Showing posts with label biashara. Show all posts
Showing posts with label biashara. Show all posts

MBARAWA AFUNGUA MILANGO YA AJIRA ZA BAHARINI KWA VIJANA WASIOSOMA SAYANSI

Kajunason June 25, 2026 Add Comment

Uchumi wa Bluu Kunufaika na Elimu ya Ubaharia

Na Mwandishi Wetu, Kigoma

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Serikali itaendelea kukiunga mkono Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) katika jitihada zake za kuanzisha kozi ya awali ya ubaharia itakayowawezesha vijana wengi zaidi wa Kitanzania kupata elimu ya sekta hiyo na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa bluu.

Profesa Mbarawa ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la DMI katika kilele cha Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika mkoani Kigoma, ambapo alieleza kuwa kozi hiyo ni suluhisho kwa vijana wengi wenye ndoto za kuwa mabaharia lakini ambao hawakupata nafasi ya kusoma masomo ya sayansi yanayohitajika kujiunga na taaluma hiyo.

Alisema DMI imebuni mpango huo mahsusi ili kuwapa vijana hao fursa ya kupata msingi wa masomo muhimu yatakayowawezesha kuendelea na mafunzo ya ubaharia na hatimaye kuingia katika soko la ajira la sekta ya usafiri wa majini.

“DMI inafanya kazi kubwa ya kuangalia namna ya kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa za elimu ya ubaharia. Kozi hii ya awali itawasaidia wale ambao hawakusoma masomo ya sayansi kupata msingi unaohitajika na hatimaye kujiunga na mafunzo ya ubaharia,” alisema Profesa Mbarawa.
Alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuongeza idadi ya mabaharia wenye ujuzi na sifa zinazotambulika kitaifa na kimataifa, huku ikilenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika ajira za sekta ya bahari na usafiri wa majini duniani.

Waziri huyo pia alimpongeza Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, kwa ubunifu na juhudi zake za kuendeleza programu mbalimbali za mafunzo zinazowawezesha mabaharia wa Tanzania kufikia viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika sekta ya usafiri wa majini.

“Tunakipongeza DMI kwa juhudi zake za kubuni na kuendeleza mafunzo yanayowawezesha mabaharia wetu kuwa na sifa zinazokubalika kimataifa. Mabaharia wanazunguka dunia nzima, hivyo ni lazima waandaliwe kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya sekta ya kimataifa,” alisema Profesa Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha DMI, Profesa Tumaini Gurumo, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho katika kuzalisha wataalamu wenye tija na ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Profesa Gurumo alisema kutokana na asili ya kazi ya ubaharia inayowafanya mabaharia kufanya kazi na kusafiri katika mataifa mbalimbali duniani, ni muhimu kwao kupata elimu na stadi zinazotambulika kimataifa ili waweze kushindana kwa ufanisi katika soko la ajira la dunia.

Aliongeza kuwa DMI itaendelea kupanua na kuboresha mafunzo ya bahari ili kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata elimu na ujuzi unaohitajika kwa taifa kunufaika na fursa zilizopo katika uchumi wa bluu na sekta ya usafiri wa majini.

Maadhimisho ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani yamewakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya bahari na usafiri wa majini kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa mabaharia katika kukuza biashara, uchumi na maendeleo ya jamii duniani.

SMZ YATAJA MAFANIKIO YA BIMA YA LAZIMA KWA WAGENI

Kajunason June 07, 2026 Add Comment
Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 kutangaza mafanikio ya mpango wa bima ya lazima kwa wasafiri, ikieleza kuwa umeimarisha usalama wa wageni na kuchangia ukuaji wa sekta ya afya pamoja na mapato ya utalii visiwani humo.

Mpango huo ulioanza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024, unawataka wageni wote wa kimataifa wanaoingia Zanzibar kuwa na bima ya usafiri kabla ya kuwasili. Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato, ukiingiza wastani wa dola za Marekani milioni moja, sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.6 kila mwezi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenye viwanja vya Magereza jijini Arusha, Ofisa Mauzo wa shirika hilo, Abdul-Halim Muhammad, alisema maonesho hayo yamewapa fursa ya kutoa elimu kwa watalii, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuhusu umuhimu wa bima hiyo.

“Tunashiriki Karibu-KiliFair kuongeza uelewa kuhusu bima hii ya lazima na kueleza namna inavyowanufaisha wageni huku ikichangia maendeleo ya huduma muhimu Zanzibar,” alisema.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, wageni wengi wa kimataifa hulipa dola 44 za Marekani kwa kila safari ya kuingia Zanzibar, huku wageni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakilipia dola 22 pekee. Watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 hulipa dola 22, huku walio chini ya umri huo wakisamehewa.

Muhammad alisema bima hiyo inawawezesha wageni kupata huduma za matibabu ya dharura na msaada mwingine muhimu wanapokuwa Zanzibar, hatua inayopunguza changamoto za kifedha na kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka wanapozihitaji.

Alisema sehemu ya mapato yanayokusanywa kupitia mfuko huo hutumika kugharamia huduma za afya kwa wageni waliokatiwa bima, huku fedha zinazobaki zikielekezwa katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi na wageni kwa ujumla.
“Mpango huu ulianzishwa baada ya mamlaka kubaini kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya watalii na wawekezaji kuhitaji matibabu ya dharura huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani angegharamia huduma hizo. Sasa mfumo huu umeondoa changamoto hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KiliFair Promotions, Dominic Shoo, alisema Karibu-KiliFair 2026 imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama maonesho makubwa ya utalii na biashara Afrika Mashariki kwa kuwakutanisha wadau kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.

Alisema maonesho hayo yamevutia zaidi ya waoneshaji 500 na wanunuzi wa huduma za utalii wapatao 20,000, hatua inayochochea uwekezaji, ushirikiano wa kibiashara na upanuzi wa masoko ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Karibu-KiliFair ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kimataifa. Kadri wadau wanavyoongezeka kushiriki, ndivyo fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa sekta ya utalii zinavyozidi kuongezeka,” alisema Shoo. 

MAADHIMISHO YA 11 YA UTAFITI NA UBUNIFU UDSM KUANGAZIA UCHUMI WA KIDIJITALI

Kajunason June 07, 2026 Add Comment
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinatarajia kuadhimisha Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu kuanzia Juni 9 hadi 11, 2026, katika Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, huku Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Maadhimisho hayo yatakayowakutanisha watafiti, wabunifu, wanafunzi, sekta binafsi, taasisi za umma na wadau wa maendeleo, yanalenga kuonesha mchango wa utafiti na ubunifu katika kuharakisha maendeleo ya taifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti, Profesa Nelson Boniface, alisema maadhimisho ya mwaka huu yataongozwa na kaulimbiu isemayo: "Kutumia Utajiri wa Madini wa Tanzania katika Kukuza Nishati Jadidifu, Mageuzi ya Kidijitali na Usalama wa Jamii."

Alisema kaulimbiu hiyo imechaguliwa kutokana na umuhimu wa madini katika maendeleo ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Mnemba (AI), vituo vya kuhifadhi taarifa (Data Centres), magari ya umeme na nishati jadidifu.

“Tunataka kuonesha namna Tanzania inaweza kutumia rasilimali zake za madini kuchochea mageuzi ya kidijitali, kuimarisha usalama wa nishati na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Profesa Boniface.

Aliongeza kuwa maadhimisho hayo yatahusisha maonesho ya tafiti na ubunifu, mawasilisho ya kitaaluma, makongamano pamoja na majadiliano ya ushirikiano wa kimkakati yatakayowawezesha washiriki kubadilishana maarifa na kujenga mitandao ya kitaaluma na kibiashara.

Kwa mujibu wa UDSM, maadhimisho hayo yatatoa nafasi kwa watafiti na wabunifu kuonesha suluhisho mbalimbali za kisayansi na kiteknolojia zinazolenga kukabiliana na changamoto za maendeleo nchini katika sekta za madini, nishati, kilimo, afya na uchumi wa kidijitali.

Profesa Boniface alisema chuo kinaendelea kutumia maadhimisho hayo kama jukwaa la kuunganisha taaluma, ubunifu na maendeleo ya taifa kwa kuwafikia wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo.

"Utafiti na ubunifu ni msingi wa maendeleo endelevu. Tunawaalika Watanzania wote kushiriki katika Maadhimisho ya 11 ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu UDSM 2026 ili kujionea kazi na mafanikio ya watafiti na wabunifu wetu," alisema.

TEMESA NA TOYOTA WAJADILI MAGEUZI YA HUDUMA ZA MATENGENEZO YA MAGARI NCHINI

June 03, 2026 Add Comment

.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania - TEMESA, Bw. Kheri Mahimbali, leo tarehe 02 Juni 2026 amekutana na viongozi wa kampuni ya TOYOTA Tanzania katika ofisi zao eneo la Posta, jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili kuhusu jitihada za Serikali katika kuendelea kuboresha huduma za matengenezo ya magari hapa Nchini. 

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mahimbali amesema TEMESA imejipanga kuhakikisha huduma za ufundi na matengenezo ya magari ya Serikali  zinatolewa kwa viwango vya juu kwa kutumia teknolojia za kisasa na za viwango vya kimataifa.

“TEMESA inaona fursa kubwa katika kuimarisha ushirikiano na TOYOTA kupitia miradi ya pamoja itakayowezesha taasisi hizi mbili kubadilishana utaalamu kwa mafundi na kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa kwa wadau wetu,” amesema Mtendaji Mkuu.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa TOYOTA Tanzania, Bw. Jatin Pandya amehakikisha utayari wa kampuni hiyo kuendelea kushirikiana na TEMESA katika mafunzo ya kitaalamu kwa mafundi, ushauri wa kiufundi, matumizi ya teknolojia mpya na kuimarisha mifumo ya usalama wa magari.

“Sisi TOYOTA tunatanguliza usalama wa watumiaji wa magari na ubora wa huduma. Tunaamini ushirikiano huu utachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za matengenezo ya magari nchini na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani,” amesisitiza Pandya.

Aidha, mara baada ya kikao hicho, Mtendajji mkuu pia alipata fursa ya kufanya ziara fupi katika karakana za TOYOTA ili kujionea teknolojia mpya zinazotumika katika matengenezo ya magari.

Miongoni mwa mambo waliyojadili katika kikao hicho ni pamoja na uwezekano wa kuanzisha ushirikiano kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi - PPP. Hatua inayotarajiwa kuimarisha uwezo wa karakana na kuongeza ufanisi wa huduma katika sekta ya matengenezo ya magari.

Kikao hicho kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya TEMESA na TOYOTA, huku kikitarajiwa kuwa chachu ya mageuzi makubwa katika sekta ya ufundi wa magari nchini.


JUKWAA LA WANAWAKE NA KODI NI HATUA MUHIMU YA KUENDELEZA USAWA WA KIJINSIA NA KUKUZA UCHUMI SHIRIKISHI -CPA CASTRO

May 14, 2026 Add Comment



 Na Paskal Mbunga, Tanga

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga imesema kwamba Jukwaa la Wanawake na Kodi ni hatua muhimu inayodhihirisha dhamira ya kuendeleza usawa wa kijinsia na kukuza uchumi shirikishi nchini.

Hayo yalisemwa na  Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Tanga, CPA Castro John wakati akifungua Jukwaa la Wanawake na Kodi ambapo  alisema ni dhamira ya dhati ya kujenga mfumo wa kodi unaoshirikisha makundi yote ya jamii, hususan wanawake ambao ni nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa.


Alisema takwimu zinaonesha wanawake wanachangia kwa kiwango kikubwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo biashara ndogondogo, kilimo, huduma, viwanda vidogo pamoja na biashara za kati na kubwa.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024/2025, wanawake nchini, wakiwemo wa Mkoa wa Tanga, wanakadiriwa kushiriki katika nguvu kazi kwa asilimia 80, huku wakimiliki asilimia 54 ya biashara ndogo, za kati na kubwa.

“Bila ushiriki wa wanawake, juhudi za kuongeza wigo wa walipa kodi na kuongeza mapato ya ndani haziwezi kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema CPA Casto John.

Alifafanua kuwa TRA imeanzisha Jukwaa hilo maalumu kwa lengo la kutoa elimu sahihi ya kodi, kusikiliza changamoto za wanawake wafanyabiashara, kujenga ushirikiano wa karibu pamoja na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati.

Aidha, alisema TRA imejikita katika kuboresha huduma kwa kuzingatia ushirikishwaji, uwazi, weledi na urahisi wa upatikanaji wa huduma. Aliongeza kuwa elimu ya kodi na mahusiano bora ni msingi muhimu wa kuongeza utii wa kodi.

Kupitia jukwaa hilo, wanawake watapata nafasi ya kupata ushauri kuhusu masuala ya kodi, kujifunza fursa mbalimbali pamoja na kuelewa wajibu wao wa kikodi.

“Tunataka mwanamke ajisikie salama, aheshimiwe na ashiriki kikamilifu katika mfumo wa kodi bila hofu wala kikwazo chochote,” alisema.

CPA Casto John alisisitiza kuwa kodi ndiyo injini ya maendeleo ya Taifa kwani mapato yake yanagharamia huduma muhimu kama elimu, afya, barabara, maji safi na miradi mingine ya kimkakati.

“Kila mwanamke anayelipa kodi anakuwa mshirika wa moja kwa moja wa Serikali katika kujenga Tanzania yenye uchumi imara na huduma bora kwa wananchi wake,” aliongeza.

Pia aliwataka wanawake kutumia jukwaa hilo kujifunza, kuuliza maswali na kuwa mabalozi wa utamaduni wa kulipa kodi katika jamii zao.

Aidha, aliwataka wadau wa sekta mbalimbali pamoja na taasisi za kifedha kuendelea kushirikiana na TRA katika kuwawezesha wanawake kukuza biashara zao kwa kuzingatia misingi ya kikodi.

Kwa upande mwingine, aliwahimiza wanawake wafanyabiashara kujisajili katika mfumo wa kodi na kutekeleza wajibu wao kwa hiari na kwa wakati.

“Kulipa kodi si wajibu wa kisheria tu, bali ni mchango wa moja kwa moja katika kujenga Taifa. Wanawake wakisimama kiuchumi, familia na jamii vinaimarika,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisisitiza umuhimu wa kutumia mipaka rasmi ya biashara kwa wafanyabiashara wanaovuka mipaka kupitia maeneo ya Horohoro na Pangani, huku akiwataka kuachana na biashara za magendo na matumizi ya njia zisizo rasmi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, JW Ismail Masound, alisema jukwaa hilo lina umuhimu mkubwa kutokana na malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050 ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuwa mhimili mkubwa wa ukuaji wa uchumi.

Alisema majukwaa hayo yanasaidia kuwawezesha wanawake na wafanyabiashara kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa kwa kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake Mkoa wa Tanga (TWCC), Aziza Ramadhani, alisema jukwaa hilo litawasaidia wanawake kuelewa umuhimu wa kulipa kodi katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.

“Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha Mkoa wa Tanga unalipa kodi kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya jamii,” alisema.

Aliongeza kuwa jukumu la jukwaa hilo ni kuwaunganisha wanawake wa Mkoa wa Tanga ili kuwapa nafasi ya kujifunza, kushirikiana na kupata fursa mbalimbali za kiuchumi ndani na nje ya mkoa huo.

Aidha, alisema wamekuwa wakitoa mafunzo mbalimbali ikiwemo kuanzisha mashamba darasa kwa vijana wa kiume na wa kike, huku akiwakaribisha wanawake wajasiriamali kushiriki katika shughuli za maendeleo zinazochangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla.