Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ally Gugu, amewahimiza wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa katika usajili na utambuzi wa wananchi.
Gugu alitoa wito huo tarehe 3 Januari, 2025, alipokuwa akifungua rasmi mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa NIDA uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Julius Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
“Nawapongeza kwa utendaji mzuri wa kazi, lakini nawasisitiza muendelee kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usajili, kwani NIDA ni taasisi muhimu sana katika maendeleo ya taifa,” alisema Gugu.
Alisisitiza kuwa NIDA inatekeleza majukumu nyeti yenye maslahi makubwa kwa taifa, hivyo wafanyakazi wanapaswa kuonesha uzalendo na uadilifu katika kulinda na kusimamia vyema taarifa binafsi za wananchi walizokabidhiwa.
Aidha, aliwahimiza wananchi ambao bado hawajachukua vitambulisho vyao vya taifa kufika katika ofisi za NIDA za wilaya ili kuvichukua, akibainisha kuwa vitambulisho hivyo ni nyaraka muhimu za utambulisho na kwamba serikali imetumia gharama kubwa kuvizalisha.
Vilevile, Gugu aliipongeza NIDA kwa kuanzisha huduma ya Msimbo Mfupi (Short Code) inayowawezesha wananchi kupata mrejesho wa huduma za vitambulisho kupitia simu za mkononi bila malipo.
Alisema huduma hiyo itanufaisha zaidi wakazi wa maeneo ya vijijini kwa kuwawezesha kupata taarifa kuhusu hali ya usajili wao na taarifa binafsi wakiwa maeneo yao, bila ya kusafiri umbali mrefu hadi ofisi za wilaya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, alieleza kuwa zaidi ya vitambulisho vya taifa 300,000 bado havijachukuliwa katika ofisi za NIDA za wilaya mbalimbali.
“Natumia fursa hii kuwasihi wananchi kwenda kuchukua vitambulisho vyao, kwani serikali imetumia fedha nyingi katika uzalishaji wake,” alisema Kaji.
Aidha, aliwashauri wananchi wenye makosa katika taarifa zao binafsi kutumia kibali maalum cha mwaka mmoja kurekebisha taarifa hizo, akisisitiza kuwa baada ya kibali hicho kuisha, hakutakuwa na muda wa nyongeza.




EmoticonEmoticon