ENG.JOYCE BARAVUGA- SHULE ZIHAKIKISHE MAFUNZO YA TEHAMA YANAENDELEA

September 14, 2026

Mratibu wa Mafunzo ya Kidijitali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Eng. Joyce Baravuga, amesema mafanikio ya Mradi wa Kuziba Pengo la Kidijitali: Kuhakikisha Elimu ya Ujuzi wa Kidijitali Inayozingatia Usawa wa Kijinsia kwa Wanawake na Wasichana (Closing the Digital Divide: Ensuring Gender-Transformative Digital Skills Education for Women and Girls) yatategemea kwa kiasi kikubwa utayari wa shule kuendeleza mafunzo na shughuli za Klabu za TEHAMA (ICT Clubs) baada ya kumalizika kwa Kambi ya Mafunzo (Boot Camp).

Eng. Baravuga amewapongeza wakuu wa shule zilizochaguliwa kushiriki katika programu hiyo, akisema utayari na uthubutu wa shule ni miongoni mwa vigezo vilivyozingatiwa katika uteuzi.

Amesema shule hizo zinapaswa kuwa wadau muhimu wa programu hiyo kwa kuhakikisha maarifa na ujuzi unaopatikana kupitia mafunzo unaendelea kutumika shuleni na kuwafikia wanafunzi wengine.

Amewataka walimu na wakuu wa shule kuhakikisha Klabu za TEHAMA zinaendelea baada ya wanafunzi kurejea shuleni, ili kuwapa wasichana nafasi ya kuendelea kujifunza, kufanya mazoezi na kuendeleza ubunifu wao katika teknolojia.

Aidha, amewataka walimu, hususan wanaohusika na TEHAMA, kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo na kuhakikisha maarifa yanayopatikana hayabaki kwa wanafunzi walioshiriki pekee, bali yanawafikia wanafunzi wengine shuleni.

Eng. Baravuga pia amesisitiza umuhimu wa kukusanya taarifa za utekelezaji wa shughuli za mafunzo kila siku, akisema taarifa hizo zitasaidia kupima mafanikio ya programu, kubaini changamoto na mapungufu, pamoja na kuweka msingi wa kuboresha utekelezaji katika hatua zijazo.

Amesema ukusanyaji wa taarifa kwa wakati utasaidia pia kutambua maeneo yanayohitaji kupewa msukumo zaidi na kuhakikisha malengo ya programu yanafikiwa.

Vilevile, amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kuchaguliwa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa bila upendeleo, ili kuhakikisha fursa zinazotolewa kupitia programu hiyo zinawafikia walengwa kwa usawa.

Eng. Baravuga amesema ushiriki wa shule, walimu na viongozi wa shule ni muhimu katika kuhakikisha Kambi ya Mafunzo haibaki kuwa tukio la muda mfupi, bali inakuwa mwanzo wa kujenga mazingira endelevu ya kujifunza, kutumia na kubuni kupitia TEHAMA miongoni mwa wanafunzi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »