
Na Paskal Mbunga, Tanga.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Tanga itaanza matumizi ya drones ikiwa ni moja ya jitihada ya kupambana na biashara ya wakwepa kodi hasa katika maeneo ya mipakani.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Meneja Msaidizi wa Mkoa anayesimamia Forodha na Ushuru, Joseph Raymond alisema hatua hiyo inatokana na ongezeko la wafanyabiashara wasio waaminifu wanaopitisha biashara zao kwa kificho bila kulipia kodi stahili hasa katika maeneo ya mipakani na hivyo kukwepa kulipa kodi/ushuru kwa Mamlaka husika (TRA).
Alisema kuwa pamoja na kwamba Mkoa wa Tanga kuvuka malengo yao waliojiwekea kwa mwaka uliopita, lakini upo uwezekano mkubwa ungeongezeka zaidi iwapo ingezibwa mianya ya mipakani inayotumiwa na wafanyabiashara wasio waaminifu.
Meneja huyo wa Forodha na Ushuru alibainisha kwamba kijiografia, mkoa wa Tanga una 'matobo' mengi ya kuingia na kutoka kwa sababu ya unapakana na bahari kubwa ya India kuanzia kusini hadi kaskazini ambapo kunahitajika raslimali watu na nyenzo ili kuweza kuthibiti magendo yanayopitishwa katika bahari hiyo.
Alisema pia kwamba pamoja na kikwazo cha ba hari katika ukusanyaji mapato, lakini Mkoa wa Tanga unapakana na Kenya sehemu ya Horohoro ambako pia kuna hitajika ulinzi madhubuti ili kuweza kupapambana na biashara ya magendo.
Katika mazungumzo yake na waandishi hao wa habari ambao walitokea Horohoro kwa ziara maalumu ya kikazi, Meneja Joseph Raymond alielezea matumizi ya drones yataleta maboresho makubwa katika kupambana na utoroshaji wa bidhaa za magendo mipakani
Awali, waandishi wa habari walipewa fursa na Meneja wa TRA Mkoa, Thomas Masese kutembelea kituo cha mpakani cha Hirohoro ambapo Kaimu Mkuu wa kituo cha Forodha cha Horohoro, Lives Mapandwe alielezea mafanikio ya kituo hicho kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wasafiri wanaopitia katika kituo hicho wakiwemo watalii na mizigo kutoka Mombasa, Kenya.
Alusema kituo cha Horohoro kimepewa nyenzo za kufanyia kazi ikiwemo magaru, lakini akapendekeza waletewe pia na pikipiki kwani hizo zinaweza kutumika hadi ndanindani ya mapori wanakojificha wafanyabiashara na walanguzi wanaokwepa kulipa kodi na ushuru.
Mwisho.

EmoticonEmoticon