Showing posts with label Kilimo. Show all posts
Showing posts with label Kilimo. Show all posts

MKOA WA TANGA KUENDELEA KUIMARIKA KATIKA USALAMA WA CHAKULA

December 19, 2025 Add Comment


 Na MASHAKA MHANDO, Tanga


MKOA wa Tanga umeendelea kuimarika katika usalama wa chakula baada ya kurekodi ziada ya zaidi ya tani milioni moja, huku Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dkt. Batilda Burian, akiwataka wananchi na viongozi kuchukua hatua madhubuti kudhibiti mfumuko wa bei na uharibifu wa mazao.


Akizungumza katika mahojiano maalum jana kufuatia agizo la hivi karibuni la Serikali kuhusu utunzaji wa akiba ya chakula nchini, Dkt. Batilda alisema kuwa licha ya ongezeko la idadi ya watu, mkoa unajitosheleza kwa wastani wa tani 668,776 za chakula kikavu kwa mwaka.

Dkt. Batilda alibainisha kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanga ina takriban watu 2,615,597. Kutokana na kasi ya ongezeko la watu ya asilimia 2.5 kwa mwaka, idadi hiyo inakadiriwa kufikia watu 2,816,711 kwa sasa, ambao wote wana uhakika wa chakula kutokana na msimu wa kilimo wa 2024/2025.

"Kulingana na uzalishaji wa msimu uliopita, mkoa umezalisha jumla ya tani 1,814,285 za chakula kikavu kutoka katika hekta 102,076 zilizolimwa. Hii inatupa ziada ya tani 1,145,509 baada ya kukidhi mahitaji ya wakazi wote wa mkoa wa Tanga," alisema Balozi Batilda.


Changamoto ya mvua za vuli.


Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa alionyesha wasiwasi juu ya mwenendo wa mvua za vuli (Oktoba–Desemba). Alisema kiwango cha mvua kilichorekodiwa ni kidogo mno (milimita 6.9) ikilinganishwa na hitaji la milimita 450 hadi 550, jambo linaloweza kuathiri msimu ujao kama hatua za tahadhari hazitachukuliwa.

Kufuatia hali hiyo, Dkt. Batilda aliwataka wananchi kuwa makini na bei ya mahindi ambayo kwa sasa inacheza kati ya Sh. 80,000 hadi 120,000 kwa gunia katika wilaya za Handeni na Kilindi. 


"Nawataka wananchi kununua na kukitunza chakula sasa kabla bei haijapanda zaidi hapo baadaye," alisisitiza.


Biashara na mfumo wa stakabadhi ghalani


Katika hatua nyingine, RC Batilda alisisitiza matumizi ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani, akitolea mfano mafanikio yaliyopatikana katika zao la Kakao na Ufuta. Aidha, aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kudhibiti uuzaji holela wa mazao nje ya mkoa ili kulinda usalama wa chakula ndani ya Tanga.


Pia alitoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za kilimo cha mbogamboga, akitaja soko la Zanzibar na ongezeko la shughuli za kiuchumi mkoani Tanga kama fursa adhimu ya kujiingizia kipato.


Mradi wa ujenzi wa bwawa la Mkomazi


Kuhusu miundombinu, Dkt. Batilda alieleza kuwa mradi wa bwawa la umwagiliaji la Mkomazi wenye thamani ya Sh. bilioni 18 umefikia asilimia 85. Alimpa mkandarasi hadi Februari 2026 kukamilisha mradi huo, ambao uliwekwa jiwe la msingi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Machi mwaka huu.


Alimtaka mkandarasi akamilishe bwawa Hilo ili wananchi waweze kupewa maeneo yao ya kulima kuwahi Msimu wa mvua za masika ambazo zitaanza kuonyesha mwezi Machi mwakani.

Mwisho

WAZIRI BASHE AAGIZA KUANZISHWA KWA BIMA YA USHIRIKA KULINDA WAKULIMA WA TUMBAKU

WAZIRI BASHE AAGIZA KUANZISHWA KWA BIMA YA USHIRIKA KULINDA WAKULIMA WA TUMBAKU

October 08, 2025 Add Comment

 

Na.Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, amesema wadau wote wa zao la tumbaku watakaoshindwa kushiriki katika zoezi la usajili wa wakulima hawataruhusiwa kufanya kazi na wakulima, ikiwemo vyama vya ushirika nchini.

Mhe. Bashe ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 8, 2025, mjini Tabora, wakati wa kikao kazi kilicholenga kuboresha huduma ya bima ya mazao na kuhakikisha mkulima analindwa dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri uzalishaji.

Amesema bima kwa wakulima ni jambo la lazima kwa sasa, kwani inalenga kuwalinda wanapokumbwa na changamoto kama ukame, magonjwa au majanga mengine ya asili. Alibainisha kuwa Serikali ina muelekeo mahsusi wa kuhakikisha kila mkulima nchini anakuwa na bima ya mazao, ili kujenga misingi ya kilimo biashara chenye tija.

“Ni lazima tuweke mazingira mazuri kwa wakulima kufanya kilimo biashara. Tunataka kila mkulima wa tumbaku awe amesajiliwa na awe na bima ya mazao yake,” amesema  Mhe. Bashe.

Aidha, ameelekeza kuanzishwa kwa bima ya ushirika itakayosimamiwa na Benki ya Ushirika, ambayo itamlinda mkulima kuanzia hatua za maandalizi ya shamba hadi mavuno ya tumbaku.

“Kwa pamoja tumekubaliana kuwa wakulima wa zao hilo mkoani Tabora wafanyiwe usajili wa mashamba yao na wapate bima ya zao hilo, kwani jukumu la Serikali ni kumlinda mkulima,” ameoneza

Pia, Mhe. Bashe ametoa agizo kwa kampuni za ununuzi wa tumbaku kuhakikisha zimelipa madeni yao kwa wakulima kabla ya Oktoba 30 mwaka huu, vinginevyo hazitaruhusiwa kupewa leseni ya kununua tumbaku katika mkoa wa Tabora.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, amemshukuru Waziri Bashe kwa hatua anazochukua kulinda maslahi ya wakulima, huku akisisitiza haja ya kufanya mapitio ya mfumo wa sasa wa bima ya tumbaku kutokana na mapungufu yaliyopo ambayo yamekuwa yakiwaathiri wakulima.

Amesema kuna umuhimu wa kuwepo mkakati wa kitaifa wa kuwalinda wakulima dhidi ya hasara zinazotokana na majanga mbalimbali.

.