RISITI YA SH1.4 MILIONI YAMUINGIZA MATATANI

September 15, 2026




Na Mwandishi Wetu, LUSHOTO

MAHAKAMA ya Wilaya ya Lushoto imemtia hatiani mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi katika eneo la Soni, Issack Vitales Msigiti, kwa kosa la rushwa baada ya kushindwa kutoa risiti ya EFD yenye thamani ya Sh1,497,057.

Mshtakiwa huyo amehukumiwa kulipa faini ya Sh500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia katika Shauri la Rushwa Na.17811/2026.

Akizungumza katika Taarifa yake hivi karibuni Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga Ramadhani Ndwatah alisema hukumu  hiyo ilitolewa Agosti 11, 2026, mbele ya Hakimu Kavumo Masewa Mndeme, ambaye alisikiliza shauri hilo lililoendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), John Chihangala.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka TAKUKURU, Msigiti alikutwa na hatia kwa kujipatia manufaa kwa kutotoa risiti ya EFD ya Sh1,497,057, jambo lililosababisha kukadiriwa kwa kiwango pungufu cha kodi katika makadirio ya mwaka uliofuata.

Taarifa hiyo ilisema suala hilo lilianza kubainika kupitia taarifa za kiintelijensia zilizopokelewa Agosti 5, 2026, na baadaye kufanyika kwa uchunguzi maalumu uliodumu kwa siku tatu, kuanzia Agosti 8 hadi 10, 2026.

Mshtakiwa alishtakiwa kwa kosa la rushwa kinyume na Kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329, Marejeo ya 2024.

Baada ya mahakama kumtia hatiani, ilimpa chaguo la kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miaka mitatu.

Hata hivyo, Msigiti alilipa faini hiyo na hivyo kuepuka kutumikia kifungo.

TAKUKURU imeendelea kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuzingatia sheria na taratibu za kodi, ikiwamo utoaji wa risiti za EFD, ili kuepusha migogoro na hatua za kisheria.


TAKUKURU (M) TANGA – LUSHOTO

Septemba 15, 2026

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »