Na. Philipo Hassan - Zanzibar.
Kamishna wa Uhifadhi, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) CPA Musa Nassoro Kuji leo Januari 05, 2025 amesema TANAPA itatumia maonesho mbalimbali ya Kimataifa yanayofanyika ndani na nje ya nchi ili kufikia lengo la Taifa la watalii milioni nane au zaidi ifikapo 2030.
Kamishna Kuji aliyasema hayo alipozuru katika banda la TANAPA wanaoshiriki Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (ZITF), yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho Fumba mjini Zanzibar.
Ushiriki wa TANAPA katika maonesho haya unaakisi dhamira ya Shirika ya kuimarisha na kutangaza utalii kwa kuwaleta karibu wadau wa sekta, wawekezaji na wananchi, huku ikihusisha umuhimu wa elimu ya uhifadhi wa maliasili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Ephraim Balozi Mafuru amewahamisha watanzania kutembelea banda la TANAPA kujifunza na kupata taarifa mbalimbali za utalii hususani Hifadhi ya Taifa Serengeti iliyoshinda Tuzo ya kimataifa (World Travel Awards) katika kipengele cha hifadhi bora inayoongoza dunia kwa utalii wa Safari.
Kupitia jukwaa la ZITF, TANAPA inaendelea kuimarisha mahusiano, kubadilishana maarifa na kufungua milango ya ushirikiano mpya unaolenga kukuza mchango wa utalii katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Maonesho haya ni sehemu ya mkakati mpana wa Kitaifa wa kuitangaza Tanzania Kimataifa, huku TANAPA ikihamasisha wananchi kujivunia na kutembelea Hifadhi za Taifa kama nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa.





EmoticonEmoticon