MANARA: AWESO CUP INA DOUMBIA WENGI

September 13, 2026



Na Oscar Assenga, PANGANI

MSEMAJI wa Timu za Taifa za Tanzania, Haji Manara, amesema mashindano ya Aweso Cup 2026 yameibua vipaji vingi vya soka ambavyo kwa uwezo wake vinaweza kuizidi hata thamani ya mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Doumbia.

Manara alitoa kauli hiyo wakati akizungumza katika uzinduzi rasmi wa michuano hiyo uliofanyika katika Uwanja wa Sakura, Pangani, Mkoa wa Tanga, akisisitiza kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji vinavyohitaji kuibuliwa na kuendelezwa.

Kwa utani ulioibua shangwe na vicheko kutoka kwa mashabiki waliohudhuria uzinduzi huo, Manara alisema kiwango cha baadhi ya wachezaji alichokiona katika michuano hiyo kinaonyesha kuwa Pangani inaweza kuwa chanzo cha wachezaji wengi wenye uwezo wa kucheza soka la juu.

“Huyu Doumbia wa Simba anaweza kupatikana mara tano ndani ya michuano hii. Tumeshuhudia vipaji vikubwa sana hapa Pangani,” alisema Manara.

Kauli hiyo aliitoa huku akitumia fursa hiyo kuwataka wadau wa soka nchini kuendelea kuwekeza katika vipaji vya ndani badala ya kutegemea zaidi usajili wa wachezaji kutoka nje ya nchi.

Alisema Tanzania ina vijana wengi wenye uwezo mkubwa ambao wakipewa nafasi, mafunzo na mazingira mazuri wanaweza kufikia viwango vya juu na kuwa sehemu ya mafanikio ya soka la Taifa.

“Wakati mwingine badala ya kuwekeza kutafuta vipaji nje, tuna vipaji bora zaidi ndani ya Tanzania. Tusiishie tu kutafuta wachezaji nje, hata nyumbani hapa Pangani tumeona mechi zimechangamka,” alisema.

Manara, ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kariakoo, alisema idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Aweso Cup ni ishara kwamba eneo hilo lina msingi mzuri wa kukuza vipaji vya soka.

Alisema kuwepo kwa takribani timu 80 katika jimbo moja la uchaguzi kunapaswa kuwa chachu kwa viongozi na wadau wa michezo kuangalia namna ya kuviendeleza vipaji hivyo kwa ajili ya soka la baadaye.

Katika hotuba yake, Manara pia alikumbusha historia ya Pangani katika kuzalisha wachezaji wenye majina makubwa, akimtaja nyota wa zamani wa Yanga, Fadili Bwanga, ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Michuano ya Aweso Cup 2026 imeandaliwa chini ya usimamizi wa Mbunge wa Pangani ambaye pia ni Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ikiwa na lengo la kuibua na kukuza vipaji vya soka katika jimbo hilo.

Mashindano hayo yalizinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘MwanaFA’, katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na mashabiki wa soka.

Manara alimpongeza Aweso kwa kuandaa mashindano hayo na kusema hatua hiyo ni muhimu katika kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.

Aidha, aliahidi kuendelea kufuatilia michuano hiyo hadi hatua ya fainali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »