Showing posts with label biashara. Show all posts
Showing posts with label biashara. Show all posts

STENDI KANGE KUFANYA KAZI USIKU NA MCHANA

September 01, 2026 Add Comment

 



Na Oscar Assenga, TANGA

STENDI Kuu ya Mabasi Kange, iliyopo Jiji la Tanga, inatarajiwa kuanza kutumika kwa saa 24 ndani ya wiki moja, baada ya uamuzi huo kufikiwa na uongozi wa Mkoa, Jiji na wadau wa sekta ya usafirishaji.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Burian, kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jiji pamoja na wadau wa sekta ya usafirishaji kuhusu matumizi ya stendi hiyo.

Dk. Burian alisema utekelezaji wa mpango huo utaanza ndani ya wiki moja na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 8, mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho mbalimbali katika eneo hilo ili kuwezesha shughuli za usafirishaji kufanyika kwa ufanisi.

Alisema mabasi yatakuwa yakifika na kuondoka Kange, huku usafiri wa mabasi madogo, daladala na bajaji ukitumika kuwaunganisha abiria na maeneo mbalimbali ya Jiji.

“Wenye mabasi wapo tayari na wameonyesha nia ya kuanza kutumia stendi hii. Pia kutakuwa na mabasi madogo kwa ajili ya kupeleka abiria kutoka mjini kwenda Kange na kinyume chake,” alisema.

Alisema Jiji limetenga eneo maalumu kwa ajili ya maegesho ya magari madogo ya abiria na magari binafsi, hatua ambayo itasaidia kurahisisha huduma za usafiri katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa, mpango huo pia unalenga kuifanya Kange kuwa eneo muhimu la shughuli za kiuchumi, badala ya kuwa kituo cha mabasi pekee.

Alisema abiria watakaoshushwa upande mmoja wa eneo hilo watapita katikati ya kitega uchumi kilichopo Kange na hivyo kupata fursa ya kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na wafanyabiashara na wawekezaji.

“Hatuitazami Kange kama eneo la abiria pekee. Tunataka eneo hili liwe kitega uchumi na tutaendelea kuwavutia wawekezaji ili shughuli mbalimbali za kiuchumi zifanyike hapa,” alisema.

Alisema eneo hilo tayari lina taasisi na huduma mbalimbali, ikiwamo chuo cha utalii, ofisi za Serikali na baadhi ya wafanyabiashara wenye migahawa, huku jitihada zikiendelea kuwavutia wawekezaji zaidi.

Dk. Burian alisema Tanga ni lango muhimu la kiuchumi kwa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hivyo uwekezaji katika maeneo kama Kange ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Jiji.

Alisema eneo hilo pia lina nafasi ya kutumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwamo harusi, mikutano na shughuli nyingine, huku Jiji na taasisi za Serikali zikitakiwa kutumia jengo hilo kwa shughuli zao na kulipia huduma hizo.
 
MABORESHO

Dk. Burian alisema kabla ya kuanza matumizi kamili ya stendi hiyo, maboresho kadhaa yatafanyika, ikiwamo kufanya leveling ya eneo la maegesho, kupaka rangi, kutenga eneo la ibada na kukamilisha uwekaji wa viti katika eneo la abiria.

Aidha, alisema eneo limetengwa kwa ajili ya Jeshi la Polisi kuweka vifaa na huduma zinazohitajika kwa ajili ya kuimarisha usalama.

Alisema Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nalo litakuwa na gari katika eneo hilo ili kukabiliana na dharura na kuimarisha usalama, akiwashukuru wananchi kwa juhudi za kuhakikisha mazingira ya stendi yanakuwa salama.

LATRA YAWEKA MSIMAMO

Awali, Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Mkoa wa Tanga, alisema mabasi yanayofanya safari za kimataifa yanapaswa kuzingatia utaratibu wa kutumia vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuhudumia abiria.

Alitoa mfano wa basi linalotoka Mombasa nchini Kenya kwenda Dar es Salaam, akisema Tanga ndiyo kituo cha kwanza linapoingia nchini Tanzania.

Alisema kwa utaratibu huo, basi hilo linapaswa kuingia katika stendi ya Tanga kwa ajili ya kuhudumia abiria, huku vituo vingine vikifuata kulingana na mahitaji ya wasafiri.

Alisema uwezo wa stendi ya mkoa unapaswa kutumika ipasavyo, ikiwamo kuwezesha magari yanayofanya safari za ndani na nje ya nchi kufika kwa ajili ya ukaguzi na huduma nyingine zinazohitajika.

Alisema magari yanayofanya safari za Tanzania na nje ya nchi yataendelea kusimamiwa kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa na mamlaka husika.

PROF. SHEMDOE AELEKEZA WAFANYABIASHA 30 SOKO LA NDIZI MABIBO KUREJESHWA SOKONI

PROF. SHEMDOE AELEKEZA WAFANYABIASHA 30 SOKO LA NDIZI MABIBO KUREJESHWA SOKONI

September 01, 2026 Add Comment






Na: OWM – TAMISEMI, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, ameelekeza waliokuwa wafanyabiashara 30 wa soko la ndizi Mabibo (Mahakama ya Ndizi) kurejea kufanya biashara kwa udhamini wa maandishi kutoka ofisi za Serikali za Mitaa.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo Agosti 31, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo ya OWM- TAMISEMI jijini Dar es Salaam, mara baada ya kupokea taarifa ya timu ya ufuatiliaji wa malalamiko ya wafanyabiashara hao wa soko la ndizi Mabibo, wakati wa kikao kazi chake na wafanyabiashara hao.

Aidha, Prof. Shemdoe ameilekeza Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kufanya tathmini ya mali ya Bw. Frego Njovu aliyewasilisha madai ya kuomba kurejeshewa fedha alizotumia kukarabati choo kilichopo sokoni hapo ambacho alikuwa akikisimamia.

Katika kuhakikisha haki inatendeka, Prof. Shemdoe ameelekeza bidhaa za mfanyabiashara Bw. Enock Kimwayeya aliyekuwa Mwenyekiti wa Wafanyabiashara waliowasilisha malalamiko kwa Prof. Shemdoe, arejeshewe bidhaa zake alizoziacha kwenye kibanda cha biashara pindi alipoondolewa, kwani taarifa ya timu ya ufuatiliaji imeainisha kuwa Halmashauri imekiri kwamba bidhaa za mfanyabiashara huyo zipo.

Ili kuimarisha usimamizi wa soko, Prof. Shemdoe amemuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kumpeleka meneja wa soko mwingine kulisimamia soko hilo na aliyepo kupangiwa majukumu mengine.

Maelekezo hayo ya Prof. Shemdoe yametokana na maafikiano baina ya pande zote katika kikao kazi cha Waziri huyo na walalamikaji (wafanyabiashara) na walalamikiwa ambao ni Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.

Malalamiko ya wafanyabiashara hao 30 yaliwasilishwa kwa Prof. Shemdoe kupitia andiko lao la tarehe 15/01/2026 lililohusu Sakata la soko la Ndizi Mabibo wakilalamikia kupigwa marufuku kuingia sokoni, kutaifishwa na kuuzwa kwa maeneo yao ya biashara, aidha Manispaa ya Ubungo iliwaondoka sokoni wafanyabiashara hao kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kutoitambua manispaa hiyo kama msimamizi wa soko.

NMB: ELIMU, UJUZI NGUZO MUHIMU YA UCHUMI WA KIPATO CHA JUU

August 25, 2026 Add Comment

Na Oscar Assenga, TANGA

BENKI ya NMB imesema Tanzania haiwezi kufikia uchumi wa kipato cha juu bila kuwekeza katika elimu, ujuzi wa vitendo na ubunifu unaowawezesha Watanzania kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili nchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Meneja Mwandamizi wa Maabara ya Ubunifu ya NMB, Maria Mwamyalla, wakati akitoa salamu za wadhamini kwa niaba ya wadhamini wote katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyofanyika mkoani Tanga.

Mwamyalla alisema kaulimbiu ya mwaka huu, “Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” inaendana na mkakati wa NMB wa kuwekeza katika teknolojia, ubunifu, vijana na ujumuishaji wa kifedha.

Alisema kupitia Agenda 2030, benki hiyo imeweka teknolojia, ubunifu, uwekezaji kwa vijana na ujumuishaji wa kifedha kuwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa ukuaji.

“Mwelekeo huo unaendana moja kwa moja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi wa ushindani unaotumia maarifa, ujuzi na teknolojia,” alisema.

Mwamyalla alisema teknolojia pekee haiwezi kuleta matokeo yanayotarajiwa bila kuwapo kwa watu wenye maarifa na ujuzi wa kuitumia ipasavyo.

NMB YATOA BILIONI 2 KUSOMESHA VIJANA

Alisema kupitia NMB Foundation, benki hiyo imeendelea kuwekeza katika elimu na malezi ya uongozi kwa vijana, hususan wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi.

Alisema kupitia programu ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni mbili tangu mwaka 2022, kwa ajili ya kuwafadhili wanafunzi 121 katika vyuo vikuu 11 nchini.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, wanafunzi hao wamekuwa wakisaidiwa mahitaji mbalimbali yakiwamo ada, malazi na vitendea kazi kama kompyuta mpakato.

Alisema wanafunzi 21 tayari wameingia katika soko la ajira, huku wengine 42 wakitarajiwa kuhitimu mwaka huu.


“Tunatarajia kufungua dirisha la tatu la programu hii mwezi Septemba mwaka huu,” alisema.

WATAKA VIJANA WAPEWE UJUZI

Aidha, Mwamyalla alisema NMB inaendelea kutekeleza programu ya SEP kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Save the Children pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Alisema programu hiyo inalenga kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa kuwapatia vijana elimu ya vitendo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na vyuo vya VETA.

NMB YAWEKEZA BILIONI 232 TEKNOLOJIA

Katika eneo la teknolojia na ubunifu, Mwamyalla alisema NMB imewekeza zaidi ya Sh bilioni 232, huku sehemu kubwa ya suluhisho za kiteknolojia zikitengenezwa na wataalamu wazawa.

Alisema uwekezaji huo unalenga kujenga utaalamu wa Watanzania, kuimarisha usalama wa mifumo pamoja na kupunguza muda wa kupeleka bidhaa za kidijitali sokoni.

Alitaja miongoni mwa suluhisho hizo kuwa ni huduma ya NMB Mkononi, inayowawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki kupitia simu zao za mkononi, ikiwamo kutuma na kupokea malipo ya kielektroniki.

Kwa mujibu wa Mwamyalla, huduma hizo zimechangia kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha kwa zaidi ya wateja milioni 10 wa NMB.

Alisema kupitia programu ya PesaTek, iliyoanzishwa mwaka 2022, benki hiyo imezindua Innovation Sandbox na kuendelea kuwawezesha vijana pamoja na wabunifu katika sekta ya teknolojia kupima na kuendeleza suluhisho zao.

Mwamyalla alisema NMB itaendelea kushirikiana na Serikali na taasisi za elimu kuhakikisha elimu, ujuzi na ubunifu vinageuzwa kuwa suluhisho zinazochochea biashara na kuchangia maendeleo ya Taifa.


SERIKALI YAWEKA MKAKATI WA KUPUNGUZA MUDA WA MELI ZA MAFUTA BANDARINI

August 15, 2026 Add Comment




DAR ES SALAAM. 


Serikali imeweka mkakati wa kupunguza muda ambao meli za mafuta hutumia bandarini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi katika upokeaji, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za mafuta nchini.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, anayeshughulikia Mafuta na Gesi Dkt. James Mataragio, amesema hayo wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya mafuta katika eneo la Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Tanzania International Petroleum Reserves Limited (TIPER), Leo Augosti 14,2026 Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mataragio amesema Serikali inalenga kuhakikisha meli zinazowasili nchini zinapata huduma kwa wakati, zinashusha mafuta kwa ufanisi na kuondoka bandarini bila ucheleweshaji usio wa lazima.

“Ni matarajio ya Serikali kuona meli zikifika, zinashusha mafuta na kuondoka. Kila taasisi inapaswa kufahamu jukumu lake na kujipanga ipasavyo,” amesema.


Ameeleza kuwa moja ya changamoto zinazochangia meli kukaa bandarini kwa muda mrefu ni kasi ndogo ya upokeaji na uondoshwaji wa mafuta katika baadhi ya maghala binafsi. Hali hiyo husababisha meli kusubiri na kuongeza msongamano bandarini.

Kutokana na changamoto hiyo, Dkt. Mataragio ameutaka Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuimarisha usimamizi wa wamiliki wa maghala binafsi na kuhakikisha wanaweka miundombinu inayokidhi mahitaji ya uendeshaji.


Amesema wamiliki wa maghala wanapaswa kuboresha pampu na vifaa vingine vinavyotumika kupokea mafuta, hasa vinapokuwa vimechakaa au havina uwezo unaohitajika.



Kwa mujibu wa Dkt. Mataragio, ucheleweshaji wa meli bandarini huongeza gharama za uendeshaji, zikiwemo gharama za meli kusubiri, ambazo hatimaye zinaweza kuathiri bei ya mafuta kwa mwananchi.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Simon, amesema taasisi hiyo itakutana na wadau muhimu katika sekta ya mafuta, wakiwemo kampuni za uuzaji wa mafuta (OMCs) na TPA, kwa ajili ya kupitia na kuboresha Mwongozo wa Taratibu za Uendeshaji (Standard Operating Procedure Manual).


Amesema mapitio hayo yanalenga kuweka wazi majukumu, muda wa utekelezaji na uwajibikaji wa kila mdau katika mchakato wa upokeaji na uhamishaji wa mafuta.


Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha uratibu kati ya meli na maghala ya kupokea mafuta, kupunguza muda wa meli kukaa bandarini na kudhibiti gharama zinazotokana na ucheleweshaji.


Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio aliambatana na Kamishna wa Mafuta kutoka Wizara ya Nishati, Bw. Goodluck Shirima; Mtendaji Mkuu wa PBPA, Bw. Erasto Simon; Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Abed Gallus Abed; pamoja, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Mashariki, Mhandisi Lorivii Long’idu na wataalam kutoka Wizara ya Nishati.

MBARAWA AFUNGUA MILANGO YA AJIRA ZA BAHARINI KWA VIJANA WASIOSOMA SAYANSI

Kajunason June 25, 2026 Add Comment

Uchumi wa Bluu Kunufaika na Elimu ya Ubaharia

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kukiunga mkono Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) katika jitihada zake za kuanzisha kozi ya awali ya ubaharia itakayowawezesha vijana wengi zaidi wa Kitanzania kupata elimu ya sekta hiyo na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa bluu.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la DMI katika kilele cha Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma, ambapo alieleza kuwa kozi hiyo ni suluhisho kwa vijana wengi wenye ndoto za kuwa mabaharia lakini ambao hawakupata nafasi ya kusoma masomo ya sayansi yanayohitajika kujiunga na taaluma hiyo.

Alisema DMI imebuni mpango huo mahsusi ili kuwapa vijana hao fursa ya kupata msingi wa masomo muhimu yatakayowawezesha kuendelea na mafunzo ya ubaharia na hatimaye kuingia katika soko la ajira la sekta ya usafiri wa majini.

“DMI inafanya kazi kubwa ya kuangalia namna ya kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa za elimu ya ubaharia. Kozi hii ya awali itawasaidia wale ambao hawakusoma masomo ya sayansi kupata msingi unaohitajika na hatimaye kujiunga na mafunzo ya ubaharia,” alisema Profesa Mbarawa.
Alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya mabaharia wenye ujuzi na sifa zinazotambulika kitaifa na kimataifa, huku ikilenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika ajira za sekta ya bahari na usafiri wa majini duniani.

Waziri huyo pia alimpongeza Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, kwa ubunifu na juhudi zake za kuendeleza programu mbalimbali za mafunzo zinazowawezesha mabaharia wa Tanzania kufikia viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika sekta ya usafiri wa majini.

“Tunakipongeza DMI kwa juhudi zake za kubuni na kuendeleza mafunzo yanayowawezesha mabaharia wetu kuwa na sifa zinazokubalika kimataifa. Mabaharia wanazunguka dunia nzima, hivyo ni lazima waandaliwe kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sekta ya kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho katika kuzalisha wataalamu wenye tija na ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Profesa Gurumo alisema kutokana na asili ya kazi ya ubaharia inayowafanya mabaharia kufanya kazi na kusafiri katika mataifa mbalimbali duniani, ni muhimu kwao kupata elimu na stadi zinazotambulika kimataifa ili waweze kushindana kwa ufanisi katika soko la ajira la dunia.

Aliongeza kuwa DMI itaendelea kupanua na kuboresha mafunzo ya bahari ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata elimu na ujuzi unaohitajika kwa taifa kunufaika na fursa zilizopo katika uchumi wa bluu na sekta ya usafiri wa majini.

Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya bahari na usafiri wa majini kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa mabaharia katika kukuza biashara, uchumi na maendeleo ya jamii duniani.

SMZ YATAJA MAFANIKIO YA BIMA YA LAZIMA KWA WAGENI

Kajunason June 07, 2026 Add Comment
Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 kutangaza mafanikio ya mpango wa bima ya lazima kwa wasafiri, ikieleza kuwa umeimarisha usalama wa wageni na kuchangia ukuaji wa sekta ya afya pamoja na mapato ya utalii visiwani humo.

Mpango huo ulioanza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024, unawataka wageni wote wa kimataifa wanaoingia Zanzibar kuwa na bima ya usafiri kabla ya kuwasili. Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato, ukiingiza wastani wa dola za Marekani milioni moja, sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.6 kila mwezi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenye viwanja vya Magereza jijini Arusha, Ofisa Mauzo wa shirika hilo, Abdul-Halim Muhammad, alisema maonesho hayo yamewapa fursa ya kutoa elimu kwa watalii, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuhusu umuhimu wa bima hiyo.

“Tunashiriki Karibu-KiliFair kuongeza uelewa kuhusu bima hii ya lazima na kueleza namna inavyowanufaisha wageni huku ikichangia maendeleo ya huduma muhimu Zanzibar,” alisema.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, wageni wengi wa kimataifa hulipa dola 44 za Marekani kwa kila safari ya kuingia Zanzibar, huku wageni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakilipia dola 22 pekee. Watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 hulipa dola 22, huku walio chini ya umri huo wakisamehewa.

Muhammad alisema bima hiyo inawawezesha wageni kupata huduma za matibabu ya dharura na msaada mwingine muhimu wanapokuwa Zanzibar, hatua inayopunguza changamoto za kifedha na kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka wanapozihitaji.

Alisema sehemu ya mapato yanayokusanywa kupitia mfuko huo hutumika kugharamia huduma za afya kwa wageni waliokatiwa bima, huku fedha zinazobaki zikielekezwa katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi na wageni kwa ujumla.
“Mpango huu ulianzishwa baada ya mamlaka kubaini kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya watalii na wawekezaji kuhitaji matibabu ya dharura huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani angegharamia huduma hizo. Sasa mfumo huu umeondoa changamoto hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KiliFair Promotions, Dominic Shoo, alisema Karibu-KiliFair 2026 imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama maonesho makubwa ya utalii na biashara Afrika Mashariki kwa kuwakutanisha wadau kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.

Alisema maonesho hayo yamevutia zaidi ya waoneshaji 500 na wanunuzi wa huduma za utalii wapatao 20,000, hatua inayochochea uwekezaji, ushirikiano wa kibiashara na upanuzi wa masoko ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Karibu-KiliFair ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kimataifa. Kadri wadau wanavyoongezeka kushiriki, ndivyo fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa sekta ya utalii zinavyozidi kuongezeka,” alisema Shoo. 

MAADHIMISHO YA 11 YA UTAFITI NA UBUNIFU UDSM KUANGAZIA UCHUMI WA KIDIJITALI

Kajunason June 07, 2026 Add Comment
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinatarajia kuadhimisha Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu kuanzia Juni 9 hadi 11, 2026, katika Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, huku Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Maadhimisho hayo yatakayowakutanisha watafiti, wabunifu, wanafunzi, sekta binafsi, taasisi za umma na wadau wa maendeleo, yanalenga kuonesha mchango wa utafiti na ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya taifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface, alisema maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo: "Kutumia Utajiri wa Madini wa Tanzania katika Kukuza Nishati Jadidifu, Mageuzi ya Kidijitali na Usalama wa Jamii."

Alisema kaulimbiu hiyo imechaguliwa kutokana na umuhimu wa madini katika maendeleo ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Mnemba (AI), vituo vya kuhifadhi taarifa (Data Centres), magari ya umeme na nishati jadidifu.

“Tunataka kuonesha namna Tanzania inaweza kutumia rasilimali zake za madini kuchochea mageuzi ya kidijitali, kuimarisha usalama wa nishati na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Profesa Boniface.

Aliongeza kuwa maadhimisho hayo yatahusisha maonesho ya tafiti na ubunifu, mawasilisho ya kitaaluma, makongamano pamoja na majadiliano ya ushirikiano wa kimkakati yatakayowawezesha washiriki kubadilishana maarifa na kujenga mitandao ya kitaaluma na kibiashara.

Kwa mujibu wa UDSM, maadhimisho hayo yatatoa nafasi kwa watafiti na wabunifu kuonesha suluhisho mbalimbali za kisayansi na kiteknolojia zinazolenga kukabiliana na changamoto za maendeleo nchini katika sekta za madini, nishati, kilimo, afya na uchumi wa kidijitali.

Profesa Boniface alisema chuo kinaendelea kutumia maadhimisho hayo kama jukwaa la kuunganisha taaluma, ubunifu na maendeleo ya taifa kwa kuwafikia wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo.

"Utafiti na ubunifu ni msingi wa maendeleo endelevu. Tunawaalika Watanzania wote kushiriki katika Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu UDSM 2026 ili kujionea kazi na mafanikio ya watafiti na wabunifu wetu," alisema.

TEMESA NA TOYOTA WAJADILI MAGEUZI YA HUDUMA ZA MATENGENEZO YA MAGARI NCHINI

June 03, 2026 Add Comment

.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania - TEMESA, Bw. Kheri Mahimbali, leo tarehe 02 Juni 2026 amekutana na viongozi wa kampuni ya TOYOTA Tanzania katika ofisi zao eneo la Posta, jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili kuhusu jitihada za Serikali katika kuendelea kuboresha huduma za matengenezo ya magari hapa Nchini. 

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mahimbali amesema TEMESA imejipanga kuhakikisha huduma za ufundi na matengenezo ya magari ya Serikali  zinatolewa kwa viwango vya juu kwa kutumia teknolojia za kisasa na za viwango vya kimataifa.

“TEMESA inaona fursa kubwa katika kuimarisha ushirikiano na TOYOTA kupitia miradi ya pamoja itakayowezesha taasisi hizi mbili kubadilishana utaalamu kwa mafundi na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wadau wetu,” amesema Mtendaji Mkuu.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa TOYOTA Tanzania, Bw. Jatin Pandya amehakikisha utayari wa kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na TEMESA katika mafunzo ya kitaalamu kwa mafundi, ushauri wa kiufundi, matumizi ya teknolojia mpya na kuimarisha mifumo ya usalama wa magari.

“Sisi TOYOTA tunatanguliza usalama wa watumiaji wa magari na ubora wa huduma. Tunaamini ushirikiano huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za matengenezo ya magari nchini na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani,” amesisitiza Pandya.

Aidha, mara baada ya kikao hicho, Mtendajji mkuu pia alipata fursa ya kufanya ziara fupi katika karakana za TOYOTA ili kujionea teknolojia mpya zinazotumika katika matengenezo ya magari.

Miongoni mwa mambo waliyojadili katika kikao hicho ni pamoja na uwezekano wa kuanzisha ushirikiano kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi - PPP. Hatua inayotarajiwa kuimarisha uwezo wa karakana na kuongeza ufanisi wa huduma katika sekta ya matengenezo ya magari.

Kikao hicho kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya TEMESA na TOYOTA, huku kikitarajiwa kuwa chachu ya mageuzi makubwa katika sekta ya ufundi wa magari nchini.


JUKWAA LA WANAWAKE NA KODI NI HATUA MUHIMU YA KUENDELEZA USAWA WA KIJINSIA NA KUKUZA UCHUMI SHIRIKISHI -CPA CASTRO

May 14, 2026 Add Comment



 Na Paskal Mbunga, Tanga

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imesema kwamba Jukwaa la Wanawake na Kodi ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya kuendeleza usawa wa kijinsia na kukuza uchumi shirikishi nchini.

Hayo yalisemwa na  Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga, CPA Castro John wakati akifungua Jukwaa la Wanawake na Kodi ambapo  alisema ni dhamira ya dhati ya kujenga mfumo wa kodi unaoshirikisha makundi yote ya jamii, hususan wanawake ambao ni nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa.


Alisema takwimu zinaonesha wanawake wanachangia kwa kiwango kikubwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo biashara ndogondogo, kilimo, huduma, viwanda vidogo pamoja na biashara za kati na kubwa.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024/2025, wanawake nchini, wakiwemo wa Mkoa wa Tanga, wanakadiriwa kushiriki katika nguvu kazi kwa asilimia 80, huku wakimiliki asilimia 54 ya biashara ndogo, za kati na kubwa.

“Bila ushiriki wa wanawake, juhudi za kuongeza wigo wa walipa kodi na kuongeza mapato ya ndani haziwezi kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema CPA Casto John.

Alifafanua kuwa TRA imeanzisha Jukwaa hilo maalumu kwa lengo la kutoa elimu sahihi ya kodi, kusikiliza changamoto za wanawake wafanyabiashara, kujenga ushirikiano wa karibu pamoja na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati.

Aidha, alisema TRA imejikita katika kuboresha huduma kwa kuzingatia ushirikishwaji, uwazi, weledi na urahisi wa upatikanaji wa huduma. Aliongeza kuwa elimu ya kodi na mahusiano bora ni msingi muhimu wa kuongeza utii wa kodi.

Kupitia jukwaa hilo, wanawake watapata nafasi ya kupata ushauri kuhusu masuala ya kodi, kujifunza fursa mbalimbali pamoja na kuelewa wajibu wao wa kikodi.

“Tunataka mwanamke ajisikie salama, aheshimiwe na ashiriki kikamilifu katika mfumo wa kodi bila hofu wala kikwazo chochote,” alisema.

CPA Casto John alisisitiza kuwa kodi ndiyo injini ya maendeleo ya Taifa kwani mapato yake yanagharamia huduma muhimu kama elimu, afya, barabara, maji safi na miradi mingine ya kimkakati.

“Kila mwanamke anayelipa kodi anakuwa mshirika wa moja kwa moja wa Serikali katika kujenga Tanzania yenye uchumi imara na huduma bora kwa wananchi wake,” aliongeza.

Pia aliwataka wanawake kutumia jukwaa hilo kujifunza, kuuliza maswali na kuwa mabalozi wa utamaduni wa kulipa kodi katika jamii zao.

Aidha, aliwataka wadau wa sekta mbalimbali pamoja na taasisi za kifedha kuendelea kushirikiana na TRA katika kuwawezesha wanawake kukuza biashara zao kwa kuzingatia misingi ya kikodi.

Kwa upande mwingine, aliwahimiza wanawake wafanyabiashara kujisajili katika mfumo wa kodi na kutekeleza wajibu wao kwa hiari na kwa wakati.

“Kulipa kodi si wajibu wa kisheria tu, bali ni mchango wa moja kwa moja katika kujenga Taifa. Wanawake wakisimama kiuchumi, familia na jamii vinaimarika,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisisitiza umuhimu wa kutumia mipaka rasmi ya biashara kwa wafanyabiashara wanaovuka mipaka kupitia maeneo ya Horohoro na Pangani, huku akiwataka kuachana na biashara za magendo na matumizi ya njia zisizo rasmi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, JW Ismail Masound, alisema jukwaa hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050 ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuwa mhimili mkubwa wa ukuaji wa uchumi.

Alisema majukwaa hayo yanasaidia kuwawezesha wanawake na wafanyabiashara kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa kwa kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Mkoa wa Tanga (TWCC), Aziza Ramadhani, alisema jukwaa hilo litawasaidia wanawake kuelewa umuhimu wa kulipa kodi katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.

“Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha Mkoa wa Tanga unalipa kodi kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii,” alisema.

Aliongeza kuwa jukumu la jukwaa hilo ni kuwaunganisha wanawake wa Mkoa wa Tanga ili kuwapa nafasi ya kujifunza, kushirikiana na kupata fursa mbalimbali za kiuchumi ndani na nje ya mkoa huo.

Aidha, alisema wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali ikiwemo kuanzisha mashamba darasa kwa vijana wa kiume na wa kike, huku akiwakaribisha wanawake wajasiriamali kushiriki katika shughuli za maendeleo zinazochangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.




TANGA YAZIDI KUFUNGUKA KIUCHUMI, WAWEKEZAJI WAMIMINIKA

May 03, 2026 Add Comment


Na Oscar Assenga, Tanga

Mkoa wa Tanga unaendelea kuandika historia mpya ya kiuchumi kufuatia kuongezeka kwa kasi kwa wawekezaji na kuimarika kwa miundombinu, hatua inayotajwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara na mapato ya serikali.

Akifungua kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, alisema lengo la kikao hicho ni kujadili kwa kina namna ya kuboresha mazingira ya biashara ili yawe rafiki na wezeshi zaidi, pamoja na kuibua fursa za uwekezaji na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha mfumo wa kodi, akieleza kuwa tayari Rais aliunda tume maalum iliyopitia kodi mbalimbali na kutoa mapendekezo.

Alibainisha kuwa mkoa unasubiri utekelezaji wa mapendekezo hayo ili kusaidia kuondoa migongano ya kodi, hususan zile za halmashauri zilizokuwa zikilalamikiwa na wafanyabiashara.

Katika hatua nyingine, Balozi Burian alisema Tanga imekuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji, huku Jiji la Tanga likiongoza kwa kupokea wawekezaji wengi zaidi.
 

Aliongeza kuwa uwekezaji huo sasa umeanza kusambaa hadi wilaya za Muheza na Korogwe, ambako kunatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa cha sukari pamoja na kuanzishwa kwa bandari kavu.

Akizungumzia mafanikio ya Bandari ya Tanga, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la shehena ya mizigo kutoka tani 470,000 sasa wanapokea zaidi ya tani milioni 1.3, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi.

Alifafanua kuwa kwa sasa takriban meli 60 huingia bandarini kila mwezi, ikilinganishwa na meli 18 hapo awali, huku kila meli ikiingiza Bandarini wastani wa shilingi bilioni 2 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Tunafanya jitihada kuhakikisha ufanisi wa bandari unaongezeka zaidi kwa kupunguza muda wa kuhudumia meli na kuondoa msongamano, ili kuongeza tija kwa sekta binafsi na serikali kwa ujumla,” alisema.

Kuhusu miradi ya kimkakati, Balozi Burian alisema mradi wa bomba la mafuta wa EACOP umefikia hatua za mwisho, huku ukitarajiwa kuanza rasmi kupitisha mafuta kati ya mwezi Juni na Julai.

Alisema mradi huo tayari umetoa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa wananchi na kutoa ajira kwa zaidi ya watu 1,700.

Katika sekta ya miundombinu, ujenzi wa barabara ya Tanga–Pangani unaendelea, licha ya changamoto za mvua, huku serikali ikiahidi kuhakikisha shughuli za biashara haziathiriki.

Aidha, uwanja wa ndege wa Tanga unaendelea kuboreshwa kwa gharama ya shilingi bilioni 63, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la abiria, uzio na upanuzi wa njia ya kurukia ndege ili kuruhusu ndege kubwa kutua.

Kwa upande wa viwanda, serikali ya mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kufuatlia viwanda vilivyokuwa vimekufa na kuvifufua viwanda vilivyokufa na kuvutia uwekezaji mpya.

Ikiwemo kutaka Maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa kupitia TISEZA sasa yanasimamiwa kwa karibu zaidi na kuwekwa alama ili wawekezaji wanapokwenda waweze kuwekeza na tayari mwekezaji mmoja ameonyesha nia ya kujenga kiwanda cha nondo.

Sekta ya utalii nayo imeelezwa kuwa na fursa kubwa, hususan katika maeneo ya fukwe za Pangani na Mking ambapo alisema kwamba Pangani wana maeneo ya Kipumbwi wanayagawa kwa ajili ya uwekezaji kwenye fukwe na Mkinga katika maeneo ya Kwale na maeneo mengine ya Fukwe .


Aliongeza pia kwamba kuna uwekezaji mkubwa katika soko la Samaki na ni juzi tu Rais alizindua Meli kubwa ya Uvuvi wa Bahari ya Kuu na Meli hiyo itavua mpaka Tanga lakini katika meli nne zitakapotimia nadhani moja itakuja kufanya shughuli zake hapa Tanga .


Akisisitiza wana imani wataanza kutumia rasilimali za bahari kwa ufanisi na itakuwa na mchango mkubwa kutokana na kwamba kuwepo na masoko ya Samaki ikiwemo ,Mkinga,Tanga eneo la Deepsea na soko la Samaki la Kimataifa la Kipumbwi.

Sambamba na hilo, uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa samaki na kuimarisha masoko, ikiwemo soko la kimataifa la samaki la Kipumbwi.

Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, alisema Baraza la Biashara ni jukwaa muhimu linaloleta pamoja sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kujenga mazingira bora ya biashara, kuimarisha uaminifu na kuhakikisha sekta binafsi inakuwa endelevu.


MH. LUSWETULA: TRA IHARAKISHE TATHMINI YA MAHITAJI YA VITUO VYA FORODHA.

April 08, 2026 Add Comment


Na. Saidina Msangi, WF, Dodoma.

Serikali imesema kuwa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea kufanya tathmini ya mahitaji ya ujenzi wa Kituo cha Forodha katika Jimbo la Momba, ikiwemo upembuzi yakinifu, upatikanaji na utambuzi wa eneo, gharama za mradi na utayari wa nchi jirani.

Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Momba, Mhe. Condester Michael Sichalwe, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itajenga kituo cha forodha katika Jimbo la Momba mkoa wa Songwe.

Alisema eneo hilo linaangaliwa kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za biashara na umuhimu wake katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa biashara mipakani.

’’Ujenzi wa vituo vya forodha, ikiwemo katika Jimbo la Momba, hufanyika kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, ukamilifu wa taratibu na kanuni za kiforodha, utayari wa nchi jirani tunazopakana nazo, masuala ya kiusalama, upatikanaji wa rasilimali fedha, pamoja na tathmini ya umuhimu wa eneo husika katika shughuli za biashara za mipakani,’’ alifafanua Mhe. Luswetula.

Aliongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho utaanza mara baada ya kukamilika kwa maandalizi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa fedha za utekelezaji wa mradi katika bajeti ya Serikali na kutangazwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, Mhe. Luswetula alieleza kuwa TRA inaendelea na maandalizi na itatoa taarifa rasmi pindi ratiba ya utekelezaji wa ujenzi itakapokamilika na kuielekeza TRA kuharakisha tathmini hiyo ambayo iko katika hatua za mwisho.

TANZANIA YANG’ARA KIMATAIFA KWA USIMAMIZI BORA WA DENI LA SERIKALI

March 28, 2026 Add Comment

  Na Joseph Mahumi, WF


Serikali ya Tanzania imeendelea kung’ara katika jukwaa la kimataifa baada ya kuibuka mshindi wa jumla wa mwaka katika Tuzo za Usimamizi wa Deni la Umma za Jumuiya ya Madola na tuzo ya Ofisi Bora Kanda ya Afrika kupitia Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha (Debt Management Division), ambazo zilitangazwa tarehe 26 Machi 2026 wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Jumuiya ya Madola kuhusu Usimamizi wa Deni la Umma, uliofanyika jijini London, nchini Uingereza.

Ushindi huo mkubwa unatokana na juhudi za Serikali katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa deni la umma, ikiwemo kuunganisha vyema mifumo ya kifedha ya Serikali na kuboresha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo, ambapo Jopo huru la wataalamu lililochambua mawasilisho kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola lilizingatia vigezo vya ubunifu, uimara na uendelevu katika kutoa tuzo hizo.

Akifungua hafla ya utoaji tuzo hizo, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Bw. Tanmaya Lal, alisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuendelea kubuni mbinu madhubuti za kusimamia deni la umma ili kulinda uchumi dhidi ya misukosuko ya kifedha duniani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Mwandamizi wa Idara ya Uchumi, Maendeleo, Biashara na Uwekezaji wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola, Bi. Ruth Kattumuri, aliipongeza Tanzania kwa mageuzi makubwa iliyoyafanya katika kuimarisha usimamizi wa deni la umma.

Alieleza kuwa mafanikio hayo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya nchi katika kujenga uchumi imara na unaostahimili mishtuko ya kiuchumi.

Aidha, Bi. Kattumuri, alisema kuwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola itaendelea kuisaidia Tanzania katika juhudi zake za kuboresha sera na mifumo ya usimamizi wa deni, sambamba na utekelezaji wa maazimio ya Kikao cha 72 cha Kundi la Mawaziri wa Jumuiya ya Madola.

Mkutano huo wa Jukwaa la Jumuiya ya Madola uliofanyika kwa muda wa wiki moja uliwakutanisha wataalamu wa usimamizi wa deni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujifunza na kujadili mbinu bora za kukopa, kusimamia na kulipa deni la umma, na umeandaliwa ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Mwaka wa Jumuiya ya Madola wa Deni Imara, Bunifu na Endelevu, ambapo Tanzania imejitokeza kama kinara na mfano wa kuigwa barani Afrika na katika Jumuiya nzima ya Madola.
Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Omary Khama (Katikati) akiwa ameshika tuzo mbili ambazo Tanzania imepata kwa kuibuka Mshindi wa jumla wa mwaka katika Tuzo za Usimamizi wa Deni la Umma za Jumuiya ya Madola na Tuzo ya Ofisi bora Kanda ya Afrika kupitia Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha (Debt Management Division), ambazo zilitangazwa tarehe 26 Machi 2026 wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Jumuiya ya Madola kuhusu Usimamizi wa Deni la Umma, uliofanyika jijini London, nchini Uingereza. Wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Bw. Tanmaya Lal (kushoto) na  Mkurugenzi Mkuu Mwandamizi wa Idara ya Uchumi, Maendeleo, Biashara na Uwekezaji wa Sekretarieti ya Jumuiya hiyo, Bi. Ruth Kattumuri.
Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Omary Khama, akionesha tuzo mbili ambazo Tanzania imepata kwa kuibuka Mshindi wa jumla wa mwaka katika Tuzo za Usimamizi wa Deni la Umma za Jumuiya ya Madola na Tuzo ya Ofisi bora Kanda ya Afrika kupitia Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha (Debt Management Division), ambazo zilitangazwa tarehe 26 Machi 2026 wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Jumuiya ya Madola kuhusu Usimamizi wa Deni la Umma, uliofanyika jijini London, nchini Uingereza.
Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Omary Khama (Katikati) Aakiwa ameshika tuzo mbili ambazo Tanzania imepata kwa kuibuka Mshindi wa jumla wa mwaka katika Tuzo za Usimamizi wa Deni la Umma za Jumuiya ya Madola na Tuzo ya Ofisi Bora Kanda ya Afrika kupitia Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha (Debt Management Division), ambazo zilitangazwa tarehe 26 Machi 2026 wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Jumuiya ya Madola kuhusu Usimamizi wa Deni la Umma, uliofanyika jijini London, nchini Uingereza. Wengine katika picha ni washindi wenngine wa tuzo hizo kutoka nchi ya Barbados ambayo iliibuka mshindi wa Msimamizi bora wa deni katika ukanda wa nchi za Caribbean na Sri Lanka Msimamizi bora wa deni katika ukanda wa nchi za Asia.

AIRTEL TANZANIA YAZINDUA MADUKA 17 YA SMART SHOPS DAR ES SALAM ,KUKUZA HUDUMA ZA KIDIJITALI

March 25, 2026 Add Comment

  Airtel Tanzania, kampuni inayoongoza huduma za mawasiliano nchini, imezindua maduka mapya 17 ya Airtel Smart Shops jijini Dar es Salaam. Maduka haya ni sehemu ya mtandao wa maduka 31 nchini kote, ukiwa na lengo la kupanua huduma za kidijitali na kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi.


Uzinduzi huo uliofanyika Machi 12, 2026, ulihudhuriwa na Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, pamoja na viongozi wa serikali, wajasiriamali, na vyombo vya habari.

Waziri Kairuki alieleza kuwa uwekezaji huu ni ishara ya nia ya dhati kwa Airtel kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano na kuonyesha imani yake katika mazingira ya biashara Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Maduka haya mapya yanaonyesha dhati ya Airtel katika kuleta huduma karibu na wananchi huku yakiboresha uzoefu wa wateja. Pia unaashiria imani thabiti katika mazingira ya biashara Tanzania,” alisema Waziri Kairuki.


Kwa upande wake, Charles Kamoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, alisema maduka haya hayako tu kama maduka ya rejareja. Yameundwa kama vituo vya kisasa vya huduma za kidijitali, vinavyotoa usajili wa SIM, intaneti ya kasi, huduma za kifedha kupitia Airtel Money, mauzo ya simu, na suluhisho za kibiashara kwa SMEs.


Maduka haya yamewekwa katika maeneo yenye shughuli nyingi jijini Dar es Salaam, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakazi na wajasiriamali. Uzinduzi huu ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa “Airtel Kila Kona”, unaolenga kufanikisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano hata katika maeneo ya vijijini.

Kampuni pia imewekeza katika kupanua mtandao wake wa 4G, kuanzisha teknolojia ya 5G, na kuongeza uunganishaji wa kimataifa kupitia mfumo wa nyaya za chini ya bahari wa 2Africa Submarine Cable System.



Adriana Lyamba, Mkurugenzi wa Uzoefu wa Wateja Airtel Tanzania, alisema maduka haya yameundwa kutoa huduma haraka, bila karatasi, na kwa ufanisi. Maduka haya yanatarajiwa pia kuunda ajira na kusaidia SMEs na wajasiriamali wa ndani kwa kuwapatia zana za kifedha za kidijitali na huduma za mawasiliano za kisasa.