WAKUU WA TAASISI ZA MUUNGANO WATAKIWA KUIMARISHA UTOAJI HUDUMA KWA WANANCHI

September 19, 2026
ZANZIBAR, Septemba 19, 2026 — Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka Wakuu wa Taasisi za Muungano kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa majukumu yao ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora bila kujali wanaishi upande gani wa Muungano.

Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo leo Septemba 19, 2026, wakati akifungua kikao maalum cha Wakuu wa Taasisi za Muungano kilichofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Airport, Zanzibar.

Kikao hicho kimejadili masuala mbalimbali yanayohusu uratibu na utekelezaji wa masuala ya Muungano, huku Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Dkt. Erasmus Kipesha, akiwa miongoni mwa Wakuu wa Taasisi walioshiriki.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ndejembi amesema kila Mkuu wa Taasisi anapaswa kuwa na uelewa wa maana ya Muungano pamoja na dhana na majukumu yanayohusiana na masuala ya Muungano.

Amesema kila Mtanzania anahitaji huduma bora na kwamba jukumu la kuhakikisha huduma hizo zinapatikana ni la Taasisi za Muungano, ambazo zinapaswa kushirikisha Serikali zote mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

“Lengo la kikao hiki ni kukumbushana, kuboresha na kuimarisha Muungano kwa kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora zinazotolewa na taasisi zetu,” amesema Mhe. Ndejembi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa Wakuu wa Taasisi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, akieleza kuwa wananchi wanachohitaji zaidi ni huduma bora, bila kujali mipaka ya kiutendaji au kitaasisi.

Amesema Serikali na Taasisi zake zinapaswa kutambua kuwa “tunajenga nyumba moja”, hivyo kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi na kushirikiana na taasisi nyingine kwa maslahi ya wananchi.

Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uratibu na utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Muungano katika kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinazingatia misingi ya ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »