📌 *Mradi wa EACOP kuleta mabadiliko ya kiuchumi, ajira na huduma za kijamii Afrika Mashariki*
📌*Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda aisifu Tanzania kwa kasi ya utekelezaji*
📌*Tanzania yafikia asilimia 79 ya ujenzi wa mradi*
📌*Mhe. Salome asema Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan na Yoweri Museveni imekuwa nguzo ya mafanikio*
TANGA
Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, ameipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda.
Dkt. Nankabirwa ametoa pongezi hizo leo tarehe 6 Januari, 2026 jijini Tanga, wakati wa ziara yake ya kikazi akiongozana na ujumbe kutoka Uganda, waliotembelea eneo la Chongoleani mkoani Tanga ambako ujenzi wa mradi huo unaendelea.
Muonekano wa visima vinne vya kuhifadhi Mafuta eneo la Karibu na gati ya Kuegesha meli kwa ajili ya kupokelea Mafuta eneo la Chongoleani Tanga
Amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, ajira na maendeleo kwa nchi hizo mbili na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Ameitaka Wizara ya Nishati ya Tanzania na Uganda kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika ili shughuli zote za utekelezaji wa mradi ziendelee bila kukwama.
Ameongeza kuwa mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi mikubwa duniani na Afrika Mashariki, hivyo wananchi wa pande zote mbili wana sababu ya kujivunia mafanikio yanayopatikana, yakiongozwa na dhamira ya dhati ya Marais wa Tanzania na Uganda.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati wa Tanzania, Salome Makamba, amesema dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, imewezesha utekelezaji mzuri wa mradi huo unaotarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika nyanja za kiuchumi, kijamii, ajira na uboreshaji wa huduma za jamii.
Ameipongeza Kampuni ya EACOP kwa kazi kubwa inayoendelea na kuitaka kuendelea kutoa fursa za ajira na zabuni kwa makampuni na wazawa wa Tanzania na Uganda, kama ilivyoelekezwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Kwa mujibu wa taarifa za utekelezaji, hadi sasa ujenzi wa mradi kwa upande wa Tanzania umefikia asilimia 79 na unagharimu kiasi cha zaidi ya dola bilioni 5.
Awali kabla ya kutembelea eneo la mradi, ujumbe wa Waziri wa Uganda na ule wa Tanzania ulioongozwa na Naibu Waziri wa Nishati walitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dkt. Batilda Buriani.
Amesema Mkoa wa Tanga umenufaika kwa kiasi kikubwa na uwepo wa mradi huo, hususan katika ajira kwa vijana wa maeneo yanayopitiwa na bomba pamoja na upatikanaji wa huduma za kijamii kama maji, umeme na miundombinu mingine.
Ameipongeza EACOP kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira, bayoanuai na usalama wakati wote wa utekelezaji wa mradi, kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
ujumbe wa Tanzania na Uganda unaotembelea kukagua maendeleo ya mradi wa EACOP mkoani TangaMradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki ulianza mwaka 2022 na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu. Mradi huo unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kupunguza msukumo wa mafuta, vituo sita vya kuongeza msukumo wa mafuta, pamoja na ujenzi wa mabomba ya kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Muonekano wa visima vinne vya kuhifadhi Mafuta eneo la Karibu na gati ya Kuegesha meli kwa ajili ya kupokelea Mafuta eneo la Chongoleani TangaKatika ziara hiyo, ujumbe wa pande zote mbili ulitembelea pia eneo la gati la kuegesha meli kwa ajili ya upakiaji wa mafuta, matenki ya kuhifadhia mafuta ghafi pamoja na miundombinu yake.
Mwisho








EmoticonEmoticon