RAS TANGA AHAKIKISHA UTAYARI WA WIKI YA FEDHA

January 15, 2026

                  

                 Na Chedaiwe Msuya na Eva Ngowi, WF, Tanga


Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga (RAS), Bw. Rashid Mchatta, amewahakikishia wadau wa sekta ya fedha kuwa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yatakayofanyika jijini Tanga yatakuwa na mafanikio makubwa kutokana na maandalizi madhubuti na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau husika.

Bw. Mchatta alitoa kauli hiyo ofisini kwake jijini Tanga wakati alipokutana na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, waliowasili mkoani humo kwa ajili ya maandalizi ya maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026, katika Viwanja vya Usagara.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Mchatta alisema Serikali ya Mkoa imejipanga kikamilifu kuhakikisha maadhimisho hayo yanawafikia wananchi wengi iwezekanavyo, akibainisha kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Halmashauri na Taasisi nyingine za Serikali zitatumika kuhamasisha ushiriki wa wananchi.

“Tutahakikisha uhamasishaji unafanyika vya kutosha ili wananchi wa makundi yote wakiwemo watumishi wa umma, wajasiriamali, vikundi mbalimbali, waendesha bodaboda na wakazi wote wa Jiji la Tanga wanashiriki kikamilifu,” alisema Bw. Mchatta.

Kwa upande wao, wataalamu kutoka Wizara ya Fedha walieleza kuwa lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuwawezesha wananchi kupata elimu sahihi ya fedha, ili waweze kutumia huduma za kifedha kwa tija na hatimaye kujikwamua kiuchumi.

Walifafanua kuwa licha ya wananchi wengi kupata mikopo, ruzuku na fursa mbalimbali za uwezeshaji, changamoto ya uelewa mdogo wa elimu ya fedha imekuwa ikiwafanya washindwe kufikia matokeo yaliyokusudiwa, hali inayochangia kushindwa kwa miradi mingi ya kiuchumi.

Katika kuimarisha maandalizi, Bw. Mchatta aliomba Wizara ya Fedha kuendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Halmashauri, huku akiahidi ushirikiano wa dhati na utatuzi wa changamoto zozote zitakazojitokeza kabla na wakati wa maadhimisho.

Naye Mchumi Mkuu, kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Thobias Kanyoki, kwa niaba ya Timu ya Wizara ya Fedha, alimshukuru Bw. Mchatta na uongozi wa Mkoa wa Tanga kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha tangu kuwasili kwao mkoani humo.

Alisema ushiriki wa Serikali ya Mkoa ni muhimu sana, hasa katika kuhakikisha wananchi wengi wanapata elimu ya fedha, kwani taasisi zote za kifedha zinatarajiwa kushiriki na kutoa huduma pamoja na elimu katika Viwanja vya Usagara wakati wa maadhimisho hayo.

“Wananchi wa Jiji la Tanga wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha ili kupata elimu ya fedha kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi. Hudhuria Wiki ya Huduma za Fedha – Jifunze, Jiwezeshe, Jikwamue Kiuchumi.” Alisema Bw. Kanyoki.


Katibu Tawala Mkoa wa Tanga (RAS), Rashid Mchatta, akizungumza na Timu ya Uratibu ya Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kutoka Wizara ya Fedha katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jiji la Tanga kuhusu maandalizi ya maonyesho hayo, yanayotarajia kufanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga.
Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu, kutoka Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bw. Salim Kimaro, akifafanua jambo kwa Katibu Tawala Mkoa wa Tanga (RAS), Rashid Mchatta, katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jiji la Tanga kuhusu maandalizi ya maonyesho hayo, yanayotarajia kufanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga.
 Picha ya Pamoja ya Katibu Tawala Mkoa wa Tanga (RAS), Rashid Mchatta,(katikati) akiwa na Timu ya Uratibu kutoka Wizara ya katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Jiji la Tanga kuhusu maandalizi ya maonyesho hayo, yanayotarajia kufanyika katika Viwanja vya Usagara jijini Tanga. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Tanga) 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »