Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

BALOZI DKT.BATILDA MAZINGIRA DAY YAZINDULIWA,WANAOTUPA TAKA OVYO WAPEWA ONYO.

October 03, 2026 Add Comment

 


Na Oscar Assenga,TANGA

MKUU wa Mkoa wa Tanga amezindua zoezi la Msaragambo Maalumu wa kila Mwei katika Mkoa huo  maarufu Balozi Dk. Batilda Mazingira Day,unaolenga kuhamasisha wananchi kushiriki katika usafi na utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi za Mitaa na Vijiji huku watakaobainika kutupa taka ovyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza mara baada ya kushiriki kufanya usafi,Dkt Batilda alisema kwamba wameunda kikosi  kazi maalumu cha vijana 50 kitakachohusika na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira, kubaini maeneo yenye changamoto ya uchafu na kuchukua hatua kwa watakaobainika kutupa taka ovyo.

Kikosi hicho pia kitatekeleza sheria ndogo za mazingira zilizopo chini ya Halmashauri, ambapo watakaokiuka sheria hizo watakabiliwa na faini ya kuanzia Sh50,000.

Alisema kwamba kikosi hicho kitakuwa na jukumu la kukusanya taarifa na kubaini maeneo yanayohitaji usafi, kisha taarifa hizo kuwasilishwa kwenye Halmashauri husika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua, ikiwamo kupeleka magari ya kuzolea taka.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwamba watakuwa na kamati ya ukaguzi itakayohusika na kubaini changamoto, kutoa elimu na maelekezo yatatolewa na pale sheria itakapokiukwa na wahusika wakionekana kuendelea kukaidi  hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa miongozo. 

"Niwaambie kwamba lazima tuhakikishe tunatunza mazingira na usafi ili baadaye tusije tukalaumiana na faini imeandikwa kwenye sheria ndogo za mazingira na Halmashauri  faini ya chini ni Sh50,000," Alisema"Alisema RC huyo

Alisema kikosi hicho kimekaguliwa na kutambuliwa rasmi na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambalo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga litatoa ithibati na ruksa kwa kikosi hicho kushughulikia watakaokiuka sheria za mazingira.

Dk. Burian alisema faini zitakazokusanywa zitaingizwa katika mfumo rasmi wa ukusanyaji mapato, huku akisisitiza kuwa kikosi hicho hakitaruhusiwa kutumia nguvu wala kupokea rushwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.

"Timu hii haitakuwa juu ya sheria, watakula kiapo, hawatapokea rushwa wala kutumia nguvu kukamata na tozo zote zitakazokusanywa kisheria kupitia POS-Mashine na risiti zitatolewa. Tunataka kuhakikisha kwamba kosa linathibitishwa na hatua zinachukuliwa lakini tambueni kwamba hatukusudii  kutoza faini kwa wananchi, tunakusudia kuboresha mazingira yetu," alisema.

Aliwataka wananchi kushiriki kwa hiari katika zoezi hilo, huku akizitaka Halmashauri zote 11 zilizopo mkoani Tanga, chini ya usimamizi wa Wakuu wa Wilaya, kuhakikisha zinatekeleza Msaragambo huo ambao umepewa jina la Balozi Dk. Batilda Mazingira Day, ukiwa na kaulimbiu maalumu ya utunzaji wa mazingira.

Dk. Burian alisema Mkoa wa Tanga unachangia Sh bilioni sita kwa mwezi katika pato la Taifa na kushika nafasi ya sita kati ya mikoa yote nchini, akisisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha mazingira yanakuwa safi kuanzia ngazi ya kaya.

Akimwakilisha Mkurugenzi wa NEMC Kanda ya Kaskazini, Meneja wa NEMC Kanda ya Bagamoyo, Ndimbumi Mboneke, alisema kisheria kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mazingira yanayomzunguka yanakuwa safi na salama wakati wote.

Alisema wananchi pia wana wajibu wa kutoa taarifa katika mamlaka husika pale wanapoona uharibifu wa mazingira.

"Sheria ya mazingira imetoa haki kwa kila Mtanzania kuishi katika mazingira safi na salama, lakini pia imetoa wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na salama na imempa wajibu wa kutoa taarifa anapoona kuna uharibifu wowote. Hivyo tunatoa wito kwa kila mmoja kuiga mfano huu," alisema Mboneke.

Katika tukio hilo, NEMC ilimkabidhi cheti maalumu cha shukrani Mwananchi wa Mkoa wa Tanga, Mohamed Hilal, kwa kutambua mchango wake katika kuhamasisha na kushiriki katika shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Mustafa Seleboss, alisema Halmashauri hiyo iko tayari kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa, ikiwamo kuondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga waliopanga biashara zao katikati ya stendi ya daladala.

Aliseam zoezi huilo wamelipokea huku wakihaidi kuendelea kulienzi Jina lake kwa kuhakikisha kila tarehe moja ya kila mwezi wanafanya  usafi maalumu na kuanzia sasa wataviondoa vibanda vyote ambapo vimekuwa vimekuwa na uchafu mwingi. 

Mwisho.

INNOIP YAFUNGUA FURSA MPYA KWA WABUNIFU

August 22, 2026 Add Comment

 



Na OSCAR ASSENGA, Tanga


SERIKALI imezindua programu ya InnoIP Tanzania, inayolenga kuwasaidia zaidi ya wabunifu 5,000 nchini kulinda kazi zao kisheria, kuzigeuza kuwa fursa za biashara na kuchochea uundaji wa ajira.


Programu hiyo pia inalenga kukabiliana na changamoto ya wizi wa mawazo na ubunifu inayowakabili wabunifu wengi, hasa wanaoweka wazi mawazo yao kabla ya kuchukua hatua za kuyakinga kisheria.


Uzinduzi huo umefanywa Agosti 22, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.




Akizungumza na mamia ya wadau wa sekta ya sayansi na ubunifu, Dkt. Batilda alisema Tanzania inapaswa kuhakikisha ubunifu wa ndani unalindwa kisheria na kuunganishwa na masoko makubwa ili kuongeza thamani ya bidhaa na teknolojia zinazozalishwa na Watanzania.

Alisema baadhi ya wabunifu hupoteza fursa kwa kuweka wazi mawazo yao mapema bila kuwa na makubaliano yanayoeleweka kuhusu umiliki wa ubunifu huo.


Kwa mujibu wa Dkt. Batilda, hali hiyo inaweza kumsababishia mbunifu kukosa ulinzi wa kisheria wa kazi yake na kuwafanya wawekezaji kusita kuwekeza katika kampuni changa ambazo hazina uthibitisho wa umiliki wa haki zao za miliki bunifu.


FURSA WOMEN KULENGA WANAWAKE


Sambamba na uzinduzi wa InnoIP Tanzania, Mkuu wa Mkoa alitangaza kuanza kwa programu ya Fursa Women, inayolenga kuwawezesha wanawake wajasiriamali kutumia teknolojia na mifumo ya kidijitali kukuza biashara zao.


Dkt. Batilda alisema matumizi ya teknolojia yanaweza kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuwawezesha wafanyabiashara kuwafikia wateja wengi kwa haraka zaidi.

Aidha, alizitaka vyuo vikuu na taasisi za utafiti kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinageuzwa kuwa bidhaa na suluhisho halisi zinazowanufaisha wananchi, badala ya kuishia kwenye makabrasha na makabati.



Pia aliwataka wawekezaji na taasisi za fedha kushirikiana na wabunifu wa Kitanzania kwa kununua bidhaa zao, kuwekeza katika teknolojia zao na kuwawezesha kupata mitaji kwa ajili ya kukuza biashara.


Akizungumzia ushiriki wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mkurugenzi wa Miliki, Loy Mhando, aliyemwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu, alisema InnoIP Tanzania haimaanishi kuwa kila ubunifu lazima upatiwe hataza (Patent).


Alisema programu hiyo itawasaidia wabunifu kutambua aina sahihi ya ulinzi wa kisheria kulingana na aina ya ubunifu wao, ikiwemo hataza, alama za biashara, hakimiliki na siri za biashara.


Alifafanua kuwa InnoIP inasimamiwa na BRELA na kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), kupitia atamizi za Dar Teknohama Business Incubator (DTBi) na Buni Innovation Hub.


Programu hiyo inalenga kuwasaidia kampuni changa, watafiti, wanafunzi wa vyuo vikuu, biashara ndogo na za kati pamoja na wajasiriamali kutambua, kulinda na kubiasharisha haki zao za miliki bunifu.


Mhando alisema katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji, programu hiyo inalenga kufanya uchambuzi wa kina wa mahitaji ya wabunifu 120 wa awali, ambao watasaidiwa kisheria na kifedha kulinda kazi zao na baadaye kuunganishwa na wawekezaji.



Alisema uteuzi wa wabunifu hao utazingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo umuhimu wa ubunifu husika kwa jamii pamoja na uwezo wake wa kuzalisha faida.


Kwa mujibu wa Mhando, programu hiyo itawasaidia wabunifu kupitia hatua saba: utambuzi na uhamasishaji; mafunzo na warsha za vitendo; uchambuzi wa mahitaji; maandalizi ya ramani ya ulinzi; uwasilishaji wa maombi ya usajili; ubiasharishaji kwa kuwaunganisha na wawekezaji; pamoja na ufuatiliaji endelevu.


Aliwataka wabunifu na kampuni changa kutumia fursa hiyo mapema badala ya kusubiri hadi mgogoro wa umiliki unapotokea, mawazo yao yanaponakiliwa au mwekezaji anapohitaji uthibitisho wa kisheria kuhusu umiliki wa biashara.

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, alisema miliki bunifu si suala la kisheria pekee, bali ni rasilimali muhimu ya kiuchumi inayoweza kuwa msingi wa kuvutia uwekezaji, utoaji wa leseni kwa viwanda vingine, uhamishaji wa teknolojia na ujenzi wa biashara zinazoweza kukua hadi masoko ya kimataifa.


“Changamoto yetu kuu kwa sasa nchini si ukosefu wa mawazo; ni kuhakikisha kuwa mawazo mazuri ya vijana, watafiti na wabunifu wetu yanalindwa kisheria, yanaendelezwa na hatimaye yanafikishwa sokoni,” alisema Dkt. Nungu.


Alisema mafanikio ya InnoIP hayatapimwa kwa idadi ya watu watakaohudhuria mafunzo na semina pekee, bali kwa matokeo, ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya ubunifu unaolindwa kisheria, teknolojia mpya kuingia sokoni, biashara kukua, uwekezaji kuvutiwa na ajira mpya kuzalishwa.



Akizungumzia programu ya Fursa Women, Dkt. Nungu aliishukuru Airtel Tanzania kwa kushirikiana na COSTECH katika kufadhili programu hiyo.


Alisema ushirikiano huo unaonesha umuhimu wa sekta ya umma na binafsi kufanya kazi kwa pamoja katika kujenga jamii yenye ujuzi wa kidijitali.


Alifafanua kuwa kupitia Fursa Women, wanawake watajengewa uelewa kuhusu matumizi sahihi na salama ya mifumo ya kidijitali katika kutangaza bidhaa, kuwafikia wateja, kufanya na kupokea malipo mtandaoni pamoja na kuhifadhi kumbukumbu za biashara zao.


Dkt. Nungu alitoa wito kwa wawekezaji na sekta binafsi kutambua kuwa ubunifu wa Kitanzania ni fursa ya uwekezaji ambayo bado haijatumika kikamilifu.


Aliwaalika kushirikiana na Serikali katika kujaribu, kununua na kupanua matumizi ya teknolojia pamoja na suluhisho mbalimbali zinazozalishwa na Watanzania.


Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanatarajiwa kufungwa Jumatatu na Waziri Mkuu, Mhe. Mwigulu Nchemba.

BALOZI SALUM AZITAKA FCC, TBS NA WMA KUPAMBANA NA BIDHAA BANDIA NA DUNI

August 21, 2026 Add Comment
Mameneja wa Kanda na Mikoa wa Taasisi za Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) wameagizwa kuhakikisha hakuna bidhaa bandia na duni katika maeneo yao wanayoyasimamia kiutendaji.

RC BURIAN ATOA MWELEKEO KWA WANANCHI 66 WA MSAKANGOTO

August 21, 2026 Add Comment



Na Oscar Assenga, MUHEZA

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amewataka wananchi 66 wa Kitongoji cha Bago Maisha Plus ,Kijiji cha Msakangoto, Kata ya Kigombe wilayani Muheza, kuondoka katika eneo walilokuwa wakiishi na kuhamia eneo jipya lililotengwa na Serikali ya Kijiji, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuwasaidia katika kipindi cha mpito.

Wananchi hao wamekumbwa na changamoto hiyo baada ya nyumba zao kubomolewa kufuatia utekelezaji wa amri ya mahakama iliyotokana na mgogoro wa umiliki wa eneo hilo.

Balozi Burian alitoa kauli hiyo leo alipofanya ziara katika eneo hilo na kukutana na wananchi hao, ambapo alisema Serikali haina mamlaka ya kuzuia utekelezaji wa amri ya mahakama.

Alisema baada ya kubaini kuwa eneo hilo lilikuwa ndani ya hati ya umiliki ya mwekezaji wa Mashamba ya Mkonge ambaye tayari alikuwa amefungua kesi mahakamani na kupata amri ya kuwaondoa wananchi, Serikali ililazimika kuheshimu uamuzi huo.

“Serikali haiwezi kupingana na sheria ya mahakama. Aliyekuja kubomoa alikuwa anatekeleza maelekezo ya mahakama. Hata hivyo, sisi kama Serikali tuliona ni lazima tuzungumze na wananchi na mwekezaji ili kutafuta suluhisho la kibinadamu,” alisema.

Alisema awali wananchi hao walipelekwa katika eneo hilo na Serikali ya Kijiji, huku wakiwa na vielelezo vilivyoonyesha kuwa waliruhusiwa kuishi katika eneo hilo, jambo lililopelekea Serikali ya Mkoa kuingilia kati baada ya mgogoro kujitokeza.

Balozi Burian alisema Serikali ya Mkoa imefanya mazungumzo na mwekezaji kupitia Wizara inayohusika na Uwekezaji, hatua iliyosaidia kuwezesha kupatikana kwa eneo jingine kwa ajili ya kuwahamishia wananchi hao.

Alisema eneo lililotengwa awali kwa ajili ya makazi mapya lilibainika kuwa halifai kutokana na kuwa na maji, hivyo Serikali ililazimika kutafuta eneo jingine.

“Wawakilishi wenu wamekuja ofisini kwangu mara tatu. Hatua ya kwanza ilikuwa kwenda kuzungumza na mwekezaji, hatua ya pili mwekezaji akakubali kutoa Sh200,000 na hatua nyingine ni kuhakikisha hakuna mtu anayewasumbua wakati taratibu za kuwahamisha zikikamilishwa,” alisema.


Balozi Burian alisema maturubai  ambayo  wanayatumia kwa  muda wakati wakijiandaa kujenga makazi yao mapya.

“Kesho asubuhi tutahamisha maturubai hayo kwenda kwenye eneo ambalo mtaenda kuhamia. Mtayatumia kwa mwezi mmoja wakati mkiendelea kujipanga kujenga makazi yenu,” alisema.

Alisema Serikali itaendelea kutafuta wadau na wasamaria wema watakaoweza kusaidia katika ujenzi wa makazi mapya kwa wananchi hao.

Aidha, aliwataka wananchi hao kutokata tamaa na kuacha kuchukua hatua zinazoweza kuwaingiza katika mgogoro mwingine wa kisheria.

“Ndugu zangu, mchakato mzima nimewaeleza. Sina mamlaka ya juu zaidi ya hapa. Kila mhimili una kiwango chake cha kushughulikia jambo. Likishafika mahakamani, Serikali haiingilii tena,” alisema.

Alisema wananchi wanapaswa kuanza maisha katika eneo jipya huku wakiamini kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Ally Mohamed, mkazi wa Maisha Plus, alisema suala la fidia limekuwa miongoni mwa changamoto kubwa zilizowafanya kuwa na wasiwasi kuhusu kuhamia eneo jipya.

Alisema baadhi yao walitumia mafao waliyopata kutoka Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kujenga nyumba zao, hivyo kubomolewa kwa nyumba hizo kumewasababishia hasara kubwa.

“Baadhi yetu tulitumia mafao yetu ya NSSF kujenga nyumba. Sasa nyumba zimebomolewa na tunajiuliza tutaanzaje maisha upya,” alisema.

Akijibu suala hilo, Balozi Burian alisema wananchi waliokuwa na madai ya fidia wakati shauri likiendelea walikuwa na nafasi ya kuyawasilisha mahakamani.

Hata hivyo, alisema Serikali ya Mkoa imeendelea kufanya mazungumzo na mwekezaji kwa lengo la kutafuta namna ya kuwasaidia wananchi hao katika kipindi hiki cha mpito.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kigombe (CCM) Shahongwe Mgandi aliishukuru Serikali ya Mkoa kwa hatua iliyochukua, akisema viongozi wa kata watahakikisha wananchi hao wanapata usalama na huduma muhimu katika eneo jipya.

Alisema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeanza maandalizi ya kufikisha huduma ya umeme katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kusimika nguzo.

Alisema pia maeneo ambayo wananchi hao watahamia yatatambuliwa kisheria na kutambuliwa kama kitongoji, huku Serikali ikiendelea kuboresha barabara na huduma nyingine muhimu.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Maisha Plus alishukuru Serikali ya Mkoa kwa hatua hiyo na kuiomba iruhusu wananchi hao, inapowezekana, kuhamisha baadhi ya miti waliyokwishaipanda katika eneo la awali ili kuitumia katika mazingira ya makazi mapya.

Hatua hiyo, alisema, itawasaidia wananchi hao kuanza maisha mapya huku wakitunza mazingira katika eneo watakalohamia.

TRA KARIAKOO NA MABALOZI JENGO WAIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA KUTOA ELIMU YA KODI KWA WALIPAKODI

August 21, 2026 Add Comment
Kariakoo, 20 Agosti, 2026

‎ Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Kariakoo imeimarisha ushirikiano na uongozi wa Mabalozi Jengo kwa lengo la kuwafikia walipakodi na wadau mbalimbali kwa ufanisi zaidi.

AIRTEL AFRICA YAANDIKA HISTORIA KWA KUZINDUA INTANETI YA SATELAITI KWA SIMU DRC

August 21, 2026 Add Comment

Kinshasa, 17 Agosti 2026: Airtel Africa imeandika historia baada ya kuwa kampuni ya kwanza ya mawasiliano barani Afrika kuzindua kibiashara intaneti ya satelaiti kwa simu nchini Jamhuriya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ikifungua ukurasa mpya katika upatikanaji wa mawasilianokatika maeneo yasiyofikiwa na minara ya kawaida ya simu.