RAIS SAMIA: MAGEUZI YA ELIMU NA SAYANSI KUJENGA UCHUMI ENDELEVU

January 09, 2026


NA EMMANUEL MBATILO, ZANZIBAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa katika sekta za elimu, sayansi, utafiti na ubunifu ili kujenga uchumi imara, shindani na endelevu.

Mhe. Rais ameyasema hayo Januari 8, 2026, Buyu visiwani Zanzibarbaada ya kuzindua Jengo la Taaluma na Utawala la Taasisi ya Sayansi za Bahari Zanzibar (UDSM–IMS), akisisitiza kuwa taasisi hiyo ni mdau muhimu wa Serikali katika kukuza uchumi shirikishi, hususan uchumi wa buluu.

Amesema uwepo wa taasisi hiyo ya kimkakati utaimarisha uvuvi endelevu, utalii wa baharini pamoja na ulinzi na matumizi bora ya rasilimali za bahari.

Mhe. Samia ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kusimamia kwa ufanisi Mradi wa HEET, ambao umeleta matokeo chanya katika miundombinu na ubora wa elimu ya juu, huku akiwahimiza vijana kutumia fursa hiyo kusoma na kupata elimu pamoja na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

Katika hatua nyingine, amewapongeza viongozi na watumishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kukamilisha mradi huo kwa wakati na kwa viwango vya juu, na ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mradi wa HEET.

Aidha, Rais amewataka wahadhiri na watafiti kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili tafiti na bunifu ziweze kuleta tija ya moja kwa moja kwa maendeleo ya Taifa, huku akiwahimiza wanafunzi kuwa walinzi na mabalozi wa rasilimali za bahari.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema ameiomba Serikali kushirikiana na Benki ya Dunia ili kuwepo Awamu ya Pili ya Mradi wa HEET, itakayowezesha kukamilisha maeneo ya utekelezaji ambayo bado hayajakamilika.

Dkt. Kikwete amesema majengo mapya yaliyozinduliwa ni msingi muhimu wa kuendeleza tafiti za kisasa, kutoa mafunzo bora na kukuza uchumi wa buluu, sambamba na kuchochea maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa William Anangisye, amesema uwekezaji huo utaongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wanafunzi katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS).

Amesema kwa sasa IMS ina uwezo wa kudahili takribani wanafunzi 172 kwa mwaka, lakini baada ya kukamilika kwa ujenzi huo, uwezo utaongezeka hadi wanafunzi 472 kwa mwaka, sawa na ongezeko la wanafunzi 300.

Prof. Anangisye amesema IMS sasa inaingia awamu mpya ya maendeleo baada ya kuzinduliwa rasmi kwa miundombinu ya kisasa katika eneo la Buyu, pamoja na kuimarishwa kwa vituo vya Mizingani na Pangani.

“Miundombinu hii, inayojumuisha maabara za kisasa, kumbi za mihadhara na vifaa vya mafunzo na utafiti, itaongeza uwezo wa taasisi kufundisha, kufanya tafiti na kuendeleza bunifu,” amesema Prof. Anangisye.










Share this

Related Posts

Previous
Next Post »