MWANA FA AZINDUA RASMI AWESO CUP ,TIMU 80 KUCHUKUANA KUMPATA BINGWA

September 13, 2026






Na Oscar Assenga, PANGANI

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’, amezindua rasmi Mashindano ya Aweso Cup katika Kijiji cha Sakura wilayani Pangani huku akizitaka klabu kubwa nchini pamoja na wadau wa soka, kufuatilia mashindano hayo kwa lengo la kuibua vipaji vipya.

Mwinjuma amesema  hayo katika Kijiji cha Sakura, Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga, wakati akizindua rasmi Mashindano ya Kombe la Aweso, yanayoshirikisha jumla ya timu 80 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Ambapo alisema Pangani ina vijana wengi wenye vipaji ambao wanahitaji kupewa nafasi ya kuonekana na watu wanaoweza kuwasaidia kufikia viwango vya juu.

Amesema uwekezaji unaofanyika leo katika michezo unaweza kuleta matokeo makubwa kwa vijana na Taifa kwa ujumla hapo baadaye.

“Ukiwekeza leo, kuna faida kubwa kesho. Tunawekeza kwenye michezo, maendeleo na utalii. Tunataka kuitoa Pangani pangoni na kuipandisha hadi kupaa angani,” amesema Mwinjuma.

Amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo, huku ikiweka mkazo pia katika ugunduzi, malezi na utunzaji wa vipaji vya vijana.

TIMU YA U17 MFANO

Mwinjuma ametumia mafanikio ya timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 (U17) kama mfano wa matokeo ya uwekezaji katika vipaji.

Amesema timu hiyo imeonyesha uwezo mkubwa kwa kufika fainali ya michuano ya Afrika, kabla ya kupoteza mchezo huo, na baadaye kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa Mwinjuma, Serikali imeendelea kusambaza mawakala na wataalamu katika maeneo mbalimbali ambako kuna mashindano ili kuhakikisha vipaji vinagunduliwa na kuendelezwa.

“Wadau wa michezo, Aweso Cup ina vipaji vingi. Kuna zaidi ya timu 80 zinazoshiriki. Tunawaomba wadau wa timu za Taifa, Simba, Yanga na klabu nyingine waje kuwaona vijana hawa kwa sababu wanaweza kufanya mambo makubwa,” amesema.

Amesema ni wakati sasa kwa wadau wa michezo kuanza “kuwathamini vyao” kwa kuwapa vijana wa Pangani na maeneo mengine nafasi ya kuonyesha uwezo wao.

Mashindano ya Aweso Cup yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa vijana wa Pangani kuonyesha vipaji vyao, huku wadau wa michezo wakitarajiwa kutumia mashindano hayo kama sehemu ya kutafuta wachezaji wenye uwezo wa kuendelezwa zaidi.

Awali akizungumza  Waziri wa Maji na Mbunge wa Pangani kwa tiketi ya CCM, Jumaa Aweso, amewataka wadau wa michezo nchini kujitokeza katika mashindano mbalimbali ili kubaini na kuendeleza vipaji vya vijana.

Amesema mashindano hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwapa vijana nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika michezo, huku akisisitiza kuwa uwepo wa viongozi, makocha na wadau wengine ni muhimu katika kuwasaidia vijana wenye vipaji kufikia hatua kubwa zaidi.

“Wadau wa michezo tunapaswa kujitokeza katika mashindano kama haya kwa sababu hapa ndipo vipaji vinapopatikana. Vijana wanahitaji kuonekana, kutambuliwa na kupewa nafasi ya kuendeleza vipaji vyao,” alisema Aweso.

Amesema uwekezaji katika michezo unaweza kuwa sehemu muhimu ya kuwainua vijana kiuchumi, ikiwamo kuwapatia ajira na fursa nyingine kupitia michezo pamoja na sekta ya utalii.

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo (DAS), Esther Gama, alisema mashindano hayo yatachezwa kwa mfumo wa mtoano (Knock-out) na kutaja zawadi nono zinazowasubiri washindi ambapo Mshindi wa Kwanza (Bingwa):Tsh Milioni 10, Mshindi wa Pili: Tsh Milioni 5,Mshindi wa Tatu: Tsh Milioni 3 huku Kikundi Bora cha Ushangiliaji: Pikipiki aina ya Boxer.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »