Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limetoa tahadhari kwa wananchi kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya utapeli wa mitandaoni vinavyotumia majina, picha na nembo za viongozi wa Serikali, taasisi na watu maarufu kwa lengo la kuwalaghai wananchi na kujipatia fedha kwa njia zisizo halali.
Katibu Mkuu wa TRAMEPRO ambaye pia ni mtaalamu wa tiba asili, Boniventura Mwalongo, alisema matapeli wamekuwa wakisambaza matangazo yanayodai viongozi, wafanyabiashara au taasisi mbalimbali zinatoa mikopo, ruzuku, misaada au fursa za uwekezaji wa haraka, huku wakitumia ushuhuda wa uongo kuwashawishi wananchi.
Mwalongo aliwataka wananchi kutothamini taarifa hizo bila kuzithibitisha kupitia mamlaka au taasisi husika, akisisitiza kuwa ni muhimu kutumia taarifa zinazotolewa kupitia njia rasmi pekee na kuepuka kutuma fedha, nyaraka au taarifa binafsi kwa watu wasiojulikana.
Alisema matumizi mabaya ya nembo za vyombo vya habari na majina ya viongozi wa kitaifa katika kusambaza taarifa za uongo yanachochea upotoshaji wa umma, hupunguza imani kwa taasisi na yanaweza kuhatarisha usalama, amani na mshikamano wa Taifa.
Mbali na hilo, TRAMEPRO imeeleza kuwa bado kuna haja ya kuimarisha mapambano dhidi ya mila potofu zinazodhuru afya, utu na haki za binadamu, ikibainisha kuwa baadhi ya vitendo hivyo vinaendelea kufanyika kwa siri katika maeneo mbalimbali nchini.
Shirika hilo limeitaka Serikali kuimarisha mapambano dhidi ya utapeli wa mitandaoni kwa kushirikisha vyombo vya dola na mamlaka zinazohusika, huku ikiendelea kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii na huduma za kidijitali.
Aidha, TRAMEPRO imezitaka mamlaka za mawasiliano na usalama kuchukua hatua za haraka dhidi ya akaunti bandia na mitandao inayotumiwa kufanya utapeli, pamoja na kushirikiana na kampuni za mitandao ya kijamii kuziondoa akaunti zinazojifanya viongozi au taasisi.
Mwalongo amewataka wananchi kutokuwa wepesi wa kuamini matangazo yanayoahidi fedha, mikopo au ruzuku bila uthibitisho, akisisitiza umuhimu wa kuhakiki taarifa kupitia ofisi au tovuti rasmi.
Alisema jamii salama na yenye maendeleo endelevu hujengwa kwa msingi wa ukweli, elimu, uwajibikaji na ushirikiano, huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya utapeli wa mitandaoni, taarifa za uongo na mila potofu.

EmoticonEmoticon