Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akitoa nasaha kwa waumini (hawapo pichani) waliohudhuria
Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid
Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waumini wa
dini ya Kiislamu waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid
Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro
wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa nasaha za Eid,
tarehe 26 Juni, 2017. (
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiteta jambo na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally wakati wa stafutahi kwenye Ikulu ndogo ya Moshi, mara baada ya Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally mara baada ya stafutahi kwenye Ikulu ndogo ya Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha maombolezo, nyumbani kwa marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akitoa pole na neno la faraja kwa wanafamilia, nyumbani
kwa marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akimpa pole mjane wa marehemu, mama Ndehorio P.
Ndesamburo alipofika nyumbani kwao eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa Dk. Philemon Ndesamburo, leo tarehe 26 Juni, 2017.
Kaka wa
marerehemu Dk. Philemon Ndesamburo, Bw. Zablon Sindato Kihwelu
akimshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika nyumbani kwao eneo la
Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa Dk. Philemon Ndesamburo, leo tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Anna Mgwira (wa tatu
kushoto), mjane wa marehemu na Kaka wa marehemu wakiomba dua na
wanafamilia kwenye kaburi la Dk. Philemon Ndesamburo, aliyezikwa
nyumbani kwake eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro. Wa kwanza kulia ni mtoto wa marehemu.
……………………………………………………………………….
*Ahimiza nyumba za ibada zisaidie vita ya dawa za kulevya
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi
kuanzia leo. “Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao
ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha
uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni
lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo
(Jumatatu, Juni 26, 2017) wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid
lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi,
mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid.
“Jana nimeona kwenye televisheni
taarifa kuhusu malori 10 yaliyokamatwa Tarakea yakiwa na mahindi tayari
kuvushwa mpaka. Mheshimiwa RC akasema chakula hicho ni lazima
yarudishwe kwa ajili ya usagaji.”
“Mimi nasema kuanzia leo, yeyote
atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho
kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na
litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo la kuwalinda
Watanzania tusikumbwe na baa la njaa.”
Akitoa tahadhari kuhusu uuzwaji
wa chakula nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na wimbi kubwa la
usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila kibali. “Hilo ni kosa
kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu kupata baa la njaa huko mbele,”
amesema.
Amesema mipaka ya Tarakea,
Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari imekuwa inapitisha
kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jambo ambalo ni
hatari sana. “Hii ni kwa sababu chakula cha ndani hakitoshelezi
mahitaji. Kwa sababu nchi zote za jirani hazina chakula cha kutosha.
Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia njaa.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuwasihi wafanyabiashara wa ndani, wachukue mahindi kutoka maeneo yenye
mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu zenye mavuno kidogo.
“Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe huku kwenye mavuno
mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako wanayahitaji au tukanunue
Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine yenye upungufu,”
alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewataka viongozi wa dini waisadie Serikali katika mapambano dhidi
ya dawa za kulevya kwa kupitia kwenye nyumba za ibada. “Naomba
tuendelee kushirikiana kupambana na janga hili la dawa za kulevya kwa
ustawi wa nchi yetu. Naamini viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa katika
mapambano haya, kwa kuwafunda vijana wetu kuishi katika maadili ya
kidini na kutojiingiza kwenye janga hilo.”
Alisema Serikali kwa upande wake
itaendeleza mapambano hayo bila ajizi wala mzaha. “Tunaomba wananchi
wote watuunge mkono kwa kutoa taarifa sahihi za wanaojihusisha na
uzalishaji, utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya
pindi tu wanapowabaini.”
Wakati huo huo, akitoa tafsiri ya
Qur’aan tukufu kwenye Baraza la Eid, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Sheikh
Shaaban Juma alisema kila nguzo katika Uislamu inapaswa kufuatwa na
kwamba mtu akiharibu nguzo moja tu anakuwa ameharibu nguzo zote tano.
Alisema siku ya kiyama, watatokea
watu wenye thawabu kama milima ya Usambara ama Upareni na akawataka
Waislamu wote nchini wadumu katika kutenda mema ili wapate thawabu.
Mapema, akitoa khutba katika swala ya Eid el Fitr iliyoswaliwa
kwenye msikiti huohuo wa Masjid Riadha, Sheikh Mlewa Shaban alisema
sikukuu ya Eid ni siku ya kujiepusha na madhambi kama ulevi, kamari na
lugha chafu, bali aliwataka waumini wote waitumie siku hiyo kuwapa
furaha maskini, yatima na wajane.
“Mtu asiseme mwezi wa Ramadhan
umepita, sasa narudia mambo yangu ya zamani. Adhabu za Mwenyezi Mungu
hazina mipaka na wale waliotulizana watapata thawabu yao, kumbukeni
neema na Mwenyezi Mungu na mcheni Mwenyezi Mungu.”
“Kitu tunachopaswa kufanya kila
wakati ni kumcha Mwenyezi Mungu. Lazima tupendane, tuondoe tofauti zetu
na tuujenge Uislam. Hatuwezi kuujenga uislam kama hatupendani. Lazima
tuilinde ibada yetu kwa sababu hatuna garantii, ni lini tutaondoka,”
alisema.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na
Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally;
Wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe; Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira; IGP
Mstaafu, Bw. Said Mwema; Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Jaffary Michael;
Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.
EmoticonEmoticon