



Na Oscar Assenga, TANGA

STENDI Kuu ya Mabasi Kange, iliyopo Jiji la Tanga, inatarajiwa kuanza kutumika kwa saa 24 ndani ya wiki moja, baada ya uamuzi huo kufikiwa na uongozi wa Mkoa, Jiji na wadau wa sekta ya usafirishaji.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jiji pamoja na wadau wa sekta ya usafirishaji kuhusu matumizi ya stendi hiyo.

Dk. Burian alisema utekelezaji wa mpango huo utaanza ndani ya wiki moja na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 8, mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho mbalimbali katika eneo hilo ili kuwezesha shughuli za usafirishaji kufanyika kwa ufanisi.

Alisema mabasi yatakuwa yakifika na kuondoka Kange, huku usafiri wa mabasi madogo, daladala na bajaji ukitumika kuwaunganisha abiria na maeneo mbalimbali ya Jiji.

“Wenye mabasi wapo tayari na wameonyesha nia ya kuanza kutumia stendi hii. Pia kutakuwa na mabasi madogo kwa ajili ya kupeleka abiria kutoka mjini kwenda Kange na kinyume chake,” alisema.

Alisema Jiji limetenga eneo maalumu kwa ajili ya maegesho ya magari madogo ya abiria na magari binafsi, hatua ambayo itasaidia kurahisisha huduma za usafiri katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, mpango huo pia unalenga kuifanya Kange kuwa eneo muhimu la shughuli za kiuchumi, badala ya kuwa kituo cha mabasi pekee.

Alisema abiria watakaoshushwa upande mmoja wa eneo hilo watapita katikati ya kitega uchumi kilichopo Kange na hivyo kupata fursa ya kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na wafanyabiashara na wawekezaji.

“Hatuitazami Kange kama eneo la abiria pekee. Tunataka eneo hili liwe kitega uchumi na tutaendelea kuwavutia wawekezaji ili shughuli mbalimbali za kiuchumi zifanyike hapa,” alisema.

Alisema eneo hilo tayari lina taasisi na huduma mbalimbali, ikiwamo chuo cha utalii, ofisi za Serikali na baadhi ya wafanyabiashara wenye migahawa, huku jitihada zikiendelea kuwavutia wawekezaji zaidi.

Dk. Burian alisema Tanga ni lango muhimu la kiuchumi kwa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo uwekezaji katika maeneo kama Kange ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Jiji.

Alisema eneo hilo pia lina nafasi ya kutumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwamo harusi, mikutano na shughuli nyingine, huku Jiji na taasisi za Serikali zikitakiwa kutumia jengo hilo kwa shughuli zao na kulipia huduma hizo.
 
MABORESHO

Dk. Burian alisema kabla ya kuanza matumizi kamili ya stendi hiyo, maboresho kadhaa yatafanyika, ikiwamo kufanya leveling ya eneo la maegesho, kupaka rangi, kutenga eneo la ibada na kukamilisha uwekaji wa viti katika eneo la abiria.

Aidha, alisema eneo limetengwa kwa ajili ya Jeshi la Polisi kuweka vifaa na huduma zinazohitajika kwa ajili ya kuimarisha usalama.

Alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nalo litakuwa na gari katika eneo hilo ili kukabiliana na dharura na kuimarisha usalama, akiwashukuru wananchi kwa juhudi za kuhakikisha mazingira ya stendi yanakuwa salama.

LATRA YAWEKA MSIMAMO

Awali, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Tanga, alisema mabasi yanayofanya safari za kimataifa yanapaswa kuzingatia utaratibu wa kutumia vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuhudumia abiria.

Alitoa mfano wa basi linalotoka Mombasa nchini Kenya kwenda Dar es Salaam, akisema Tanga ndiyo kituo cha kwanza linapoingia nchini Tanzania.

Alisema kwa utaratibu huo, basi hilo linapaswa kuingia katika stendi ya Tanga kwa ajili ya kuhudumia abiria, huku vituo vingine vikifuata kulingana na mahitaji ya wasafiri.

Alisema uwezo wa stendi ya mkoa unapaswa kutumika ipasavyo, ikiwamo kuwezesha magari yanayofanya safari za ndani na nje ya nchi kufika kwa ajili ya ukaguzi na huduma nyingine zinazohitajika.

Alisema magari yanayofanya safari za Tanzania na nje ya nchi yataendelea kusimamiwa kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa na mamlaka husika.

PROF. SHEMDOE AELEKEZA WAFANYABIASHA 30 SOKO LA NDIZI MABIBO KUREJESHWA SOKONI

PROF. SHEMDOE AELEKEZA WAFANYABIASHA 30 SOKO LA NDIZI MABIBO KUREJESHWA SOKONI

September 01, 2026 Add Comment






Na: OWM – TAMISEMI, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameelekeza waliokuwa wafanyabiashara 30 wa soko la ndizi Mabibo (Mahakama ya Ndizi) kurejea kufanya biashara kwa udhamini wa maandishi kutoka ofisi za Serikali za Mitaa.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Agosti 31, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo ya OWM- TAMISEMI jijini Dar es Salaam, mara baada ya kupokea taarifa ya timu ya ufuatiliaji wa malalamiko ya wafanyabiashara hao wa soko la ndizi Mabibo, wakati wa kikao kazi chake na wafanyabiashara hao.

Aidha, Prof. Shemdoe ameilekeza Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kufanya tathmini ya mali ya Bw. Frego Njovu aliyewasilisha madai ya kuomba kurejeshewa fedha alizotumia kukarabati choo kilichopo sokoni hapo ambacho alikuwa akikisimamia.

Katika kuhakikisha haki inatendeka, Prof. Shemdoe ameelekeza bidhaa za mfanyabiashara Bw. Enock Kimwayeya aliyekuwa Mwenyekiti wa Wafanyabiashara waliowasilisha malalamiko kwa Prof. Shemdoe, arejeshewe bidhaa zake alizoziacha kwenye kibanda cha biashara pindi alipoondolewa, kwani taarifa ya timu ya ufuatiliaji imeainisha kuwa Halmashauri imekiri kwamba bidhaa za mfanyabiashara huyo zipo.

Ili kuimarisha usimamizi wa soko, Prof. Shemdoe amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kumpeleka meneja wa soko mwingine kulisimamia soko hilo na aliyepo kupangiwa majukumu mengine.

Maelekezo hayo ya Prof. Shemdoe yametokana na maafikiano baina ya pande zote katika kikao kazi cha Waziri huyo na walalamikaji (wafanyabiashara) na walalamikiwa ambao ni Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

Malalamiko ya wafanyabiashara hao 30 yaliwasilishwa kwa Prof. Shemdoe kupitia andiko lao la tarehe 15/01/2026 lililohusu Sakata la soko la Ndizi Mabibo wakilalamikia kupigwa marufuku kuingia sokoni, kutaifishwa na kuuzwa kwa maeneo yao ya biashara, aidha Manispaa ya Ubungo iliwaondoka sokoni wafanyabiashara hao kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kutoitambua manispaa hiyo kama msimamizi wa soko.

NMB: ELIMU, UJUZI NGUZO MUHIMU YA UCHUMI WA KIPATO CHA JUU

August 25, 2026 Add Comment

Na Oscar Assenga, TANGA

BENKI ya NMB imesema Tanzania haiwezi kufikia uchumi wa kipato cha juu bila kuwekeza katika elimu, ujuzi wa vitendo na ubunifu unaowawezesha Watanzania kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili nchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja Mwandamizi wa Maabara ya Ubunifu ya NMB, Maria Mwamyalla, wakati akitoa salamu za wadhamini kwa niaba ya wadhamini wote katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika mkoani Tanga.

Mwamyalla alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaendana na mkakati wa NMB wa kuwekeza katika teknolojia, ubunifu, vijana na ujumuishaji wa kifedha.

Alisema kupitia Agenda 2030, benki hiyo imeweka teknolojia, ubunifu, uwekezaji kwa vijana na ujumuishaji wa kifedha kuwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa ukuaji.

“Mwelekeo huo unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa ushindani unaotumia maarifa, ujuzi na teknolojia,” alisema.

Mwamyalla alisema teknolojia pekee haiwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila kuwapo kwa watu wenye maarifa na ujuzi wa kuitumia ipasavyo.

NMB YATOA BILIONI 2 KUSOMESHA VIJANA

Alisema kupitia NMB Foundation, benki hiyo imeendelea kuwekeza katika elimu na malezi ya uongozi kwa vijana, hususan wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi.

Alisema kupitia programu ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni mbili tangu mwaka 2022, kwa ajili ya kuwafadhili wanafunzi 121 katika vyuo vikuu 11 nchini.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, wanafunzi hao wamekuwa wakisaidiwa mahitaji mbalimbali yakiwamo ada, malazi na vitendea kazi kama kompyuta mpakato.

Alisema wanafunzi 21 tayari wameingia katika soko la ajira, huku wengine 42 wakitarajiwa kuhitimu mwaka huu.


“Tunatarajia kufungua dirisha la tatu la programu hii mwezi Septemba mwaka huu,” alisema.

WATAKA VIJANA WAPEWE UJUZI

Aidha, Mwamyalla alisema NMB inaendelea kutekeleza programu ya SEP kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Save the Children pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Alisema programu hiyo inalenga kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kuwapatia vijana elimu ya vitendo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na vyuo vya VETA.

NMB YAWEKEZA BILIONI 232 TEKNOLOJIA

Katika eneo la teknolojia na ubunifu, Mwamyalla alisema NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni 232, huku sehemu kubwa ya suluhisho za kiteknolojia zikitengenezwa na wataalamu wazawa.

Alisema uwekezaji huo unalenga kujenga utaalamu wa Watanzania, kuimarisha usalama wa mifumo pamoja na kupunguza muda wa kupeleka bidhaa za kidijitali sokoni.

Alitaja miongoni mwa suluhisho hizo kuwa ni huduma ya NMB Mkononi, inayowawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki kupitia simu zao za mkononi, ikiwamo kutuma na kupokea malipo ya kielektroniki.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, huduma hizo zimechangia kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa zaidi ya wateja milioni 10 wa NMB.

Alisema kupitia programu ya PesaTek, iliyoanzishwa mwaka 2022, benki hiyo imezindua Innovation Sandbox na kuendelea kuwawezesha vijana pamoja na wabunifu katika sekta ya teknolojia kupima na kuendeleza suluhisho zao.

Mwamyalla alisema NMB itaendelea kushirikiana na Serikali na taasisi za elimu kuhakikisha elimu, ujuzi na ubunifu vinageuzwa kuwa suluhisho zinazochochea biashara na kuchangia maendeleo ya Taifa.


SERIKALI YAWEKA MKAKATI WA KUPUNGUZA MUDA WA MELI ZA MAFUTA BANDARINI

August 15, 2026 Add Comment




DAR ES SALAAM. 


Serikali imeweka mkakati wa kupunguza muda ambao meli za mafuta hutumia bandarini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi katika upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za mafuta nchini.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, anayeshughulikia Mafuta na Gesi Dkt. James Mataragio, amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya mafuta katika eneo la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), Leo Augosti 14,2026 Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mataragio amesema Serikali inalenga kuhakikisha meli zinazowasili nchini zinapata huduma kwa wakati, zinashusha mafuta kwa ufanisi na kuondoka bandarini bila ucheleweshaji usio wa lazima.

“Ni matarajio ya Serikali kuona meli zikifika, zinashusha mafuta na kuondoka. Kila taasisi inapaswa kufahamu jukumu lake na kujipanga ipasavyo,” amesema.


Ameeleza kuwa moja ya changamoto zinazochangia meli kukaa bandarini kwa muda mrefu ni kasi ndogo ya upokeaji na uondoshwaji wa mafuta katika baadhi ya maghala binafsi. Hali hiyo husababisha meli kusubiri na kuongeza msongamano bandarini.

Kutokana na changamoto hiyo, Dkt. Mataragio ameutaka Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuimarisha usimamizi wa wamiliki wa maghala binafsi na kuhakikisha wanaweka miundombinu inayokidhi mahitaji ya uendeshaji.


Amesema wamiliki wa maghala wanapaswa kuboresha pampu na vifaa vingine vinavyotumika kupokea mafuta, hasa vinapokuwa vimechakaa au havina uwezo unaohitajika.



Kwa mujibu wa Dkt. Mataragio, ucheleweshaji wa meli bandarini huongeza gharama za uendeshaji, zikiwemo gharama za meli kusubiri, ambazo hatimaye zinaweza kuathiri bei ya mafuta kwa mwananchi.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Simon, amesema taasisi hiyo itakutana na wadau muhimu katika sekta ya mafuta, wakiwemo kampuni za uuzaji wa mafuta (OMCs) na TPA, kwa ajili ya kupitia na kuboresha Mwongozo wa Taratibu za Uendeshaji (Standard Operating Procedure Manual).


Amesema mapitio hayo yanalenga kuweka wazi majukumu, muda wa utekelezaji na uwajibikaji wa kila mdau katika mchakato wa upokeaji na uhamishaji wa mafuta.


Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha uratibu kati ya meli na maghala ya kupokea mafuta, kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kudhibiti gharama zinazotokana na ucheleweshaji.


Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio aliambatana na Kamishna wa Mafuta kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Goodluck Shirima; Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Simon; Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus Abed; pamoja, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Mashariki, Mhandisi Lorivii Long’idu na wataalam kutoka Wizara ya Nishati.

MBARAWA AFUNGUA MILANGO YA AJIRA ZA BAHARINI KWA VIJANA WASIOSOMA SAYANSI

Kajunason June 25, 2026 Add Comment

Uchumi wa Bluu Kunufaika na Elimu ya Ubaharia

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kukiunga mkono Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) katika jitihada zake za kuanzisha kozi ya awali ya ubaharia itakayowawezesha vijana wengi zaidi wa Kitanzania kupata elimu ya sekta hiyo na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa bluu.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la DMI katika kilele cha Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma, ambapo alieleza kuwa kozi hiyo ni suluhisho kwa vijana wengi wenye ndoto za kuwa mabaharia lakini ambao hawakupata nafasi ya kusoma masomo ya sayansi yanayohitajika kujiunga na taaluma hiyo.

Alisema DMI imebuni mpango huo mahsusi ili kuwapa vijana hao fursa ya kupata msingi wa masomo muhimu yatakayowawezesha kuendelea na mafunzo ya ubaharia na hatimaye kuingia katika soko la ajira la sekta ya usafiri wa majini.

“DMI inafanya kazi kubwa ya kuangalia namna ya kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa za elimu ya ubaharia. Kozi hii ya awali itawasaidia wale ambao hawakusoma masomo ya sayansi kupata msingi unaohitajika na hatimaye kujiunga na mafunzo ya ubaharia,” alisema Profesa Mbarawa.
Alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya mabaharia wenye ujuzi na sifa zinazotambulika kitaifa na kimataifa, huku ikilenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika ajira za sekta ya bahari na usafiri wa majini duniani.

Waziri huyo pia alimpongeza Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, kwa ubunifu na juhudi zake za kuendeleza programu mbalimbali za mafunzo zinazowawezesha mabaharia wa Tanzania kufikia viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika sekta ya usafiri wa majini.

“Tunakipongeza DMI kwa juhudi zake za kubuni na kuendeleza mafunzo yanayowawezesha mabaharia wetu kuwa na sifa zinazokubalika kimataifa. Mabaharia wanazunguka dunia nzima, hivyo ni lazima waandaliwe kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sekta ya kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho katika kuzalisha wataalamu wenye tija na ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Profesa Gurumo alisema kutokana na asili ya kazi ya ubaharia inayowafanya mabaharia kufanya kazi na kusafiri katika mataifa mbalimbali duniani, ni muhimu kwao kupata elimu na stadi zinazotambulika kimataifa ili waweze kushindana kwa ufanisi katika soko la ajira la dunia.

Aliongeza kuwa DMI itaendelea kupanua na kuboresha mafunzo ya bahari ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata elimu na ujuzi unaohitajika kwa taifa kunufaika na fursa zilizopo katika uchumi wa bluu na sekta ya usafiri wa majini.

Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya bahari na usafiri wa majini kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa mabaharia katika kukuza biashara, uchumi na maendeleo ya jamii duniani.