HABARI

SIASA

ELIMU

Recent Posts

DKT. BITEKO AZINDUA MRADI UTAKAOWAKWAMUA VIJANA KIUCHUMI KATIKA MAENEO YANAYOPITIWA NA BOMBA LA MAFUTA GHAFI (EACOP)

August 18, 2025 Add Comment





📌 Unahusisha kuongezea vijana ujuzi, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuondoa vikwazo vya ujasiriamali na ajira binafsi

📌 Ataka ujuzi unaotolewa kwa vijana uende sambamba na utoaji wa mitaji

📌 Awaasa Vijana kuchangamkia fursa na kuwa waaminifu wanapopata nafasi

 📌 Wanawake 6,130, Wanaume 4,905 na Makundi maalum 1,226 kufikiwa


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amezindua Mpango wa Uwezeshaji wa Kiuchumi kwa Vijana (YEE) ambao unagusa maeneo yanayopitiwa na mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ikiwa ni jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha kuwa jamii zilizo karibu na miradi zinanufaika na miradi hiyo.



Akizindua mradi huo katika Kijiji cha Bukombe, wilayani Bukombe, Mkoa wa Geita tarehe 18 Agosti 2025, Dkt. Biteko amesema mradi huo wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ni moja ya miradi iliyopangwa kuwezeshwa na Kampuni ya EACOP kwa kipindi cha ujenzi na baada ya ujenzi ikiwa ni sehemu ya Uwajibikaji wa Kampuni hiyo kwa jamii. 



Amesema mradi huo umepangwa kuwafikia zaidi ya vijana 12,261 ambapo miongoni mwao wanawake ni 6,130; wanaume 4,905 na makundi maalumu ni 1,226 katika awamu ya kwanza inayohusisha Mikoa ya Geita, Kagera, Tabora na Tanga. 


" Tunapozindua mradi huu hatuna budi kuwashukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda. Viongozi wetu hawa kwa nia yao  ya dhati na moyo wa uzalendo wameuendeleza na kuusimamia kikamilifu mradi huu wa EACOP ambao umefikia asilimia 65, tumefikia hapa sababu ya msukumo wao wa kutekeleza mradi huu" Amesema Dkt. Biteko
Ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi wa EACOP mwaka 2022 hadi sasa, jumla ya Watanzania 9,194 wamepata nafasi za kufanya kazi ndani ya mradi na hivyo kuwa fursa kwao ya kujipatia kipato, mwaka 2024 kampuni ilitoa mafunzo maalumu kwa Vijana 170 na kuwapatia kazi kwenye mradi, Vijana wengine 110 wapo katika masomo na wanatarajiwa kujumlishwa pia katika Mradi huo pamoja na kutoa ufadhili wa Vijana 238 katika vyuo mbalimbali nchini. 
Amesema wananchi wanaopitiwa na miradi wanayo haki ya kunufaika na miradi lakini wana wajibu wa kulinda miundombinu ya mradi na kuufanya kuwa ni sehemu yao kwani unachangia pia kubadilisha maisha ya wananchi.
 Pia, Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya EACOP  na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kusimamia kwa ufanisi mradi huo huku akisisitiza kuwa, ili wananchi waone mradi huo ni sehemu yao lazima waone faida zake  hivyo miradi kama ya YEE inawapa chachu wananchi kulinda miundombinu ya EACOP kwa  wivu mkubwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, kampuni mbalimbali zinazotekeleza miradi kuhakikisha kuwa hawaweki mkazo  kwenye kuongeza ujuzi tu kwa wananchi bali wanawapatia mitaji ili waweze kufanya vizuri zaidi.

Aidha, amewaasa vijana kuchangamkia fursa zinazotokea kwenye miradi, wajitume, wawe waaminifu pale wanapopata fursa na kueleza kuwa Serikali itaendelea kuwatengenezea fursa  ili wajikwamue kiuchumi na kuleta maendeleo nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Mhe. Patrobas Katambi amesema Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametengeneza mipango mikakati ya kuhakikisha vijana wanapewa fursa za ajira na mitaji kwenye maeneo mbalimbali ambapo mpango wa YEE ni kielelezo cha matokeo ya mipango hiyo.
Ameeleza kuwa, kumekuwa na programu mbalimbali ikiwemo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo kupitia programu hiyo zaidi ya shilingi trilioni tatu zilitolewa kwa Watanzania  takriban milioni 24 ikiwemo Wanawake, Vijana na Makundi maalum kwa lengo la kuwawezesha kujikwamua kiuchumi

Mkuu wa Mkoa Geita, Martine Shigella akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa inayopitiwa na mradi wa EACOP amesema kuwa mradi wa EACOP ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo wananchi wa Geita wamenufaika nayo kwa namna mbalimbali ikiwemo ajira za moja kwa moja na muda na mfupi pamoja na  mnyororo wa thamani kupitia biashara ya vyakula, mbogamboga, matunda n.k
Amesema Mpango wa uwezeshaji wa vijana kiuchumi ni matunda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kuhakikisha vijana wanapata elimu na ujuzi hivyo mpango wa YEE unaongeza chachu hiyo ya utoaji elimu na ujuzi kwa wananchi wakiwemo vijana.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP wenye urefu wa km 1443 ni moja ya miradi 17 inayotekelezwa na Wizara ya Nishati ikiwemo mradi wa Julius Nyerere ( MW 2,115) ambao umekamilika, miradi ya umeme ya Ruhudji, Rumakali na Malagarasi pamoja miradi mingine ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia ukiwemo wa Eyasi Wembere.
Katika mradi wa EACOP amesema Serikali imechangia shilingi trilioni 1.12 ambazo ni hisa za Tanzania na kuna kampuni za kitanzania 200 ambazo zinafanya kazi mbalimbali katika mradi ambazo zitalipwa jumla ya shilingi trilioni 1.325 ikiwa ni moja ya matunda ya uwepo wa mradi huo nchini.

Akieleza sababu za kufanyika.kwa uzinduzi wa mradi wa YEE wiiayani Bukombe amesema kuwa Bukombe  kuna  kituo kikubwa zaidi cha kusukuma mafuta yatakayotoka nchini Uganda hadi Chongoleani Tanga, kuna kambi kubwa ya mradi wa EACOP na pia kilometa 20 za bomba hilo la mafuta zinapita katika eneo la Bukombe.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Makame ameeleza kuwa, TPDC imeendelea kushirikiana na kampuni ya EACOP kuhakikisha kuwa mahitaji ya wananchi yanabainishwa na kuzingatiwa katika utekelezaji wa mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Ameeleza kuwa mahitaji yaliyoainishwa katika mradi wa YEE yaliandaliwa kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa kwa ngazi ya vijiji, Kata na Halmashauri zilizopo maeneo linapopita bomba la mafuta. 
Awali Clare Haule - Meneja wa Uwekezaji na Uwajibikaji kwa Jamii katika kampuni ya EACOP alisema mradi wa YEE umeanzishwa kwa kutambua kwamba zaidi ya asilimia 65 ya idadi ya watu wa Tanzania ni vijana chini ya umri wa miaka 35. Hata hivyo, vijana wengi hasa katika maeneo ya vijijini wanakumbana na vikwazo vingi kama vile ukosefu wa ajira, ukosefu wa mafunzo ya ufundi stadi , na ugumu wa kupata mitaji ya kuanzisha au kukuza biashara.
Alisema awamu ya kwanza ya Mradi wa YEE  utawawezesha kiuchumi vijana katika mikoa ya Geita, Kgera, Tabora na Tanga pamoja na mikoa mingine inayobaki itanufaika katika awamu ya pili ambayo ni Singida, Shinyanga, Dodoma na Manyara ambapo vijana watapewa ujuzi  unaolingana na mahitaji ya soko, kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, na kuondoa vikwazo vya ujasiriamali na ajira binafsi.
Aliongeza kuwa, Mradi wa YEE ni sehemu ya Sera ya Uendelevu ya EACOP, chini ya nguzo ya Vizazi Vijavyo, inayolenga kujenga uwezo wa vijana na kuongeza upatikanaji wa fursa za kiuchumi katika jamii zinazoguswa na mradi.
Mwisho.

REA KUSAMBAZA MAJIKO BANIFU 10650 MKOANI PWANI

August 18, 2025 Add Comment


*📌RC Kunenge aipongeza REA kwa kuhamasisha matumizi nishati safi*


*📌Mifumo ya umeme jua kuchochea upatikanaji wa umeme

kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030*


📍Pwani


Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetoa jumla ya Majiko Banifu 10,650 Mkoani Pwani ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuhakikisha  kila mwananchi anatumia Nishati Safi ya kupikia nchini. 


Akizungumza leo tarehe 18 Agosti, 2025 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Meneja wa Teknolojia za Nishati kutoka REA, Mha. Michael Kyessi amesema mradi huo unalenga kuuza na kusambaza Majiko Banifu kwa bei ya ruzuku ambapo mwananchi atachangia asilimia ishirini (20%) za gharama ya jiko huku asilimia themanini (80%) zikitolewa na Serikali. 

“Mwananchi wa kawaida atachangia 20% tu za gharama za jiko ambapo bei ya jiko ni 56,000 na mwananchi atagharamika kuchangia shilingi 11,200 tu baada ya ruzuku kutolewa na Serikali” amesema Mha. Kyessi. 



Sambamba na hilo Mha. Kyessi amebainisha thamani ya mradi huo kwa ujumla ni milioni 596,400,00 ambapo Serikali kupitia REA imetoa ruzuku ya shilingi milioni 477,120,00 ambayo ni sawa na asilimia themanini. 

Katika hatua nyingine, REA inatekeleza lengo la Serikali ya Tanzania kufikia mpango wa Umoja wa Mataifa wa "Nishati Endelevu kwa Wote" (SE4ALL) wa upatikanaji wa nishati 

kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2030. Mradi huu utatumia nishati Jadidifu ili kuweza kufikia wananchi wa maeneo ya visiwani na utekelezaji wake ni kwa kupitia mradi wa Ufadhili unaotegemea Matokeo (RBF) kupitia Benki ya Dunia. 

"Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kufunga mifumo ya umeme jua maeneo ya visiwani kwa 

kutoa ruzuku kwa bei ya mwisho ya mtumiaji wa mfumo wa Umeme Jua ili kufanikisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo yaliyo mbali na Gridi ya Taifa, " Amesema Mha. Kyessi. 

Mha. Kyessi amesema katika Mkoa wa Pwani mradi wa umeme jua unategemea kuhudumia visiwa 13 na jumla ya watoa huduma wawili (2) wanategemea kuhudumia visiwa hivyo kupeleka jumla ya mifumo 2,243 ndani ya kipindi cha miaka miwili (2) na gharama za mradi kwa mkoa wa Pwani ni shilingi  bilioni 1.372 ambapo ruzuku ni shilingi milioni 935.7 sawa na asilimia 69 ya gharama zote ya mradi na shilingi milioni 436.6 ni fedha toka kwa wanufaika. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge ameipongeza REA kwa mkakati wa kuendelea kuongeza matumizi ya Nishati safi na kuondoa kero kwa wananchi kuhusu matumizi ya kuni na mkaa ambayo ni hatarishi kwa afya zao. 

 

Mradi huo utatekelezwa kwa muda wa miezi 15 katika mkoa wa Pwani na jumla ya Majiko Banifu 10,650 yatasambazwa kwa wananchi.

HAMADI –NITAFANYA KAZI KWA UADILIFU KUHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA MAENDELEO

August 18, 2025 Add Comment


KADA ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Hamadi Shamisi Hamadi leo amechukua fomu ya kuwania Udiwani Kata ya Msambweni Jijini Tanga huku akihaidi kufanya kazi kwa uadilifu.

Hamadi aliyasema hayo leo mara baada ya kuchukua fomu katika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Msambweni huku akiwa amesindikizwa na wanachama wa chama hicho wakiwemo wananchi.

Alisema kwamba lengo lake ni kuhakikisha anawatumikia wananchi wa kata hiyo na kuwa kiungo cha maendeleo ya wananchi na hivyo kuchochea ukuaji wa maendeleo.

“Nawaambia tutafanya kazi kwa dhati na kutanguliza uaminifu na uadilifu kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na shahidi ni Baba yangu mzazi ambaye ananisindikiza hapa”Alisema

Awali akizungumza Mwenyekiti wa CCM kata ya Msambweni alisema kwamba hicho ni kishindo cha kwanza ila Agosti 28 wanaanza kampeni zao na wanafungua kwenye tawi la Msambweni B eneo la Komesho watakuwa na Mbunge wa Tanga Jijini kampeni za wilaya zitafunguliwa hapo.

Alisema Agosti 29 utakuwa uzinduzi wa kampeni wa Diwani wa Kata ya Msambweni na zitazinduliwa Mtaa wa Madina eneo la Mabanda ya Papa huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo.

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa zamani wa Mtaa wa Madina Godfrey Mazimu alisema kwamba amefurahi kuona wanachama wenzake na wananchi wa Msambweni huku akiwataka kuendelea kuunganisha nguvu za pamoja mpaka mwisho na wasiachane.


TARURA MUSOMA WAPONGEZWA UJENZI WA MIRADI KULINGANA NA THAMANI YA FEDHA

August 18, 2025 Add Comment


Na Mwandishi Wetu, Mara.


Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Ndugu Ismail Ali Ussi amewapongeza wafanyakazi wa TARURA wilaya ya Musoma kwa kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanajenga miradi ya miundombinu ya barabara kulingana na thamani halisi ya fedha.

Ndugu Ussi ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya Nyabisarye Mahakama kuu Kanda ya Musoma yenye urefu wa Mita 700 kwa kiwango cha lami .

Ussi amesema kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa lengo la kuwarahisishia wananchi huduma katika maeneno yao ili waweze kufanya shughuli zao za kiuchumi na kujiingizia kipato.

Kwa upande wake Kaimu Meneja Wilaya ya Musoma Mhandisi Mohamed Etanga amesema jumla ya shilingi Milioni 600.97 zimetengwa kwaajili ya ujenzi wa barabara ya Nyabisarye- Mahakama Kuu yenye urefu wa Mita 700 kwa kiwango cha lami .

Amebainisha kuwa ujenzi wa barabara hiyo ulianza Oktoba mwaka jana na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2025.

Mhandisi Etanga ameongeza kusema kuwa barabara hiyo endapo itakamilika itakuwa kiunganishi cha Kata ya Bweri na Kata ya Rwamlimi na kuwa kiungo kikubwa kwa wananchi katika kupata mahitaji ya kijamii kwa wepesi.




WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKISAFIRI KWA TRENI YA UMEME YA KIWANGO CHA KIMATAIFA (SGR) KUTOKA DODOMA KUELEKEA DAR ES SALAAM LEO AGOSTI

August 18, 2025 Add Comment


 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisafiri kwa Treni ya umeme ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Dodoma kuelekea Dar es Salaam, Agosti 18, 2025.



KIKWETE : SERIKALI KUSAINI MUONGOZO WA KIMA CHA CHINI CHA MSHAHARA KWA SEKTA BINAFSI

August 18, 2025 Add Comment


SERIKALI imesema hivi karibuni inatarajia kusaini kuwa Sheria miongozo Wa kima cha chini Cha mshahara kwa TaasisiI binafsi zinazofanywa kazi nchini.


Imesema katika miongozo huo inatarajia kuainisha viwango vipya vya mshahara ambapo wafanyakazi Wa sekta binafsi watakuwa wanalipwa.

Waziri Wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira  Vijana Na Wenye Ulemavu  ,Ridhiwan Kikwete amesema hayo jijini Arusha katika uzinduzi wa jengo la  biashara Shirikisho La Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) lililoko mkabala na soko kuu.

Kuhusu miongozo huo amesema mazungumzo yameshafanyika baina ya wadau ambao ni Taasisi binafsi na wasimamizi wa sera lakini pia uongozi wa timu Ya Wizara iliyopewa jukumu la kusimamia marekebisho hayo.


Amesema kikao kilichobakia ni Cha mashauri ambapo watashauriana na wenzao juu ya viwango vilivyowekwa na baada ya hapo mapema mwezi ujao huenda wakasaini marekebisho hayo.

“Hivyo nawaambia Wafanyakazi kuwa Rais Dkt Samia anathamini sana maslahi yenu,” amesema Ridhiwan na kuongeza kuwa serikali Itaendelea kuboresha sheria za Wafanyakazi Ili ziendane na mahitaji ya wafanyakazi.

Amesema  Serikali  itaendelea kushirikiana na Wafanyakazi  bega kwa bega katika:Kutekeleza mikakati ya kuongeza ajira;Kulinda haki za wafanyakazi;Kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo.

DKT. TULIA AKOSHWA NA CRDB BANK MARATHON IKIKUSANYA BILIONI 2 KUSAIDIA AFYA NA UWEZESHAJI JAMII

August 17, 2025 Add Comment

 


Dar es Salaam, 17 Agosti 2025 - Maelfu ya wakimbiaji na wapenda michezo kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza leo katika viwanja vya The Green, Oysterbay, kushiriki CRDB Bank Marathon 2025, mbio za hisani ambazo mwaka huu zimekusanya Shilingi Bilioni 2 ili kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, wakinamama wenye ujauzito hatarishi, na vijana kupitia programu ya iMBEJU.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, aliongoza maelfu ya washiriki kwenye msimu huu wa sita wa CRDB Bank Marathon.
Akitoa salamu zake, Dkt. Tulia alipongeza ubunifu wa CRDB Bank Foundation katika kuunganisha jamii kupitia michezo na kusaidia wenye uhitaji, akieleza kuwa mbio hizo ni mfano wa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya wengi.

“Ushiriki wetu katika CRDB Bank Marathon ni tendo la huruma linaloleta faraja kwa watoto na wakinamama na familia zao. Ni ushahidi kwamba tukishirikiana, tunaweza kubadilisha maisha,” alisema.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, aliipongeza Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation kuendelea kuandaa mbio hizo.

Alisema, “CRDB Bank Marathon si tu imekuwa ikikuza afya na mshikamano wa kijamii, bali pia imekuwa ikifungua milango ya ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana wetu. Michezo ni sekta inayoweza kubadili maisha, na ninapongeza sana kitendo cha kuweka zawadi nono kwa washindi. Hizi ni fursa ambazo zinaweza kuwa mtaji wa kuanzisha biashara na kuimarisha maisha ya vijana wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama CRDB Bank Foundation kuhakikisha michezo inakuwa chachu ya maendeleo ya taifa.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alibainisha kuwa msimu wa sita wa CRDB Bank Marathon umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, na kuendelea kupanua wigo wa matokeo yake ndani na nje ya Tanzania. Kwa mara ya pili, mbio hizi zimefanyika pia nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zikikusanya fedha kwa ajili ya miradi ya afya na ustawi wa jamii katika nchi hizo.

Nsekela alisema kuwa mbio za mwaka huu zimeweza kuvutia zaidi ya washiriki 16,000, na kufanikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 2 ambapo pamoja na kusaidia maandalizi ya mbio hizo, shilingi milioni 450, zimeelekezwa kusaidia wenye uhitaji katika jamii.

Kati ya hizo shilingi milioni 100 zimekwenda hospitali ya CCBRT kusaidia wakinama wenye ujauzito hatarishi kujifungua salama, shilingi milioni 100 zimekwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kusaidia upasuaji wa Watoto wenye matatizo ya moyo, na shilingi 250 zitaelekezwa katika uwezeshaji wa vijana.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alieleza kuwa safari ya msimu wa sita imeanzia Lubumbashi, DRC, ambako zilikusanywa Dola za Marekani 70,000 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali ya Jeshi la Ruashi, na kuendelea Bujumbura, Burundi, ambapo zilipatikana Faranga za Burundi milioni 175 kusaidia bima ya afya kwa zaidi ya watu 58,000 wasiojiweza.

Mwambapa alisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya mshikamano wa kipekee wa serikali za nchi shiriki, wadhamini na washiriki, akiwashukuru wadau wote waliotoa jitokeza kuchangia ikiwamo kampuni za bima za Sanlam Life na Alliance Life ambao wamekuwa sehemu ya mbio hizi tangu kuanzishwa kwake.

Washindi wa mbio za mwaka huu upande wa Tanzania kwa Kilometa 42 upande wa wanawake ni Joyloyce Kemuma kutoka Kenya, upande wa wanaume mshindi ni Abraham Kiptum kutoka Kenya. Kilometa 21 upande wa wanawake ni Catherine Syokau kutoka Kenya, na upande wa wanaume ni Joseph Panga kutoka Tanzania. Kilometa 10 upande wa wanawake ni Silia Ginoka kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Boayi Maganga kutoka Tanzania.

Joseph Panga mshindi wa mbio za Kilometa 21 upande wa wanawake ameeleza furaha yake kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa ushindi wake ni sehemu ya kusaida matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na matibabu ya wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT.

“Mimi kama Mtanzania najisikia fahari kubwa kushiriki kusambaza tabasamu kwa watoto na wakinamama. Ni muhimu watu kufahamu kuwa afya bora ni haki ya kila mtoto, na hakuna mama anayestahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Tunawashukuru CRDB Bank Foundation kwa kutuleta pamoja katika harakati hizi za kuokoa maisha,” amesema.
CRDB Bank Marathon imekuwa jukwaa muhimu la kuchochea ustawi wa kijamii katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na kati hivi karibuni ikipata heshima ya kutambuliwa kimataifa kwa kushinda tuzo ya jukwaa bora la taasisi za fedha katika kusaidia kusaidia jamii.