BI. NGASONGWA AONGOZA ZIARA YA FCC KUIMARISHA USHIRIKIANO NA ZFCC

January 20, 2026

Na Mwandishi wetu.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, amefanya ziara ya kikazi katika Tume ya Ushindani Halali wa Biashara Zanzibar (ZFCC) ikiwa ni hatua ya kuimarisha mashirikiano kati ya taasisi hizo mbili katika masuala ya ushindani, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia.

Bi. Ngasongwa alipokelewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ZFCC, Bi. Aliya Juma ambapo viongozi hao walifanya mazungumzo kuhusu kuendeleza ustawi wa taasisi hizo na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza katika ziara hiyo iliyofanyika tarehe 14 Januari, 2026 katika ofisi za ZFCC - Zanzibar, Bi. Ngasongwa alisema ushirikiano kati ya taasisi hizo unaendelea kuimarika kupitia utekelezaji wa Hati ya Makubaliano (MoU) yaliyokwisha sainiwa.

"FCC na ZFCC tayari zimeanza kutekeleza kwa vitendo maeneo ya ushirikiano ikiwemo kujengeana uwezo, kubadilishana uzoefu na kufanya ukaguzi wa pamoja ili kudhibiti bidhaa bandia na kulinda haki za watumiaji wa bidhaa au huduma."alisema Bi. Ngasongwa

Katika ziara hiyo, Bi. Ngasongwa pia alikutana na kuzungumza na menejimenti ya ZFCC ambapo walijadili namna ya kuendeleza mpango wa pamoja wa kuboresha mifumo ya utendaji kazi na kubadilishana taarifa.

Kikao hicho cha siku moja kilihitimishwa kwa pande zote mbili kuahidi kuendeleza juhudi za pamoja ili kuhakikisha mazingira ya biashara yanaendelea kuwa shindani, salama na rafiki kwa mlaji.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »