
Na Oscar Assenga, Tanga
Mkoa wa Tanga unaendelea kuandika historia mpya ya kiuchumi kufuatia kuongezeka kwa kasi kwa wawekezaji na kuimarika kwa miundombinu, hatua inayotajwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa biashara na mapato ya serikali.
Akifungua kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian, alisema lengo la kikao hicho ni kujadili kwa kina namna ya kuboresha mazingira ya biashara ili yawe rafiki na wezeshi zaidi, pamoja na kuibua fursa za uwekezaji na kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha mfumo wa kodi, akieleza kuwa tayari Rais aliunda tume maalum iliyopitia kodi mbalimbali na kutoa mapendekezo.
Alibainisha kuwa mkoa unasubiri utekelezaji wa mapendekezo hayo ili kusaidia kuondoa migongano ya kodi, hususan zile za halmashauri zilizokuwa zikilalamikiwa na wafanyabiashara.
Katika hatua nyingine, Balozi Burian alisema Tanga imekuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji, huku Jiji la Tanga likiongoza kwa kupokea wawekezaji wengi zaidi.

Aliongeza kuwa uwekezaji huo sasa umeanza kusambaa hadi wilaya za Muheza na Korogwe, ambako kunatarajiwa kujengwa kiwanda kikubwa cha sukari pamoja na kuanzishwa kwa bandari kavu.
Akizungumzia mafanikio ya Bandari ya Tanga, alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la shehena ya mizigo kutoka tani 470,000 sasa wanapokea zaidi ya tani milioni 1.3, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi.
Alifafanua kuwa kwa sasa takriban meli 60 huingia bandarini kila mwezi, ikilinganishwa na meli 18 hapo awali, huku kila meli ikiingiza Bandarini wastani wa shilingi bilioni 2 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Tunafanya jitihada kuhakikisha ufanisi wa bandari unaongezeka zaidi kwa kupunguza muda wa kuhudumia meli na kuondoa msongamano, ili kuongeza tija kwa sekta binafsi na serikali kwa ujumla,” alisema.
Kuhusu miradi ya kimkakati, Balozi Burian alisema mradi wa bomba la mafuta wa EACOP umefikia hatua za mwisho, huku ukitarajiwa kuanza rasmi kupitisha mafuta kati ya mwezi Juni na Julai.

Alisema mradi huo tayari umetoa fidia ya zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa wananchi na kutoa ajira kwa zaidi ya watu 1,700.
Katika sekta ya miundombinu, ujenzi wa barabara ya Tanga–Pangani unaendelea, licha ya changamoto za mvua, huku serikali ikiahidi kuhakikisha shughuli za biashara haziathiriki.
Aidha, uwanja wa ndege wa Tanga unaendelea kuboreshwa kwa gharama ya shilingi bilioni 63, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la abiria, uzio na upanuzi wa njia ya kurukia ndege ili kuruhusu ndege kubwa kutua.

Kwa upande wa viwanda, serikali ya mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kufuatlia viwanda vilivyokuwa vimekufa na kuvifufua viwanda vilivyokufa na kuvutia uwekezaji mpya.
Ikiwemo kutaka Maeneo ya uwekezaji yaliyotengwa kupitia TISEZA sasa yanasimamiwa kwa karibu zaidi na kuwekwa alama ili wawekezaji wanapokwenda waweze kuwekeza na tayari mwekezaji mmoja ameonyesha nia ya kujenga kiwanda cha nondo.
Sekta ya utalii nayo imeelezwa kuwa na fursa kubwa, hususan katika maeneo ya fukwe za Pangani na Mking ambapo alisema kwamba Pangani wana maeneo ya Kipumbwi wanayagawa kwa ajili ya uwekezaji kwenye fukwe na Mkinga katika maeneo ya Kwale na maeneo mengine ya Fukwe .
Aliongeza pia kwamba kuna uwekezaji mkubwa katika soko la Samaki na ni juzi tu Rais alizindua Meli kubwa ya Uvuvi wa Bahari ya Kuu na Meli hiyo itavua mpaka Tanga lakini katika meli nne zitakapotimia nadhani moja itakuja kufanya shughuli zake hapa Tanga .
Akisisitiza wana imani wataanza kutumia rasilimali za bahari kwa ufanisi na itakuwa na mchango mkubwa kutokana na kwamba kuwepo na masoko ya Samaki ikiwemo ,Mkinga,Tanga eneo la Deepsea na soko la Samaki la Kimataifa la Kipumbwi.
Sambamba na hilo, uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa samaki na kuimarisha masoko, ikiwemo soko la kimataifa la samaki la Kipumbwi.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, alisema Baraza la Biashara ni jukwaa muhimu linaloleta pamoja sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kujenga mazingira bora ya biashara, kuimarisha uaminifu na kuhakikisha sekta binafsi inakuwa endelevu.
Sambamba na hilo, uwekezaji katika uvuvi wa bahari kuu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa samaki na kuimarisha masoko, ikiwemo soko la kimataifa la samaki la Kipumbwi.
Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Rashid Mchatta, alisema Baraza la Biashara ni jukwaa muhimu linaloleta pamoja sekta ya umma na binafsi kwa lengo la kujenga mazingira bora ya biashara, kuimarisha uaminifu na kuhakikisha sekta binafsi inakuwa endelevu.

EmoticonEmoticon