Showing posts with label elimu. Show all posts
Showing posts with label elimu. Show all posts

SHIRIKA LA UWASHEM KUWAFIKIA WAKULIMA WA MWANI NA WAVUVI 800 MKINGA

November 20, 2025 Add Comment




Na Oscar Assenga, MKINGA

WAVUVI na Wakulima wa Mwani 800 wilayani Mkinga mkoani Tanga wanatarajiwa kupatiwa elimu ya utendaji wa shughuli zao kwa usalama ili kuwaepusha na changamoto za baharini zinazotokana na uwepo wa mwigiliano wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Shirika la Uwashem Hussein Msagati wakati wa kikao cha wavuvi na wakulima wa mwani katika kata ya Boma wilayani humo ikiwa ni kutambulisha mradi wa kujenga uwezo kwa matumizi bora ya rasilimali za bahari ngazi ya Kata .

Mradi huo unaendeshwa na Shirika la Umoja wa Wasaidizi wa Sheria wilayani Mkinga (Uwashem) ukifadhiliwa na Shirika la 4 H Tanzania pamoja na We World ambapo sasa utasaidia kuwaweka kwenye hali ya amani ili waweze kushirikiana kwa pamoja kufanya kazi zao na kutokuwepo kwa mivutano ya hapa na pale.

Alisema kwamba umuhimu wa elimu hiyo ni mkubwa kutokana na changamoto za baharini zinazotokana na kuwepo kwa mwingiliano wa maeneo kwa sababu wavuvi wanaotumia makokoro wanaingia kwenye maeneo yanayolimwa mwani kufanya shughuli za uvuvi.

Aidha alisema kwamba hatua hiyo inapelekea kuharibu mazao ya mwani jambo ambalo sio zuri hivyo ikiwezekana washirikiane kwa pamoja ili kuepusha migongano katika shughuli zao za kila siku.

Awali akizungumza Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Mkinga Hilda Muro alilipongeza Shirika hilo kwa kuandaa vikao kati ya wavuvi na wakulima wa mwani akieleza kwamba itasaidia kuleta tija kwa kuwaepusha na migogoro au kuitatua pindi inapotokea baina yao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao baharini.

Alisema kwamba wanapotokea wadau kama hao kuwaletea elimu ya kutatua migigoro kwa njia za mazungumzo inapendeza zaidi hivyo wanalishukuru shirika hilo kuwapelekea elimu na wanaamini kupitia elimu hiyo kwa wananchi itakuwa ni mwanzo wa amani kwa jamii za pwani.

“Kutokana na kila mtu atafanya shughuli zake bila kukutana na vikwazo au kubuguziwa na mtu mwengine yoyote na hivyo kutengeneza amani na mazingira ya uzalishaji kuwa bora kuanzia sasa”Alisema

Hata hivyo alisema kwamba elimu itasaidia uzalishaji mwani na wavuvi kutokana na kwamba watakuwa wakitekeleza majukumu yao wakiwa kwenye hali ya usalama baharini.


Hata hivyo mmoja wa Wavuvi wilayani humo Yasin Baraza alisema kwamba midahalo hiyo inayoendeshwa na Shirika hilo itawasaidia kuweza kutatua migogoro kati ya wavuvi na wakulima wa mwani na tatizo hilo liweze kuondoka moja kwa moja .


Mwisho.

DKT JAKAYA KIKWETE AMPONGEZA MHITIMU UDSM KWA KUVUNJA REKODI YA MIAKA 32 KWA KUPATA DARAJA LA KWANZA LAW SCHOOL

November 20, 2025 Add Comment

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Mhitimu wa Shahada ya Awali ya Sheria ambaye alivunja rekodi iliyodumu miaka 32 kwa  kupata Daraja la Kwanza katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania), rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Profesa wa sheria UDSM  Prof. Hamudi Majamba.

Bi Mary Barney Laseko anakuwa mwanamke wa pili kupata daraja la kwanza kutoka Law School of Tanzania, wa kwanza akiwa Katibu Mkuu wa `CCM Dkt. Asha-Rose Migiro. 


Hii imetokea leo wakati wa Mahafali ya 55 (Duru la Tatu) ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam.


Kwenye Mahafali hayo Dkt Kikwete ametunuku Shahada na Stashahada kwa jumla ya wahitimu 2,452 ambapo 1,386 ama asilimia 56.6 ni wanawake. Picha na Issa Michuzi


Ends





 

WALIMU TUJIENDELEZE KUENDANA NA MABADILIKO DUNIANI-DKT. BITEKO

October 17, 2025 Add Comment

 



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza walimu nchini wasichoke kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea kutokea Duniani.

Dkt. Biteko amesema hayo Oktoba 16, 2025 katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara wakati akifungua Semina ya Viongozi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kanda ya Ziwa na Ziwa Magharibi iliyoshirikisha viongozi kutoka mikoa minane.

SHULE ZINAZOTUMIA KUNI KAMA NISHATI YA DHARURA ZAELEKEZWA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

October 09, 2025 Add Comment


📌 *Mkurugenzi Nishati Safi ya Kupikia apongeza jitihada za Shule zilizohamia kwenye nishati salama na rafiki kwa afya na Mazingira.*


📌 *Atoa wito kwa Wadau kuwekeza katika uzalishaji wa kuni/mkaa mbadala kutokana na kuhitajika kwake*

Mkurugenzi wa Nishati safi  ya kupikia, Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, ametoa wito kwa shule zote nchini  kuhakikisha zinaachana na matumizi ya kuni na badala yake kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi, majiko banifu, na mkaa mbadala.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha  ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya nishati safi ya kupikia inayotekelezwa chini ya mpango wa CookFund katika Mkoa wa Mwanza, Mlay amesema kuwa shule nyingi bado zinategemea kuni kama nishati ya dharura, hali inayochangia uharibifu wa mazingira na madhara kwa afya ya watumiaji.

“Katika ziara hii nimebaini Shule nyingi zinatumia kuni kama nishati ya dharura hivyo nitoe wito kwa uongozi wa shule mkishirikiana na Afisa Elimu kuanza kutumia mkaa mbadala ambao ni rafiki kwa mazingira na unachangia katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa." Amesema Mlay

Aidha, Bw. Mlay amepongeza baadhi ya shule ambazo tayari zimeanza kutumia nishati safi, ambazo hazifadhiliwi na mradi wa Cookfund ikiwemo shule ya Sekondari ya wavulana Musabe pamoja na Shule ya Msingi Buhongwa A akizitaja kuwa mfano bora kwa taasisi nyingine nchini.

Amesema matumizi ya nishati safi huchangia kwa kiasi kikubwa kulinda afya ya wanafunzi na walimu dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji, yanayosababishwa na moshi kutoka kwa kuni na mkaa wa kawaida.

“Tunapongeza juhudi za shule zinazohamia kwenye nishati safi ya kupikia kwani hii hatua ni kubwa katika kulinda afya, mazingira na hata kuongeza ufanisi wa shughuli za kila siku shuleni hivyo nitoe wito kwa shule zote ambazo bado hazijaanza kutumia nishati safi ya kupikia, kuanza kutumia nishati safi kwani ni nafuu na zinaokoa muda." Ameongeza Bw. Mlay

vilevile, Mlay amehimiza Serikali za Mitaa, Wakuu wa Shule na wadau wa elimu kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha taasisi za elimu zinapata vifaa vya kisasa vya kupikia kwa kutumia nishati safi.

 Amesisitiza kuwa mradi wa CookFund na mipango mingine ya kitaifa iko tayari kusaidia shule zinazotaka kuhamia kwenye mfumo huo wa kisasa wa kupikia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati  wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024 - 2034 ambao unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.

Mlay  ametoa wito kwa wawekezaji mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa kuni na mkaa mbadala ili kufanikisha azma ya nchi kuhamia kwenye nishati safi na kulinda mazingira.


“Ni muhimu kuwekeza kwa dhati katika uzalishaji wa kuni na mkaa mbadala, hasa kwa ajili ya taasisi kwani kukosekana kwa wazalishaji hawa kunaweza kusababisha athari kubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira hapo baadaye hivyo tunahimiza wadau wote kujitokeza, kushirikiana, na kuwekeza katika mabadiliko haya yenye tija kwa taifa na vizazi vijavyo”. Amesisitiza Bw. Mlay


Naye Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Jiji la Mwanza Bw. Rodrick Kazinduki ameeleza kuwa  kupitia mkakati wa Nishati Safi ya kupikia, Tanzania itaondokana na changamoto za uharibifu wa mazingira na afya zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi huku akieleza kuwa  kupitia ushirikiano wa Serikali, Mashirika ya Kimataifa na jamii kwa ujumla, kuna matumaini kuwa shule nyingi zaidi zitaweza kuhama kutoka kwenye kuni na mkaa wa kawaida, na kuingia katika zama mpya za nishati safi, salama na endelevu.

WALIMU NI NGUZO YA MAENDELEO -WAZIRI MKUU MAJALIWA

October 04, 2025 Add Comment











📌 Asema Walimu ni fahari ya nchi na chimbuko la uvumbuzi na ubunifu


📌 Dkt. Biteko asema ualimu ndio taaluma inayomtengeneza mtu awe bora kuliko hata ualimu wenyewe

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa walimu ni nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote hapa duniani kwani ndio wanaotoa rasilimali watu yenye elimu ambayo ni muhimu zaidi kwa Taifa.

Amesema kuwa mafanikio ya kielimu, kijamii na kiuchumi yanatokana na juhudi za walimu kwani walimu ni fahari ya familia, jamii na nchi na kupitia mikono yao vijana wa kitanzania wanajengewa maarifa, stadi na maadili ya uzalendo.

Amesema hayo Oktoba 03, 2025 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani ambayo kiwilaya imeadhimishwa Bukombe mkoani Geita katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Ushirombo.

"Kila hatua ya ustawi wa kijamii na kiuchumi inaanzia darasani kupitia juhudi na maarifa ya walimu. bila walimu, hakuna taaluma, hakuna viongozi wa kesho na hakuna Taifa linaloweza kusimama imara, walimu ndio chimbuko la uvumbuzi na ubunifu wa kizazi kipya.".

Amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kada ya ualimu hapa nchini, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya kada hiyo ikiwemo kwa kupandisha madaraja na kuimarisha mafunzo kwa walimu.

Ameongeza kuwa ili kukabiliana na upungufu wa walimu nchini Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuthamini na kuwekeza katika kada ya ualimu kwa kuajiri walimu wapya kila mwaka. 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Ofisi ya Rais - UTUMISHI kufanya msawazo wa walimu ndani ya mikoa husika kwa kuhakikisha kila shule inapata walimu ili watoto wa Kitanzania wapate elimu bora.

"Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Vyuo vya Ualimu na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imarisheni mafunzo ya kitaaluma na endelevu kwa walimu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya dunia ya leo". Amesema Mhe. Majaliwa.

Naye, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amesema kuwa taaluma ya ualimu ndio taaluma pakee inayomtengeneza mtu awe bora kuliko hata ualimu wenyewe na wakati wowote hujinyima muda wake na nguvu zake zote kumtengeneza mtu kuwa mume au mke bora au hata mzazi bora.

"Taaluma ya ualimu humfanya mtu kuwa raia mwema kwenye nchi na zaidi sana humfanya kuwa mtumishi, mfanyakazi na mzalishaji mali bora, wakati wote wa maisha yake, hii ni taaluma ambayo tunaamini ni ya uumbaji wa pili baada ya mwanadamu kuzaliwa na wazazi wake, kazi ya pili huendelea hapa duniani na muumbaji huwa ni mwalimu," amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa Mwalimu ndiye anayetoa mwelekeo wa maisha ya kila mtu na ukiona jamii yoyote yenye ustaarabu na kustaarabika huhitaji kupiga ramli kujua nani chanzo chake bali mwalimu ndio sababu yake.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Caroline Nombo amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya shughuli mbalimbali zinazowawezesha walimu kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya ikiwemo ujenzi wa miundombinu shuleni na lengo ni kukuza ujifunzaji na ufundishaji.

Ameongeza  “ Serikali inathamini jitihada zinazofanywa na walimu kwani wamekuwa kiini cha mafanikio. "Kila mmoja wetu amepita kwenye mikono ya walimu, tunawashukuru walimu wote wanaotoa nguvu na maarifa yao kuwawezesha Watanzania"


Mwisho