CHAMA cha Wataalamu wa Masuala ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (TOHASA) kwa kushirikiana na OSHA, WCF, SAFETY AND SECURITY, JAFFERJEE na TMHS GROUP wamezindua kampeni ya “Kuwa Makini Okoa Maisha” inayolenga kuwajengea madereva wa bodaboda uelewa wa sheria na matumizi salama ya barabara ili kupunguza ajali na kuokoa maisha.
Kampeni hiyo imeanza rasmi leo Julai 25, 2026, katika eneo la Tangi Bovu-Kawe, wilayani Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, ambapo madereva hao wamepewa elimu kuhusu usalama barabarani pamoja na vifaa kinga vya kuwasaidia kujilinda wanapokuwa kazini.
Akizungumza na madereva hao wakati wa kampeni hiyo, Rais wa TOHASA, Caroline Baraza, amesema wameamua kuja na mpango huo baada ya kubaini umuhimu wa kuongeza elimu kwa madereva wa bodaboda kuhusu sheria za usalama barabarani na namna ya kujikinga dhidi ya ajali.
Amesema baadhi ya ajali zinazotokea barabarani zinaweza kuzuilika iwapo madereva watakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria, alama za barabarani na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika mazingira mbalimbali.
“Lengo ni kuwapatia elimu maofisa usafirishaji ili wawe makini na kuheshimu sheria, kwa sababu tunaangalia ajali nyingi zinazotokea na takwimu zinaonesha watu wengi wanakosa elimu na kutokujua wafanye nini wakati gani,” amesema Baraza.
Amesema lengo kuu la kampeni hiyo ni kuokoa maisha, ndiyo maana wamechagua kaulimbiu ya “Kuwa Makini Okoa Maisha” ambayo pia imewekwa kwenye viakisi mwanga wanavyowapatia madereva hao.
Baraza amewataka madereva wa bodaboda kuzingatia sheria za barabarani kwa kuwa zimewekwa kwa ajili ya usalama wa watumiaji wote wa barabara, huku akiwataka pia kuwaelimisha wenzao pale wanapobaini wanakiuka sheria.
“Wito wa TOHASA kwa maofisa usafirishaji wafuate sheria za barabarani kwani hazina mtu huyu na huyu, bali ziko kwa ajili yetu sote tunaotumia barabara. Pia kuwa makini pale inapobidi, unapoona mwenzako anavunja sheria wewe kuwa makini na mfundishe au kumuelekeza,” amesema.
Amesema TOHASA inahusisha wataalamu kutoka hospitali na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa watu wanaopata dharura, hivyo kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za kuzuia ajali na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Polisi Kawe/Mbweni, Mkoa wa Kinondoni, Adrian Kamara, amesema Jeshi la Polisi limeendelea kushirikiana na TOHASA katika kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki kuhusu matumizi sahihi ya barabara na umuhimu wa kuzingatia sheria.
Kamara amesema katika kampeni hiyo wamewakumbusha madereva kuzingatia usalama wao pamoja na abiria, kuheshimu vivuko na kutumia barabara kwa usahihi.
“Tumeshirikiana na TOHASA ambao wanahusika na usalama mahala pa kazi kuwakumbusha madereva pikipiki kuzingatia usalama na abiria pamoja na utumiaji sahihi wa barabara, watii sheria za usalama barabarani kwa maana ya kuheshimu vivuko, kutokuendesha pembeni ya barabara,” amesema.
Amesema madereva wa bodaboda ni watumiaji rasmi wa barabara na wanatambulika kisheria, hivyo wanapaswa kutumia barabara kwa utaratibu unaotakiwa na si kuendesha pembeni kama ambavyo baadhi yao wamekuwa wakifanya.
“Tumewafahamisha wao ni watumiaji rasmi na wanatambulika kisheria, hivyo waendeshe pikipiki zao katikati ambako ni sehemu sahihi. Kama ni kushoto au kulia kufuata utaratibu kama magari yanavyotembea,” amesema.
Aidha, Kamara amesisitiza umuhimu wa madereva hao kuvaa viakisi mwanga (reflecta), hasa wakati wa usiku au wanapoendesha katika maeneo yenye mwonekano hafifu, ili waweze kuonekana kwa urahisi na madereva wengine.
Pia amewakumbusha umuhimu wa kuvaa kofia ngumu wakati wote wanapoendesha pikipiki bila kujali umri, huku TOHASA ikiwa imewapatia baadhi ya madereva reflecta pamoja na miwani ya kujikinga dhidi ya vumbi.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa TOHASA, Gerald Mrema, amesema taasisi hiyo imeamua kuanzisha kampeni hiyo kutokana na ongezeko la vifo, majeruhi pamoja na ulemavu wa kudumu unaotokana na ajali za barabarani.
Mrema amesema TOHASA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusika na utoaji wa vifaa kinga vya usalama mahali pa kazi, imelenga kuhakikisha madereva wa bodaboda wanapata elimu na vifaa vitakavyowasaidia kujilinda.
“Taasisi yetu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi mbalimbali ambazo zinatoa vifaa kinga vya usalama mahala pa kazi tumetoa elimu kwa bodaboda tukiwa na kusudi kubwa baada ya elimu hii watahakikisha wanaendesha vyombo vya moto kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi kwa kufuata alama za barabarani kwa kutopakia abiria zaidi ya mmoja,” amesema Mrema.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwafanya madereva hao kuwa na utamaduni wa kutumia vifaa kinga wanapokuwa kazini, akitaja reflecta kuwa miongoni mwa vifaa muhimu kwa ajili ya kuwafanya waonekane kwa urahisi na watumiaji wengine wa barabara.
Mrema pia amewataka madereva hao kuvaa viatu kinga ambavyo vinaweza kusaidia kulinda miguu yao iwapo ajali itatokea, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya ukaguzi wa pikipiki mara kwa mara.
Amesema ukaguzi huo unapaswa kufanyika kabla ya kuanza kazi kila siku ili kubaini kama chombo kiko katika hali salama na kinafaa kutumika barabarani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tangi Bovu, Athuman Kitunguu, amesema wanashukuru kwa kupatiwa elimu ya usalama barabarani pamoja na vifaa kinga, akieleza kuwa eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ajali.
Kitunguu amesema elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa madereva kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani.
“Kwasasa tunashukuru Jeshi la Polisi limepoa na wanatupa ushirikiano mzuri na elimu ambazo tunapatiwa zinatuongezea uelewa kuhusu kufuata sheria za usalama barabarani,” amesema.
Amesema elimu hiyo inapaswa kuendelea kutolewa mara kwa mara ili kuhakikisha madereva wanaendelea kufahamu sheria na taratibu za usalama barabarani, hatua ambayo itasaidia kupunguza ajali na madhara kwa madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara.





















EmoticonEmoticon