NA MASHAKA MHANDO
WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kupitia Taasisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA), inatarajia kuweka historia mpya kwa kugawa zaidi ya shilingi bilioni moja kama mirabaha kwa wasanii wa makundi mbalimbali nchini ifikapo Januari 23, 2026.
Hatua hiyo inakuja baada ya majadiliano ya kimkakati kati ya Naibu Waziri wa sekta hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma (MwanaFA), na uongozi wa COSOTA, yaliyolenga kujibu kiu ya muda mrefu ya wasanii kuhusu malipo ya haki zao.
Akizungumza katika mahojiano maalum, MwanaFA alisema kuwa Serikali imejipanga kufanya ugawaji huo kuwa shughuli kubwa na ya kihistoria kutokana na kiwango kikubwa cha fedha kilichokusanywa.
"Kama msanii na kama Naibu Waziri, nimekuwa nikipokea maswali mengi kutoka kwa wasanii wenzangu wakitaka kujua hatma ya mirabaha yao. Nimefanya majadiliano (discussion) nzuri na COSOTA na tumekubaliana kuwa Januari 23 mwakani, tunakwenda kutoa zaidi ya shilingi bilioni moja na ushee. Hiki ni kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kutokea nchini," alisema MwanaFA.
MwanaFA alibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na hatua ya Bunge kubadilisha sheria inayoruhusu kuanzishwa kwa Taasisi za Pamoja za Kusimamia Hakimiliki (Collective Management Organizations - CMOs).
Alieleza kuwa hadi sasa, leseni mbili zimetolewa kwa kampuni za CMO ambazo zimeshirikiana na taasisi za kimataifa, ikiwemo Taasisi ya Afrika Kusini inayosimamia mirabaha ya kidijitali (CAPASSO) kupata fedha hizo zinazokwenda kutolewa Januari.
Aidha, alitaja kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya fedha hizo ni pamoja na kodi ya vifaa vinavyobeba kazi za sanaa na ada zinazotokana na Vibali vya Jumla vya kupiga nyimbo kwenye Redio na Televisheni (Blanket License).
"Tumepata zaidi ya shilingi bilioni moja kupitia mfumo wa Blanket License. Fedha hizi zitawanufaisha wasanii, huku sehemu ikiongoza Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, COSOTA, pamoja na kodi ya Serikali," aliongeza.
Alifafanua kuwa tofauti na zamani, safari hii wigo umepanuliwa ambapo wanufaika watatoka katika makundi ya Muziki, Filamu, Sanaa za Maonyesho, Sanaa za Ufundi, pamoja na Waandishi wa Vitabu.
Hata hivyo, MwanaFA alitoa rai kwa wasanii wote: "ili unufaike na fedha hizi, ni lazima usajili kazi zako COSOTA. Usajili ndio utambulisho pekee utakaorahisisha utaratibu wa wewe kupata mirabaha yako pindi kazi zako zinapotumika au kuchezwa."
Mwisho

.jpg)











