








HABARI NA MATUKIO MBALIMBALI









Naibu Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko amesema kuwa mashindano ya ngalawa race ni miongoni mwa matukio makubwa ya kiburudani yanayoipamba Kizimkazi Festival 2026.
Mashindano hayo yamefanyika Kizimkazi, Kusini Unguja Agosti 12, 2026 yaliyokuwa na ushindani mkubwa ambapo Nassor Pandu wa Mkunguni ameibuka mshindi wa mashindano ya ngalawa ikiwa ni sehemu ya shughuli mbalimbali zinazoendelea katika Tamasha la Kizimkazi.
“ Ni dhahiri kwamba mashindano haya yamekuwa muhimu kwa vijana na jamii kwa ujumla. Tukio hili limewaleta pamoja wadau mbalimbali na kuchangia kwa kiasi kikubwa juhudi za kuboresha mazingira ya michezo na burudani,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa mashindano ya Ngalawa race Kizimkazi Festival yameendelea kutoa fursa za kiuchumi kwa vijana mbalimbali katika kushindana hadi kupata timu mbili bora za Mchangamle na Mkunguni ambapo kila timu imehusisha manahodha 10.
Mwisho.

Na Mwandishi Wetu, Muheza
Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani
Tanga, Ayoub Sebabili, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika
shughuli za mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2026, akisema ushiriki mkubwa wa
wananchi utasaidia wilaya hiyo kufanya vizuri katika mashindano ya Kitaifa ya Mwenge
wa Uhuru.
Sebabili ametoa wito huo wakati wa
zoezi la Jogging lililoandaliwa kama sehemu ya maandalizi ya mapokezi ya Mwenge
wa Uhuru, ambapo aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki
shughuli hiyo.
Alisema Mwenge wa Uhuru unatarajiwa
kuwasili wilayani Muheza Juni 23, 2026 ukitokea Wilaya ya Mkinga na kupokewa
katika eneo la Kilapura, huku ukitarajiwa kulala katika Uwanja wa Jitegemee.
"Niwashukuru kwa namna mlivyojitokeza leo. Ushiriki wenu unaonyesha dhamira ya kuhakikisha Muheza inafanya vizuri katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru. Kila mmoja wetu awe balozi wa kuhamasisha wananchi wengine kujitokeza kwa wingi," alisema Sebabili..
Kwa upande wake, Mratibu wa Mwenge
wa Uhuru Wilaya ya Muheza Amiri Msuya alisema maandalizi yanaendelea vizuri na kuwa
viongozi katika ngazi zote wamepewa jukumu la kuhamasisha wananchi wa makundi
mbalimbali, wakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kushiriki
kikamilifu katika shughuli hizo.
Alisema Mwenge wa Uhuru utapitia
maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuzindua na kukagua miradi ya
maendeleo pamoja na kutoa ujumbe wa umoja, uzalendo na mshikamano wa kitaifa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa,
Mwenge wa Uhuru utaanzia Kata ya Mlingano kabla ya kuelekea Machemba kwa
uzinduzi wa mradi na ukaguzi wa banda la lishe litakaloonyesha juhudi za
Halmashauri ya Muheza katika kupambana na utapiamlo, malaria na maambukizi ya
Virusi vya Ukimwi.
Baadaye utaelekea katika Shule ya
Venance Mabeyo na Kata ya Mpapayu kwa ajili ya uzinduzi wa miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Katika Kata ya Genge, Mwenge wa
Uhuru utazindua maabara katika Shule ya Sekondari Chief Mang'enya iliyojengwa
kwa nguvu za wananchi na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa madarasa mapya
kwa ajili ya maandalizi ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2027.
Mratibu huyo alisema pia kutakuwa na
shughuli za Klabu ya Wapinga Rushwa pamoja na programu mbalimbali za elimu kwa
jamii.
Katika Kata za Magila na Majengo,
Mwenge wa Uhuru utatembelea kikundi kilichonufaika na mkopo wa asilimia 10 wa
Halmashauri unaotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo
kikundi hicho kimepata Sh25 milioni kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya
kiuchumi.
Aidha, katika eneo la Mikwamba
kutakuwa na maonesho ya fursa za zabuni kupitia PPRA, yakilenga kuhamasisha
vikundi maalumu kushiriki katika zabuni zinazotengwa kwa makundi hayo.
Ratiba hiyo itahitimishwa kwa
shughuli mbalimbali katika Kata ya Tongwe na eneo la Mpaa, ikiwemo uzinduzi wa
daraja la karavati, uzinduzi wa Jengo la Havest Inn na mkesha wa Mwenge wa
Uhuru katika Uwanja wa Jitegemee.
Viongozi hao wamewataka wananchi
kuzingatia amani, utulivu na usalama katika kipindi chote cha shughuli hizo,
huku wakisisitiza kuwa vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani havitavumiliwa.
Akizungumza katika hafla hiyo,
Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) wa Muheza, Mohamed Mfaki, aliwashukuru wananchi
kwa ushirikiano wao katika maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na
kuwataka kuendelea kushiriki kikamilifu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dk Juma Mhina, alisema wilaya hiyo imejipanga
kufanya vizuri zaidi mwaka huu na inalenga kushika nafasi ya kwanza kitaifa
katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru
"Malengo yetu ni kuona wananchi
wanajitokeza kwa wingi katika shughuli zote za Mwenge wa Uhuru. Tunataka Muheza
iwe mfano wa mafanikio na ushirikiano katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru
2026," alisema Dk Mhina.
mwisho
Mamia ya wananchi wa Kata ya Kalemawe, Kijiji cha karamba wilayani Same, wamejitokeza kwa wingi kumpokea nyumbani kwao nyota chipukizi wa soka, Issa Chole, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Serengeti Boys chini ya umri wa miaka 17.
Mapokezi hayo yaliongozwa na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango, pamoja na viongozi mbalimbali wa eneo hilo na wananchi waliokusanyika kumpongeza kijana huyo kwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya AFCON 2026 kwa vijana chini ya miaka 17.
Shangwe na nderemo zilitawala katika kijiji hicho huku wananchi wakionesha fahari yao kwa mafanikio ya Issa Chole, ambaye ameibuka kuwa mmoja wa vijana wanaolipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa kupitia mchezo wa soka.
Akizungumza katika hafla hiyo, Anne Kilango alisema mafanikio ya Issa Chole ni jambo kubwa kwa wakazi wa Same Mashariki na Taifa kwa ujumla kwani yanaonesha kuwa vijana wa eneo hilo wana uwezo wa kufikia ndoto zao wanapopewa fursa sahihi.
Alisema ujio wa mchezaji huyo nyumbani ni heshima kubwa kwa jimbo hilo na ushahidi kwamba uwekezaji katika michezo unaweza kuzaa matokeo chanya kwa vijana na jamii kwa ujumla.
Kilango alibainisha kuwa Issa Chole ni miongoni mwa vijana waliopitia mashindano ya Samia Cup, yanayoandaliwa kila mwaka katika Jimbo la Same Mashariki kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vya michezo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, zaidi ya timu 91 kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo hushiriki mashindano hayo, ambayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwapa vijana nafasi ya kuonesha uwezo wao.
Alisema kupitia mashindano hayo, vijana wengi wameanza kuonekana katika ngazi za juu za soka na wengine wamepata nafasi ya kujiendeleza katika taaluma ya michezo.
“Leo tunashuhudia matunda ya Samia Cup. Issa ametufanya tujivunie kama wananchi wa Same Mashariki na kama Watanzania. Hii ni ishara kwamba tuna vijana wengi wenye vipaji ambao wanahitaji kuungwa mkono,” alisema Kilango.
Aliongeza kuwa ataendelea kuimarisha mashindano hayo ili kuhakikisha vipaji zaidi vinaibuliwa na kupata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Mbunge huyo pia aliahidi kuanzisha na kuendeleza michezo mingine ikiwemo mpira wa miguu kwa wasichana na mpira wa pete, kwa lengo la kuwapa vijana na watoto wa kike fursa zaidi za kukuza vipaji na kujenga ajira kupitia michezo.
Kwa upande wake, Issa Chole aliwashukuru wananchi wa Kalemawe pamoja na Anne Kilango kwa mapokezi makubwa aliyoyapata, akisema hakuwahi kutarajia kupokelewa kwa namna hiyo baada ya kurejea kutoka majukumu ya timu ya taifa.
Alisema mafanikio yake yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mashindano ya Samia Cup yaliyompa nafasi ya kuonekana na kuanza safari yake ya soka la ushindani, huku akiwataka vijana wengine kushiriki mashindano hayo kwa nidhamu, kujituma na kuwa na malengo makubwa maishani.
Baba mzazi wa mchezaji huyo, Mzee Musa Chole, alisema anajivunia maendeleo ya mwanawe katika soka na kusisitiza kuwa nidhamu, mazoezi na kujituma ndiyo msingi wa mafanikio katika mchezo huo.Aidha, alimuomba Mbunge Anne Kilango kuendelea kuunga mkono vijana kupitia Samia Cup ili vipaji zaidi viweze kuibuliwa na kuendelezwa.
Naye mmoja wa wananchi wa Kata ya Kalemawe alisema jitihada za mbunge huyo katika kuendeleza michezo zimekuwa na manufaa makubwa kwa vijana, kwani zimewapa hamasa ya kujituma, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, ulevi na vitendo vingine vinavyoweza kuharibu maisha yao, huku akimpongeza kwa kujitokeza kushiriki mapokezi hayo ambayo yameonesha mshikamano mkubwa kati ya viongozi na wananchi.