
Uchumi wa Bluu Kunufaika na Elimu ya Ubaharia
Na Mwandishi Wetu, Kigoma
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kukiunga mkono Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) katika jitihada zake za kuanzisha kozi ya awali ya ubaharia itakayowawezesha vijana wengi zaidi wa Kitanzania kupata elimu ya sekta hiyo na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa bluu.
Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la DMI katika kilele cha Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma, ambapo alieleza kuwa kozi hiyo ni suluhisho kwa vijana wengi wenye ndoto za kuwa mabaharia lakini ambao hawakupata nafasi ya kusoma masomo ya sayansi yanayohitajika kujiunga na taaluma hiyo.
Alisema DMI imebuni mpango huo mahsusi ili kuwapa vijana hao fursa ya kupata msingi wa masomo muhimu yatakayowawezesha kuendelea na mafunzo ya ubaharia na hatimaye kuingia katika soko la ajira la sekta ya usafiri wa majini.
“DMI inafanya kazi kubwa ya kuangalia namna ya kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa za elimu ya ubaharia. Kozi hii ya awali itawasaidia wale ambao hawakusoma masomo ya sayansi kupata msingi unaohitajika na hatimaye kujiunga na mafunzo ya ubaharia,” alisema Profesa Mbarawa.
Alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya mabaharia wenye ujuzi na sifa zinazotambulika kitaifa na kimataifa, huku ikilenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika ajira za sekta ya bahari na usafiri wa majini duniani.
Waziri huyo pia alimpongeza Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, kwa ubunifu na juhudi zake za kuendeleza programu mbalimbali za mafunzo zinazowawezesha mabaharia wa Tanzania kufikia viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika sekta ya usafiri wa majini.
“Tunakipongeza DMI kwa juhudi zake za kubuni na kuendeleza mafunzo yanayowawezesha mabaharia wetu kuwa na sifa zinazokubalika kimataifa. Mabaharia wanazunguka dunia nzima, hivyo ni lazima waandaliwe kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sekta ya kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho katika kuzalisha wataalamu wenye tija na ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
Profesa Gurumo alisema kutokana na asili ya kazi ya ubaharia inayowafanya mabaharia kufanya kazi na kusafiri katika mataifa mbalimbali duniani, ni muhimu kwao kupata elimu na stadi zinazotambulika kimataifa ili waweze kushindana kwa ufanisi katika soko la ajira la dunia.
Aliongeza kuwa DMI itaendelea kupanua na kuboresha mafunzo ya bahari ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata elimu na ujuzi unaohitajika kwa taifa kunufaika na fursa zilizopo katika uchumi wa bluu na sekta ya usafiri wa majini.
Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya bahari na usafiri wa majini kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa mabaharia katika kukuza biashara, uchumi na maendeleo ya jamii duniani.
Share this
EmoticonEmoticon