Showing posts with label habari. Show all posts
Showing posts with label habari. Show all posts

DC ITUNDA AZINDUA OFISI YA WAENDESHA BAJAJI MBEYA

September 14, 2025 Add Comment


Na Mwandishi Wetu, Mbeya


MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amezindua rasmi Ofisi mpya ya Umoja wa Waendesha na Wamiliki wa Bajaji katika kanda ya Old Airport jijini Mbeya. 


Hafla hiyo ilihudhuriwa na mamia ya vijana, wajasiriamali, viongozi wa Serikali za mitaa na wadau wa sekta ya usafirishaji, ikiwa ni ishara ya kuimarisha mshikamano na kuchochea maendeleo ya vijana katika jiji hilo.

Katika hotuba yake, DC Itunda aliwataka vijana kutumia fursa zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan hususani mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa makundi ya kinamama, vijana, na watu wenye ulemavu.


Ameeleza kuwa kwa mwaka wa Fedha 2024–2025, Halmashauri ya Jiji la Mbeya imefanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya shilingi bilioni 3.2, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Mkuu huyo wa Wilaya alimshukuru na kumpongeza Mhe. Rais kwa kuboresha mazingira ya kibiashara, hasa katika sekta ya usafirishaji.


Itunda amebainisha kuwa maboresho ya miundombinu, sera rafiki za kiuchumi, na uwezeshaji wa kifedha vimewapa nguvu vijana wajasiriamali ya kujiendeleza na kuchangia maendeleo ya Taifa. 


Uzinduzi huo umekuwa sehemu ya jukwaa la kujenga mshikamano, kuhamasisha uwajibikaji, na kuendeleza maadili ya kazi na utu akiwahimiza vijana kuendelea kushirikiana, kuwa na nidhamu ya kazi, na kutumia fursa zilizopo kwa manufaa ya muda mrefu. 



Ameisitiza kuwa maendeleo ya kweli hujengwa kwa juhudi za pamoja, mshikamano wa kijamii, na uongozi wenye maono.


Tukio hilo limeacha alama ya matumaini na mwelekeo mpya kwa sekta ya bajaji jijini Mbeya.

Mwisho

TUGHE KUWANOA WAFANYAKAZI NA WAAJIRI ILI KUBORESHA UTENDAJI KAZI

September 14, 2025 Add Comment
14 Septemba 2025, ARUSHA

Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimeandaa mafunzo yatakayowakutanisha Wafanyakazi na Waajiri yanayojulikana kama “Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE yatakayofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 15-18 Septemba 2025.

DKT.NCHIMBI AMNADI KOOLA NA MADIWANI VUNJO,AMPONGEZA DKT.KIMEI

September 13, 2025 Add Comment

MGOMBEA Mwenza wa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John  Nchimbi, amewahutubia Wananchi wa kata ya Himo,jimbo la Vunjo  katika uwanja wa Polisi Himo Wilayani ya Vunjo,akiendelea na mikutano yake ya Kampeni  leo Jumamosi Septemba 13,2025 mkoani Kilimanjaro.

Baada ya kuwasalimia Wananchi hao,Dkt Nchimbi ambae ni mgombea mwenza wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,pia alitumia nafasi hiyo kuwanadi Wagombea Ubunge wa Mkoa huo akiwemo Mgombea Ubunge wa Jimbo la  Vunjo,Ndugu Enock Zadock Koola  pamoja na Madiwani.

Dkt.Nchimbi ambae ameingia Kanda ya Kaskazini,akianzia mikutano yake ya Kampeni Mkoani Arusha na  sasa ameingia mkoa wa Kilimanjaro kusaka kura za ushindi wa Kishindo za Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dkt. Nchimbi ameendelea kuinadi Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2025-2030, ambayo kimsingi imelenga kwenda kuboresha maisha ya wananchi na ustawi wa maendeleo katika miaka mitano ijayo.

Ngombea mwenza huyo amekuwa akitumia  nafasi hiyo kuwaomba wananchi kumchagua mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa chama hicho kwa kura za kishindo ifikapo Oktoba 29,2025.

Wanachama wa CCM wa jimbo hilo wamepongezwa na Dk Nchimbi wakiwemo waliotia nia ya kugombea ubunge akisema anashukuru kutokuwa na mpasuko baada ya kumalizika zoezi la uteuzi ndani ya chama hicho.

Dk Nchimbi pia amempongeza aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Dk Charles Kimei akimsifia kwa kuendele kukipigania chama cha CCM kwa kuwaombea kura Rais Samia, mbunge wa jimbo hilo na madiwani.



INEC YAMTEUA MPINA KUGOMBEA URAIS

September 13, 2025 Add Comment





Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jacobs Mwambegele akimkakabidhi nakala ya fomu za uteuzi kwa Mgombea wa Kiti cha Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT - WAZALENDO), Mhe. Luhaga Joelson Mpina aliyeambatana na Mgombea Mwenza, Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej (kushoto) leo Septemba 13, 2025 Jijini Dar es Salaam, baada ya wagombea hao kuteuliwa na Tume kuwania nafasi hizo katika uchaguzi Mkuu wa utakao fanyika Oktoba 29, 2025. (Picha na INEC).



Mroki Mroki
Online Reporter/Blogger
Mob: +255 755 373999
Email: mrokim@gmail.com.
Blog: https://mrokim.blogspot.com/
DODOMA, TANZANIA

MWANA FA AWAOMBA WANA MUHEZA WAMPE KURA NYINGI ZA KUTOSHA MGOMBEA URAIS WA CCM DKT SAMIA SULUHU NA YEYE OCTOBA 29

September 13, 2025 Add Comment




MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Muheza (CCM) Hamisi Mwinjuma alimaarufu Mwana FA amesema hana wasiwasi na watu wa Tarafa ya Amani na wilaya ya Muheza isipokuwa amewaomba kila atakayekwenda kupiga kuwa Octoba 29 amchukue na mwenzake ili wilaya hiyo iongoze kwa kura nyingi za Rais na Madiwani wa CCM katika Kata 37 za Muheza waweze kushinda akiwemo yeye.

Mwana FA aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni zake za Ubunge zilizofanyika Septemba 10 katika Kijiji cha Bulwa tarafa ya Amani ambapo MwanaFA alisema wananchi wa Muheza waendelee kukiamini chama hicho na wagombea wake kwa kuwa katika miaka mitano iliyopita wameweza kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kiwango kikubwa.



Alisema kimsingi wapinzani waliopo kwa Sasa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi, wameishiwa na hawana hoja na tena wangetamani kuwa wagombea wa CCM lakini hawakuweza kutokana na ushindani uliokuwepo kwenye chama hicho.

“Naombeni mnipigie kura na wagombea udiwani wa CCM kwakuwa mimi siyo mbunge mpya bali ni sheikh yule yule isipokuwa kanzu mpya na nimedhamiria kutatua changamoto za wilaya hii nikiwa mwakilishi wenu kwakuwa miaka mitano iliyopita tumeshirikiana vema na wananchi na tumetekeleza miradi mingi yenye tija”Alisema Mwana FA.



Mgombea huyo alisisitiza umuhimu wa wananchi kuhakikisha wanampa kura nyingi za kutosha wagombea wa CCM akiwemo Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuhakikisha wilaya ya Muheza inaongoza ili waendelee kushirikiana kuleta maendeleo.

Amesema kwamba serikali imeanza kufanyia kazi na amewahakikishia wawekezaji wote wilayani Muheza,ambao wamehodhi mashamba pamoja na viwanda ambavyo hawajavifanyia kazi, watanyang'anywa na kurejeshwa kwa wananchi ili wayafanyie shughuli zao za kiuchumi.



Alisema kila jambo ambalo ni changamoto wilayani humo ameaahidi anakwenda kuyafanyia kazi kama ambavyo miaka mitano iliyokwisha amefanya na kutekelezaji miradi mingi ya maendeleo.



Awali diwani wa kata ya Misalai Said Mtunguja akizungumza kwa naiba ya madiwani wote walioshiriki uzinduzi huo, alisema kuwa hawana deni la mbunge Wala Rais Dkt Samia kwa namna walivyoshirikiana kutatua changamoto kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu pamoja na huduma za jamii.



Diwani huyo alisema kwamba kwa sasa tarafa hiyo changamoto pekee iliyokuwepo ni suala la wafanyakazi wa kampuni ya chai ya Usambara Mashariki (EUTCO) kukabiliwa na tatizo la kukosa mishahara kwa wakati.



Alisema wafanyakazi hao wanaweza kukaa miezi mitatu hadi minne hawalipwi mishahara yao na kufanya maisha kwa upande wao kuwa magumu ikiwemo kukabiliwa na madeni mitaani.



Pia alisema kuwa kutokana na kata hiyo kuzungukwa na mashamba makubwa ya chai, serikali ingewasaidia wananchi kupata maeneo ambayo mwekezaji ameshindwa kuyaendeleza wapewe wananchi wafanye Makazi pamoja na mashamba ya kulima.



Mapema mgeni rasmi katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Tanga, Nassor Makau aliyemwakilisha Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah aliwataka wananchi wa Muheza kuwachagua wagombea wa CCM kwa kuwa Chama hicho kimekuja na ilani inayotekelezeka.



Alisema wananchi Wana Kila sababu ya kuwachagua wagombea wa CCM kwakuwa katika kipindi cha miaka mitano miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati imetekelezwa kwa kiwango kikubwa katika mkoa wa Tanga na Muheza kwa ujumla.



Amewaomba wananchi wampigie kura mgombea Urais wa Chama hicho Dkt Samia Suluhu Hassan, mbunge pamoja na madiwani ili waweze kushirikiana kuleta maendeleo na kamwe wasiwachague wagombea wa upinzani.



Mwisho