Showing posts with label elimu. Show all posts
Showing posts with label elimu. Show all posts

JK AENDELEA KUWA KINARA WA ELIMU DUNIANI

December 08, 2025 Add Comment


Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiongea na wajumbe wa Bodi ya GPE baada ya kumalizika kwa mkutano huo mjini Brussels, Ubelgiji. Pamoja naye ni Afisa Mtengaji Mkuu wa GPE, Bi Laura Frigenti


Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) ameendelea na jitihada za kukuza elimu duniani.

Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya GPE alisimamia Mkutano wa mwisho wa Bodi hiyo wa kuhitimisha Mpango wa 4 wa Miaka 5 wa Mzunguko wa Ufadhili wa GPE (4th financing campaign 2021 - 2025) ambao ulifanikiwa kukusanya takriban Dola za Kimarekeni bilioni 4.1 kwa ajili ya kugharamia uboreshaji wa elimu ya awali na ya msingi kwa watoto wanaoishi katika nchi za kipato cha chini na zinazoendelea, hususan watoto wa kike na wale wanaojikuta kwenye mazingira magumu kama vile ya vita, ukame, mafuriko, nk.

Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo uliofanyika wiki hii huko Brussels, Ubelgiji ulitathmini mkakati wa kukusanya fedha uliofanyika kwa mafanikio katika kukusanya fedha kupitia utaratibu wa misaada (grants) na ufadhili wa pamoja (co - financing) ambapo nchi zinazonufaika na miradi ya GPE huchangia kiasi cha fedha kwenye sekta ya elimu na GPE huongezea kiasi kinachobakia kwa makubaliano maalumu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na GPE, kiasi hicho cha Dola za Marekani milioni 4.7 kilichopatikana kimesaidia kuboresha elimu kwa watoto takriban milioni 372 duniani kote huku watoto milioni 10 zaidi wakiandikishwa shule. Aidha, kupitia ufadhili wa GPE, walimu milioni 4.7 kote duniani walipatiwa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi.

Aidha, Mkutano huo ulipokea taarifa ya mkakati wa utekelezaji wa mpango mpya wa 5 wa kampeni ya ufadhili wa GPE utakaoanza mwaka 2026 hadi 2030. Kampeni hiyo imelenga kukusanya Dola za Marekani milioni 5 na itaongozwa kwa pamoja kati ya Rais Bola Tinubu wa Nigeria na Waziri Mkuu Giorgia Meloni wa Italia. Fedha zitakazopatokana kutokana na kampeni hiyo zitaongeza wigo wa GPE kuhudumia watoto takriban milioni 750 kote duniani kwa kuwapatia elimu bora zaidi inayoendana na mahitaji ya karne ya 21.

Vilevile, Mkutano huo ulishukuru baadhi ya nchi ambazo zimeahidi kuendeleza ushirikiano na GPE kama vile Ujerumani ambayo tayari imeahidi kuchangia kampeni hii mpya ya GPE kiasi cha Dola za Marekani milioni 320 kwa kipindi cha miaka 6 ijayo.

Kwa kuzingatia mabadiliko ya sasa ya hali ya kifedha duniani ambapo wafadhili mbalimbali, hususan nchi zilizoendelea, zinabadilisha vipaumbele vyao vya maeneo ya kuelekeza ufadhili, Taasisi ya GPE imelenga kuendelea kuhakikisha inasimamia na kutumia vizuri fedha zinazotolewa na wafadhili ili kuwanufaisha watoto wengi zaidi duniani. Vilevile, GPE imepanga kuendelea kuzishawishi nchi ambazo siyo wafadhili waliozoeleka wa GPE (non traditional donors) kama vile nchi za mashariki ya kati ili ziweze kuoanisha programu zao za kusaidia elimu duniani na zile za GPE, na kuongeza fedha zaidi wanazochangia kwa GPE.

Kama sehemu ya kutekeleza mkakati huo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya GPE Dkt. Kikwete leo amepata fursa ya kushiriki Mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Qatar ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza utayari wa GPE kuendelea kushirikiana na Serikali ya Qatar katika jitihada zake za kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya kielimu kote duniani.

Aidha, katika mazungumzo yake na Viongozi mbalimbali wa Taifa la Qatar pambezoni mwa Mkutano huo ameeleza nia ya GPE amepongeza mchango mkubwa wa Qatar katika elimu duniani na kuihakikishia utayari wa GPE kuendelea kushirikiana na Serikali ya Qatar na Shirika la Qatar la Education Above All Foundation.

GPE ni Taasisi iliyoanzishwa na Kundi la Nchi zenye Uchumi na Utajiri Mkubwa Duniani (G7) mwaka 2002 ili kuharakisha ufikiwaji wa lengo la elimu la kuhakikisha kila mtu, bila kujali umri, jinsia au hali ya kijamii, anapata elimu ya msingi bila malipo na kwa usawa. Tanzania ni moja ya nchi 90 zinazonufaika na miradi inayotekelezwa na GPE ambapo tangu ilipojiunga mwaka 2013 imeshapokea zaidi ya misaada yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 344 kusaidia jitihada zinazofanywa na Serikali kuendeleza elimu ya awali na ya msingi.

Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiteta jambo na Bi. Christine nHogan, Makama mwenyekiti wa GPE wakati wa mkutano wao mjini Brussels, Ubelgiji.
Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akishiriki Mkutano wa 23 wa Kimataifa wa Qatar mjini Doha

Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education - GPE) akiteta jambo na Dkt Hamad bin Abdulaziz Al Kawari, Waziri wa Nchi na Naibu Waziri Mkuu wa Qatar, mjini Doha leo. Kulia ni Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe Habib Awesi Mohamed.



MKUU WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM RAIS MSTAAFU DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE AONGOZA MAHAFALI YA 17 YA CHUO KISHIRIKI CHA ELIMU CHA MKWAWA MJINI IRINGA

November 26, 2025 Add Comment


Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa William Anangisye wakimsubiri Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Kheri James akivalishwa joho kabla ya kuelekea kwenye sherehe za mahafali ya 17 ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwakwa mjini Iringa leo.


: Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi Cheti cha Ubora mhitimu aliyeng’ara zaidi, Lekishin Koipa, aliyepata ufaulu wa daraja la kwanza kwa wastani wa Wakia (GPA) ya 4.8 ikiwa ndiyo alama ya juu zaidi miongoni mwa wahitimu wote wa MUCE kwa mwaka huu wa 2025.



Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameongoza mahafali ya 17 ya Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) mjini Iringa leo, ambapo ametunuku shahada mbalimbali za umahiri na za awali kwa wahitimu.



Katika ngazi ya umahiri, amewatunuku Digrii ya Umahiri wa Sayansi na Ualimu (Master of Science with Education) kwa wahitimu wanne: Joyce Dismas, Osia Peter Mwanyesya, Deogras Yonah Emmanuel na Samwel Joseph Lungo.



Aidha, wanafunzi wawili—Mbazi Yonazi Senkondo na Joseph Athanas Luoga—wamepata Digrii ya Umahiri wa Sayansi katika Ubunifu wa Kihisabati (Master of Science in Mathematical Modelling), huku John Ngazime Josephat akitunukiwa Digrii ya Umahiri wa Elimu Jamii na Ualimu (Master of Arts with Education).

Kwa upande wa Shahada za Awali, jumla ya wahitimu 565 wamepata Digrii ya Awali ya Elimu Jamii na Ualimu (Bachelor of Arts with Education).

Wahitimu wengine 365 wametunukiwa Digrii ya Elimu katika Sayansi (Bachelor of Education in Science), 334 wakipewa Digrii ya Awali ya Sayansi na Ualimu (Bachelor of Science with Education), na 17 wakitunukiwa Digrii ya Awali ya Sayansi katika Kemia (Bachelor of Science in Chemistry).


Katika kilele cha hafla hiyo, Mkuu wa Chuo amekabidhi pia Cheti cha Ubora kwa mhitimu aliyeng’ara zaidi, Lekishin Koipa, aliyepata ufaulu wa daraja la kwanza kwa wastani wa Wakia (GPA) ya 4.8, ikiwa ndiyo alama ya juu zaidi miongoni mwa wahitimu wote wa MUCE kwa mwaka huu wa 2025



SHIRIKA LA UWASHEM KUWAFIKIA WAKULIMA WA MWANI NA WAVUVI 800 MKINGA

November 20, 2025 Add Comment




Na Oscar Assenga, MKINGA

WAVUVI na Wakulima wa Mwani 800 wilayani Mkinga mkoani Tanga wanatarajiwa kupatiwa elimu ya utendaji wa shughuli zao kwa usalama ili kuwaepusha na changamoto za baharini zinazotokana na uwepo wa mwigiliano wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Shirika la Uwashem Hussein Msagati wakati wa kikao cha wavuvi na wakulima wa mwani katika kata ya Boma wilayani humo ikiwa ni kutambulisha mradi wa kujenga uwezo kwa matumizi bora ya rasilimali za bahari ngazi ya Kata .

Mradi huo unaendeshwa na Shirika la Umoja wa Wasaidizi wa Sheria wilayani Mkinga (Uwashem) ukifadhiliwa na Shirika la 4 H Tanzania pamoja na We World ambapo sasa utasaidia kuwaweka kwenye hali ya amani ili waweze kushirikiana kwa pamoja kufanya kazi zao na kutokuwepo kwa mivutano ya hapa na pale.

Alisema kwamba umuhimu wa elimu hiyo ni mkubwa kutokana na changamoto za baharini zinazotokana na kuwepo kwa mwingiliano wa maeneo kwa sababu wavuvi wanaotumia makokoro wanaingia kwenye maeneo yanayolimwa mwani kufanya shughuli za uvuvi.

Aidha alisema kwamba hatua hiyo inapelekea kuharibu mazao ya mwani jambo ambalo sio zuri hivyo ikiwezekana washirikiane kwa pamoja ili kuepusha migongano katika shughuli zao za kila siku.

Awali akizungumza Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Mkinga Hilda Muro alilipongeza Shirika hilo kwa kuandaa vikao kati ya wavuvi na wakulima wa mwani akieleza kwamba itasaidia kuleta tija kwa kuwaepusha na migogoro au kuitatua pindi inapotokea baina yao wakati wa utekelezaji wa majukumu yao baharini.

Alisema kwamba wanapotokea wadau kama hao kuwaletea elimu ya kutatua migigoro kwa njia za mazungumzo inapendeza zaidi hivyo wanalishukuru shirika hilo kuwapelekea elimu na wanaamini kupitia elimu hiyo kwa wananchi itakuwa ni mwanzo wa amani kwa jamii za pwani.

“Kutokana na kila mtu atafanya shughuli zake bila kukutana na vikwazo au kubuguziwa na mtu mwengine yoyote na hivyo kutengeneza amani na mazingira ya uzalishaji kuwa bora kuanzia sasa”Alisema

Hata hivyo alisema kwamba elimu itasaidia uzalishaji mwani na wavuvi kutokana na kwamba watakuwa wakitekeleza majukumu yao wakiwa kwenye hali ya usalama baharini.


Hata hivyo mmoja wa Wavuvi wilayani humo Yasin Baraza alisema kwamba midahalo hiyo inayoendeshwa na Shirika hilo itawasaidia kuweza kutatua migogoro kati ya wavuvi na wakulima wa mwani na tatizo hilo liweze kuondoka moja kwa moja .


Mwisho.

DKT JAKAYA KIKWETE AMPONGEZA MHITIMU UDSM KWA KUVUNJA REKODI YA MIAKA 32 KWA KUPATA DARAJA LA KWANZA LAW SCHOOL

November 20, 2025 Add Comment

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Rais Mstaafu Wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Mhitimu wa Shahada ya Awali ya Sheria ambaye alivunja rekodi iliyodumu miaka 32 kwa  kupata Daraja la Kwanza katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania), rekodi iliyokuwa inashikiliwa na Profesa wa sheria UDSM  Prof. Hamudi Majamba.

Bi Mary Barney Laseko anakuwa mwanamke wa pili kupata daraja la kwanza kutoka Law School of Tanzania, wa kwanza akiwa Katibu Mkuu wa `CCM Dkt. Asha-Rose Migiro. 


Hii imetokea leo wakati wa Mahafali ya 55 (Duru la Tatu) ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam.


Kwenye Mahafali hayo Dkt Kikwete ametunuku Shahada na Stashahada kwa jumla ya wahitimu 2,452 ambapo 1,386 ama asilimia 56.6 ni wanawake. Picha na Issa Michuzi


Ends





 

WALIMU TUJIENDELEZE KUENDANA NA MABADILIKO DUNIANI-DKT. BITEKO

October 17, 2025 Add Comment

 



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza walimu nchini wasichoke kujiendeleza kitaaluma ili kuendana na mabadiliko yanayoendelea kutokea Duniani.

Dkt. Biteko amesema hayo Oktoba 16, 2025 katika Manispaa ya Musoma, mkoani Mara wakati akifungua Semina ya Viongozi wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kanda ya Ziwa na Ziwa Magharibi iliyoshirikisha viongozi kutoka mikoa minane.

SHULE ZINAZOTUMIA KUNI KAMA NISHATI YA DHARURA ZAELEKEZWA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

October 09, 2025 Add Comment


📌 *Mkurugenzi Nishati Safi ya Kupikia apongeza jitihada za Shule zilizohamia kwenye nishati salama na rafiki kwa afya na Mazingira.*


📌 *Atoa wito kwa Wadau kuwekeza katika uzalishaji wa kuni/mkaa mbadala kutokana na kuhitajika kwake*

Mkurugenzi wa Nishati safi  ya kupikia, Wizara ya Nishati, Bw. Nolasco Mlay, ametoa wito kwa shule zote nchini  kuhakikisha zinaachana na matumizi ya kuni na badala yake kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwemo gesi, majiko banifu, na mkaa mbadala.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha  ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya nishati safi ya kupikia inayotekelezwa chini ya mpango wa CookFund katika Mkoa wa Mwanza, Mlay amesema kuwa shule nyingi bado zinategemea kuni kama nishati ya dharura, hali inayochangia uharibifu wa mazingira na madhara kwa afya ya watumiaji.

“Katika ziara hii nimebaini Shule nyingi zinatumia kuni kama nishati ya dharura hivyo nitoe wito kwa uongozi wa shule mkishirikiana na Afisa Elimu kuanza kutumia mkaa mbadala ambao ni rafiki kwa mazingira na unachangia katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa." Amesema Mlay

Aidha, Bw. Mlay amepongeza baadhi ya shule ambazo tayari zimeanza kutumia nishati safi, ambazo hazifadhiliwi na mradi wa Cookfund ikiwemo shule ya Sekondari ya wavulana Musabe pamoja na Shule ya Msingi Buhongwa A akizitaja kuwa mfano bora kwa taasisi nyingine nchini.

Amesema matumizi ya nishati safi huchangia kwa kiasi kikubwa kulinda afya ya wanafunzi na walimu dhidi ya magonjwa ya mfumo wa upumuaji, yanayosababishwa na moshi kutoka kwa kuni na mkaa wa kawaida.

“Tunapongeza juhudi za shule zinazohamia kwenye nishati safi ya kupikia kwani hii hatua ni kubwa katika kulinda afya, mazingira na hata kuongeza ufanisi wa shughuli za kila siku shuleni hivyo nitoe wito kwa shule zote ambazo bado hazijaanza kutumia nishati safi ya kupikia, kuanza kutumia nishati safi kwani ni nafuu na zinaokoa muda." Ameongeza Bw. Mlay

vilevile, Mlay amehimiza Serikali za Mitaa, Wakuu wa Shule na wadau wa elimu kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha taasisi za elimu zinapata vifaa vya kisasa vya kupikia kwa kutumia nishati safi.

 Amesisitiza kuwa mradi wa CookFund na mipango mingine ya kitaifa iko tayari kusaidia shule zinazotaka kuhamia kwenye mfumo huo wa kisasa wa kupikia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati  wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024 - 2034 ambao unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.

Mlay  ametoa wito kwa wawekezaji mbalimbali kujitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa kuni na mkaa mbadala ili kufanikisha azma ya nchi kuhamia kwenye nishati safi na kulinda mazingira.


“Ni muhimu kuwekeza kwa dhati katika uzalishaji wa kuni na mkaa mbadala, hasa kwa ajili ya taasisi kwani kukosekana kwa wazalishaji hawa kunaweza kusababisha athari kubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira hapo baadaye hivyo tunahimiza wadau wote kujitokeza, kushirikiana, na kuwekeza katika mabadiliko haya yenye tija kwa taifa na vizazi vijavyo”. Amesisitiza Bw. Mlay


Naye Afisa Elimu Taaluma Halmashauri ya Jiji la Mwanza Bw. Rodrick Kazinduki ameeleza kuwa  kupitia mkakati wa Nishati Safi ya kupikia, Tanzania itaondokana na changamoto za uharibifu wa mazingira na afya zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo safi huku akieleza kuwa  kupitia ushirikiano wa Serikali, Mashirika ya Kimataifa na jamii kwa ujumla, kuna matumaini kuwa shule nyingi zaidi zitaweza kuhama kutoka kwenye kuni na mkaa wa kawaida, na kuingia katika zama mpya za nishati safi, salama na endelevu.