Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinatarajia kuadhimisha Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu kuanzia Juni 9 hadi 11, 2026, katika Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, huku Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Maadhimisho hayo yatakayowakutanisha watafiti, wabunifu, wanafunzi, sekta binafsi, taasisi za umma na wadau wa maendeleo, yanalenga kuonesha mchango wa utafiti na ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya taifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface, alisema maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo: "Kutumia Utajiri wa Madini wa Tanzania katika Kukuza Nishati Jadidifu, Mageuzi ya Kidijitali na Usalama wa Jamii."
Alisema kaulimbiu hiyo imechaguliwa kutokana na umuhimu wa madini katika maendeleo ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Mnemba (AI), vituo vya kuhifadhi taarifa (Data Centres), magari ya umeme na nishati jadidifu.
“Tunataka kuonesha namna Tanzania inaweza kutumia rasilimali zake za madini kuchochea mageuzi ya kidijitali, kuimarisha usalama wa nishati na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Profesa Boniface.
Aliongeza kuwa maadhimisho hayo yatahusisha maonesho ya tafiti na ubunifu, mawasilisho ya kitaaluma, makongamano pamoja na majadiliano ya ushirikiano wa kimkakati yatakayowawezesha washiriki kubadilishana maarifa na kujenga mitandao ya kitaaluma na kibiashara.
Kwa mujibu wa UDSM, maadhimisho hayo yatatoa nafasi kwa watafiti na wabunifu kuonesha suluhisho mbalimbali za kisayansi na kiteknolojia zinazolenga kukabiliana na changamoto za maendeleo nchini katika sekta za madini, nishati, kilimo, afya na uchumi wa kidijitali.
Profesa Boniface alisema chuo kinaendelea kutumia maadhimisho hayo kama jukwaa la kuunganisha taaluma, ubunifu na maendeleo ya taifa kwa kuwafikia wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo.
"Utafiti na ubunifu ni msingi wa maendeleo endelevu. Tunawaalika Watanzania wote kushiriki katika Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu UDSM 2026 ili kujionea kazi na mafanikio ya watafiti na wabunifu wetu," alisema.

EmoticonEmoticon