TUME YA TAIFA YA UNESCO YASHIRIKI JUKWAA LA NNE LA KIMATAIFA LA MAADILI YA AKILI UNDE RIYADH RIYADH, SAUDI ARABIA:

September 15, 2026



 Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki katika Jukwaa la Nne la Kimataifa la Maadili ya Akili Unde linaloendelea mjini Riyadh, Saudi Arabia, likiwakutanisha wawakilishi kutoka nchi mbalimbali duniani kujadili namna ya kuhakikisha maendeleo na matumizi ya akili unde yanaongozwa na maadili, uwajibikaji na kuhudumia maslahi ya jamii.

Jukwaa hilo linatoa nafasi kwa nchi na wadau mbalimbali kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayohusu mustakabali wa akili unde, ikiwemo namna ya kuimarisha mifumo ya sera na utawala, kujenga uwezo na kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa kuzingatia haki za binadamu, usalama, usawa na uwajibikaji.

Kwa Tume ya Taifa ya UNESCO, ushiriki huo ni sehemu ya kuendelea kuunganisha Tanzania na UNESCO katika mijadala na ajenda za kimataifa zinazohusu sayansi, teknolojia, elimu, utamaduni na maendeleo ya jamii.

Tume inawakilishwa katika jukwaa hilo na Bi Fides Mallya, Afisa Programu kutoka Sekta ya Sayansi Jamii ya Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anayeshiriki katika shughuli na mijadala mbalimbali inayoendelea katika jukwaa hilo.

TUME YASHIRIKI MJADALA WA AFRIKA

Katika jukwaa hilo, Tume ya Taifa ya UNESCO inashiriki pia katika mjadalawa viongozi na wadau kutoka Afrika unaolenga kujadili namna bara hilo linavyoweza kuwezeshwa ili kunufaika kikamilifu na maendeleo ya teknolojia ya akili unde.

Mjadala huo unaangazia umuhimu wa Afrika kuimarisha uwezo wake katika sayansi, teknolojia, utafiti, ubunifu na ujuzi wa kidijitali, pamoja na kujenga mazingira bora ya kisera na kitaasisi yatakayowezesha matumizi salama na yenye tija ya akili unde.

Kwa kushiriki katika mjadala huo, Tume inaendelea kufuatilia mwelekeo wa kimataifa kuhusu akili unde na kuchangia katika mijadala inayolenga kuhakikisha maendeleo ya teknolojia hiyo yanazingatia mahitaji ya jamii na yanachangia maendeleo jumuishi na endelevu.

USHIRIKI WA TUME WAIUNGANISHA TANZANIA NA UNESCO

Ushiriki wa Tume katika jukwaa hilo unaonesha nafasi yake muhimu kama kiungo kati ya Tanzania na UNESCO, kwa kuwezesha ushiriki wa nchi katika mijadala, programu na ajenda za UNESCO katika ngazi ya kimataifa.

Kupitia majukwaa hayo, Tume inaendelea kufuatilia maendeleo na mwelekeo wa kimataifa katika maeneo ya UNESCO, kubadilishana uzoefu na nchi nyingine na kutafuta fursa za ushirikiano zinazoweza kuchangia maendeleo ya Tanzania.

Katika eneo la akili unde, ushiriki huo unaipa Tume fursa ya kufuatilia mijadala kuhusu maadili, utawala na matumizi yanayowajibika ya teknolojia hiyo, huku ikiendelea kuhusisha mijadala ya kimataifa na mahitaji ya maendeleo ya Tanzania.

UJUMBE WA TUME WAKUTANA NA BALOZI

Katika mwendelezo wa ushiriki wa Tume katika jukwaa hilo, ujumbe wa Tanzania unaoshiriki katika shughuli za jukwaa umepata fursa ya kufanya kikao na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia.

Kikao hicho kimekuwa fursa ya kubadilishana taarifa kuhusu ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo na kuimarisha uratibu kati ya ujumbe wa Tanzania na Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia katika masuala yanayohusu shughuli za kimataifa.

Jukwaa la Nne la Kimataifa la Maadili ya Akili Unde linaendelea mjini Riyadh likiwa sehemu ya juhudi za kimataifa za kuimarisha ushirikiano katika kuhakikisha maendeleo ya akili unde yanaenda sambamba na maadili, uwajibikaji, haki za binadamu na maendeleo jumuishi.


Share this

Related Posts

Previous
Next Post »