Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts

WADAU WA SEKTA YA AFYA ZAIDI YA 3000 KUSHIRIKi MKUTANO WA KIMATAIFA WA HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI

September 06, 2026 Add Comment




Na: OWM – TAMISEMI, Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe,  amesema zaidi ya wadau wa sekta ya afya 3000 kutoka nchi mbalimbali Duniani  watashiriki katika Mkutano wa pili wa Kimataifa wa Huduma za Afya ya Msingi (IPHCC), jijini Arusha. 



Prof. Shemdoe  amesema hayo mapema leo Septemba 06, 2026 akiwa jijini Dodoma, kabla ya kuelekea Arusha na kuwakaribisha washiriki hao kwenye mkutano huo utakaofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 11 Septemba, 2026  katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).


Prof. Shemdoe amesema, yeye binafsi atashiriki katika mkutano huo wenye tija katika kuboresha utoaji wa huduma za afya msingi nchini na afrika kwa ujumla.


Prof. Shemdoe amesema mkutano huo umelenga kutoa uzoefu wa Tanzania katika uboreshaji wa huduma za afya ya msingi, ikiwamo afua zilizopelekea kupunguza vifo vya akina mama na watoto ambapo Tanzania kupitia jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ni kinara katika eneo hilo barani Afika.


Prof. Shemdoe amefafanua kuwa, mkutano huo umelenga pia kubadilishana uzoefu wa maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika katika huduma za afya ya msingi duniani pamoja na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuboresha huduma za afya ya msingi ili kufikia malengo ya kitaifa na Kimataifa, ikiwamo upatikanaji wa Huduma za Afya kwa wote na malengo endelevu ya maendeleo.


Mkutano huo wa kihistoria utawakutanisha washiriki zaidi ya 3000 kutoka Tanzania na mataifa mengine duniani wakiwamo; wataalam wa afya wanaofanya kazi ya kutoa huduma za afya ya msingi, watunga sera, wadau wa maendeleo, watafiti, wahadhiri, wanafunzi, asasi za kiraia na sekta binafsi, ambapo washiriki hao wamejisajiri kupitia tovuti ya   https://iphcconference.tamisemi.go.tz .

NHIF TANGA YATOA ELIMU YA BIMA NA KUFANYA UPIMAJI WA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA KANISA LA KKKT USHIRIKA WA MAKORORA TANGA

July 06, 2026 Add Comment



Na Oscar Assenga,TANGA

Wazazi, walezi na waajiri nchini wamehimizwa kuhakikisha watoto wanawakatia bima ya afya mapema ili kuwaepusha na changamoto za gharama kubwa za matibabu na kuwawezesha kupata huduma za afya kwa wakati wanapougua.

Wito huo umetolewa leo na Afisa Matekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tanga, Macrina Clemens, wakati wa utoaji wa elimu kuhusu bima ya afya ulioambatana na zoezi la upimaji wa afya na usajili wa wanachama wa vifurushi mbalimbali katika Kanisa la KKKT Ushirika wa Makorora, jijini Tanga.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo, Macrina alisema afya ni mtaji muhimu kwa maendeleo ya familia na Taifa, hivyo kujiunga na bima ya afya ni uwekezaji unaowalinda wananchi dhidi ya gharama zisizotarajiwa za matibabu.

Alisema wazazi wanaowakatia watoto wao bima ya afya hupata uhakika wa matibabu wakati wowote mtoto anapougua, jambo linalowapa utulivu wa akili na kuwawezesha watoto kuendelea na masomo bila kukatishwa na changamoto za kifedha.

“Mzazi anapokuwa na bima ya afya kwa mtoto wake anakuwa na uhakika wa kupata matibabu kwa wakati, hivyo kuepuka usumbufu wa kutafuta fedha za dharura kila ugonjwa unapojitokeza,” alisema.

Macrina alisema wanafunzi wanaosoma katika shule mbalimbali wanaweza kujiunga na bima ya afya kupitia shule zao kwa gharama ya Sh50,400 kwa mwaka mzima wa masomo, huku watoto ambao bado hawajaanza shule wakijiunga kupitia vifurushi mbalimbali vinavyotolewa na NHIF.

Alisema Serikali inaendelea kutekeleza azma ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya, hivyo akazitaka taasisi za elimu, wazazi, walezi, waajiri na wamiliki wa kampuni binafsi kutumia fursa hiyo kuwaandikisha watoto na wafanyakazi wao.

“Bima ya afya si gharama, ni kinga ya maisha. Ukiwa na bima unakuwa na uhakika wa kupata daktari, dawa na huduma za matibabu bila kubeba mzigo mkubwa wa kifedha pale unapougua,” alisema.

NHIF imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya wananchi kuhusu umuhimu wa bima ya afya ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na huduma hiyo na kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.




ZAIDI YA WANANCHI 6000 KUNUFAIKA NA ZAHANATI YA MUUNGANO,MWENGE WA UHURU WARIDHISHWA NA MRADI

June 23, 2026 Add Comment


Na Oscar Assenga, Muheza

WANANCHI 6,258 wa Kijiji cha Muungano, Wilaya ya Muheza, wanatarajiwa kunufaika na huduma bora za afya kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati ya Muungano, mradi ambao umepokelewa na kuridhiwa na Mwenge wa Uhuru 2026 baada ya kukaguliwa na kupokea taarifa ya utekelezaji wake.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 Wazo Mwang'onda alisema kukamilika kwa zahanati hiyo kutasaidia kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi na kupunguza changamoto ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Alisema Serikali tayari imepeleka vifaa tiba pamoja na watumishi wa afya watakaotoa huduma katika zahanati hiyo, hatua inayoonesha dhamira ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, hususan katika maeneo ya vijijini.

“Mradi huu ni muhimu kwa wananchi wa Muungano na maeneo jirani kwa sababu unasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuongeza ustawi wa jamii,” alisema.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa mafanikio ya mradi huo yametokana na ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo, hususan Taasisi ya Islamic Help, iliyochangia ujenzi wa zahanati hiyo, huku Serikali ikigharamia vifaa tiba na watumishi wa afya.

Aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kijamii, na kuwataka kuendeleza ushirikiano huo ili kusaidia kuboresha huduma muhimu kwa wananchi.

Aidha, aliwahimiza wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, akisema kuwa mazingira hayo yanawezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuvutia wadau zaidi kushirikiana na Serikali.

Kwa upande wake, akitoa taarifa ya mradi huo, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Dk. Fani Mussa, alisema ujenzi wa Zahanati ya Muungano ulianza Machi 2, 2025 na kukamilika kwa gharama ya Shilingi milioni 165.94.

Alieleza kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi milioni 141.55 zilitumika kwa ujenzi, huku Shilingi milioni 24.39 zikitumika kununua vifaa tiba.

Kwa mujibu wa Dk. Mussa, zahanati hiyo itahudumia wakazi 6,258 wa Kijiji cha Muungano, wakiwemo wanaume 3,089 na wanawake 3,169, na inatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hilo.

Baada ya ukaguzi huo, Mwenge wa Uhuru 2026 ulieleza kuridhishwa na ubora wa utekelezaji wa mradi huo, ukibainisha kuwa ni hatua muhimu katika kusogeza huduma za afya karibu na wananchi na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya afya nchini.









ZAIDI YA KAYA 7,800 TANGA ZANUFAIKA NA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

June 09, 2026 Add Comment

 

Na Oscar Assenga,TANGA

Zaidi ya wananchi 20,000 kutoka kaya masikini mkoani Tanga wameanza kunufaika na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu kwa kaya zenye kipato cha chini.

Mpango huo, unaotekelezwa kwa awamu ya kwanza na ya pili, unalenga kuwafikia wananchi walio katika mazingira magumu kiuchumi ili kuwawezesha kupata huduma za afya bila kikwazo cha gharama za matibabu. Ufadhili wa mpango huo unatolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ukiwa na lengo la kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa kaya masikini.

Hadi sasa, zaidi ya wanufaika 20,000 kutoka kaya 7,816 wamepatiwa kadi za bima ya afya na wameanza kutumia huduma hizo tangu Machi mwaka huu. Hatua hiyo imeelezwa kuwa imeleta matumaini mapya kwa wananchi wengi ambao hapo awali walikabiliwa na changamoto ya kumudu gharama za matibabu.

Akizungumza katika Maonesho ya Kibiashara ya Mwahako, Daktari Lawi Kupaza kutoka Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tanga amesema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, huku wengi wa walengwa waliostahili tayari wakikabidhiwa kadi zao.

Amesema zoezi hilo linaendelea vizuri katika halmashauri zote za mkoa huo, huku awamu ya pili ikitarajiwa kufikia kaya nyingine 1,300.

“Kwa sasa tunaendelea na ugawaji wa kadi pamoja na uhakiki wa taarifa za wanufaika. Tunawahamasisha wananchi kujitokeza kuhakiki taarifa zao ili waweze kupata huduma kwa wakati,” amesema Dkt. Kupaza.

Hata hivyo, amekiri kuwepo kwa changamoto ya kuwafikia wanufaika wote kwa wakati kutokana na ukubwa wa maeneo ya utekelezaji na ratiba za shughuli mbalimbali.

“Kuna changamoto ya kuwafikia wanufaika wote kwa wakati kutokana na ratiba na ukubwa wa eneo la utekelezaji. Hata hivyo, watendaji wa kata na vijiji wanaendelea kusaidia katika uhamasishaji,” ameongeza.

Kwa upande wake, Afisa Madai wa NHIF, Neema Kisinga, ameitaka jamii kuendelea kujiunga na bima ya afya ili kujikinga na gharama kubwa za matibabu.

Amesema mfuko huo una vifurushi mbalimbali vinavyowezesha wananchi kupata huduma za afya kwa gharama nafuu, ikiwemo kifurushi cha Tarangire ambacho kinatoa huduma za matibabu, vipimo na ushauri wa daktari kwa gharama nafuu kwa mwaka mzima.

“Kuwa na bima ya afya kunapunguza mzigo wa kulipia huduma kila unapougua au kuhitaji matibabu. Hii ni njia bora ya kujilinda na gharama zisizotarajiwa za afya,” amesema Kisinga.

Mpango huo unaendelea kuonekana kama hatua muhimu katika juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wote, hususan wa kipato cha chini, wanapata huduma bora za afya bila kuathiriwa na changamoto za kifedha.

SMZ YATAJA MAFANIKIO YA BIMA YA LAZIMA KWA WAGENI

Kajunason June 07, 2026 Add Comment
Na Mwandishi Wetu, Arusha.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 kutangaza mafanikio ya mpango wa bima ya lazima kwa wasafiri, ikieleza kuwa umeimarisha usalama wa wageni na kuchangia ukuaji wa sekta ya afya pamoja na mapato ya utalii visiwani humo.

Mpango huo ulioanza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024, unawataka wageni wote wa kimataifa wanaoingia Zanzibar kuwa na bima ya usafiri kabla ya kuwasili. Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato, ukiingiza wastani wa dola za Marekani milioni moja, sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.6 kila mwezi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenye viwanja vya Magereza jijini Arusha, Ofisa Mauzo wa shirika hilo, Abdul-Halim Muhammad, alisema maonesho hayo yamewapa fursa ya kutoa elimu kwa watalii, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuhusu umuhimu wa bima hiyo.

“Tunashiriki Karibu-KiliFair kuongeza uelewa kuhusu bima hii ya lazima na kueleza namna inavyowanufaisha wageni huku ikichangia maendeleo ya huduma muhimu Zanzibar,” alisema.

Kwa mujibu wa utaratibu huo, wageni wengi wa kimataifa hulipa dola 44 za Marekani kwa kila safari ya kuingia Zanzibar, huku wageni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakilipia dola 22 pekee. Watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 hulipa dola 22, huku walio chini ya umri huo wakisamehewa.

Muhammad alisema bima hiyo inawawezesha wageni kupata huduma za matibabu ya dharura na msaada mwingine muhimu wanapokuwa Zanzibar, hatua inayopunguza changamoto za kifedha na kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka wanapozihitaji.

Alisema sehemu ya mapato yanayokusanywa kupitia mfuko huo hutumika kugharamia huduma za afya kwa wageni waliokatiwa bima, huku fedha zinazobaki zikielekezwa katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi na wageni kwa ujumla.
“Mpango huu ulianzishwa baada ya mamlaka kubaini kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya watalii na wawekezaji kuhitaji matibabu ya dharura huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani angegharamia huduma hizo. Sasa mfumo huu umeondoa changamoto hiyo,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KiliFair Promotions, Dominic Shoo, alisema Karibu-KiliFair 2026 imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama maonesho makubwa ya utalii na biashara Afrika Mashariki kwa kuwakutanisha wadau kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.

Alisema maonesho hayo yamevutia zaidi ya waoneshaji 500 na wanunuzi wa huduma za utalii wapatao 20,000, hatua inayochochea uwekezaji, ushirikiano wa kibiashara na upanuzi wa masoko ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Karibu-KiliFair ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kimataifa. Kadri wadau wanavyoongezeka kushiriki, ndivyo fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa sekta ya utalii zinavyozidi kuongezeka,” alisema Shoo.