KAMPUNI ya Oryx Gas imekabidhi mitungi ya gesi ya kupikia 600 kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wakimo mama lishe huku Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Subira Mgalu akieleza kuwa uamuzi wa Oryx kugawa mitungi hiyo kunakwenda kuondoa kabisa athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati chafu kama kuni na mkaa.
Mgalu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge na Nishati na Madini ameyasema hayo leo Julai 24,2026 katika Tamasha la Samaki wilayani Bagamoyo ambapo kupitia tamasha hilo limetumika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo yametolewa pia mafunzo ya matumizi salama ya nishati hiyo.
“Oryx Gas wamekuwa wadau wakubwa katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia ya gesi ya LPG kwa vitendo na kupitia Samaki Festival wameamua kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kugawa mitungi ya gesi kwa makundi mbalimbali yakiwemo ya Mama na Baba Lishe na wafanyabiashara wa soko la Samaki Bagamoyo.
“Tunafahamu kabla ya Serikali inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati Afrika kuja na kampeni ya nishati safi ya kupikia kulikuwa na matumizi makubwa ya kuni na mkaa hali iliyosababisha watumiaji wa nishati hiyo kuwa na athari za kiafya huku watu 32000 wakipoteza maisha kutokana na madhara ya kutumia kuni na mkaa,”amesema Mgalu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Oryx Energies Tanzania Imani Mtafya amesema katika kuunga mkono juhudi za Serikali kuhamasisha nishati safi ya kupikia wamekabidhi mitungi ya gesi 600 yenye thamani ya Sh.milioni 48 kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali.
Pia amesema kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2026 wameshatoa mitungi 72000 yenye thamani ya Sh.bilioni 5.7 , lengo likiwa kuunga mkono juhudi za Serikali ambayo imeweka lengo ifikapo 2034 watumiaji wa nishati safi ya kupikia wawe wamefikia asilimia 80 kutoka asilimia 29 iliyopo sasa .
Mtafya amesema juhudi wanazofanya zinalenga pia kukomesha utumiaji wa kuni na mkaa ambao unaathiri kubwa sio tu kwa mazingira lakini kwa afya ya mtumiaji huku akifafanua kwasasa wanafanya uwekezaji mkubwa ili kuendana na sera ya Serikali ya kuhamasisha nishati safi ya kupikia.
“Tumewekeza katika ujenzi wa miundombinu ya ghala jipya la kuhifadhi gesi ambalo litagharimu Sh.bilioni 40 ili kuhakikisha tunaongeza usambazaji wetu wa gesi nchi nzima.”
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Shaibu Ndemanga aliyekuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Samaki ametumia nafasi hiyo kuelezea mkakati wao katika kuhamasisha nishati safi ya kupikia na kwamba uamuzi wa Oryx Gas kugawa mitungi 600 ni hatua inayoonesha dhamira ya kuachana na kuni na mkaa hasa kwa wakaanga Samaki wa Soko la Bagamoyo .











EmoticonEmoticon