HIMIZENI WANANCHI, VIJANA NA WANAFUNZI KUTEMBELEA MRADI WA BOMBA LA MAFUTA- WAZIRI NANKABIRWA

January 07, 2026




📌*Lengo ni makundi hayo kuwa sehemu ya miradi na kupata ufahamu*


📌*Aipongeza Tanzania kwa kasi ya utekelezaji wa mradi wa bomba la EACOP*


📌 *Ahitimisha ziara yake mkoani Tanga kwa kutembelea kambi namba 16 wilaya ya Muheza*


TANGA


Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, ametoa wito kwa nchi zinazotekeleza mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kuhimiza wananchi, vijana na wanafunzi kutembelea mradi huo akisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uelewa wao, hasa ikizingatiwa kuwa wao ndio wanufaika wakubwa wa mradi.

Dkt. Nankabirwa ametoa wito huo leo tarehe 7 Januari, 2026 jijini Tanga, wakati wa ziara yake katika Kambi namba 16, ambayo ni kipande cha mwisho kutoka upande wa Uganda katika mchakato wa uunganishaji wa mabomba yatakayosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi eneo la Chongoleani mkoani Tanga.

Akiwa katika kambi hiyo, Waziri Nankabirwa alijionea shughuli za uunganishaji wa mabomba katika eneo lenye urefu wa kilomita 2.5, na kueleza kuridhishwa kwake na ubora wa kazi inayotekelezwa na upande wa Tanzania, akisema ni ya kupongezwa sana.


Aidha, alipata fursa ya kutembelea mmoja wa wanufaika wa mradi kupitia utekelezaji wa huduma za kijamii, ambaye amejengewa nyumba ya kuishi kama sehemu ya manufaa ya mradi huo kwa jamii zinazozunguka mradi.

Hadi sasa, ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la EACOP umefikia asilimia 79. Mradi huo unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa takribani kilomita 1,445 kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, ambapo jumla ya vipande vya mabomba 86,000 vinatumika katika utekelezaji wake.

Ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2026.


#NishatiTupoKazini

#TanzaniaNchiYetuSote

#NchiYetuKwanza

#MaendeleoEndelevu

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »