DAR ES SALAAM .
Kikundi cha kijamii cha TUFANIKISHE PAMOJA kimeungana na uongozi wa The Valentine Home Centre kilichopo Kata ya Buza, Wilaya ya Temeke, kusaidia watoto yatima na wenye uhitaji.
Kituo hicho, kinachoendeshwa chini ya Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Dar es Salaam, kimekuwa kikitoa huduma za malezi, ulinzi na mahitaji muhimu kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mwenyekiti wa TUFANIKISHE PAMOJA, Bw. Daudi Tuli Abdallah, alisema msaada huo ni sehemu ya dhamira ya kikundi kurudisha kwa jamii na kusisitiza kuwa jitihada za kuwasaidia watoto zitakuwa endelevu.
> “Tunaamini kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuwajali watoto walio katika mazingira hatarishi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kituo hicho, Bw. Gao John Gao, aliipongeza TUFANIKISHE PAMOJA kwa mchango wao, akisema msaada huo haukidhi tu mahitaji ya kimwili bali pia huleta faraja na matumaini mapya kwa watoto.
Katika tukio hilo, TUFANIKISHE PAMOJA ilishiriki pia katika shughuli za kijamii ikiwemo kilimo na upandaji wa miti, pamoja na kutoa msaada wa vyakula, vifaa vya shule na mahitaji mengine ya uendeshaji wa kituo hicho.
The Valentine Home Centre kilianzishwa mwaka 2015 na kinaendelea kutoa huduma kwa watoto yatima na walio katika mazingira hatarishi Temeke na maeneo jirani.





EmoticonEmoticon