DKT. TULIA AKOSHWA NA CRDB BANK MARATHON IKIKUSANYA BILIONI 2 KUSAIDIA AFYA NA UWEZESHAJI JAMII

August 17, 2025

 


Dar es Salaam, 17 Agosti 2025 - Maelfu ya wakimbiaji na wapenda michezo kutoka ndani na nje ya Tanzania wamejitokeza leo katika viwanja vya The Green, Oysterbay, kushiriki CRDB Bank Marathon 2025, mbio za hisani ambazo mwaka huu zimekusanya Shilingi Bilioni 2 ili kusaidia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, wakinamama wenye ujauzito hatarishi, na vijana kupitia programu ya iMBEJU.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, aliongoza maelfu ya washiriki kwenye msimu huu wa sita wa CRDB Bank Marathon.
Akitoa salamu zake, Dkt. Tulia alipongeza ubunifu wa CRDB Bank Foundation katika kuunganisha jamii kupitia michezo na kusaidia wenye uhitaji, akieleza kuwa mbio hizo ni mfano wa vitendo vya huruma vinavyogusa maisha ya wengi.

“Ushiriki wetu katika CRDB Bank Marathon ni tendo la huruma linaloleta faraja kwa watoto na wakinamama na familia zao. Ni ushahidi kwamba tukishirikiana, tunaweza kubadilisha maisha,” alisema.
Akitoa salamu zake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, aliipongeza Benki ya CRDB na CRDB Bank Foundation kuendelea kuandaa mbio hizo.

Alisema, “CRDB Bank Marathon si tu imekuwa ikikuza afya na mshikamano wa kijamii, bali pia imekuwa ikifungua milango ya ajira na fursa za kiuchumi kwa vijana wetu. Michezo ni sekta inayoweza kubadili maisha, na ninapongeza sana kitendo cha kuweka zawadi nono kwa washindi. Hizi ni fursa ambazo zinaweza kuwa mtaji wa kuanzisha biashara na kuimarisha maisha ya vijana wetu. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kama CRDB Bank Foundation kuhakikisha michezo inakuwa chachu ya maendeleo ya taifa.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alibainisha kuwa msimu wa sita wa CRDB Bank Marathon umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Benki ya CRDB, na kuendelea kupanua wigo wa matokeo yake ndani na nje ya Tanzania. Kwa mara ya pili, mbio hizi zimefanyika pia nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zikikusanya fedha kwa ajili ya miradi ya afya na ustawi wa jamii katika nchi hizo.

Nsekela alisema kuwa mbio za mwaka huu zimeweza kuvutia zaidi ya washiriki 16,000, na kufanikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 2 ambapo pamoja na kusaidia maandalizi ya mbio hizo, shilingi milioni 450, zimeelekezwa kusaidia wenye uhitaji katika jamii.

Kati ya hizo shilingi milioni 100 zimekwenda hospitali ya CCBRT kusaidia wakinama wenye ujauzito hatarishi kujifungua salama, shilingi milioni 100 zimekwenda Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kusaidia upasuaji wa Watoto wenye matatizo ya moyo, na shilingi 250 zitaelekezwa katika uwezeshaji wa vijana.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, alieleza kuwa safari ya msimu wa sita imeanzia Lubumbashi, DRC, ambako zilikusanywa Dola za Marekani 70,000 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali ya Jeshi la Ruashi, na kuendelea Bujumbura, Burundi, ambapo zilipatikana Faranga za Burundi milioni 175 kusaidia bima ya afya kwa zaidi ya watu 58,000 wasiojiweza.

Mwambapa alisisitiza kuwa mafanikio haya ni matokeo ya mshikamano wa kipekee wa serikali za nchi shiriki, wadhamini na washiriki, akiwashukuru wadau wote waliotoa jitokeza kuchangia ikiwamo kampuni za bima za Sanlam Life na Alliance Life ambao wamekuwa sehemu ya mbio hizi tangu kuanzishwa kwake.

Washindi wa mbio za mwaka huu upande wa Tanzania kwa Kilometa 42 upande wa wanawake ni Joyloyce Kemuma kutoka Kenya, upande wa wanaume mshindi ni Abraham Kiptum kutoka Kenya. Kilometa 21 upande wa wanawake ni Catherine Syokau kutoka Kenya, na upande wa wanaume ni Joseph Panga kutoka Tanzania. Kilometa 10 upande wa wanawake ni Silia Ginoka kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Boayi Maganga kutoka Tanzania.

Joseph Panga mshindi wa mbio za Kilometa 21 upande wa wanawake ameeleza furaha yake kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa ushindi wake ni sehemu ya kusaida matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na matibabu ya wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT.

“Mimi kama Mtanzania najisikia fahari kubwa kushiriki kusambaza tabasamu kwa watoto na wakinamama. Ni muhimu watu kufahamu kuwa afya bora ni haki ya kila mtoto, na hakuna mama anayestahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Tunawashukuru CRDB Bank Foundation kwa kutuleta pamoja katika harakati hizi za kuokoa maisha,” amesema.
CRDB Bank Marathon imekuwa jukwaa muhimu la kuchochea ustawi wa kijamii katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na kati hivi karibuni ikipata heshima ya kutambuliwa kimataifa kwa kushinda tuzo ya jukwaa bora la taasisi za fedha katika kusaidia kusaidia jamii.

Share this

Related Posts

Latest
Previous
Next Post »