RC DKT BATILDA -MIKOKO NI UHAI WA PWANI ISIHARIBIWE

July 28, 2026



Na Oscar Assenga,TANGA

 Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, amewataka wananchi kuacha ukataji holela wa mikoko na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wake, akisema misitu hiyo ni muhimu kwa kulinda fukwe, kuhifadhi viumbe wa majini na kuimarisha uchumi wa jamii za pwani.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian, ameitaka jamii kuachana na tabia ya ukataji holela wa miti ya mikoko katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi, akionya kuwa endapo vitendo hivyo vitaendelea vinaweza kuhatarisha makazi ya viumbe wa majini, maisha ya wananchi wanaotegemea rasilimali za bahari pamoja na usalama wa fukwe.



Dkt. Burian alitoa kauli hiyo Juni 28 wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Uhifadhi wa Ikolojia ya Mikoko yaliyofanyika katika eneo la Donge Mnyanjani, Jijini Tanga. 

Alisema Mkoa wa Tanga umebarikiwa kuwa na ukanda mpana wa pwani pamoja na misitu ya mikoko yenye umuhimu mkubwa wa kiikolojia na kiuchumi katika wilaya za Mkinga, Pangani, Muheza na Jiji la Tanga.

Alieleza kuwa mikoko ni ngao muhimu inayolinda mwambao wa bahari dhidi ya mmomonyoko wa ardhi, huku pia ikiwa mazalia ya samaki na makazi ya viumbe wengine wa majini wanaochangia kuimarisha sekta ya uvuvi na kipato cha wananchi wa maeneo ya pwani.


"Mikoko ya Tanga si tu inalinda mwambao wa bahari dhidi ya mmomonyoko wa ardhi, bali ni chanzo muhimu cha maisha ya wavuvi na jamii nyingi za pwani. Kwa miaka ya hivi karibuni Mkoa wa Tanga umeendelea kuwa mfano wa uhifadhi wa mazingira unaokwenda sambamba na maendeleo ya utalii wa ikolojia," alisema Dkt. Batilda Burian.

Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza umuhimu wa kurejesha maeneo yaliyoharibiwa kwa kupanda mikoko mipya ili kurejesha mazingira katika hali yake ya awali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, aliwataka viongozi wa serikali za mitaa, vikundi vya wavuvi, wanawake, vijana, wanafunzi pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo Scouts kuendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa mikoko huku wakizingatia sheria na taratibu za usimamizi wa misitu.


"Tunapanda mikoko leo, lakini bado tunakabiliwa na changamoto kubwa ya uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na mifuko ya plastiki, chupa na taka nyingine zinazotupwa ovyo kwenye fukwe zetu. Ni wajibu wetu kuendelea kutoa elimu kwa watoto na vijana kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mikoko, kwa sababu tunapohifadhi mikoko tunalinda maisha yetu, chakula chetu, uchumi wetu na mazingira ya watoto wetu," alisisitiza Dkt. Burian.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Husein Msuya, alisema Siku ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Ikolojia ya Mikoko huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 28, baada ya kuanzishwa na UNESCO mwaka 2015 kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa mifumo ya ikolojia ya mikoko na wajibu wa kuihifadhi.

Alisema Tanzania ina takribani hekta 158,100 za misitu ya mikoko iliyopo katika wilaya mbalimbali za ukanda wa pwani, zikiwemo Tanga, Pangani na Mkinga, ambapo misitu hiyo ina mchango mkubwa katika kuhifadhi bioanuwai, kuzuia mmomonyoko wa fukwe, kuhifadhi kaboni na kukuza uchumi kupitia uvuvi pamoja na utalii wa ikolojia.
Wananchi wahamasisha uhifadhi wa mikoko

Mkazi wa Jiji la Tanga, Abdalah Mwalimu, alisema wananchi wana wajibu wa kutunza mikoko kwa kuwa ndiyo kinga ya kwanza dhidi ya athari za mawimbi makubwa na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri maeneo ya pwani.


"Mikoko ni uhai wetu. Tukiiharibu, tutakuwa tumeharibu mazalia ya samaki, tumepunguza kipato cha wavuvi na kuhatarisha usalama wa fukwe. Kila mmoja wetu anapaswa kushiriki kupanda na kuitunza," alisema Abdalah Mwalimu.

Kwa upande wake, mkazi mwingine wa Jiji la Tanga, Fatuma Omari, alisema elimu ya uhifadhi wa mazingira inapaswa kuendelea kutolewa kwa wananchi wote ili kuongeza uelewa wa umuhimu wa kupanda mikoko na kulinda fukwe.


"Kupanda mikoko ni uwekezaji wa maisha ya baadaye. Tunapaswa kuwafundisha watoto wetu kupenda mazingira ili waendeleze jukumu hili na kuhakikisha fukwe zetu zinabaki salama kwa vizazi vijavyo," alisema Fatuma Omari.

Fatuma aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, serikali na taasisi zinazoshughulika na uhifadhi wa mazingira ni muhimu katika kuhakikisha mikoko inaendelea kulindwa na kurejeshwa katika maeneo yaliyoharibiwa.

Abdalah naye alihimiza vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kampeni za upandaji wa mikoko na usafi wa fukwe, akisema hatua hiyo itasaidia kuhifadhi mazingira, kuongeza uzalishaji wa samaki na kukuza uchumi wa jamii za pwani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.









Share this

Related Posts

Previous
Next Post »