Showing posts with label Nishati. Show all posts
Showing posts with label Nishati. Show all posts

WAZIRI NDEJEMBJ AFUNGUA KIKAO CHA 55 CHA BARAZA KUU LA WAFANYAKAZI wA TANESCO DODOMA

January 22, 2026 Add Comment




📌 Amshukuru Mhe.Rais Dkt Samia  kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi


📌 Asisitiza usimamizi bora wa masuala ya haki za wafanyakazi na utoaji wa elimu kwa umma na kuboresha utoaji wa huduma za umeme nchini.


Waziri wa Nishati Mhe. Deogratius Ndejembi, leo tarehe 22 Januari, 2026 amefungua rasmi Kikao cha 55 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kinachofanyika mkoani Dodoma.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Waziri Ndejembi amemshukuru Mhe. Rais Dkt Samia kwa kuboresha maslahi na stahiki za wafanyakazi wa TANESCO, huku akisisitiza usimamizi madhubuti wa masuala ya haki za wafanyakazi na kuimarisha ushirikiano mahali pa kazi, pamoja na kuendeleza utoaji wa elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu huduma ya umeme. 

"Natambua mmekutana hapa  kujadili kwa kina mambo yanayowahusu wafanyakazi naomba mhakikishe mnazungumza yote na kukubaliana ili kuendelea kuboresha utendaji wa shirika na maslahi ya wafanyakazi''.


Amehimiza pia umuhimu wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora na za uhakika za umeme kwa wateja wake nchini.

Akimkaribisha katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la umeme Bw. Lazaro Twange amemshukuru Mhe Waziri kwa kukubali wito wa kuja kufungua kikao hicho na kumuahidi kuwa wataendelea kusimamia haki za wafanyakazi na kuhakikisha wanakuwa na matokeo katika utendaji.

“Kipekee nikushukuru kwa kuitikia wito wa kuja kutufungulia kikao hiki, kama Mwenyekiti wa baraza hili nikuahidi kuwa nitaenda kuyasimamia yote tutakayojadili hapa kwa ajili ya kuleta tija na maendeleo ya Shirika hili na kuongeza ufanisi katika kuhudumia wananchi”, alieleza Twange. 

Kikao hicho kimewakutanisha viongozi wa TANESCO, wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi (TUICO), Wakurugenzi wa Kanda, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi kutoka kampuni tanzu na ofisi mbalimbali za mikoa nchini.

SIKU 100 ZA RAIS SAMIA: KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA KASI YA WIZARA YA NISHATI

January 20, 2026 Add Comment




Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa ndani ya siku 100 za uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo kuanza kusambaza umeme katika vitongoji 9,009, hatua inayoonesha mwelekeo chanya wa utendaji wa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Pongezi hizo zimetolewa Januari 20, 2026 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Subira Mgalu, wakati wa kikao cha kwanza kati ya Wizara ya Nishati, taasisi zilizo chini yake pamoja na Kamati hiyo. 

Kikao hicho kimelenga kuijengea Kamati uelewa kuhusu muundo na majukumu ya Wizara ya Nishati, pamoja na sera na sheria mbalimbali zinazosimamiwa na Wizara hiyo katika kuendeleza Sekta ya Nishati nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Mgalu amesema mafanikio yaliyopatikana ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Samia ni ushahidi wa dhamira ya Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa wananchi. 

“Niwapongeze sana Wizara ya Nishati na taasisi zake kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya katika kuijenga Sekta ya Nishati. Mafanikio haya yamejidhihirisha wazi ndani ya siku 100 za uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumeshuhudia uzinduzi wa Kituo cha Umeme cha Mtera ambacho kitaimarisha upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Dodoma na Iringa, pamoja na uzinduzi wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 9,009 nchini,” amesema Mgalu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Wizara itaendelea kuhakikisha Sekta ya Nishati inachangia ipasavyo katika kufikiwa kwa malengo ya kitaifa na kimataifa, sambamba na kukuza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi.

Amebainisha Serikali itaendeleza matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati ambavyo Tanzania imebarikiwa navyo ili kufanikisha mpango wa kuzalisha megawati 8,000 za umeme ifikapo mwaka 2030, pamoja na kuongeza matumizi ya umeme kwa wananchi hadi kufikia wastani wa kilowati saa (KWh) 3,000 kwa kila mtu ifikapo mwaka 2050.

Kuhusu nishati safi ya kupikia, Mhe. Ndejembi amesema Wizara inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kuongeza vituo vya upatikanaji wa nishati hiyo pamoja na kubuni na kuendeleza teknolojia rafiki kwa mazingira.

Aidha, ameahidi kuwa Wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu na Kamati hiyo na kuzingatia maoni na ushauri wa Kamati hiyo katika utekelezaji wa majukumu yake kwa maendeleo ya Sekta ya Nishati na Taifa kwa ujumla.

Viongozi wengine wa Wizara ya Nishati waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

MKURUGENZI MKUU REA AWAFUNDA WAHANDISI WA MIKOA

January 19, 2026 Add Comment


*📌Asisitiza kuimarisha Mawasiliano na Uhusiano*


*📌Awakumbusha kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo*


*📌Awasisitiza kushirikiana kwa karibu na Jamii eneo la Mradi*


*📌Awasisitiza kushirikiana kwa karibu na Taasisi zingine za Serikali*


*📌Watakiwa kufanya kazi kwa uharaka na usahihi*


*📌Kumsimamia Mkandarasi kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa*


📍Dodoma


Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amewaelekeza Wasimamizi wa Miradi wa Mikoa kuhakikisha wanaimarisha Mawasiliano na Ushirikiano na wadau mbalimbali kwenye maeneo ya miradi ili kurahisisha utekelezaji wake. 


Ametoa maelekezo hayo leo Januari 19, 2026 jijini Dodoma katika kikao chake na Watumishi wa REA wanaohusika na Usimamizi wa Miradi wa Mikoa mara baada ya Kusaini mikataba ya kusambaza umeme katika Vitongoji 9,009 Tanzania Bara.

"Tarehe 17 Januari, 2026 tulisaini mikataba na Wakandarasi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji 9,009 na tunaelekea kwenye hatua ya utekelezaji, nimewaiteni hapa ili tukumbushane namna bora ya kuimarisha utendajikazi wetu," amesisitiza Mha. Saidy.


Amesema Watanzania wanayo matumaini na REA na kwamba ni wajibu wao kuhakikisha hawawaangushi kwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Miongozo ya Serikali.


"Imarisheni mawasiliano na ushirikiano na Wabunge, Viongozi wa Mikoa, Wilaya, TANESCO, Wakandarasi, Serikali za Vijiji na Vitongoji pamoja na wanufaika wa miradi," amesisitiza Mha. Saidy

Halikadhalika Mha. Saidy amewasisitiza kuendelea kuwasimamia kwa karibu Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya nishati vijijini ikiwemo kuwa na ratiba yao ya kila siku na  kuhakikisha wanatoa taarifa za mara kwa mara kwa viongozi katika ngazi mbalimbali kuanzia vitongoji hadi ngazi ya mkoa ili kuwapa nafasi ya kutambua hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi.


"Hakikisheni mkandarasi anaripoti kwenye uongozi wa kitongoji kabla hajaanza kutekeleza kazi yoyote ya mradi na pia msisitize katika suala la kutoa ajira kwa wananchi eneo la mradi," ameelekeza Mha. Saidy. 


Vilevile amewataka kuhakikisha wanawasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi kwa viongozi huko walipo kwenye maeneo yao ya miradi ili iweze kujulikana na namna inavyoendelea kutekelezwa ikiwepo kutambua changamoto zilizopo na kuzitafutia suluhisho mapema. 


Pia, amewasisitiza kushirikiana na Taasisi zingine za Serikali ili kurahisisha utekelezaji wa miradi hasa ikizingatiwa kuwa mradi unapitia hatua mbalimbali za utekelezaji na Kila hatua inakuwa inahitaji ushirikiano na wadau wengine zikiwemo baadhi ya taasisi zinazotekeleza miradi ya maendeleo maeneo ya vitongoji ikiwemo TARURA na TFS.


Kikao hicho kicho kimelenga kujadili namna  bora ya kusimamia utekelezaji wa miradi, hatua zilizofikiwa na mikakati ya kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na kasi ili ikamilike ndani ya muda. 


*Mwisho*

TANESCO KIGAMBONI YATOA ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA SHULE YA MSINGI MALAIKA

January 16, 2026 Add Comment


📍TANESCO yawapa  wazazi na waalimu  elimu ya nishati safi ya kupikia kwa umeme


📍Jiko la Nishati safi ya kupikia latolewa kuendelea kuhimiza matumizi ya kupika kwa umeme 


Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, TANESCO Mkoa wa Kigamboni ilitoa elimu ya matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia katika Shule ya Msingi Malaika iliyopo Kigamboni. 


Elimu hiyo ilitolewa wakati wa siku maalum ya ufunguzi wa shule tarehe 13 Januari, 2026  (Back to School), iliyowakutanisha wazazi na walimu.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Kigamboni, Bi. Tumaini Mahwaya, alisema kuwa lengo la kutumia fursa hiyo  ni kuhakikisha wazazi na waalimu wanapata uelewa wa kina kuhusu faida za kutumia nishati ya umeme kupikia akibainisha faida zake kuwa ni nishati salama, gharama nafuu na rafiki kwa mazingira.

“Shirika linakenga kuhakikisha wazazi na walimu wanaelewa kuwa kupikia kwa umeme ni salama, ni nafuu na kunalinda afya pamoja na mazingira. Tukibadili mtazamo wetu leo, tutakuwa tumewekeza kwenye maisha bora ya baadaye,” alisema Tumaini.

Vile vile, ili kuunga mkono utekelezaji wa matumizi ya nishati safi ya umeme katika taasisi za elimu, TANESCO ilikabidhi jiko la umeme aina ya Pressure Cooker lenye ujazo wa kilo 15 kwa uongozi wa shule hiyo ambalo litawarahisishia kupika shuleni hapo. 

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Malaika Bw. Ahmed Abdallah Fataki aliishukuru TANESCO Mkoa wa Kigamboni kwa msaada huo na kuahidi kulitumia kikamilifu, hatua itakayosaidia kuachana na matumizi ya nishati zisizo salama shuleni hapo.

“Jiko hili litatusaidia sana kuboresha huduma za chakula kwa wanafunzi na kutuondolea utegemezi wa nishati zisizo salama. Tunaishukuru TANESCO kwa kutukumbuka na kutuunga mkono katika ajenda ya nishati safi,” alisema Bw. Fataki.

Nao wazazi wa wanafunzi hao walionesha mwitikio mkubwa kwa kutembelea banda la TANESCO kupata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuahidi kuacha matumizi ya nishati zisizo salama, ili kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.



TANZANIA YATAJA MAFANIKIO YAKE YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KATIKA JUKWAA LA KIMATAIFA LA IRENA -ABU DHABI

January 11, 2026 Add Comment





ABU DHABI, UAE


Imeelezwa kuwa, Tanzania inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata nishati safi, salama na nafuu ya kupikia, kwa kuhakikisha fedha za kuwezesha miradi ya nishati safi ya kupikia zinapatikana kutoka Serikalini, Sekta Binafsi, Wadau na Mashirika ya Kimataifa yanayounga mkono jitihada za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia duniani.

Akizungumza katika Mkutano wa pembeni wa Baraza la Kimataifa Nishati Jadidifu (IRENA), uliohusu suala la upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya Nishati Safi ya Kupikia, Abu Dhabi katika Falme za Kiarabu, Mhandisi Anita Ringia kutoka Wizara ya Nishati, amesema Tanzania imeendeelea kutenga na kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia na matokeo yake yanaonekana kupitia upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

Amesema.upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 23.2 mwaka 2025, ikiwa ni zaidi ya mara tatu ndani ya kipindi cha miaka minne pekee.

Amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifanya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha kitaifa na nguzo muhimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katika hatua nyingine, Ringia amesema Tanzania katika mwaka wa fedha 2025/26 inaendelea na miradi mbalimbali ikiwemo usambazaji wa majiko banifu 200,000 yenye ruzuku, kulipia majiko ya umeme 480 kupitia bili ya umeme kwa kushirikiana na TANESCO katika mradi wa majaribio, na kusambaza mitungi zaidi ya 450,000 ya gesi ya LPG kwa bei ya ruzuku.

Ameongeza kuwa Serikali pia imepiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa katika taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 100 kwa siku, hatua iliyolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika zaidi ya taasisi za umma 31,000 uwekezaji unaohitaji zaidi ya bilioni 1 za kimarekani, sambamba na kuimarisha kampeni za uhamasishaji na kusaidia biashara ndogo na za kati katika sekta hiyo.

Mhandisi Ringia amebainisha kuwa mafanikio hayo yameungwa mkono pia Sekta binafsi nchini kupitia ongezeko la uwekezaji wa taasisi za kifedha za ndani, zikiwemo Benki ya NMB na CRDB, ambazo zimeanza kutoa mikopo kwa riba nafuu kwa wajasiriamali wa nishati safi ya kupikia ili kupanua mitandao ya usambazaji nchi nzima.

Katika Mkutano huo, Mhandisi Ringia ametangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kusambaza nishati safi ya kupikia, ujenzi wa viwanda vya ndani vya kutengeneza majiko, vifaa, na mitungi na uwepo wa fursa bunifu za kuwezesha wananchi kulipia nishati kupitia mifumo ya kulipia kidogo kidogo (PAYGO), kulipia kwa riba nafuu na kulipia kupitia bili za umeme.

Akizungumza kuhusu suala la mchango wa kimataifa katika kuwezesha fedha za kutekeleza Ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, Mhandisi Anita amesema Tanzania inaunga mkono wito wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za kifedha, na washirika wa maendeleo ili kuziba pengo la ufadhili wa nishati safi ya kupikia, hususan barani Afrika ambako karibu watu bilioni moja bado hawana huduma hiyo.

Wataalam wengine wakiongozwa na Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Imani Mruma walishiriki vikao vya awali vilivyohusu masuala ya utungaji wa sheria, udhibiti, uandaaji wa mipango na uwekezaji wa miradi ya Nishati Jadidifu.

Katika vikao hivyo Tanzania ilieleza kuhusu juhudi inazochukua katika kuhakikisha Nishati Jadidifu inakuwa na mchango wa kutosha katika gridi ya Taifa ili kuendana na maendeleo endelevu ya matumizi ya nishati jadidifu duniani (SDG 7) .

Katika Nishati Jadidifu Tanzania imeeleza kuwa inazidi kupiga hatua ambapo mchango wake unaoingizwa kwenye gridi ya taifa ni asilimia 68 huku juhudi nyingine zikiendelea.ikiwemo ya ujenzi wa mradi wa umeme Jua wa Kishapu wa MW 150 ambao ifikapo Februari mwaka huu utakuwa umeanza kuzalisha umeme kiasi cha MW 50.

Aidha vyanzo vingine vya Nishati Jadidifu vinavyoendelezwa ni pamoja na vyanzo vya Jotoardhi katika ziwa Ngozi (70MW) Songwe (5MW) kiejombaka (60MW), Natron (60MW) na Luhoi (5MW).

Akifungua Mkutano wa IRENA katika siku yake ya kwanza, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa IRENA, Gaun Singh amehimiza kila nchi wanachama kuzidi kuwekeza kwenye miradi ya nishati jadidifu ambapo lengo la kidunia ni kuwa na umeme wa GW 11,000 zinazotokana na nishati jadidifu ifikapo 2030.


Mkutano wa IRENA 2026 unaongozwa na kaulimbiu ya “Matumizi ya Nishati Jadidifu kwa manufaa ya pamoja kwa kila binadamu” yaani “Powering Humanity: Renewable Energy for Shared Prosperity”.

     

HIMIZENI WANANCHI, VIJANA NA WANAFUNZI KUTEMBELEA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA- WAZIRI NANKABIRWA

January 07, 2026 Add Comment




📌*Lengo ni makundi hayo kuwa sehemu ya miradi na kupata ufahamu*


📌*Aipongeza Tanzania kwa kasi ya utekelezaji wa mradi wa bomba la EACOP*


📌 *Ahitimisha ziara yake mkoani Tanga kwa kutembelea kambi namba 16 wilaya ya Muheza*


TANGA


Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, ametoa wito kwa nchi zinazotekeleza mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kuhimiza wananchi, vijana na wanafunzi kutembelea mradi huo akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wao, hasa ikizingatiwa kuwa wao ndio wanufaika wakubwa wa mradi.

Dkt. Nankabirwa ametoa wito huo leo tarehe 7 Januari, 2026 jijini Tanga, wakati wa ziara yake katika Kambi namba 16, ambayo ni kipande cha mwisho kutoka upande wa Uganda katika mchakato wa uunganishaji wa mabomba yatakayosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi eneo la Chongoleani mkoani Tanga.

Akiwa katika kambi hiyo, Waziri Nankabirwa alijionea shughuli za uunganishaji wa mabomba katika eneo lenye urefu wa kilomita 2.5, na kueleza kuridhishwa kwake na ubora wa kazi inayotekelezwa na upande wa Tanzania, akisema ni ya kupongezwa sana.


Aidha, alipata fursa ya kutembelea mmoja wa wanufaika wa mradi kupitia utekelezaji wa huduma za kijamii, ambaye amejengewa nyumba ya kuishi kama sehemu ya manufaa ya mradi huo kwa jamii zinazozunguka mradi.

Hadi sasa, ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la EACOP umefikia asilimia 79. Mradi huo unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa takribani kilomita 1,445 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ambapo jumla ya vipande vya mabomba 86,000 vinatumika katika utekelezaji wake.

Ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2026.


#NishatiTupoKazini

#TanzaniaNchiYetuSote

#NchiYetuKwanza

#MaendeleoEndelevu

BILIONI 10 ZALIPWA FIDIA KWA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA

January 07, 2026 Add Comment


Na Oscar Assenga,TANGA

BILIONI 10 zimelipwa kama sehemu ya fidia kwa wananchi ambao wameweza kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongeleani Tanga,Tanzania.


Hayo yalibainishwa na Naibu Waziri wa Nishati Salome Makamba wakati wa ziara ambayo aliambatana na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa ya kujionea hatua ambayo imefikiwa ya ujenzi wa mradi huo katika eneo la Chongoleani Jijini Tanga.

Ambapo pia katika mradi huo zaidi ya wananchi 9800 waliopo katika mkoa wa Tanga wameweza kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa bomba la mafuta ghafi.

Naibu Waziri huyo alisema mradi huo kwa upande wa Tanzania umeweza kufikia asilimia 86 ya utekelezaji wake ukihusisha maeneo ya ulazaji wa mabomba,ujenzi wa matankiya kuhifadhia mafuta ghafi sambamba na eneo la gati ya kushushia mafuta hayo.


Aidha alisema kuwa mpaka sasa mradi huo upo katika hatua nzuri ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai mwaka huu.

Makamba alisema kuwa mradi huo utaongeza usambazaji wa mafuta nchini na kupunguza gharama za usafirishaji, na kuufanya uwe na tija kwa wananchi wa mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla.



Mradi huu umewanufaisha kwa kiasi kikubwa wananchi wa Tanzania tofauti na wenzetu wa uganda kutokana na eneo kubwa kuwa upande wa nchi yetu"alisema Naibu Waziri Makamba.


Hata hivyo Makamba alisema kwamba dhamira ya dhati ya Rais Dkt Samia Suluhu na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni imewezesha utekelezaji mzuri wa mradi huo unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika Nyanja za kiuchumi ,kijami,ajira na uboreshaji wa huduma za jamii


Kwa upande wake Waziri wa Uganda Nankabirwa alisema kuwa mradi huo umeweza tekelezwa katika viwango bora vya usalama huku ukizingatia ulinzi wa athari za kimazingira


"Tayari wananchi wetu wameweza wameweza kunufaika na sehemu ya kurudisha kwa jamii kwa kuwekewa miundombinu ya maji safi,ujenzi w barabara sambamba na shughuli za michezo kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya mradi huo"alisema Waziri huyo.

Aidha aliwataka wananchi wa nchi hizo mbili kuutunza na kuulinda mradi huo kwani utakapoanza kazi utaweza kuketa manufaa makubwa ya kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.


Ziara hiyo ililenga kuona hatua za utekelezaji wa mradi huo na kuhakikisha kuwa unatekelezwa kwa viwango vya juu vya ubora na usalama.